-Aomba wakulima watumie mbolea zinazozalishwa nchini
WAZIRI MKUU Dkt. Mwigulu Nchemba amesema kuanza uzalishaji kwa kiwanda cha saruji cha Kigoma kutasaidia kuondoa tatizo la kupanda bei kwa bidhaa hiyo kwenye mikoa ya Magharibi mwa Tanzania.
Amesema Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan amesisitiza katika dira yake ya uwekezaji kwamba kuwe na viwanda katika kanda mbalimbali za nchi ili kupunguza changamoto za gharama za usafirishaji. “Pale gharama za usafirishaji zinapopanda, bei ya bidhaa nayo hupanda,” amesema.
Ametoa kauli hiyo Bungeni jijini Dodoma, leo (Alhamisi, Septemba 03, 2026) wakati akijibu swali la Mbunge wa Kasulu Vijijini, Bw. Edibily Kazala Kinyoma, kwenye kipindi cha maswali ya papo kwa papo kwa Waziri Mkuu ambaye alitaka kujua kauli ya Serikali kuhusu kuanzisha tathmini ya gharama halisi za uzalishaji wa saruji nchini ili kuwe na bei elekezi itakayotoa unafuu kwa wananchi na kuchochea sekta ya ujenzi Tanzania.
Mbunge huyo amesema pamoja na uwekezaji uliofanyika kwenye sekta ya viwanda, bado kuna changamoto katika upande wa saruji kwani bei yake imekuwa ikipanda kwa kasi na baadhi ya maeneo imefikia zaidi ya sh. 25,000.
“Habari njema ni kwamba Mheshimiwa Rais tayari ameelekeza watu wanaotaka kuwekeza katika bidhaa hizi wapewe kipaumbele. Kwa taarifa nilizonazo, kule Kigoma kuna kiwanda kimojawapo cha saruji ambacho kiko katika hatua za utekelezaji. Lengo ni kuwa na viwanda vingine vinavyozalisha bidhaa hii katika maeneo ya magharibi mwa nchi ikiwemo Kigoma, Kagera na Katavi,” amesema.
Dkt. Mwigulu amesema kuwepo kwa viwanda kama hivyo kwenye mikoa na kanda tofauti kutasaidia kupunguza gharama za kusafirisha saruji kutoka Mtwara au Tanga kwenda upande mwingine wa nchi, jambo ambalo linaongeza gharama za usafirishaji na usambazaji.
Amesema amepanga kuitisha kikao kitakachowahusisha wasambazaji mbalimbali nchini ili kujadiliana nao namna ya kudhibiti ongezeko la bei na kuhakikisha wananchi hawaathiriki kwa kiwango kikubwa, jambo ambalo anaamini litasaidia kupunguza gharama za ujenzi na kuchochea maendeleo.
“Jambo hili la bei ya saruji linagusa maisha ya kila Mtanzania na kupanda kwa bei ya saruji hivi karibuni kumehusishwa pia na kupanda kwa bei za mafuta, jambo ambalo limeongeza gharama za usafirishaji. Serikali imeshakaa na wadau wa usafirishaji na kutafuta namna ya kupunguza gharama hizo. Nimekwishakutana na wasafirishaji wa abiria, na nimepanga pia kukutana na wasafirishaji wa mizigo ili kuangalia maeneo tunayoweza kuyarekebisha na kupunguza gharama za usafirishaji,” amesema.
Katika hatua nyingine, akijibu swali kuhusu upatikanaji wa mbolea, Waziri Mkuu amesema Serikali imechukua hatua za muda wa kati kwa kukaa na waagizaji wa mbolea na kuwaelekeza waangalie uwezekano wa kuagiza bidhaa hiyo kutoka nchi mbadala badala ya kutegemea nchi za Ulaya Mashariki.
“Tumefanya hivyo pia kwa bidhaa nyingine, ikiwemo sukari. Kwa upande wa mbolea, tumeagiza kutoka nchi za Afrika, ikiwemo Morocco, na pia kuwaelekeza waagizaji waangalie masoko ya China ili kuhakikisha bidhaa hizo zinakuwepo nchini,” amesema.
Alikuwa akijibu swali la Mbunge Momba, Bi. Condester Sichalwe aliyetaka kujua Serikali imejipangaje kuhakikisha mbolea za ruzuku na pembejeo nyingine zinazolenga kumfanya mkulima kuwa mwekezaji na kilimo kuwa biashara zinafika kwa wakati na kuleta tija.
Dkt. Mwigulu amesema ili kupunguza utegemezi wa bidhaa kutoka nje na kuepuka matatizo ya usafirishaji, kwa muda mrefu, Serikali imeendelea kuhamasisha uwekezaji katika viwanda vya kuzalisha mbolea hapa nchini.
“Kiwanda kilichopo Dodoma kimeanza kufanya kazi. Pia tunaendelea kuhamasisha wakulima kutumia mbolea zinazozalishwa nchini, ikiwemo mbolea ya Mijingu kutoka Arusha, ambayo inatumika kwa kiwango kikubwa katika nchi jirani kuliko hapa Tanzania. Tunaendelea pia kuhamasisha viwanda vingine, hasa vile vinavyozalisha aina muhimu za mbolea ambazo tumekuwa tukiziagiza kutoka nje.”
Amesema Serikali imeendelea kuwalipa waagizaji wa mbolea ili kuhakikisha wanakuwa na ukwasi wa kutosha wa kuagiza mbolea na pembejeo nyingine kwa wakati. Wakati huohuo, tunazihimiza taasisi zinazosimamia usambazaji wa mbolea na sekta hiyo kufanya kazi kwa wakati. “Misimu ya kilimo siyo ya dharura, inajulikana mkoa gani unaanza msimu wa kilimo lini. Kwa hiyo, tunapaswa kupanga mapema ili mbolea na pembejeo ziwepo kabla ya msimu kuanza,” amesisitiza.
Vodacom Tanzania Plc leo imezindua ripoti ya Mazingira, Jamii na Utawala (ESG) kwa mwaka uliomalizika Machi 31, 2026, ikionesha kupungua kwa asilimia 24 ya hewa chafu, sambamba na mpango mkubwa zaidi wa uboreshaji wa mtandao katika historia ya kampuni.
Kampuni pia imewekeza shilingi 3.5 bilioni katika ufanisi wa nishati kwa mwaka huu, na kufikisha uokoaji wa megawati 18,340, ikiwa zaidi ya mara sita ya megawati 2,861 zilizookolewa kwa mwaka wa 2025.
Uzalishaji wa hewa chafu ulishuka hadi tani 18,445.5, kutoka tani 24,285.6. Pia, matumizi ya mafuta dizeli yalipungua kwa asilimia 24, kutoka lita milioni 8.6 hadi lita milioni 6.6.
Upunguaji huo ulitokana na kubadilisha vifaa vya zamani vya mawasiliano ya redio katika maeneo 1,808 ndani ya miezi saba, pamoja na uimarishaji wa upatikanaji wa umeme wa gridi uliopunguza muda wa uendeshaji wa jenereta katika vituo vya data vya kampuni.
Mtandao wa Vodacom Tanzania unatumia takriban jigawati (GWh) 169.5 kwa mwaka katika zaidi ya maeneo 3,800, ambapo 2,190 kati yake yapo vijijini. Vituo vya msingi vinachukua asilimia 78.9 ya matumizi yote.
Mwaka huu, maeneo 169 yaliyokuwa nje ya gridi ya taifa yaliunganishwa kwenye gridi ya taifa. Katika kituo cha data cha Kwale, umeme wa gridi ya Taifa uliongezeka kutoka 11kVA hadi 33kVA na kupunguza matumizi ya jenereta kutoka saa 18 kwa siku hadi saa mbili, sawa na upunguzaji wa asilimia 88 wa matumizi ya dizeli katika kituo hicho.
Asilimia 57 ya nishati yote iliyotumiwa na Vodacom Tanzania ilitokana na vyanzo vya nishati jadidifu. Kampuni iliendelea kuhakikisha kuwa umeme wote wa gridi iliyonunua unaendana na nishati inayotokana na vyanzo jadidifu, hatua iliyosaidia kufikia uzalishaji sifuri wa hewa chafuzi. Aidha, Vodacom Tanzania ilihuisha tena cheti chake cha ISO 50001. Uzalishaji wa hewa chafuzi unaotokana na shughuli zake za biashara na mnyororo wake wa thamani pia ulipungua hadi tani 94,944 kutoka tani 100,455.
"Mafanikio haya ya kimazingira yametokana na kufanya uhandisi wa msingi kwa usahihi, siyo kutoka mradi tofauti wa uendelevu," alisema Mkurugenzi wa Miundombinu ya Mtandao Andrew Lupembe huku akiongeza, "kubadilisha vifaa vya zamani katika maeneo 1,808 kunampa mteja muunganisho wa haraka zaidi huku taifa likifaidika na upunguzaji wa athari za mazingira ambazo zingesababishwa na lita milioni mbili zilizopunguzwa kwenye matumizi.”
Wigo wa mtandao wa 4G ulifikia asilimia 76.3 ya wakazi, huku wateja milioni 27.7 wakiwa kwenye mtandao baada ya uzinduzi wa huduma ya kwanza ya 5G nchini Tanzania. Umiliki wa simujanja ulifikia asilimia 46.7, huku wateja 325,415 wakipata vifaa kupitia ubia wa mikopo ya rejareja.
Kwa wateja wasio na simujanja, huduma mpya ya kidijitali inayotumia akili unde inawezesha upatikanaji wa intaneti kupitia jumbefupi (SMS) na simu za sauti, ikisambaza msaada wa kidijitali hadi maeneo ya vijijini.
M-Pesa ilihudumia wateja milioni 14.1 wa ujumuishwaji wa kifedha huku M-Koba, jukwaa la kidijitali la vikundi vya akiba ambao wanachama wake wengi ni wanawake, lilifikia vikundi hai 299,420 huku akiba jumla ikiongezeka kwa asilimia 81.
Vodacom Tanzania Foundation ilifikia wanufaika milioni 2.9, kwa kushirikiana na Taasisi ya Elimu Tanzania, kampuni iliondoa gharama ya data kwenye jukwaa la kitaifa la maendeleo ya walimu, na kuwapa walimu 121,832 fursa ya kupata nyenzo za maendeleo ya kitaaluma bila gharama ya data. Miti 80,000 ya asili iliongezwa katika Msitu wa Kahe 2 katika Mlima Kilimanjaro.
Kampuni ilirekodi mwaka wa kumi na nne mfululizo bila kutokea kifo cha mfanyakazi mahali pa kazi. Mpango wa uboreshaji ulihusisha wafanyakazi 411 waliosafiri zaidi ya kilomita milioni 1.7, na awamu ya kwanza ilikamilika bila kutokea kifo au tukio kubwa. Vodacom Tanzania ina uthibitisho wa ISO 27001 kwa usalama wa data na haikurekodi faini yoyote ya ushindani usio halali au utakatishaji fedha.
"Nyuma ya kila muunganisho kuna maisha yanayobadilika, mwalimu anayefikia nyenzo za kujifunzia bila gharama ya data, kikundi cha akiba ambacho hakihifadhi tena fedha taslimu katika bati. Tutaendelea kuwajibika kwa wananchi wa Tanzania wanaotuamini kila siku,” aliongeza Philip Besiimire, Afisa Mtendaji mkuu wa kampuni hiyo.
Kwa taarifa zaidi bofya: https://vodacom.com/pdf/our-purpose/reporting-centre/20261/vodacom-tanzania-esg-snapshot-2026.pdf
Akizungumza Septemba 02, 2026 jijini Dodoma na Balozi wa Uingereza nchini Tanzania, Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. Adolf Mkenda, amesema maandalizi ya utekelezaji wa miaka 10 ya elimu ya lazima kuanzia mwaka 2028 yanaendelea, hatua itakayohitaji miundombinu, walimu na nafasi za kutosha katika shule za sekondari.
Prof. Mkenda amebainisha kuwa mpango huo utasababisha ongezeko kubwa la wanafunzi watakaoingia sekondari, hivyo Serikali imeweka mkakati wa kuhakikisha wanafunzi wote wanaostahili wanapata nafasi ya kuendelea na masomo.
Aidha, ameongeza kuwa Serikali inaendelea kuimarisha mfumo wa elimu wenye mikondo ya elimu ya jumla na elimu ya amali, ili wanafunzi wapate maarifa na stadi zinazowawezesha kuajirika au kujiajiri.
Katika mazungumzo hayo, Prof. Mkenda ameeleza kuwa Serikali inajenga vyuo vya ufundi katika maeneo mbalimbali na kuimarisha mafunzo ya ufundi ili kukidhi mahitaji ya vijana na uchumi wa Taifa.
Prof. Mkenda ameongeza kuwa Serikali inawekeza katika masomo ya sayansi, teknolojia, uhandisi na hisabati pamoja na teknolojia mpya kama akili bandia (AI), ujifunzaji wa mashine na usalama wa mtandao, ili kuandaa wataalamu wa kisasa.
Amesisitiza umuhimu wa ushiriki wa sekta binafsi katika kupanua fursa za elimu, hususan katika ujenzi wa miundombinu na utoaji wa elimu ya amali.
Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Prof. Carolyne Nombo, amesema kuwa Serikali inatazama uwezekano wa kuboresha vivutio vya kisera vitakavyoongeza uwekezaji wa sekta binafsi katika elimu.
Naye Balozi wa Uingereza nchini Tanzania, Mhe. Marianne Young, amepongeza juhudi za Tanzania na kuahidi kuendeleza ushirikiano katika elimu na na mafunzo ya ufundi, ikiwemo kuunganisha taasisi za Tanzania na vyuo vikuu vya Uingereza katika maeneo ya teknolojia ya kisasa na mazingira.
Timu ya Ujenzi Sports Club imeendelea kuunga mkono juhudi za kuwawezesha wanafunzi wenye mahitaji maalum kwa kutoa msaada wa vifaa mbalimbali kwa wanafunzi wa Shule ya Msingi Mlezi jijini Dodoma.
Msaada huo umetolewa Jumatano, Septemba 2, 2026, ikiwa ni sehemu ya juhudi za Ujenzi Sports Club kuunga mkono kazi inayofanywa na shule hiyo katika kuwawezesha wanafunzi wenye mahitaji maalum pamoja na wanafunzi wengine kupata mazingira bora ya kujifunzia.
Vifaa vilivyotolewa ni pamoja na madaftari, vyombo vya kulia chakula, vifaa vya usafi, sabuni, ndoo pamoja na fedha kwa ajili ya ununuzi wa mipira ya michezo.
Akikabidhi msaada huo, Mwenyekiti wa Ujenzi Sports Club, Arch. Ibrahim Chatila, amesema klabu hiyo inatambua na kuthamini kazi kubwa inayofanywa na walimu katika kuwawezesha wanafunzi wenye mahitaji maalum kutimiza ndoto zao kielimu na katika maisha kwa ujumla.
Amesema msaada huo ni sehemu ya jitihada za Ujenzi Sports Club kuunga mkono juhudi zinazofanywa na shule hiyo, huku akiahidi kuwa klabu itaendelea kushirikiana na kuwahamasisha wadau wengine, hususan katika sekta ya ujenzi, kujitokeza na kusaidia juhudi hizo.
“Tunatambua kazi kubwa inayofanywa na walimu katika kuwalea na kuwawezesha watoto hawa. Msaada huu ni sehemu ya mchango wetu katika kuunga mkono juhudi hizo, na tutaendelea kuwahamasisha wadau wengine kujitokeza na kusaidia,” amesema Arch. Chatila.
Akizungumza baada ya kupokea msaada huo, Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Mlezi, Bi. Magreth Kisanga, ameishukuru Ujenzi Sports Club kwa ukarimu na moyo wa kujitolea uliouonyesha kwa kuwasaidia wanafunzi hao.
Amesema msaada huo utasaidia kupunguza changamoto ya upungufu wa baadhi ya vitendea kazi vinavyohitajika katika kuwawezesha wanafunzi kupata mazingira bora ya kujifunzia na kuishi shuleni.
Kwa upande wake, mwalimu anayesimamia kitengo cha wanafunzi wenye mahitaji maalum, Mwl. Hashim Msemo, amesema wanafunzi hao wamekuwa wakifanya vizuri katika masomo yao na wameendelea kufanya vyema katika mitihani yao.
Ametoa wito kwa wadau mbalimbali kujitokeza na kuunga mkono juhudi za shule hiyo ili kuongeza fursa na mazingira bora kwa wanafunzi wenye mahitaji maalum.
Shule ya Msingi Mlezi ni shule jumuishi inayotoa elimu kwa wanafunzi wenye mahitaji maalum pamoja na wanafunzi wengine, kwa lengo la kuhakikisha kila mtoto anapata fursa sawa ya elimu na maendeleo

Kampuni hiyo ambayo ni mwanachama wa Kundi la Makampuni la VINMART inajenga kiwanda hicho Kigamboni, Dar es Salaam, na kitazalisha bidhaa ambazo hadi sasa zimekuwa zikipatikana kwa kiasi kikubwa kutoka kwa wasambazaji wa nje ya nchi. Uwekezaji huo unahusisha kiwanda, mitambo na miundombinu saidizi inayohitajika kuwezesha uzalishaji wa bidhaa hizo nchini.
Uwekezaji huo ulielezwa wakati wa ziara ya Kamishna wa Tume ya Madini ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Ushirikishwaji wa Watanzania katika Sekta ya Madini (Local Content), Dkt. Theresia Charles Numbi, aliyetembelea kiwanda hicho kutathmini maendeleo yake na mipango ya uzalishaji.
Dkt. Numbi alifanya ziara katika kiwanda hicho kipya kinachojengwa kutoka hatua za awali, kwa lengo la kutathmini maendeleo ya mradi huo pamoja na mipango ya shughuli za uzalishaji. Alisema Serikali itaendelea kuunga mkono uwekezaji unaochangia ukuaji wa sekta ya madini, kuimarisha uzalishaji wa viwandani nchini na kuchochea maendeleo ya kiuchumi ya Tanzania.
Pamoja na kupongeza uwekezaji huo, Dkt Numbi alitoa wito kwa kampuni hiyo kuhakikisha kuwa mradi huo pamoja na bidhaa zitakazozalishwa vinabuniwa kwa namna itakayowawezesha wachimbaji wadogo na wa kati katika maeneo mbalimbali nchini kunufaika na uwekezaji huo.
“Serikali itaendelea kuunga mkono uwekezaji kama huu wa MES unaolenga kuwezesha ukuaji wa sekta ya madini na kuchangia maendeleo ya kiuchumi ya nchi,” alisema Dkt. Numbi.
Kiwanda cha MES kinatarajiwa kupunguza kwa kiasi kikubwa utegemezi wa Tanzania kwa bidhaa za matumizi ya mara kwa mara katika shughuli za uchimbaji madini chini ya ardhi, ambazo kwa kiasi kikubwa zimekuwa zikiagizwa kutoka kwa wasambazaji wa nje ya nchi.
Uwekezaji huo wa TZS bilioni 35 unahusisha ujenzi wa kiwanda, mitambo pamoja na miundombinu saidizi inayohitajika kuwezesha uzalishaji wa bidhaa hizo nchini.
Kwa mujibu wa uongozi wa MES, uwekezaji huo unalenga kuchukua nafasi ya bidhaa za matumizi ya mara kwa mara katika uchimbaji wa madini chini ya ardhi, ambazo kwa sasa huagizwa kutoka nje, kwa kuzalisha bidhaa hizo hapa nchini.
Mkurugenzi Mtendaji wa MES, Bw Pulin Manek, alisema kampuni hiyo imewekeza katika uwezo mkubwa wa uzalishaji utakaokidhi mahitaji ya soko la ndani, huku ukiweka mazingira ya Tanzania kuhudumia masoko mengine ya madini katika ukanda huu.
“Sababu ya kuanzisha kiwanda hiki ni kuisaidia Tanzania kupunguza utegemezi wa bidhaa za matumizi ya mara kwa mara katika uchimbaji wa madini chini ya ardhi zinazoagizwa kutoka nje, ambazo zinaendelea kuigharimu nchi kiasi kikubwa cha fedha,” alisema Manek.
“Tumewekeza katika uwezo wa kutosha wa uzalishaji ili kukidhi mahitaji ya soko la ndani, huku tukiiweka Tanzania katika nafasi ya kuhudumia masoko mengine ya madini katika ukanda huu.” Aliongeza.
Kiwanda hicho kitakapoanza kufanya kazi kwa ukamilifu, kitakuwa na uwezo wa kuzalisha bidhaa za ‘split sets’ kwa kiwango kinachokadiriwa kuwa mara mbili na nusu ya mahitaji ya sasa ya Tanzania kwa mwezi.
“Uwezo huu unatosha kuchukua nafasi ya uagizaji wa ‘split sets’ kutoka nje, huku ukiwezesha Tanzania kuuza ziada ya bidhaa hizo katika masoko ya kikanda,” alisema Manek.
Uwezo wa kiwanda hicho wa kuzalisha ‘mine mesh’ utakuwa mkubwa zaidi, ambapo kimebuniwa kuzalisha kiasi kinachokadiriwa kuwa mara nane ya mahitaji ya sasa ya Tanzania kwa mwezi.
Manek alisema uwezo huo wa ziada umeandaliwa kwa makusudi ili kuhudumia migodi mipya ya chini ya ardhi, kusaidia migodi inayobadilisha mfumo wa uchimbaji kutoka wazi kwenda chini ya ardhi, pamoja na kukidhi mahitaji ya masoko ya nchi jirani.
“Tunazalisha zaidi ya mahitaji ya sasa ya nchi kwa sababu tunaangalia mahitaji ya baadaye ya Tanzania katika uchimbaji wa madini chini ya ardhi, pamoja na fursa zilizopo katika ukanda mpana zaidi,” alisema Manek. “Tunaamini kuwa nchi haipaswi kuendelea kuagiza bidhaa za matumizi ya mara kwa mara ambazo zinaweza kuzalishwa hapa nchini.”
Kiwanda hicho kitakuwa na njia kuu tatu za uzalishaji, ambazo ni mine mesh, friction-stabiliser split sets na dome plates. Uwekezaji wa kampuni hiyo unalenga kuhudumia sekta za nishati, usafirishaji na madini.
Kwa mujibu wa Bw Manek, MES pia ni kampuni ya kwanza nchini Tanzania kuwekeza katika mtambo wa hot-dip galvanising bath, uwekezaji unaotarajiwa kuongeza zaidi uwezo wa nchi wa kuzalisha bidhaa zinazohusiana na shughuli za madini hapa nchini.
“Mbali na kupunguza utegemezi wa bidhaa zinazoagizwa kutoka nje, mradi huu unatarajiwa kuunda fursa za ajira kwa Watanzania, hususan katika uzalishaji, uchomeleaji, galvanising na uhandisi, huku ukisaidia kuimarisha ujuzi wa kitaalamu ndani ya mnyororo wa ugavi wa sekta ya madini nchini,” aliongeza Manek.
Kampuni hiyo pia inalenga masoko ya kikanda, yakiwemo Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Zambia na Zimbabwe, ikiwa na mipango ya kutumia nafasi ya kimkakati ya Tanzania pamoja na fursa ya usafirishaji kupitia Bandari ya Dar es Salaam ili kuifanya nchi kuwa kitovu cha uzalishaji na usambazaji wa bidhaa katika ukanda huu.
Aidha, uwezo wa uzalishaji wa kiwanda hicho unatarajiwa kuiwezesha Tanzania kuhudumia soko la ndani na kuuza bidhaa zitakazozalishwa kwa ziada katika masoko ya madini ya kikanda.
Uzalishaji wa ndani unatarajiwa pia kupunguza kwa kiasi kikubwa muda wa kuwasilisha bidhaa kwa wateja. Bidhaa za matumizi ya mara kwa mara katika shughuli za uchimbaji madini zinazoagizwa kutoka nje zinaweza kuchukua kati ya wiki nane hadi 16 kufika nchini, huku MES ikitarajia bidhaa zinazozalishwa ndani ya nchi kufikishwa kwa wateja ndani ya siku chache.
Uwekezaji huo unatajwa kuendana na Sheria ya Madini ya Tanzania pamoja na Kanuni za Maudhui ya Ndani, zinazotoa kipaumbele kwa bidhaa zinazozalishwa nchini na huduma zinazotolewa na raia wa Tanzania pamoja na kampuni zilizosajiliwa nchini.
Ujenzi wa kiwanda cha MES unafanyika wakati Serikali ikiendelea na juhudi za kuongeza ushiriki wa wazawa katika mnyororo wa thamani wa madini, kuongeza uzalishaji wa viwandani nchini na kuhakikisha kuwa uwekezaji katika sekta hiyo unazalisha manufaa mapana zaidi ya kiuchumi kwa Watanzania.

Kamishna wa Tume ya Madini ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Ushirikishwaji wa Watanzania katika Sekta ya Madini (Local Content), Dkt. Theresia Charles Numbi (katikati-kushoto), akizungumza na Wakurugenzi wa Kampuni ya Mining Engineering Services Tanzania Limited (MES), kampuni mwanachama wa Kundi la Makampuni la VINMART, wakati wa ziara yake katika kiwanda cha kampuni hiyo jijini Dar es Salaam jana.

Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Mining Engineering Services Tanzania Limited (MES), Pulin Manek (katikati), akizungumza na waandishi wa habari wakati wa ziara ya Kamishna wa Tume ya Madini ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Ushirikishwaji wa Watanzania katika Sekta ya Madini (Local Content), Dkt. Theresia Charles Numbi katika kampuni hiyo jijini Dar es Salaam jana.
Mkuu wa Wilaya ya Kilombero, Mhe. Dustan Kyobya (katikati), akiwaongoza wafanyakazi wa Yas Tanzania kukabidhi vifaa tiba na vifaa vya kujifungulia katika Kituo cha Afya Kibaoni, Ifakara mkoani Morogoro, hivi karibuni. Msaada huo ni sehemu ya Kampeni ya Tumaini inayoendeshwa na wafanyakazi wa Yas, yenye lengo la kuunga mkono huduma za afya ya mama kwa kutoa vifaa muhimu katika vituo vya afya nchini..jpeg)
SERIKALI imetoa maelekezo 13 kwa umma, kamati za usimamizi wa maafa, Wizara, Taasisi, Mikoa, Halmashauri na sekta mbalimbali nchini, kwa ajili ya kujiandaa na kukabiliana na madhara yanayoweza kujitokeza kutokana na mvua za El-Nino.
Imeelekeza maeneo yote hatarishi yatambuliwe mapema, tathmini za vihatarishi zifanyike na hatua stahiki zichukuliwe, ikiwemo kuwahamasisha wananchi kuondoka katika maeneo hatarishi na kwenda maeneo salama.
Maelekezo hayo yametolewa hii leo (02 Septemba,2026) na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge, Uratibu na Wenye Ulemavu, Profesa Palamagamba Kabudi, alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari kuhusu utekelezaji wa Mpango wa Taifa wa Dharura wa Kukabiliana na Madhara ya El-Nino.
Profesa Kabudi amesema Serikali imeelekeza kuhakikisha mvua hizo zinatumika kikamilifu kwa shughuli za uzalishaji, ikiwemo kilimo, ufugaji, uvunaji wa maji na uvuvi.
Aidha, amesisitiza wananchi wanapaswa kuelimishwa na kuhimizwa kuchukua hatua za kupunguza madhara yanayoweza kusababishwa na mvua hizo, ikiwemo kufanya shughuli za kiuchumi na kijamii katika maeneo salama, kuweka akiba ya chakula, kutumia mbinu bora za kilimo na kuchagua mazao pamoja na mbegu bora kwa msimu wa Vuli.
“Kuandaa rasilimali kwa ajili ya kuzuia au kupunguza madhara, kujiandaa na kukabiliana na maafa yatakayotokea na kushirikisha wadau wote wa maafa, wakiwemo wananchi, taasisi na sekta binafsi katika maeneo yao,” amesema.
Ameongeza kuwa: “Serikali imeagiza kuandaliwa na kutekelezwa kwa mipango ya kuzuia milipuko ya magonjwa kwa binadamu, wanyama na mimea.”
Profesa Kabudi amesema Wizara, Taasisi, Mikoa na wadau wengine wanaohusika na miundombinu wanapaswa kufanya ukaguzi wa miundombinu muhimu na kuhakikisha inaimarishwa na kusafishwa, ikiwemo madaraja, makaravati na mitaro.
Amesema hatua hiyo itasaidia kuhakikisha upatikanaji wa huduma muhimu kabla, wakati na baada ya maafa kutokea, zikiwemo huduma za usafirishaji, maji na umeme.
Serikali pia imeagiza kuimarishwa kwa usimamizi wa mazingira, ikiwemo udhibiti wa taka ngumu, usafishaji na uimarishaji wa njia za maji, kingo za mito na mabwawa.
Aidha, imeelekeza kuhakikisha vifaa vya uokoaji, huduma za dharura na mifumo ya mawasiliano vinapatikana na kuwa katika hali ya utayari wakati wote.
Katika hatua nyingine, Serikali imeagiza kubainisha na kutenga maeneo salama yatakayotumika kwa ajili ya makazi ya dharura pindi maafa yatakapotokea.
Kwa upande wa sekta ya utalii, Serikali imeagiza kufanyika kwa ukaguzi na ukarabati wa miundombinu iliyopo katika maeneo ya Hifadhi za Taifa na Hifadhi za Jamii ili kuhakikisha shughuli za utalii zinaendelea wakati wote.
“Wizara, Taasisi, Mikoa na Halmashauri zote zimeagizwa kufuatilia na kuzingatia maelekezo ya kitaalamu pamoja na taarifa za utabiri wa hali ya hewa zinazotolewa na Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA), ili hatua stahiki za kujiandaa na kukabiliana na madhara ya El-Nino zichukuliwe kwa wakati.”
KUHUSU BILIONI 730
Akizungumzia taarifa iliyosambaa katika mitandao ya kijamii kuhusu makadirio ya matumizi ya Sh. bilioni 730 katika kujiandaa na kukabiliana na El-Niño, Profesa Kabudi amesema taarifa hiyo haikutoa ufafanuzi wa kina kuhusu shughuli zilizoainishwa katika mpango huo.
Amesema Sh. bilioni 730 ni makadirio ya fedha zinazohitajika kutekeleza Mpango wa Taifa wa Dharura wa Kukabiliana na Madhara ya El-Niño kabla, wakati na baada ya El-Nino kutokea.
“Kwa mujibu wa Mpango, makadirio ya fedha zinazohitajika kutumika katika kutekeleza Mpango huo ni Sh. bilioni 730,” amesema.
Hata hivyo, amesema fedha zilizotengwa katika bajeti ya Serikali ya mwaka wa fedha 2026/2027 kwa ajili ya utekelezaji wa shughuli hizo katika sekta zote ni Sh. bilioni 10.



.jpeg)
.jpeg)

.jpeg)
.jpeg)

.jpeg)
.jpeg)
.jpeg)

.jpeg)
.jpeg)
.jpeg)

.jpeg)
.jpeg)

.jpeg)


.jpeg)







.jpeg)

.jpeg)





