Rais Mhe.Dkt. Samia Suluhu Hassan ahutubia kwenye Kilele cha Maadhimisho ya Sikukuu ya Wakulima Nanenane Kitaifa katika Viwanja vya Dkt. John Samuel Malecela, Jijini Dodoma









Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan akitembelea banda la Kampuni ya pembejeo za kilimo ya Betaren ya Urusi katika Maonesho ya Kilimo ya Nanenane yanayofanyika Kitaifa katika viwanja vya Maonesho vya Dkt. John Samuel Malecela, Jijini Dodoma, tarehe 08 Agosti, 2026.










Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan akiwa kwenye Trekta baada ya uzinduzi wa magari kwa ajili ya Wakala ya Taifa ya Huduma za Ugani (NAESA) na Matrekta ya vyama vya Ushirika kwenye Maonesho ya Kilimo ya Nanenane, Kitaifa katika viwanja vya Maonesho vya Dkt. John Samuel Malecela, Jijini Dodoma, tarehe 08 Agosti, 2026.Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan akizungumza na Waziri wa Kilimo Mhe. Daniel Chongolo wakati wa Kilele cha Maadhimisho ya Sikukuu ya Wakulima Nanenane ambayo Kitaifa yanafanyika katika viwanja vya Maonesho vya Dkt. John Samuel Malecela, Jijini Dodoma, tarehe 08 Agosti, 2026.




















-ASISITIZA SERIKALI INATHAMINI MCHANGO WA TAASISI ZA DINI KATIKA MAENDELEO YA TAIFA HUSUSANI SEKTA YA AFYA NA ELIMU

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Balozi Dkt. Emmanuel Nchimbi amesema Serikali itaendelea kuthamini mchango wa Taasisi za Dini ambazo kwa namna ya pekee zimekuwa zikishiriki katika kutoa mchango kwenye sekta za Afya na Elimu hapa nchini.

Makamu wa Rais amesema hayo mara baada ya kushiriki Ibada ya Misa Takatifu Maalum ya Wanajumuiya wa Uru Seminari, iliyofanyika katika Kanisa Katoliki Parokia ya Kristo Mchungaji Mwema – Tabata Kimanga Jijini Dar es Salaam. Amesema kwa miaka mingi na kwa asilimia kubwa Taasisi za dini zimechangia katika utoaji wa huduma za elimu na afya, hivyo Serikali itaendelea kushirikiana na Taasisi hizo ili kufanikiwa zaidi katika kulijenga Taifa.

Makamu wa Rais amesema Malezi yanayotolewa katika Taasisi za elimu za dini ikiwemo Shule ya Uru Seminari ambayo husisitiza Sala, Kazi na Masomo yanapaswa kutiliwa mkazo katika malezi ya vijana wa sasa. Amesema vijana watakavyoweza kumjua Mungu, kufanya kazi kwa bidii pamoja na kupata elimu wataweza kulijenga vema Taifa kupitia ujuzi na hivyo kuepusha tabia za kupata kipato kupitia njia zisizo sahihi.

Makamu wa Rais amewashukuru, walimu, walezi na wanafunzi waliopata elimu Uru Seminari kwa ushirikiano na malezi mazuri ambayo yalifundisha kumtumikia Mungu pamoja na Wanadamu.

Amewasihi Wanajumuiya ya Uru Seminari kuendeleza umoja na kuhakikisha unakuwa wenye tija kwa Taifa, pamoja na kuendelea kuiombea nchi na Viongozi wake.

Ibada ya Misa Takatifu ya Wanajumuiya wa Uru Seminari, imeongozwa na Askofu wa Jimbo Katoliki Kigoma, Mhashamu Joseph Mlola.

Akitoa mahubiri kwa Wanajumuiya WA Uru Seminari , Askofu Mlola amewasihi kukumbuka wito muhimu walionao wa kupeleka tunu njema ya Maisha ya kiimani kuishi kwa kumpendeza Mungu pamoja na wanadamu. Amesema ni muhimu kuwa mstari wa mbele kupeleka matumaini, ukweli, amani na haki.

 Pia, Askofu Mlola amewasihi kuhakikisha uwepo wa kila mwanajumuiya wa Uru Seminari analeta upendo na matumaini, kwa kutambua huo ni wito kwao waliolelewa na kufundishwa katika malezi na maadili mema.

Uru Seminari ni Shule inayomilikiwa na Shirika la Mitume wa Yesu chini ya Kanisa Katoliki  katika Jimbo Moshi Mkoani Kilimanjaro.












Na Munir Shemweta, Itilima

WAZIRI wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Mhe. Dkt. Leonard Akwilapo, amepongeza hatua iliyofikiwa katika ujenzi wa Shule mpya ya Awali na Msingi Mwankola iliyopo Kijiji cha Lagangabilili, Wilaya ya Itilima mkoani Simiyu, huku akisisitiza kuwa elimu ni msingi muhimu wa maisha na maendeleo ya Taifa.

Dkt. Akwilapo amesema jamii inayowekeza katika elimu inaweka msingi imara wa maendeleo ya kizazi cha sasa na kijacho kwa kuwa elimu huwajengea watoto uwezo wa kujitambua, kupata maarifa na kujiandaa kushika nafasi mbalimbali za uongozi na kitaaluma.

Ametoa kauli hiyo Agosti 7, 2026 wakati wa ziara yake katika Kitongoji cha Mwankola, Kata ya Lagangabilili wilayani Itilima, ambako alikagua maendeleo ya mradi huo na kuweka jiwe la msingi la ujenzi wa shule hiyo.

Amesema wananchi wa Itilima wanapaswa kuendelea kuyapa umuhimu mkubwa masuala ya elimu na kuhakikisha watoto wanapata fursa ya kusoma katika mazingira bora, akieleza kuwa elimu ndiyo njia inayoweza kuwajengea vijana uwezo wa kuwa viongozi na wataalamu wenye mchango katika jamii.

‘’uwekezaji unaofanywa na Serikali katika miundombinu ya elimu unapaswa kuungwa mkono na wananchi, hususan wazazi na walezi, kwa kuhakikisha watoto wanahudhuria masomo na kupata mahitaji muhimu yatakayowawezesha kujifunza vizuri’’. Amesema Dkt Akwilapo

Akiwa katika eneo la mradi huo, Waziri Akwilapo aliwahimiza wazazi kutambua kuwa wao ni sehemu muhimu ya mafanikio ya elimu ya watoto wao, hivyo wanapaswa kushirikiana na Serikali na viongozi wa shule katika kuboresha mazingira ya ujifunzaji.

Pamoja na hilo, amesisitiza umuhimu wa wanafunzi kupata chakula shuleni, akibainisha kuwa upatikanaji wa chakula ni moja ya mambo yanayoweza kumsaidia mtoto kuwa katika mazingira mazuri ya kujifunza na kufuatilia masomo.

Amesema jitihada za kujenga madarasa na shule mpya zinapaswa kwenda sambamba na ushiriki wa wazazi katika ustawi wa wanafunzi ili uwekezaji unaofanywa na Serikali katika sekta ya elimu uweze kutoa matokeo yaliyokusudiwa.

Kwa upande wake, Mkuu wa mkoa wa Simiyu Mhe. Anamringi Macha amesema mkoa wake umepiga hatua katika sekta kubwa katika sekta mbalimbali ikiwemo Afya na miundombinu.

Ameeleza kuwa hatua hizo zinatokana na juhudi kubwa zinazofanywa na serikali ya awamu ya sita chini ya Mhe. Dkt Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika kuwaletea maendeleo wananchi.

Ziara hiyo ni sehemu ya mpango wa Serikali ya Awamu ya Sita wa kuwapeleka mawaziri katika maeneo mbalimbali nchini kwa lengo la kufuatilia utekelezaji wa miradi mbalimbali iliyoahidiwa kwa wananchi wakati Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, alipokuwa akiomba kura kuelekea Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 29, 2025.

Kupitia ziara hizo, Serikali inafuatilia hatua za utekelezaji wa miradi hiyo pamoja na changamoto zinazoweza kujitokeza ili kuhakikisha wananchi wanapata huduma na miradi iliyokusudiwa kwa wakati.

Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. Dkt Leonard Akwilapo akizindua mradi wa shule Mpya ya Awali na msingi katika Kijiji Cha Lagangabilili kitomgoji cha Mwankola wilayani Itilima mkoani Simiyu. Wa pili kulia ni Mkuu wa mkoa wa Simiyu Mhe. Anamringi Macha
Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. Dkt Leonard Akwilapo akimkabidhi hati milki ya Ardhi Mkuu wa Chuo Cha VETA Bw. Deogratius Muzambele wakati alipokwenda kuzindua shule Mpya ya Awali na msingi katika Kijiji Cha Lagangabilili kitongoji cha Mwankola wilayani Itilima mkoani Simiyu.
Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. Dkt Leonard Akwilapo pamoja na Mkuu wa mkoa wa Simiyu Mhe. Anamringi Macha wakiwa katika picha ya pamoja na Wananchi walikabidhiwa hati milki za ardhi wakati alipokwenda kuzindua  shule Mpya ya Awali na msingi katika Kijiji Cha Lagangabilili kitomgoji cha Mwankola wilayani Itilima mkoani Simiyu.
Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. Dkt Leonard Akwilapo akimsikiliza mkazi wa Itilima Bw. Thomas Golea aliyewasilisha kero yake wakati wa  uzinduzi wa  shule Mpya ya Awali na msingi katika Kijiji Cha Lagangabilili kitomgoji cha Mwankola wilayani Itilima mkoani Simiyu.
Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. Dkt Leonard Akwilapo pamoja na Mkuu wa mkoa wa Simiyu Mhe. Anamringi Macha wakiwa katika picha ya pamoja katika jengo la shule ya Mpya ya Awali katika Kijiji Cha Lagangabilili kitomgoji cha Mwankola wilayani Itilima mkoani Simiyu. (PICHA ZOTE NA WIZARA YA ARDHI)

Na Janeth Raphael -MichuziTv

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, ameiagiza Wizara ya Kilimo kwa kushirikiana na Wizara ya Mifugo na Uvuvi kuongeza idadi ya kanda za Maonesho ya Nane Nane ili kuwafikia wakulima, wafugaji, wavuvi na wadau wengi zaidi nchini.

Rais Samia ametoa agizo hilo wakati wa kilele cha Maonesho ya Nane Nane Kitaifa na Kimataifa yaliyofanyika jijini Dodoma, akisisitiza kuwa maonesho hayo yanapaswa kwenda zaidi ya kuonesha bidhaa na teknolojia na kuwa jukwaa la kuwaunganisha wazalishaji na masoko.

Amesema kuongeza kanda za maonesho kutatoa fursa kwa wazalishaji wengi zaidi kuonesha bidhaa zao, teknolojia, ubunifu na huduma zinazopatikana katika sekta za kilimo, mifugo na uvuvi.

“Maonesho haya yanapaswa kuwafikia watu wengi zaidi. Wizara husika zihakikishe zinaongeza kanda za maonesho ili wananchi wengi wapate fursa ya kushiriki, kujifunza na kuonesha kazi zao,” amesema.

Kwa mujibu wa Rais Samia, Nane Nane inapaswa kuwa sehemu ya kujenga mahusiano ya kibiashara, kutafuta masoko, kujifunza teknolojia mpya na kuongeza tija kwa wazalishaji, badala ya kubaki kuwa tukio la maonesho pekee.

Aidha, amesisitiza umuhimu wa kuimarisha huduma za ugani nchini ili kuwasaidia wakulima, wafugaji na wavuvi kupata maarifa sahihi kuhusu mbinu bora za uzalishaji pamoja na matumizi ya teknolojia za kisasa.

Amesema Serikali itaendelea kuwekeza katika utafiti wa kilimo, mifugo na uvuvi ili kuwezesha upatikanaji wa teknolojia na mbinu bora zitakazoongeza uzalishaji na tija katika sekta hizo.

Katika hatua nyingine, Rais Samia amesema Serikali itaendelea kushirikiana na viongozi katika ngazi mbalimbali katika kutatua migogoro baina ya wakulima na wafugaji kwa njia ya mazungumzo na kuzingatia maslahi ya pande zote.

Amesisitiza kuwa amani na utulivu katika maeneo ya uzalishaji ni msingi muhimu wa kuongeza tija na kufikia malengo ya maendeleo katika sekta za kilimo, mifugo na uvuvi.

Rais Samia pia amewapongeza waandaaji wa Maonesho ya Nane Nane pamoja na wadau walioshiriki, akisema maandalizi mazuri yamewezesha wakulima, wafugaji, wavuvi, watafiti, wafanyabiashara na wawekezaji kukutana katika jukwaa moja.

Amesema Serikali itaendelea kutoa ushirikiano ili kuhakikisha Maonesho ya Nane Nane yanakuwa makubwa zaidi na yenye manufaa kwa wananchi, hususan katika kuwaunganisha wazalishaji na masoko pamoja na kufungua fursa za biashara na uwekezaji.

Maonesho ya Nane Nane yameendelea kuwa jukwaa muhimu la kuwakutanisha wadau wa sekta za kilimo, mifugo na uvuvi, wakiwemo wazalishaji, watafiti, taasisi za fedha, wafanyabiashara na wawekezaji kwa lengo la kuongeza uzalishaji, tija na thamani ya mazao.


Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan akihutubia Viongozi, wakulima, wafanyabiashara, wageni kutoka nchi mbalimbali pamoja na Wananchi wakati wa Kilele cha Maadhimisho ya Sikukuu ya Wakulima Nanenane ambayo Kitaifa yanafanyika katika viwanja vya Maonesho vya Dkt. John Samuel Malecela, Jijini Dodoma, tarehe 08 Agosti, 2026.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan akipokea Tuzo Maalum kutoka kwa Waziri wa Kilimo Mhe. Daniel Chongolo, kwa niaba ya Kamati ya Maandalizi ya Nanenane Kitaifa, 2026 katika viwanja vya Maonesho vya Dkt. John Samuel Malecela, Jijini Dodoma, tarehe 08 Agosti, 2026.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan akikata utepe kuashiria uzinduzi wa magari kwa ajili ya Wakala ya Taifa ya Huduma za Ugani (NAESA) na Matrekta ya vyama vya Ushirika katika Maonesho ya Kilimo ya Nanenane yanayofanyika Kitaifa katika viwanja vya Maonesho vya Dkt. John Samuel Malecela, Jijini Dodoma, tarehe 08 Agosti, 2026.

Wananchi wa Kata ya Mpandangindo katika Jimbo la Peramiho wanatarajia kunufaika na ujenzi wa barabara ya Mpandangindo kupitia Parangu hadi Peramiho, baada ya Serikali kutenga zaidi ya shilingi milioni 250 kwa ajili ya utekelezaji wa mradi huo.

Akizungumza na wananchi, Mbunge wa Jimbo la Peramiho, Mhe. Dkt. Lazaro Komba Bunungu, amewahakikishia kuwa ujenzi wa barabara hiyo utaanza, akieleza kuwa mradi huo ni sehemu ya jitihada za Serikali kuboresha miundombinu na kurahisisha shughuli za kijamii na kiuchumi.

Mhe. Dkt. Bunungu amesema barabara hiyo imekuwa kero kwa muda mrefu kutokana na hali yake kutokuwa nzuri, jambo ambalo limekuwa likikwamisha usafiri na usafirishaji wa mazao pamoja na shughuli nyingine za maendeleo kwa wananchi.

Kwa upande wake, Mhandisi wa TARURA, Simon Binamu, amesema tayari bajeti ya zaidi ya shilingi milioni 250 imetengwa kwa ajili ya ujenzi wa barabara hiyo, na kwamba kwa sasa mradi upo katika hatua za utekelezaji.

Ujenzi wa barabara hiyo unatarajiwa kuboresha mawasiliano kati ya Mpandangindo, Parangu na Peramiho, kurahisisha usafiri wa wananchi, kuongeza fursa za biashara na kuchochea maendeleo ya kiuchumi katika maeneo hayo.




Na Peter Ngamilo- TAEC

Katika safari ya Tanzania kuelekea uchumi wa kisasa na wa viwanda, sekta za kilimo, mifugo na viwanda zinaendelea kuwa nguzo muhimu za maendeleo ya Taifa. Hata hivyo, ukuaji wa sekta hizo hauwezi tena kutegemea mbinu za jadi pekee, hasa katika kipindi ambacho dunia inakabiliwa na changamoto za ongezeko la watu, mabadiliko ya tabianchi, kupungua kwa rutuba ya ardhi, uhaba wa maji pamoja na kuongezeka kwa magonjwa ya mimea na mifugo.

Mataifa mbalimbali duniani yameamua kukabiliana na changamoto hizo kwa kuwekeza katika sayansi na teknolojia. Miongoni mwa teknolojia zinazobadili taswira ya uzalishaji wa chakula na usimamizi wa rasilimali ni teknolojia ya nyuklia, ambayo kwa miongo kadhaa imekuwa ikitumika kuongeza tija katika kilimo, kuboresha uzalishaji wa mifugo, kusimamia rasilimali za maji, kuimarisha tafiti za kisayansi na kuongeza ushindani wa bidhaa katika masoko ya ndani na kimataifa.

Kwa mujibu wa Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano wa Tume ya Nguvu za Atomu Tanzania (TAEC), Peter Ngamilo, bado kuna uelewa mdogo miongoni mwa wananchi kuhusu mchango wa teknolojia ya nyuklia katika maendeleo ya kila siku.

“Watu wengi wakisikia neno nyuklia hufikiria uzalishaji wa umeme au silaha. Ukweli ni kwamba sehemu kubwa ya teknolojia hii duniani inatumika kuboresha maisha ya wananchi kupitia kilimo, mifugo, maji, afya na viwanda. Hii ndiyo elimu ambayo TAEC inaendelea kuifikisha kwa wananchi kupitia Maonesho ya Nanenane,” anasema Ngamilo.


Anasema ushiriki wa TAEC katika Maonesho ya Nanenane haulengi tu kuonesha shughuli za Tume, bali pia kuwajengea wananchi uelewa kwamba teknolojia ya nyuklia ni nyenzo ya maendeleo inayoweza kuongeza uzalishaji wa chakula, kupunguza gharama za uzalishaji, kuongeza thamani ya mazao na kuchochea ukuaji wa uchumi.

KILIMO KISICHOTEGEMEA BAHATI, BALI SAYANSI

Sekta ya kilimo ni miongoni mwa nguzo kuu za uchumi wa Tanzania. Hata hivyo, uzalishaji wake bado unakabiliwa na changamoto mbalimbali, zikiwemo wadudu waharibifu, magonjwa ya mimea, matumizi yasiyo sahihi ya mbolea na athari za mabadiliko ya tabianchi.

Katika nchi mbalimbali duniani, baadhi ya changamoto hizo zimepatiwa suluhisho kupitia matumizi ya teknolojia ya nyuklia, ikiwemo mbinu ya mutation breeding, inayotumika katika kuboresha mbegu ili kupata aina za mazao zenye uwezo wa kustahimili ukame, magonjwa na wadudu, huku zikitoa mavuno bora.

Kwa mujibu wa taarifa za mashirika ya kimataifa yanayohusika na matumizi ya teknolojia ya nyuklia katika kilimo, zaidi ya aina 3,400 za mazao yaliyoboreshwa kwa kutumia mbinu za mutation breeding zimesajiliwa katika zaidi ya nchi 75 duniani.

Nchi kama China, India na Vietnam ni miongoni mwa zilizopata mafanikio katika matumizi ya mbinu hizo, ambapo aina mbalimbali za mazao zimeboreshwa kwa lengo la kuongeza uzalishaji na kukabiliana na changamoto za mazingira.

Ngamilo anasema Tanzania ina sababu ya kuwekeza zaidi katika matumizi ya teknolojia hiyo.

“Tanzania imejaliwa kuwa na ardhi kubwa, rasilimali za maji na mazingira yanayofaa kwa uzalishaji wa mazao mbalimbali. Tukichanganya rasilimali hizi na teknolojia ya kisasa, ikiwemo teknolojia ya nyuklia, tunaweza kuongeza uzalishaji wa mazao ya kimkakati, kupunguza gharama za uzalishaji na kuongeza ushindani wa bidhaa zetu katika masoko ya kikanda na kimataifa,” anasema.

KUPAMBANA NA WADUDU BILA KUHARIBU MAZINGIRA

Kila mwaka wakulima hupoteza sehemu ya mazao kutokana na wadudu waharibifu, hali inayosababisha hasara na kupunguza tija ya kilimo.

Moja ya matumizi muhimu ya teknolojia ya nyuklia katika kudhibiti wadudu ni Sterile Insect Technique (SIT), mbinu inayohusisha uzalishaji na kuachiliwa kwa wadudu wa kiume waliotiwa utasa ili wanapopandana na majike wasiweze kuzalisha kizazi kipya.

Mbinu hiyo imekuwa ikitumika katika maeneo mbalimbali duniani kudhibiti wadudu waharibifu, wakiwemo baadhi ya aina za nzi wanaoshambulia matunda na mazao mengine.

Kwa Tanzania, matumizi ya teknolojia hiyo yanaweza kuwa na mchango katika kudhibiti wadudu waharibifu, kuongeza uzalishaji wa matunda na mboga, kupunguza utegemezi wa viuatilifu na kusaidia kulinda mazingira.

“Teknolojia ya nyuklia inatufundisha kuwa si kila tatizo la kilimo linahitaji matumizi makubwa ya kemikali. Sayansi imetupa mbinu mbadala zinazoweza kusaidia kulinda mazingira na wakati huo huo kuongeza uzalishaji wa mazao,” anasema Ngamilo.

MIFUGO: KUBORESHA AFYA NA KUONGEZA UZALISHAJI

Sekta ya mifugo ina mchango mkubwa katika uchumi wa Tanzania, lakini bado inakabiliwa na changamoto za magonjwa, uzalishaji, uzazi na lishe.

Teknolojia ya nyuklia inaweza kutumika katika uchunguzi na udhibiti wa magonjwa, utafiti wa lishe ya mifugo pamoja na kufuatilia namna virutubisho vinavyotumika mwilini, hatua inayoweza kusaidia kuboresha uzalishaji wa maziwa na nyama.

Mfano unaotajwa katika matumizi ya teknolojia ya nyuklia katika kudhibiti magonjwa ya mifugo ni Zanzibar, ambako matumizi ya Sterile Insect Technique yalichangia katika udhibiti wa nzi tsetse na kupunguza tatizo la trypanosomiasis.

Ngamilo anasema uzoefu huo unaonesha kwamba Afrika inaweza kutumia sayansi na teknolojia kutatua changamoto zinazolikabili bara hilo.

“Mfano wa Zanzibar unaonesha wazi kuwa teknolojia ya nyuklia inaweza kutoa suluhisho la changamoto ambazo kwa miaka mingi zilionekana kuwa ngumu na zenye gharama kubwa kuzitatua. Huu ni ushahidi kwamba teknolojia hii inaweza kuleta matokeo yanayogusa maisha ya wananchi,” anasema.

MAJI: RASILIMALI INAYOHITAJI SAYANSI

Katika kipindi ambacho mabadiliko ya tabianchi yanaendelea kuathiri upatikanaji na usalama wa maji, teknolojia ya nyuklia inaweza kuwa nyenzo muhimu katika usimamizi wa rasilimali hiyo.

Kupitia matumizi ya Isotope Hydrology, wataalamu wanaweza kupata taarifa kuhusu chanzo cha maji, umri wa maji yaliyopo chini ya ardhi, mwelekeo wa mtiririko wake na namna yanavyorejea kwenye mifumo ya asili.

Taarifa hizo zinaweza kusaidia katika kupanga matumizi endelevu ya maji kwa ajili ya kilimo, mifugo, viwanda na matumizi ya binadamu.

“Kilimo cha kesho kitategemea siyo tu upatikanaji wa maji, bali pia uwezo wa kuyatumia kwa ufanisi. Teknolojia ya nyuklia inatupa maarifa ya kisayansi yanayotuwezesha kuelewa na kupanga matumizi bora ya rasilimali hiyo muhimu,” anaeleza Ngamilo.

SAYANSI INAYOENDESHA TAFITI NA VIWANDA

Mbali na kilimo, mifugo na maji, teknolojia ya nyuklia ina nafasi katika tafiti zinazolenga kuboresha rutuba ya udongo, matumizi sahihi ya mbolea na kuongeza ufanisi wa uzalishaji wa mazao.

Katika sekta ya viwanda, teknolojia hiyo inaweza kutumika katika upimaji wa ubora wa bidhaa, ukaguzi wa miundombinu bila kuiharibu pamoja na kuboresha ufanisi wa michakato mbalimbali ya uzalishaji.

Kwa mujibu wa Ngamilo, maendeleo ya viwanda hayawezi kutenganishwa na maendeleo ya kilimo na mifugo kwa sababu viwanda vinahitaji malighafi bora na za kutosha.

“Viwanda vinahitaji malighafi bora. Malighafi bora zinatokana na kilimo na mifugo yenye tija. Hivyo, teknolojia ya nyuklia inaunganisha mnyororo mzima wa thamani, kuanzia shambani hadi kiwandani na hatimaye sokoni,” anasema.

NANENANE: KUWEKEZA KATIKA MAARIFA

Katika Maonesho ya Nanenane mwaka 2026, TAEC inaendelea kutoa elimu kwa wananchi kuhusu matumizi salama na yenye manufaa ya teknolojia ya nyuklia katika sekta mbalimbali za maendeleo.

Ngamilo anasema wananchi wanaotembelea banda la TAEC wamekuwa wakionesha hamu ya kufahamu namna teknolojia hiyo inavyoweza kutumika kutatua changamoto zinazowakabili katika shughuli zao za kila siku.

“Tunataka wananchi waondoke katika banda la TAEC wakiwa na uelewa kwamba teknolojia ya nyuklia si teknolojia ya mbali. Ni teknolojia inayoweza kumsaidia mkulima kuongeza mavuno, mfugaji kuongeza uzalishaji wa maziwa na nyama, mtafiti kupata majibu sahihi na Taifa kujenga uchumi imara,” anasema.

TANZANIA INA FURSA YA KUONGOZA

Kwa kuwa na ardhi kubwa, rasilimali za maji, mifugo na nguvu kazi ya vijana, Tanzania ina fursa kubwa ya kutumia sayansi na teknolojia kuongeza uzalishaji wa chakula, kuimarisha usalama wa chakula, kuongeza thamani ya mazao, kukuza mauzo ya nje na kuharakisha ujenzi wa uchumi wa viwanda.

Hata hivyo, fursa hiyo inahitaji uwekezaji zaidi katika tafiti, miundombinu, wataalamu na uhamasishaji wa matumizi ya teknolojia hiyo miongoni mwa wakulima, wafugaji, wafanyabiashara na wadau wengine.

Ngamilo anasisitiza kwamba teknolojia ya nyuklia si mbadala wa mkulima au mfugaji, bali ni nyenzo inayoweza kuongeza tija, ubora na ushindani wa bidhaa zao.

“Safari ya kuelekea Tanzania yenye uchumi wa kisasa haitategemea rasilimali tulizonazo pekee, bali namna tutakavyozitumia kwa kutumia sayansi na teknolojia. Teknolojia ya nyuklia ni moja ya zana muhimu zitakazotuwezesha kufikia azma hiyo. Huu ndio ujumbe tunaoupeleka kwa Watanzania kupitia Maonesho ya Nanenane 2026,” anahitimisha Ngamilo.




Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Absa Tanzania, Bw. Obedi Laiser (katikati), pamoja na baadhi ya wachezaji wa timu ya soka ya benki hiyo, wakishangilia mara baada kupokea kikombe kutoka kwa Mweka Hazina wa Chama cha Mabenki Tanzania (TBA) , Bw. Rayson Foya,  baada ya kuibuka na ushindi kwa kuichapa timu ya benki ya Mwanga Hakika kwa bao 1-0 katika mchezo wa fainali za Ligi ya Chama TBA, katika Viwanja vya Gymkhana, jijini Dar es Salaam jana.  
Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Absa Tanzania, Bw. Obedi Laiser ( wa tatu kushoto), akipokea kikombe kutoka kwa Mweka Hazina wa Chama cha Mabenki Tanzania (TBA) , Bw. Rayson Foya( wa pili kushoto)  baada ya timu ya benki hiyo, kuibuka mshindi kwa kuichapa timu ya benki ya Mwanga Hakika kwa bao 1-0 katika mchezo wa fainali za Ligi ya Chama cha Mabenki Tanzania (TBA Footie Tournament 2026), katika Viwanja wa Gymkhana jijini Dar es Salaam jana.
Ofisa wa Wateja Binafsi wa Benki ya Absa Tanzania , Bw. Paschal John ( kushoto) akipokea tuzo ya mchezaji bora kutoka kwa Mkurugenzi wa Uchunguzi wa Chama cha Mabenki Tanzania (TBA), Bw. Dan Tandasi mara baada ya mchezo wa fainali za Ligi ya Chama cha Mabenki Tanzania (TBA Footie Tournament 2026),  uliyofanyika katika Viwanja wa Gymkhana jijini Dar es Salaam jana.

Picha mbalimbali zikionesha mtifuano mkali dhidi ya wachezaji wa timu za soka za benki ya Absa na Mwanga Hakika, katika mchezo wao wa fainali za Michuano ya TBA Footie Tournament 2026, katika Viwanja vya Gymkhana, jijini Dar es Salaam jana. Absa ilishinda mtanange huo kwa bao 1-0 hivyo kutwaa ushindi wa michuano hiyo kwa mwaka huu. 

Kikosi kabambe cha timu ya soka ya Benki ya Absa, wakipiga picha ya pamoja kabla ya kuanza mchezo wa fainali dhidi ya Mwanga Hakika Bank, katika Viwanja vya Gymkhana, jijini Dar es Salaam jana. Absa ilishinda kwa bao 1-0.