Na Farida Mangube


MGOGORO wa ardhi unaodaiwa kudumu kwa miaka kadhaa kati ya wananchi wa Kijiji cha Kitete Msindazi, Kata ya Ruhembe wilayani Kilosa, Mkoani Morogoro na Hifadhi ya Taifa ya Mikumi umechukua sura mpya baada ya Mkuu wa Wilaya ya Kilosa, Shaka Hamdu Shaka, kufika katika eneo linalolalamikiwa na kuahidi kuanza upya mchakato wa kutafuta suluhu.

Wananchi wa kijiji hicho wamekuwa wakidai utekelezaji wa maamuzi yaliyowahi kufikiwa na Serikali katika kushughulikia migogoro ya ardhi kati ya vijiji vinavyopakana na hifadhi, wakisema pamoja na baadhi ya vijiji kunufaika na hatua zilizochukuliwa, wao bado hawajaona utekelezaji wa jambo hilo katika eneo lao.

Wananchi hao wanasema changamoto hiyo imewaacha bila maeneo ya kutosha ya kilimo, huku eneo linalohusishwa na mgogoro likiwa halitumiki rasmi na wananchi, lakini likiendelea kulindwa na askari wa Hifadhi ya Taifa ya Mikumi.

Kwa mujibu wa wananchi hao, miongoni mwa maeneo yaliyowahi kufanyiwa uhakiki ni Kijiji cha Kitete Msindazi, ambapo wanadai takribani hekta 4,972 zilihusishwa na eneo la hifadhi na kwamba hatua zilizofuata zilipaswa kuweka wazi hatima ya eneo hilo na matumizi yake.

Athuman Abdi Kihombe, ambaye alijitambulisha kuwa aliwahi kuwa Mwenyekiti wa Mpango wa Matumizi ya Ardhi wa Kijiji hicho na Mratibu wa Mbunge wa Mikumi wa wakati huo, Abdulsalaam Suleiman Ameir maarufu kama SAS amesema suala hilo limefuatiliwa kwa muda mrefu katika ngazi mbalimbali bila wananchi kupata utekelezaji waliokuwa wakiutarajia.

Kihombe alikwenda na nyaraka alizozisoma mbele ya Mkuu wa Wilaya, akieleza kuwa mwaka 2011 Waziri wa Maliasili na Utalii wa wakati huo, Ezekiel Maige, alitoa majibu Bungeni kuhusu mipaka ya Hifadhi ya Taifa ya Mikumi baada ya swali la Mbunge wa Mikumi wa wakati huo, SAS.

Kihombe amesema baada ya wananchi kuona utekelezaji wa maamuzi hayo unasuasua, walimfuata aliyekuwa Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi,na kupitia timu ya mawaziri nane wa kushughulikia migogoro ya ardhi kati ya wananchi na maeneo ya hifadhi, timu maalum iliundwa katika wilaya hiyo kwa kushirikisha wananchi, wataalamu wa ardhi na wawakilishi wa Hifadhi ya Taifa ya Mikumi, ambapo uhakiki wa mipaka ulifanyika na alama zikawekwa katika maeneo yaliyohusika.

Cloud Petter, mkazi wa Kitete Msindazi, amesema changamoto kubwa kwa sasa ni uhaba wa maeneo ya kulima wakati kuna eneo ambalo wananchi wanaamini lilipaswa kufanyiwa uamuzi wa mwisho badala yake wanaona maeneo hayo yanalindwa na askari wa hifadhi bila wananchi wanaotegemea kilimo kwa maisha yao wakishindwa kuyatumia.

Cloud katika mkutano wa hadhara wa Kijiji, akamuomba mkuu wa Wilaya ya Kilosa kwenda eneo linalolalamikiwa na kujionea hali halisi ili kupata picha halisi ya changamoto inayowakabili wananchi.

Kwa upande wake, Ismail Ngwale, mkazi wa Kitete Msindazi, amesema wananchi wamekuwa wakisubiri majibu ya Serikali kwa muda mrefu na kwamba suala hilo linahitaji hatua inayoweza kuleta utulivu wa kudumu katika kijiji hicho.

Wananchi waliohudhuria mkutano huo walionyesha matumaini baada ya Mkuu wa Wilaya kukubali kwenda katika eneo walilokuwa wakilalamikia, huku baadhi yao wakisema hatua hiyo imewapa picha kwamba Serikali italifanyia kazi shauri hilo kwa kuwa umeona uhalisia

Baadhi ya wananchi walionekana kushangilia huku wengine wakijilaza mbele yake kama ishara ya kumshukuru kwa kukubali kusikiliza kilio chao na kwenda kujionea hali halisi, huku wengine wakicheza muziki kwa Furaha.

Aliporudi eneo la mkutano, Mkuu huyo wa wilaya alitaka kwanza kusikia sauti za wananchi ambapo Mwenyekiti mstaafu wa Kijiji cha Kitete Msindazi, Timilai Lunyungu, amesema baada ya kufika eneo hilo wamejiridhisha kuwa suala hilo linahitaji utulivu na hatua za Serikali badala ya wananchi kuendelea kuingia katika maeneo yenye mgogoro hivyo kuwasihi wananchi watulivu wakati Serikali ikiendelea na mchakato kulishughulikia suala hilo.

Naye Diwani wa Kata ya Ruhembe, Frank Hamis , akasema wananchi wanapaswa kuendelea kuwa watulivu ili Serikali iweze kupata nafasi ya kulishughulikia suala hilo kwa utaratibu.

Hata hivyo diwani huyo ameiomba Serikali kuangalia uwezekano wa kuruhusu mazao ambayo tayari yamepandwa katika eneo linalolalamikiwa, hasa mahindi yaliyokuwa karibu kuvunwa, yaachwe yakomae na kuvunwa badala ya kuondolewa mara moja.

Aidha akaomba wananchi waliokamatwa au wanaokabiliwa na mashauri kutokana na mgogoro huo waangaliwe kwa jicho la huruma na ikiwezekana mashauri yao yaondolewe kwenye vyombo vya Dola.

Akijibu ombi hilo, Shaka amesema Serikali imepokea hoja hiyo na itaishughulikia baada ya kushauriana na mamlaka husika, badala ya kutoa uamuzi wa moja kwa moja kuhusu mashauri yaliyo kwenye vyombo vya Dola.

Akawataka wananchi kutokwenda katika maeneo yenye mgogoro kufanya shughuli mpya za kilimo, ujenzi au maendeleo mengine wakati Serikali ikiendelea na mchakato wa kutafuta suluhu baada ya kuundwa kwa timu ya maridhiano itakayoshirikisha wawakilishi wa Wananchi, wataalamu,na wadau wengine.

Amesema Serikali ya wilaya imeona mgogoro huo unahusu maisha ya wananchi na kwamba haupaswi kuendelea bila kutafutiwa ufumbuzi.

“Mgogoro huu sio mkubwa kama ulivyokuwa ukitengenezwa. Sisi wenyewe Serikali ya wilaya tunaweza kuumaliza. Rais ametupa nyenzo zote za kufanyia kazi, tukishindwa hata kwa hili dogo tunamwangusha,” alisema Shaka.

Shaka amesema baadhi ya watu wamekuwa wakiufanya mgogoro huo uonekane mkubwa kuliko ulivyo, huku akisisitiza kuwa Serikali sasa inalenga kuufanyia kazi kwa hatua na taratibu ili pande zote ziwe salama, ziiishi kwa amani na utulivu na shughuli za uzalishaji ziendelee kama kawaida.

“Ufunguo wa suluhisho tunao, lakini tunataka utatuzi ufuate hatua na taratibu zote. La msingi na kubwa ni kuwa watulivu wakati suala hili linashughulikiwa,” akaongeza

Katika hatua nyingine, Shaka aliwapa muda wa mwezi mmoja wananchi wenye mazao yaliyopo katika eneo lenye mgogoro kuyaondoa, huku akisisitiza kuwa Serikali haitaruhusu watu wengine kuingia katika eneo hilo kwa ajili ya kuanzisha shughuli mpya na watakaokwenda kinyume watambue hawatafumbiwa macho na wataonekana ni wasiotaka mchakato wa kutafuta suluhu.






Na Janeth Raphael - MichuziTv

Mradi wa ujenzi wa Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Msalato jijini Dodoma umefikia asilimia 89.02 kwa upande wa ujenzi wa miundombinu, huku kazi za ujenzi wa majengo zikifikia asilimia 78.37, na Serikali ikieleza kuwa mradi huo unatarajiwa kuanza kukamilika katika hatua zake kuu kuanzia Novemba hadi Desemba 2026.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dodoma leo, Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS), Mhandisi Mohamed Besta, amesema Package 1 inayohusisha ujenzi wa miundombinu imepiga hatua kubwa, ambapo ujenzi wa njia ya kurukia na kutua ndege umefikia asilimia 98, taxiways asilimia 99 na apron asilimia 99.

Aidha, barabara za kuingia kiwanjani, barabara za ndani na maegesho ya magari zimefikia asilimia 75, mfumo wa maji asilimia 89, uzio na mageti asilimia 76, huku kazi za umeme na vifaa vya kuongozea ndege zikifikia asilimia 90.

Mhandisi Besta amesema kazi zilizobaki katika Package 1 ni pamoja na upandaji wa nyasi katika maeneo ya usalama ya runway na taxiways, ufungaji wa taa za kuongozea ndege ardhini na taa za barabarani, mabomba na tanki la maji la chini ya ardhi, kukamilisha uzio na mageti pamoja na kufunga mifumo ya mawasiliano ya ndege ikiwemo ILS na DVOR, ambayo tayari imewasili katika eneo la mradi.

Kwa upande wa Package 2 unaohusisha ujenzi wa majengo, amesema utekelezaji umefikia asilimia 78.37, ambapo jengo la abiria limefikia asilimia 81, mnara wa kuongozea ndege asilimia 74, kituo cha huduma za zimamoto asilimia 88, kituo kikuu na vituo vidogo vya umeme asilimia 71 na jengo la huduma za hali ya hewa (MTO) asilimia 87.

Kazi zinazoendelea ni pamoja na umaliziaji wa majengo, mifumo ya mitambo, umeme na mabomba, TEHAMA na mawasiliano, mashine za ukaguzi wa mizigo, madaraja ya kupandia abiria, vifaa vya hali ya hewa na magari ya zimamoto.

Amesema kwa mujibu wa mpango wa utekelezaji, ujenzi wa miundombinu unatarajiwa kukamilika ifikapo Novemba 27, 2026, huku ujenzi wa majengo ukitarajiwa kukamilika Desemba 30, 2026, huku TANROADS ikiendelea kufuatilia kwa karibu ratiba za kazi, upatikanaji na ufungaji wa vifaa, uratibu wa wakandarasi pamoja na utekelezaji wa kazi zinazotegemeana ili kuhakikisha mradi unakamilika kwa wakati.

Aidha, Mhandisi Besta amesema mradi huo tayari umetoa ajira 9,059 kwa Watanzania, ambapo ajira 3,571 zimetolewa kupitia Package 1 na ajira 5,488 kupitia Package 2, huku wafanyakazi wa kigeni wakiwa 47. 

Amewataka Watanzania, hususan wakazi wa Dodoma, kutumia fursa zitakazotokana na uwanja huo kukuza biashara na uchumi, ikiwemo usafirishaji wa bidhaa zinazohitaji kufika sokoni kwa haraka kama matunda, mboga mboga, samaki, kuku na maua, pamoja na kutumia fursa hiyo kukuza sekta ya utalii.






Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, amepongezwa kwa uongozi wake mahiri katika kusukuma mbele ajenda ya Afrika ya kutokomeza vifo vinavyoweza kuzuilika vya mama na mtoto, huku bara hilo likikabiliwa na karibu asilimia 70 ya vifo vya akina mama duniani na takribani theluthi mbili ya vifo vya watoto walio chini ya miaka mitano.

Akiwa Kinara wa Umoja wa Afrika katika Afya ya Mama na Mtoto, Rais Samia anaongoza ajenda ya “Malengo Matatu ya Sifuri” (Three Zeros) inayolenga kufikia sifuri ya kujifungulia nyumbani, sifuri ya vifo vinavyoweza kuzuilika vya mama na mtoto mchanga, pamoja na sifuri ya watoto wasiopata chanjo.

Ajenda hiyo imepewa msukumo katika Mkutano wa Ngazi ya Juu wa Wakuu wa Nchi kuhusu Afya ya Mama, Mtoto Mchanga na Mtoto, iliofanyika pembezoni mwa Mkutano wa 81 wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa (UNGA81), ukiwakutanisha Wakuu wa Nchi na Serikali, viongozi wa taasisi za Umoja wa Afrika, mashirika ya kimataifa ya afya na washirika wa maendeleo.

Akiwasilisha ujumbe wa Rais Samia katika mkutano huo, Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Deogratius Ndejembi, amesema ukubwa wa changamoto unahitaji Afrika kutoka kwenye ahadi na kuelekea katika hatua madhubuti zinazoweza kupimwa kwa maisha ya wanawake na watoto yanayookolewa.

Amesema, pamoja na hatua ambazo Bara la Afrika limepiga, Afrika bado inachangia karibu asilimia 70 ya vifo vya akina mama duniani na takribani theluthi mbili ya vifo vya watoto walio chini ya miaka mitano, huku sehemu kubwa ya vifo hivyo ikiwa inaweza kuzuilika.

Makamu wa Rais amesema msukumo wa Rais Samia unalenga kuimarisha mifumo ya afya ya nchi za Afrika, kuongeza ufadhili wa ndani, kuboresha huduma za dharura na mifumo ya rufaa, kuongeza upatikanaji wa wahudumu wa afya wenye ujuzi na kuhakikisha takwimu zinatumika kufuatilia matokeo na kubaini maeneo yanayohitaji hatua zaidi.

Akielezea uzoefu wa Tanzania, Makamu wa Rais amesema uwekezaji katika huduma za afya ya msingi na za dharura kwa mama na mtoto mchanga, pamoja na kuimarishwa kwa mifumo ya rufaa ikiwemo M-Mama, unaonesha namna uongozi wa kisiasa, teknolojia na utoaji wa huduma kwa wananchi vinavyoweza kuunganishwa katika kuokoa maisha.

Hatua hizo zimekwenda sambamba na kuongezeka kwa wanawake wanaojifungulia katika vituo vya afya kutoka asilimia 51 mwaka 2015 hadi asilimia 81 mwaka 2022, mafanikio yanayoonesha uwezekano wa kubadili mwenendo wa vifo vya mama na mtoto pale uwekezaji unapounganishwa na utekelezaji katika ngazi ya jamii.

Makamu wa Rais alisema ajenda anayoiongoza Rais Samia pia inatoa uzito kwa suala la Afrika kujitegemea katika afya, akisisitiza kuwa mafanikio hayapaswi kupimwa pekee kwa uwezo wa bara kugharamia, kuzalisha au kununua mahitaji yake, bali pia kwa uwezo wa kuhakikisha huduma muhimu zinamfikia kila mama na mtoto kwa wakati na mahali wanapozihitaji.

Katika kufanikisha hilo, nchi za Afrika zimehimizwa kuimarisha uwajibikaji wa kisiasa, kuongeza uwekezaji wa ndani katika huduma zinazookoa maisha na kuhakikisha rasilimali zinafika hadi katika ngazi ya utoaji huduma.

“Dhamira ni kuhakikisha hakuna mama anayepoteza maisha kwa kukosa usafiri, damu, mhudumu mwenye ujuzi au huduma ya dharura; hakuna mtoto mchanga anayefariki kwa kukosa huduma inayoweza kuokoa maisha yake, na hakuna mtoto anayebaki bila chanjo kwa sababu mfumo wa afya haukuweza kuifikia familia yake,” amesema Mhe. Ndejembi.

Makamu wa Rais amesema kulinda uhai wa mama na mtoto si suala la afya pekee, bali ni uwekezaji katika rasilimali watu, uchumi na mustakabali wa Afrika, pamoja na kuwa sehemu muhimu ya utekelezaji wa Ajenda 2063 ya Bara la Afrika.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa Africa CDC, Dkt. Jean Kaseya, alipongeza uongozi wa Rais Samia na kueleza dhamira ya Taasisi hiyo kuendelea kumuunga mkono katika jukumu lake la Kinara wa Umoja wa Afrika katika Afya ya Mama na Mtoto, huku akitaja hatua zilizopigwa na Tanzania kama mfano wa mafanikio yanayoweza kupatikana barani Afrika.

Takwimu za Africa CDC zinaonesha kuwa Tanzania imepunguza uwiano wa vifo vya uzazi kwa takribani asilimia 80, kutoka vifo 556 kwa kila vizazi hai 100,000 mwaka 2016 hadi 104 mwaka 2022, hatua inayohusishwa na kuimarishwa kwa huduma za dharura za uzazi na watoto wachanga, mifumo ya rufaa, ongezeko la wahudumu wa afya pamoja na ufuatiliaji wa vifo vya mama na watoto.

Dkt. Kaseya alisema Africa CDC itaendelea kushirikiana na Tanzania katika kusukuma mbele ajenda hiyo, akisisitiza umuhimu wa uongozi wa kisiasa, uwekezaji na mifumo imara ya afya katika kulinda uhai na ustawi wa mama na mtoto barani Afrika.

Mkurugenzi wa Shirika la Afya Duniani Dkt. Adhanom Ghebreyesus amempongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuandaa mkutano huo na kuwa kinara wa Umoja wa Mataifa wa Afya ya Mama na Mtoto. Amesema katika kipindi cha miaka sita pekee, Tanzania imepunguza kiwango cha vifo vya kina mama kwa asilimia 81. Amesema kwa kuzindua mpango mkakati huo wa sifuri tatu (Three Zeros), Tanzania inaongoza kwa mfano na inapaswa kuungwa mkono.

Amesema Shirika la Afya Duniani limejidhatiti kusaidia kila nchi mwanachama kulingana na mazingira yake na kufikia malengo yake kwa kuimarisha viwango vya huduma za kitabibu vinavyotumiwa na wahudumu walio mstari wa mbele kuokoa maisha ya kina mama na watoto wachanga.

Kupitia nafasi yake kama Kinara wa Umoja wa Afrika katika Afya ya Mama na Mtoto, Rais Samia anasukuma dhamira ya kulifanya bara hilo kufikia hatua ambayo vifo vinavyoweza kuzuilika havitachukuliwa tena kuwa jambo lisiloepukika, huku kaulimbiu ya “Jiongeze, Tuwavushe Salama” ikibeba wito wa Afrika kwenda hatua ya ziada kwa ajili ya kila mama, mtoto mchanga, mtoto na kijana balehe.

Mkutano huo, umehudhuriwa na Viongozi kutoka nchi mbalimbali za Afrika, Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Afya Duniani, Dkt. Adhanom Ghebreyesus, Mkurugenzi Mkuu wa Kituo cha Afrika cha Kudhibiti na Kuzuia Magonjwa (Africa CDC) Dkt. Jean Kaseya, Mwenza wa Rais wa Benin Bi. Nathalie Vilette Wadagni, Wadau wa Maendeleo wakiwemo, Gates Foundation, Global Fund, Gavi, UNFPA, Unicef, Suzan Thompson Buffett Foundation, Beginning Fund pamoja na Viongozi kutoka Umoja wa Afrika (AU).





Na Janeth Raphael - MichuziTv 

Hospitali ya Benjamin Mkapa (BMH) Dodoma imewataka wagonjwa kuwa sehemu ya mchakato wa matibabu kwa kufahamu haki zao na kushiriki kikamilifu katika maamuzi yanayohusu afya zao, ikiwa ni pamoja na kupewa taarifa sahihi, kuheshimiwa na kupata huduma salama kwa wakati.

Akizungumza katika kilele cha maadhimisho ya Siku ya Usalama wa Mgonjwa yaliyofanyika hospitalini hapo leo Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa BMH, Dk. Abdalah Baja, amesema mgonjwa ana haki ya kupata huduma bora na salama kulingana na mahitaji yake, kushirikishwa katika maamuzi ya matibabu, kupata maoni ya pili ya kitabibu na kuhakikishiwa faragha wakati wa kupatiwa huduma.

Dkte. Baja amesema haki nyingine ni kuheshimiwa utu wa mgonjwa, kulindwa kwa usiri wa taarifa zake za kiafya, kupewa nafasi ya kueleza changamoto zake na kusikilizwa, kuhudumiwa kwa wakati pamoja na kupata taarifa zilizo wazi kuhusu gharama, huduma anazohitaji na maendeleo ya matibabu yake. Dk. Baja alisisitiza kuwa utoaji wa taarifa sahihi humwezesha mgonjwa kuelewa huduma anayopewa na kushiriki ipasavyo katika maamuzi ya matibabu.

Pia Dkt. Baja, amesema usalama wa mgonjwa unaweza kuathiriwa na changamoto mbalimbali, ikiwamo baadhi ya wagonjwa kuchelewa kufika hospitalini katika muda waliopangiwa, kutomuona daktari au kutofanyiwa vipimo walivyoelekezwa, pamoja na changamoto za miundombinu. 

Amesema hali hizo zinaweza kuongeza hatari ya madhara kwa mgonjwa, ikiwamo matumizi yasiyo sahihi ya dawa.

Kwa upande wake, Daktari  bingwa wa Upasuaji toka BMH Kakorongo Mugisha amesema BMH inaendelea kuimarisha usalama wa wagonjwa kwa kuwajengea uwezo wataalamu wa afya na kuhakikisha huduma zinatolewa kwa kuzingatia taratibu za kitaalamu. 

Alisema pia wagonjwa wana haki ya kuamua iwapo wanataka wanafunzi washiriki wakati wa huduma zao, huku hospitali ikiendelea kutoa mafunzo ya vitendo kwa wanafunzi kwa kuzingatia ridhaa ya mgonjwa na usalama wake. 

Aidha, alisema muda wa kupata majibu ya vipimo hutegemea aina ya kipimo, ambapo baadhi ya vipimo vya kawaida vinaweza kutoa majibu ndani ya saa tatu, huku vipimo kama CT Scan na MRI vikitarajiwa kutoa majibu ndani ya saa 24 kulingana na taratibu za huduma.

Nao Baadhi ya wagonjwa waliopatiwa huduma BMH wameeleza kuridhishwa na huduma wanazopata, huku wakitoa mapendekezo ya maboresho. Omary Namganda, mkazi wa Kigoma Mjini, aliwapongeza wataalamu wa afya kwa huduma wanazowapatia wagonjwa, wakati Jasery Zacharia wa Kahama, Shinyanga, alisema amepata huduma na ufuatiliaji katika matibabu ya tatizo la figo lililohusisha mawe. Kwa upande wake, Sospiter Chibanila aliitaka hospitali kuendelea kuboresha kasi ya upatikanaji wa majibu ya vipimo vinavyohitaji muda mrefu ili kuwawezesha wagonjwa kupata huduma kwa wakati.







-DC SHAKA APIGA MARUFUKU MAFUNZO, AAGIZA FEDHA ZINUNUE VIFAA VYA DHARURA

Mkuu wa Wilaya ya Kilosa, Mhe. Shaka Hamdu Shaka ameongoza Kikao Maalum cha Kamati ya Maafa ya Wilaya kilichojumuisha Kamati ya Ulinzi na Usalama na wadau mbalimbali kujadili maandalizi ya kukabiliana na mvua kubwa za El Nino zinazotarajiwa kuanza mwishoni mwa mwezi huu kwa mujibu wa Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA).

Akifungua kikao hicho, Mhe. Shaka amesema Wilaya ya Kilosa imejifunza kutokana na athari za mafuriko ya miaka ya nyuma na safari hii maandalizi yote yatajikita kwenye vitendo, sio kwenye makaratasi.

Amefafanua kuwa uamuzi huo ni utekelezaji wa agizo la Mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan aliyeagiza mikoa na wilaya zote kuchukua tahadhari mapema na kuhakikisha taarifa za TMA hazibaki kwenye makaratasi bali zinafuatwa na hatua za vitendo.

Akizungumza kwa msisitizo, DC Shaka alisema:"Wilaya ya Kilosa tumeamua fedha zote zilizotengwa kwa ajili ya maafa zitanunua vifaa vya dharura vinavyoonekana. Sitaki kusikia mafunzo, semina na warsha. Wananchi wa Kilosa wanajua mafuriko ni nini. Wanachohitaji ni boti la kuwaokoa, blanketi la kujifunika na dawa wakiumwa."

"Nimesikia kuna fedha zimetengwa kwa ajili ya mafunzo ya maafa. Sitaki kusikia mafunzo. Sitaki kabisa. Nani hapa Kilosa hajui mafuriko? Mtoto wa miaka 10 wa Kimamba anajua mafuriko kuliko mtaalamu. Fedha zozote za maafa zisiguse mafunzo."

"Mafuriko yakija kesho, hutamwambia mama aliyekwama na watoto wawili juu ya paa - 'Mama subiri nikupe brochure ya mafunzo'. Hapana. Utamwambia - 'Mama panda boti, hiki hapa blanketi, huu hapa mchele'."

Kwa upande wao, wadau mbalimbali walioshiriki kikao hicho wamepongeza utaratibu wa Wilaya ya Kilosa wa kushirikisha makundi yote na kueleza kuwa mipango iliyopangwa itatekelezeka na kuhakikisha usalama wa wananchi katika kipindi hiki cha tahadhari.

Kikao kimeazimia kuanzishwa kwa Stoo ya Dharura ya Wilaya na kuhamishwa kwa wananchi wanaoishi maeneo hatarishi.







Na Oscar Assenga,Tanga

SHIRIKA la Uwakala wa Meli Tanzania (TASAC) limewataka wamiliki na waendeshaji wa vyombo vya usafiri majini kuhakikisha wana vifaa vya kutosha vya uokoaji ili kuwawezesha abiria kujinusuru wakati wa dharura.

Aidha, abiria wametakiwa kuzingatia maelekezo yanayotolewa na manahodha, hususan wakati chombo kinapokumbana na hitilafu au changamoto inayoweza kuhatarisha maisha yao.

Kauli hiyo hiyo ilitolewa na Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya Shirika la Uwakala wa Meli Tanzania (TASAC), Kapteni Mussa Mandia, wakati wa mazoezi ya utafutaji na uokoaji wa abiria yaliyofanyika katika Bahari ya Hindi, mkoani Tanga.

Mandia alisema mazoezi hayo yalilenga kuonesha namna shughuli za utafutaji na uokoaji zinavyofanyika wakati wa dharura, huku akisisitiza umuhimu wa abiria kufuata maelekezo ya manahodha na kutumia vifaa vya kujiokoa.

“Hii ni sehemu ya kuonesha namna utafutaji na uokoaji wa abiria unavyofanyika wakati wa safari. Natumaini itawakumbusha madereva na abiria umuhimu wa kuzingatia maelekezo ya nahodha, kuvaa vifaa vya kujiokoa na kutoa taarifa za dharura mapema,” alisema.




Aipongeza Serikali

Katika hatua nyingine, Mandia aliipongeza Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Samia Suluhu Hassan kwa hatua zinazochukuliwa kuboresha miundombinu ya usafiri na uchumi wa bahari nchini.

Alisema maboresho yaliyofanyika katika Bandari ya Tanga yameongeza uwezo wa bandari hiyo kuhudumia meli kubwa, hatua aliyosema imeendelea kufungua fursa za kiuchumi na kuitangaza Tanzania kimataifa.


“Tunaipongeza Serikali kwa juhudi kubwa za kuboresha miundombinu ya usafiri na uchumi wa bahari. Maboresho makubwa ya Bandari ya Tanga yameongeza uwezo wa bandari na kuleta matokeo chanya katika shughuli za bandari hii,” alisema.

Mandia pia alitaja hatua ya Serikali kuwezesha kupatikana kwa boti nne maalumu kwa ajili ya shughuli za utafutaji na uokoaji, ambazo zimewekwa katika maeneo mbalimbali likiwamo Bandari ya Tanga, Ziwa Victoria na Kigoma.

Alisema pia kuna boti maalumu ya kutoa huduma kwa wagonjwa iliyopo mkoani Mwanza.

Tanzania yazingatia mikataba ya IMO

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Usalama na Mazingira kutoka Wizara ya Uchukuzi ambaye pia ni Mwenyekiti wa maandalizi ya maadhimisho hayo yanayofanyika kitaifa mkoani Tanga, Stella Katondo, alisema Tanzania inaendelea kutekeleza mikataba ya kimataifa inayosimamiwa na Shirika la Kimataifa la Usafiri wa Majini (IMO) kuhusu utafutaji na uokoaji.

Katondo alisema Serikali imekuwa ikiandaa mazingira wezeshi yatakayosaidia kuimarisha usalama wa usafiri wa majini na kuhakikisha uokoaji wa maisha unakuwa kipaumbele wakati wa dharura.


“Tunafanya haya kwa kuzingatia kwamba Tanzania kama mwanachama tumeridhia mkataba wa kimataifa wa utafutaji na uokoaji unaosimamiwa chini ya SOLAS na IMO. Tuna wajibu wa kuokoa maisha kwanza, ndiyo maana tunazingatia taratibu zote,” alisema.

Alisema Serikali kupitia Wizara ya Uchukuzi inaendelea kuhakikisha kunakuwa na wataalamu wenye weledi na wanaokidhi viwango vya kimataifa katika eneo la utafutaji na uokoaji.

Wataalamu kujiweka tayari

Naye Mkaguzi wa Meli za Kitaifa na Kimataifa pamoja na vyombo vidogo kutoka TASAC, Mhandisi Ally Diwani, alisema kutokana na maboresho yanayoendelea kufanywa na Serikali katika sekta ya usafiri wa majini, wataalamu wanapaswa kufanya mazoezi ya mara kwa mara ili kujiweka tayari kukabiliana na dharura.

Alisema mazoezi hayo ni muhimu katika kuhakikisha wataalamu wanakuwa tayari wakati wote kwa ajili ya kufanya shughuli za utafutaji na uokoaji pale inapohitajika.
Na Mwandishi Wetu, New York

WAZIRI wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Dkt. Mahmoud Thabit Kombo (Mb.), amesema ushiriki wa wanawake katika michakato ya amani ni muhimu katika kupata suluhisho endelevu kwa changamoto za usalama katika eneo la Maziwa Makuu, hususan Mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC).

Mhe. Kombo ameyasema hayo katika Mkutano wa Ngazi ya Juu kuhusu kuendeleza Ajenda ya Wanawake, Amani na Usalama katika juhudi za amani eneo la Maziwa Makuu, uliofanyika pembezoni mwa Kikao cha 81 cha Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa, jijini New York, Marekani.

Amesema hali ya usalama Mashariki mwa DRC inaendelea kuwa ya kutia wasiwasi, huku wanawake na wasichana wakikabiliwa na changamoto mbalimbali, ikiwemo kuhama makazi, ukatili wa kingono na ukosefu wa mahitaji muhimu.

Kutokana na hali hiyo, Mhe. Kombo amesema Tanzania imesisitiza umuhimu wa utekelezaji wa Azimio Na. 1325 la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, linalohimiza ushiriki wa wanawake katika kuzuia na kutatua migogoro, pamoja na kujenga na kudumisha amani.

Amesema Tanzania imeandaa Mpango wa Kwanza wa Kitaifa wa Wanawake, Amani na Usalama wa 2025–2029, uliozinduliwa Agosti 19, 2025, unaolenga kuongeza ushiriki na uongozi wa wanawake katika masuala ya amani na usalama, pamoja na kuimarisha ulinzi na mifumo ya urejeshaji inayozingatia jinsia.

Aidha, Mhe. Kombo amesema Tanzania itaendelea kushiriki katika juhudi za kikanda kupitia Mkutano wa Kimataifa wa Maziwa Makuu (ICGLR), ikiwemo utekelezaji wa Mpango wa Kikanda wa Kizazi cha Pili na Mkakati wa Upatanishi na Uratibu unaozingatia jinsia.

Amesema Tanzania itaendelea kushirikiana na nchi za eneo la Maziwa Makuu katika juhudi za kujenga amani, usalama na utulivu wa kudumu.

Kwa upande wake, Mjumbe Maalum wa Umoja wa Afrika kuhusu Wanawake, Amani na Usalama, Mhe. Balozi Liberata Mulamula, amesema wanawake hawapaswi kuishia kushirikishwa katika michakato ya amani, bali wanapaswa kupewa nafasi, mamlaka na msaada unaowawezesha kushiriki kikamilifu katika maamuzi yanayounda amani.

Amesema ushiriki wa wanawake katika maamuzi ya amani ni muhimu katika kuhakikisha suluhisho zinazopatikana zinakuwa shirikishi, endelevu na zinazingatia mahitaji ya makundi mbalimbali katika jamii.





MAMIA ya wananchi wa Kata ya Pagwi, Wilaya ya Kilindi, mkoani Tanga, wamejitokeza kwa wingi kumlaki Mbunge wa Jimbo la Kilindi, Mhe. Salehe Mbwana Mhando, wakati wa ziara yake katika Vijiji vya Pagwi, Lumotio na Chamtui.

Ziara hiyo imekuwa ya aina yake baada ya Mhe. Mhando kuonyesha kwa vitendo mshikamano na wananchi katika kusukuma maendeleo, ikiwemo kubeba mwenyewe mifuko ya saruji mabegani kuelekea eneo la ujenzi wa Zahanati ya Pagwi.

Katika ujenzi huo unaotekelezwa kwa nguvu za wananchi, Mhe. Mhando alikabidhi mifuko 50 ya saruji pamoja na Sh500,000 taslimu kwa ajili ya kuunga mkono ujenzi huo.

Mbunge huyo pia aliahidi kuongeza mifuko mingine 100 ya saruji, akisema hatua hiyo inalenga kuongeza kasi ya kukamilika kwa zahanati hiyo na kuwawezesha wananchi kupata huduma za afya karibu na makazi yao.

Zahanati hiyo inatarajiwa kupunguza adha ya wananchi wa Pagwi ambao wamekuwa wakilazimika kusafiri hadi Lumotio kufuata huduma za afya.

Akizungumza na wananchi wakati wa ziara hiyo, Mhe. Mhando alisema ataendelea kuifuatilia Kata ya Pagwi na kusukuma mbele hoja za maendeleo, akisisitiza kuwa changamoto za wananchi zinapaswa kutafutiwa ufumbuzi hatua kwa hatua.


“NITAITIFUA TIFUA PAGWI HADI KIELEWEKE,” alisema Mhe. Mhando, akiahidi kuendelea kufuatilia kwa karibu masuala ya maendeleo katika kata hiyo.

Alitaja maeneo ya kipaumbele kuwa ni pamoja na barabara, maji, umeme, afya na madaraja, akisema miundombinu bora ni muhimu kwa maendeleo ya wananchi na shughuli zao za kiuchumi.

BARABARA SUNYA–PAGWI–MAKELELE

Mhe. Mhando pia alizungumzia changamoto ya barabara ya Sunya–Pagwi–Makelele, akisisitiza umuhimu wa kuendelea kuifuatilia ili kurahisisha usafiri na usafirishaji wa bidhaa kwa wananchi.

Aidha, aligusia changamoto ya Daraja la Makelele, linalounganisha maeneo ya Lumotio na Makelele, akisema wakati jitihada za kupata daraja la kudumu zikiendelea, ni muhimu kutafutwa kwa haraka kwa daraja la muda ili wananchi wasikwame katika shughuli zao.

Alisema pia kuna umuhimu wa kuendelea kufungua mawasiliano ya barabara katika njia za Sunya–Lumotio–Makelele–Sambu–Songe, pamoja na Kikunde–Chamtui–Lumotio–Sunya.

UMEME WAFIKA MALALI NA MASIMBA

Katika sekta ya umeme, Mhe. Mhando alisema maeneo ya Malali na Masimba tayari yamefikiwa na huduma hiyo, huku akisisitiza kuwa jitihada zitaendelea ili maeneo mengine nayo yaunganishwe na umeme.

ATOA SHILINGI MILIONI MOJA UJENZI OFISI YA KIJIJI.

Akiwa katika Kijiji cha Chamtui, Mhe. Mhando alitoa Sh 1 milioni kwa ajili ya ununuzi wa bati zitakazotumika katika upauaji wa jengo la Ofisi ya Kijiji hicho.

Mbali na hilo, alilipia ada vijana watano kutoka Chamtui kwenda kupata mafunzo ya ufundi katika Chuo cha VETA, hatua inayolenga kuwawezesha kupata ujuzi wa kuwaongezea fursa za kujiajiri na kushiriki katika shughuli za kiuchumi.
MICHEZO YAPATA MSUKUMO

Mhe. Mhando pia alitoa jezi kwa timu mbalimbali za soka katika maeneo aliyotembelea, zikiwemo Lipuli FC ya Chamtui, Mikocheni FC ya Mtakuja, Azam FC ya Chang’ombe na Toto FC ya Nyamaleni.

Aidha, alikabidhi jezi kwa timu mbili za Kijiji cha Pagwi pamoja na jozi moja kwa ajili ya wanafunzi.

WANANCHI 
TUMEONA JITIHADA ZA MBUNGE WETU

Kwa upande wao, wananchi wa Kata ya Pagwi walimshukuru Mhe. Mhando kwa kuwafikia, kuwasikiliza na kushirikiana nao katika kutafuta ufumbuzi wa changamoto zinazowakabili.

Walisema wamefarijika kuona Mbunge wao akijikita katika masuala yanayogusa maisha yao moja kwa moja, yakiwemo afya, barabara, maji, umeme, madaraja, elimu na fursa kwa vijana.

Wananchi hao pia walimshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kuendelea kuunga mkono utekelezaji wa miradi ya maendeleo nchini.

Ziara ya Mhe. Mhando katika Kata ya Pagwi imeweka msisitizo katika ushirikiano kati ya wananchi na viongozi katika kutafuta ufumbuzi wa changamoto za maendeleo, huku ahadi na michango iliyotolewa ikitarajiwa kuongeza kasi ya utekelezaji wa baadhi ya miradi katika eneo hilo.











Na Mwandishi Wetu, Geita

KAMPUNI ya uchimbaji wa madini ya dhahabu ya TG Goodness Group, iliyopo Nyamitondo mkoani Geita, imeshiriki katika Maonyesho ya Tisa ya Kitaifa ya Teknolojia ya Madini, yanayofanyika katika Viwanja vya Dkt. Samia Suluhu Hassan, Manispaa ya Geita.

Akizungumza katika maonyesho hayo, Katibu Mkuu wa mgodi huo, John Jande Richard, amesema baadhi ya wachimbaji wa kampuni hiyo wameshiriki maonyesho hayo na kupata mafunzo mbalimbali kwa wachimbaji wadogo yaliyotolewa na Wakala wa Usalama na Afya Mahali pa Kazi (OSHA).

Jande amesema licha ya kuwa ni mara ya kwanza kwa wafanyakazi wa kampuni hiyo kushiriki katika maonyesho hayo, wameweza kunufaika na elimu mbalimbali, hususan kuhusu usalama na afya katika shughuli za uchimbaji wa madini.

Amesema pia wamepata fursa ya kusikiliza nasaha zilizotolewa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Ajira na Mahusiano, Deus Sanga, wakati akifungua mafunzo kwa wachimbaji wa madini.

“Maonyesho ni mazuri, wachimbaji wengi wameshiriki na tumepata elimu kuhusu uchimbaji wa madini kwa usalama kupitia kaulimbiu ya ‘Tuamini Kazi Yako, Jikinge na Ajali,’” amesema Jande.


Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Deogratius Ndejembi, amesema utekelezaji wa Ajenda ya Sifuri Tatu ni muhimu katika kuokoa maisha ya mama, watoto wachanga na watoto, na kuchangia ujenzi wa afya bora, nguvu kazi na maendeleo endelevu barani Afrika.

Mhe. Ndejembi amesema hayo Septemba 23, 2026 jijini New York, Marekani, alipomwakilisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, katika Mkutano wa Ngazi ya Juu kuhusu kuharakisha utekelezaji wa Ajenda ya Sifuri Tatu kwa ajili ya uhai wa mama na mtoto barani Afrika.

Mkutano huo uliandaliwa na Serikali ya Tanzania kwa kushirikiana na Kituo cha Afrika cha Kudhibiti na Kuzuia Magonjwa (Africa CDC), pembezoni mwa Mkutano wa 81 wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa (UNGA).

Amesema Afrika bado inakabiliwa na kiwango kikubwa cha vifo vya kina mama na watoto licha ya hatua mbalimbali za maendeleo zilizopigwa katika sekta ya afya.

Kwa mujibu wa Mhe. Ndejembi, Afrika inachangia takribani asilimia 70 ya vifo vya kina mama duniani na karibu theluthi mbili ya vifo vya watoto walio chini ya umri wa miaka mitano, huku sehemu kubwa ya vifo hivyo ikiwa inaweza kuzuilika.

Amesema Ajenda ya Sifuri Tatu inalenga kufikia sifuri ya kujifungua nyumbani bila msaada wa mtaalamu mwenye ujuzi, sifuri ya vifo vinavyoweza kuzuilika vya mama na mtoto mchanga, na sifuri ya watoto wasiopata chanjo.

Mhe. Ndejembi amesema kufikia malengo hayo kunahitaji kuimarishwa kwa huduma za afya ya msingi, kuongezwa kwa wataalamu wenye ujuzi, kuboreshwa kwa mifumo ya rufaa, upatikanaji wa dawa na vifaa tiba muhimu, pamoja na kuhakikisha fedha zinafika katika ngazi ya utoaji huduma.

Aidha, amesema Tanzania imeendelea kujenga uzoefu katika kuimarisha huduma za afya ya msingi na huduma za dharura kwa mama na mtoto mchanga, ikiwemo mfumo wa rufaa wa kidijitali wa m-Mama, pamoja na mifumo ya ufuatiliaji wa vifo vya kina mama na watoto.

Amesema uzoefu huo unaonesha umuhimu wa kuunganisha uongozi wa kisiasa, uwekezaji na utekelezaji wenye uwajibikaji ili kuboresha matokeo ya afya na kuhakikisha huduma zinazookoa maisha zinawafikia wananchi kwa wakati.

Mhe. Ndejembi ametoa wito kwa viongozi barani Afrika kuimarisha uwajibikaji wa kisiasa, kuongeza uwekezaji katika huduma zinazookoa maisha na kuhakikisha ahadi zinazotolewa zinafanyiwa kazi hadi katika ngazi ya utekelezaji.

“Hakuna mwanamke anayepaswa kupoteza maisha kwa kukosa usafiri, damu au huduma yenye ujuzi, wala mtoto anayepaswa kupoteza maisha kwa kukosa huduma inayoweza kuokoa maisha au chanjo,” amesema.

Amesisitiza kuwa kaulimbiu “Jiongeze Tuwavushe Salama” ni wito wa kuchukua hatua kwa ajili ya kuhakikisha kila mama, mtoto mchanga, mtoto na kijana anapata fursa ya kuishi na kukua katika mazingira yenye afya bora.