saida karoli si hodari wa kuimba tu, hata kupiga ngoma zaidi ya moja ni stadi sana. naomba kusindikiza picha hii na insha ambayo mdau mmoja kanitumia hivi punde...

SEE FOR UR SELF. MIMI NIMECHOKA ......

This is what is happening to my life now - nimechoka kabisa kuamka asubuhi sana only to find out that my salary ends kwenye michango ya watu!

MICHANGO! Ah Mungu wangu weee... Nchi gani hii kila ukiamka, kila ukiwa njiani, ofisini au ukilala ni kusakamwa na michango tu?

Michangooo, michangooo, michangoo tu! Twatolewa weeeee mpaka tumepata pancha.

Hapana jamani. Hakikyanani tena sasa mmezidi.
Amka asubuhi utasikia hodi, ukifungua kuna mtoto wa jirani na kikadi kilichoburuzwa kwenye kompyuta kikiomba mchango wa "kitchen party." Toba! Unamwambia utawasiliana na baba yake anaondoka.
Upo kwenye daladala unawahi Pugu rodi kazini, unaombwa samahani na mtu akidai alikuwa na barua yako na anakupatia bila hiana. Mtumeee! Unafungua unakuta ni kakadi kengine ka mchango. Safari hii ni ka "chicken party na kameonyesha kiwango kabisaa. Kwa fasheni ya sasa ni 7,000/-.
Huyu ni wa aibu, hivyo unampa dala ukidai mbili utamtuma mtoto.

Unatoka kazini hujala chochote kwa vile 5,OOO/= ulitoa kwenye"chicken party" ambayo hata maana ya neno lenyewe hujui. Unakuta kengine nyumbani. Hako ni ka mchango wa "send off'. Jamani mwanitakani lakiniiii?

Unaoga, ghafla aja mtu na kadi, tena safari hii ni mchango wa harusi ya shemejiyo. unajikamuakamua ili usiadhirike ukweni. Unampatia kiasi kilichokuwa ada ya Sikujua shuleni.

Hapo bado kuhudhuria vikao vya shemejio vya harusi. Nako kuna ka mchango ka kila mkutanapo kanaitwa uchache au chakaza.Shemeji mtu tena si ni lazima wakukamue kamasi mwanangu?

Haiishii hapo. Unakuja ujumbe kuwa dada yake dada wa mama yako mzazi kafia Muhimbii yuko mochwari. Hapo achilia mbali bakuli la mchango utakalokuta linakungoja. Patakuwepo pia kitabu cha kujiorodhesha wanandugu na kiasi mtakachotoa.

Yallah! Michango haitoshi. sasa yabidi wale wa karibu yake mjazie ili iwezekane kukodisha "Fuso" ya kumpleka kwao Mbagala. Na huko nako ni lazima mkamuliwe tena hela ya kununulia mboga.

Unasema walau sasa napumua. Mara inatoka barua kwa wajomba zako kuwa ile arobaini ya babu ni mwezi ujao. Na unatakiwa mchango wa kununulia nyama na mchele kwa ulaji wa siku hiyo.
Kwani utakimbia jamii yenu kwa vile imekuwa ya michango?
Haya tena. Kazini nako wameanza kukukata mshahara kwa madeni uliyo nayo SACCOS. Mtoto wa jirani ambaye umemdhamini ubatizo naye aja akidai mchango wa kununulia gauni la "birthday".

Ebo! Sasa mwanangu? Utasahau mdogo wenu wa mwisho aliepigwa ritrenchi na sasa ana mtoto mchanga wa kubatiza... Utakwepa vipi usimchangie kitu kidogo atakapowahi kwako majogoo?

Afadhali usingezaliwa Kipatimo mwanangu.
Mwezi huu ni wa kuwacheza watoto. Utawaambla nini huko kwenu wakuelewe kama hukutuma mchango wa hilo tamasha ambapo mwezi uliopita mtaa wa pili alipochezwa Sikuzani watu walikula wakasaza?

Bado wana wewe kaka!
Mtoto wa kaka yako anapata komunio utamkwepaje mbele ya jamii iliyokuzunguka? Na asavali tajiri yako asingekuwa na mtoto Chuo Kikuu anayegradueti mwisho wa mwezi na keshakuletea kadi ya mchango.
Utachangia sana graduesheni ya sekondari, chekechea hata na darasa la saba, nini VETA...
Mtajiju ! Kwani nani aliyewatuma kuzaliwa Bongo? Asavali wanajeshi hawana sherehe hata wapatapo usaameja.

Utadhani sasa utapumua uendapo nyumba za ibada. Toba yaillahi! Huko Utakutana na michango ya ofisi ya paroko, mchango wa jengo na pikipiki ya shemasi - kama sio mchango wa madrasa, mchango wa majamvi msikitini ama mchango wa kofia ya imamu. Upo hapo?

Huko kijijini ndo usiseme. Kuna barabara, shule, maji, zahanati, ugeni wa DC, vyote vyadai mchango na mara nyingi hakuna risiti. Si ni jamaa zako una wasiwasi gani weye?

Umesahau mfereji wa kijiji, trekta la mshikamano, shamba la kijiji na kadhalika - vyote navyo vyataka michango; achilia mbali mchango wa damu Muhimbili! Ila asavali huu wa damu kwa vile hauhusu fedha.

Unafikia mahali unasema utapanchi hiyo michango. Ukiwaza hayo, mara anapita Katibu kata mwenyewe. Huyu anadai mchango wa mapokezi ya Waziri Mkuu au ya Mwenge utasemaje?

Unaambiwa hakuna cha huruma na mtu wala hakuna wa kutaka kujua kipato chako kabla hajakupa kadi ya mchango.
Shuleni watatuma barua kuhusu mchango wa kumuaga mwalimu mkuu. Bado michango ya tuisheni, uji wa saa nne, safari ya Serengeti na T-shirt za siku ya michezo shuleni.
Hapo usisahau redio ya shule ikikosa betri wazazi shurti mchangishwe. Mwashangaa nini, kwani hospitalini hamchangii?

Michango hii!
Sasa mtatukamua mpaka damu. Ipo ya kwaya, Saidia Simba Ishinde, usafi wa makaburi, basi la kijiji. Bado sijasema michango ya SACCOS na upatu kazini kwenu.
Enheee, halafu mama watoto anacheza mchezo. wiki hii zamu yake kutoa na mama nanihino kaja jana kukumbushia asicheleweshewe kama safari ileee...
Hujakaa sawa hodi! Wakala wa wazoa taka yuko mlangoni na kitabu chake cha risiti mkononi. Anang'aka kwamba safari hii usipotoa atakuripoti kwa mwenyekiti wa mtaa kwamba huna ushirikiano katika mambo ya kutunza mazingara.
We haya weee... kufa hatufi, lakini cha moto twakiona

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

Kuna Maoni 10 mpaka sasa

  1. Hiyo ni kama hapa HOUSTON

    ReplyDelete
  2. unashangaa nini hayo ndio yanaitwa maisha!!!!

    ReplyDelete
  3. Watanzania tuna safari ndefu sana. Tofauti na wananchi wa sehemu nyingine kama U.S., au U.K., shughuli za kijamii, kama arusi, graduation, financially zinawahusu immediate people in question. Kwa mfano, mtu akitaka kuoa, hachangishi watu, kwa sababu si lazima kijiji, na ukoo wote uje kwenye arusi. Watu wachache, tena wakati mwingine ni maharusi tu, wanakuwepo kwenye ceremony, mbele ya judge, au pastor. Na hii ni kutokana wenzetu huku wanakubali hali halisi. Mtu kama anaona hawezi kugharamia harusi kubwa, KAMWE HATATHUBUTU KUCHANGISHA WATU. Pia ikitokea msiba, life insurance inalipia gharama zote za msiba, tena hakuna kuchangishana. Tatizo watu wengi Tanzania wana ile kasumba kuwa lazima shughuli iwe na umati wa watu, hata kama wanaohusika ni masikini. Bado Tanzania jamii ina safari ndefu sana kufikia KUKUBALI HALI HALISI, NA UKWELI KUHUSU MAISHA. If you can't afford, make it simple, or just DON'T DO IT.

    ReplyDelete
  4. Ukiniambia mtoto anaenda shule nitachanga, nitauliza vitu gani anataka halafu nitachagua vya kununua na kumkabidhi, ukileta kadi ya mchango wa harusi utakuwa unanijazia pipa la taka sichangi ng'o, msibani pia huwa ninanunua vitu kama mchele, unga, maji n.k, ikifika siku ya harusi yangu nitawaalika wote mje mahali nitakapofungia ndoa

    ReplyDelete
  5. nakubaliana na mtoa maoni hapo juu, kama mtu hauna uwezo kifedha, why not make things simple? simple harusi, gradu etc. etc.

    ReplyDelete
  6. Sasa ni wakati muafaka kwa watanzania kubadilika. Hili suala lazima lianzie kwa wahusika kama wanaotaka kufunga ndoa, wahitimu na wazazi. Mtu lazima uchekeche mambo kuwa je unahitaji kitchen party? Birthday Party? nk. Tujaribu kuepuka gharama kwa kupunguza sherehe zisizo na lazima kama hali hairuhusu, na sio kupanga kutegemea michango. Lingine ni kwamba silazima kikao cha harusi kiwe na wajumbe 50 ili kufanikisha sherehe. Yote hii ni upotevu wa muda na pesa. Siku hizi watu wanajitangaza na taratibu ziko wazi, sioni sababu ya kundi la watu kukutana kila wiki kujadili marudio. Tunaumizana sana. Maa

    ReplyDelete
  7. Hiyo ndio Tanzania, Si unamuona hata Rais anavyoenda kuomba michango kila kukicha! Unategemea nini kwa anaowaongoza. Yote ni kumshukuru yeye aliekufanya ukazaliwa TZ

    ReplyDelete
  8. Michango ni utajiri pia Ukiwa sharp kuchangisha na ukawa huna huruma kwenye kukusanya michango.Inabidi uwe na roho ya paka kukusanya michango hasa ya send off za wanawake na wanaume, harusi,ubatizo na kipaimara,na jando za kutahiri watoto,graduation za watoto wakiwemo wanaomaliza chekechea ambao huvishwa majoho kama wahitimu wa chuo kikuu.Siku hizi watu wanatumia vitoto vichanga kuchangisha mamilioni ya pesa kwa kisingizio cha ubatizo wa mtoto na kusherekea kutahiriwa kwa kitoto.Kwa kweli inatisha na inatia huruma.Na wanaochangisha si watu wa chini tu utashangaa hata wabunge na mawaziri wamo. Kwa upande wa Raisi sina uhakika naomba michuzi tusameheane si kwamba namuogopa ila data zake za kuchangisha sina (GRADUATION YA MWANAWE HAKUNICHANGISHA WALA KUCHANGISHA MTU)Lakini kwa wengine hata ukitaka majina nitakupa na kuwaanika kwenye hii blog bila huruma kama walivyonidai michango bila huruma.

    Dawa ya kutochangishwa ni kugoma kuchangiwa.Ukichangiwa tu umefungulia bomba.Jirani yangu alipitisha kadi za kitchen party ya mwanawe.Wiki moja baadaye aliletewa kadi 80 zote zikitaka mchango ambao kiwango chake cha chini ni shilingi 20,000 kila kadi.Dawa ya kukomesha kuletewa kadi za michango usiombe uchangiwe.

    ReplyDelete
  9. Wabongo wanapenda makuu sana. Wanafanya arusi ya watu 1500, michango kibao. Ikiisha arusi wanakula ugali maarage yenye wadudu mwaka mzima, maana hata chakula hawaaford tena. Accounts zao na watu wao wa karibu zishakwanguliwa mpaka zimefungwa basi balaa tupu...

    Misiba inakaa siku tatu mpaka wiki, watu wanakula na kunywa bia hapo weee, hawaendi makwao. Hivi baada ya mazishi kwanini msionee huruma wafiwa mkawaachia wa-save hizo hela za kuwalisha nyie ambao hata machungu hayajawashika kihivyooo...

    Hapa naona kama ilikuja kasumba ya kuchangiana, basi watu wajitoe muhanga wasichange tuone kama hii michango itaendelea. Siku hizi hadi ubatizo wa mtoto utasikia, jamani mchango..WTF????..Fanya ubatizo wa mtoto ita family ije kula lunch, osha vyombo, call it a day...Dayyyyum!

    ReplyDelete
  10. Kweli kasumba yetu wabongo tumezoea kuomba sana. Tunapenda makuu wakati uwezo hatuna. Kila siku ukifungua email mchango wa harusi huko bongo. Hapa summer ya mwaka jana michango ilizidi. Heri huko mnachangishwa 7000 tshs. Huku wanasema kama unaishi kwenye state moja na mwenye sherehe sio chini ya $200 upewe card, ukiwa unatoka nje ya state $100 then one day kwenye fundraiser waliona hela hazitoki wakasema tutoe by professionals na kiwango kilikua sio chini ya $300.

    Halafu afadhali huko wanafanya party kweli huku wanakuchangisha ukienda kwenye sherehe norma kishenzi. Baada ya harusi wenzako wananunua nyumba. Na mara baada ya harusi mara card za thank you note na open house party au wangine wanaita warm house party ...Yaani watu hawana aibu wamewachangisha down payment ya nyumba halafu tena tuwanunulie funiture za nyumba some people are so crazy...tena jamaa wana register kabisa kwa hizi open/warm house parties.
    Inabidi tubadilike kidogo...too much of anything is harmul. Wakenya harambee zao ni ndugu kwa ndugu...lakini sisiiiiii.....mtu wa mbaliiii..mchango...mchango...mchangoo.....

    ReplyDelete

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...