Mwandishi gwiji Freddy Macha kaja na Kitabu kipya “Mpe Maneno Yake”

Huu ni mkusanyiko wa tungo zilizoandikwa kati ya 1976-2003 ndani ya nchi na jamii mbalimbali alizotembelea na kuishi mwandishi.

Haya hapa maneno ya mmoja wa wahakiki wengi walioshatamkiwa na buku.
Padre Privatus Karugendo anasema katika gazeti la “Mtanzania” tarehe 28 Machi, 2007:

“...Kwa mtu anayesoma Mwananchi Jumapili, atakuwa amevizoea visa hivi vya Freddy Macha, vyenye ucheshi na kejeli na kuficha masuala muhimu ya kijamii, hasa yale yanayowakumba watu wa hali duni. Visa hivi ni vifupi vifupi na vingine viko kwenye mtindo wa barua, hivyo havimchoshi msomaji, bali vinavunja mbavu, vinasisimua na wakati huo huo vinaumiza kichwa. Mtu atakisoma kitabu hiki akicheka kuanzia ukurasa wa kwanza hadi wa mwisho, lakini hawezi kutoka mikono mitupu.....”

Msomaji mwingine, kaandika katika Barua Pepe:

“Ni jana tu nimemaliza kusoma, Mpe maneno yake.Ni kitabu kizuri. Mimi sio msomaji sana wa vitabu,lakini visa vilivyomo vikanifanya nikimalize kwa siku chache sana,hakiboi. Safari moja huanzisha nyingine, ningefurahi kama mwandishi ana vitabu vingine vya namna ile ambavyo vinapatikana huku Bongo.”

Mhakiki Mwafika Merinyo katika toleo la Mwananchi, Mei Mosi, 2007:

“...Mpe Maneno Yake ni hazina ingine katika fasihi ya leo ya Kiswahili. Kitabu hiki kinatupa fursa ya kuyachungulia maisha kwa mtazamo tofauti na kujitazama sisi wenyewe kama binadamu ambao tusipokuwa makini tunajikuta tukisombwa na dunia ya maangamizi tuliyoiumba wenyewe lakini ambayo hatuitaki! Ni moja ya vitabu adimu ambavyo vinaweza kuzua mijadala chanya ya kimaisha; tofauti na maandishi yaliyolenga zaidi kusisimua na kumlevya msomaji kama bangi ya kijamii ya kuwatajirisha wachapishaji na waandishi na kuwaacha wasomaji na maneno matupu.... Uzuri wa mtindo wa visa uliotumiwa na mwandishi ni kwamba msomaji halazimiki kusoma kwa muda mrefu sana na kuchoshwa akili kama usomaji wa riwaya.”

Barua pepe ya Gwakisa Manase, Mei 12, 2007:
“…Niimekipenda sana na ukweli lazima niseme kuwa kina thamani ya zaidi hizo shilingi 3,000 ambazo kinauzwa dukani ! Kina mambo mengi sana...”

Mchambuzi wa Guardian, Pastory Nguvu, Mei 25, 2007:

“Napendekeza kitabu hiki kwa yeyote mwenye haja ya kujua matatizo ya kijamii. Dhamira zake zinaweza kuchangia kutatua matatizo ya ubaguzi wa mbari na rangi na unyanyasaji wa watoto yatima au wasio na mlezi.”

Bei ya kitabu kilichosanifiwa jalada na Paul Ndunguru (kurasa 188 - Sura 5) na hadithi zaidi ya Ishirini, ni nafuu yaani, shilingi 3,000 (Nje ya nchi ni dola 10).

Kinapatikana maduka ya vitabu Chuo Kikuu cha Dar es Salaam au TPH mtaa wa Samora Avenue. Ukitaka pia waweza kuwasiliana moja kwa moja na wachapishaji (E& D Limited) kupitia simu namba ( +255) 78481-8282 au (+255) 754275347. Ongea na Kitunga au Lema, mjini Dar es Salaam. Wachapishaji wa E& D Limited hawakuanza leo kutoa vitabu kabambe vinavyohamasisha fasihi ya Kiswahili. Miaka michache iliyopita walitoa kitabu mashuhuri kilichoandikwa na marehemu Profesa Chachage yaani “Makuadi wa Soko Huria.” Mwaka 2006 walichapisha mkusaniko wa kazi za mwandishi wa habari wa siku nyingi, Jenerali Ulimwengu : “Rai ya Jenerali.” Vitabu vyao vingi hutumika pia mashuleni na katika vyuo.

Kama unaishi mikoani wasiliana na wachapishaji upostiwe nakala. Kwa wanaoishi ughaibuni wakala maalum wa kitabu ataanza shughul ya mauzo kupitia London karibuni.

Kwa habari zaidi tuma barua pepe: kitoto2004@yahoo.co.uk
au Simu : (+44)7961-833040

Vile vile waweza kutuma barua pepe pia kuulizia moja kwa wachapishaji : weshilm@yahoo.co.uk

Au mailto:Aued@bol.co.tz

Usikose uhondo huu!!!

Imeandikwa na Sada Makinde
(Meneja Mahusiano wa Freddy Macha)

Usikose kusikiliza mahojiano ya Freddy Macha na muziki wake katika gazeti- redio moto moto la mtandao wa kileo la Pambazuka podcast: http://www.pambazukanews.org/
si vibaya pia ukimtembelea kijijini kwakehttp://www.freddymacha.com/

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...