Hapo chini ni nukuu toka kwenye ansadi za Bunge la Tanzania kuhusu michezo na habari kama zilivyonukuliwa na Dennis Londo na kuletwa hapa nami Fidelis Tungaraza.
Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi hii. Natumia nafasi hii pamoja na kwamba nilishawashukuru wananchi wangu wa Kinondoni, lakini naendelea kuwashukuru tena. Ninawashukuru kwa mara ya kwanza kabisa, wanamichezo wote wa Wilaya ya Kinondoni na Mkoa wa Dar es salaam, kwa jitihada zao walizofanya na kuhakikisha ninakuwa Mbunge wa Jimbo la Kinondoni.
Mheshimiwa Spika, nachukua nafasi hii tena, kumshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kwa kuanzisha au kuunda Wizara hii muhimu sana ya Habari, Utamaduni na Michezo.
Mheshimiwa Spika, nitakuwa mchoyo wa fadhila kama sitatoa shukrani ama kumpongeza Rais wetu wa Awamu ya Tatu, Mheshimiwa Benjamin William Mkapa na uongozi wote wa Awamu ya Tatu, kwa kitendo cha kuamua kujenga Uwanja Mkubwa na wa Kisasa Tanzania na ninafikiri katika Afrika, pale Dar es Salaam.
Mheshimiwa Spika, nachukua nafasi hii pia, kumpongeza tena Rais wetu Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete, kwa uamuzi wake wa kutuletea Makocha kwa ajili ya kuifundisha Timu yetu ya Taifa ya Mpira wa Miguu, tena wametoka katika nchi ambayo imeendelea sana katika mchezo wa mpira wa miguu.
Mheshimiwa Spika, hii inaonesha ni jinsi gani Serikali ya Awamu ya Nne, inavyopenda maendeleo ya michezo. Nina hakika ile azma ya Rais wetu kwamba, ifikapo mwaka 2008, basi angalau tucheze Fainali za Mataifa ya Afrika ambazo zitafanyika Ghana. Kitendo cha kumleta Kocha huyu, nina hakika kabisa, kitasaidia na kitaiwezesha Tanzania kucheza Fainali hizo.
Mheshimiwa Spika, pamoja na azma hiyo nzuri ya Serikali yetu, pamoja na azma nzuri ya Rais wetu, lakini mchezo wa mpira umekumbwa na migogoro mingi sana na kama Wizara hii haitakuwa makini, nina hakika azma ya Rais, haiwezi kufikiwa. Migogoro katika vyama vya michezo, migogoro katika vilabu imekuwa ni mikubwa sana.
Mheshimiwa Spika, chanzo kikubwa cha migogoro hiyo, watendaji wa Wizara yetu wanahusika sana. Nampongeza sana Waziri wa Wizara hiyo aliyepita, Mheshimiwa Prof. Juma A. Kapuya na Naibu wake, Mheshimiwa Mudhihir M. Mudhihir, kwa kazi nzuri waliyoifanya kipindi kile, lakini walikwamishwa sana na watendaji katika Wizara ile.
Mheshimiwa Spika, mahali ambapo kuna migogoro, hapawezi kuwa na maendeleo. Hiyo migogoro ndiyo ilitufikisha hapa tulipo hivi sasa. Mheshimiwa Capt. John D. Komba, alizungumzia miaka ya 1970 na alionesha jinsi gani Tanzania tulipiga hatua katika michezo, mchezo wa mpira wa miguu lakini hata michezo mingine. Lakini kuanzia miaka ya 1990 � 1995 mpaka hivi sasa, kwa kweli tumerudi nyuma sana katika michezo, lakini kubwa ni migogoro. Migogoro hii, watendaji wetu wamekuwa wakihusika kwa namna moja ama nyingine, kuisababisha itokee ama kuifanya iendelee kuwepo.
Mheshimiwa Spika, huwezi kuzungumza maendeleo ya mchezo wa mpira wa miguu Tanzania, ukakosa kuitaja Simba ama ukakosa kuitaja Yanga. Panapotokea matatizo ama migogoro katika vyama hivyo viwili, basi ujue hata Timu ya Taifa, haitafanya vizuri kwa sababu asilimia kubwa ya wachezaji ambao tunawatumia wanatoka katika vilabu hivyo.
Mheshimiwa Spika, lakini migogoro imeendelea kuwepo na naomba ninukuu baadhi ya Kanuni zilizounda Baraza la Michezo la Taifa na nina hakika kama kweli watendaji wetu wangekuwa wanazifuata, sidhani kama tungefika hapa tulipo. Tunataka maendeleo, tunataka mabadiliko, lakini mabadiliko ni lazima yaendane na sheria, taratibu na kanuni zilizopo. Leo katika Klabu ya Yanga, kuna mvutano mkubwa sana kati ya pande mbili na bahati nzuri na tunamshukuru Mwenyezi Mungu kwamba, Watanzania wote tunaongea Kiswahili. Lakini kama tungekuwa tunaongea lugha tofauti tofauti, basi sasa hivi nafikiri tungekuwa tunasema mengine katika Vilabu hivyo, tungeuwana au kutwa tungekuwa tunapigana.
Mheshimiwa Spika, Yanga wana mgogoro katika kuboresha Young African Sports Club, lipo kundi liliamua kwamba, hapana twende kibiashara kwa maana ya kuanzisha Kampuni. Sasa Young Sports Club iwe Kampuni. Lakini kwa mujibu wa Kanuni zetu za Baraza, zinapingana na hilo.
Mheshimiwa Spika, ninukuu Kanuni za Baraza la Michezo, Sheria ya Baraza la Michezo ya mwaka 1967, ikafanyiwa marekebisho mwaka 1971. Utaratibu wa kusajili vyama vya michezo, kipengele cha sita. Naomba kunukuu �Chama cha Mchezo wowote, hakitaruhusiwa kuendesha shughuli za michezo bila kusajiliwa na Msajili wa Vyama vya Michezo. Aidha, chama kilichosajiliwa, hakiruhusiwi kuwa na ushirikiano wa kimichezo na chama chochote, ambacho hakijasajiliwa.�
Mheshimiwa Spika, juzi niliuliza swali kati ya Yanga mbili hizi, Yanga Kampuni na Young African Sports Club, Naibu Waziri alinijibu kwamba, Yanga Kampuni imesajiliwa chini ya Sheria Na. 212 ya Msajili wa Makampuni. Yanga Sports Club imesajiliwa chini ya Sheria ya Msajili wa Vyama vya Michezo. Kwa mujibu wa kanini hizi za Baraza ni kwamba, ndiyo ambayo inatambulika. Lakini kwa sababu ni mpango mzuri wa kuiondoa Yanga pale ilipo, kuipeleka sasa kwenye mahali ambapo watajipatia kipato kizuri, kuifanya iwe kampuni, kuiendesha kisasa. Hapa tunakingana sasa na kanuni ya Baraza. Nawaomba viongozi wa Baraza, wazipitie na kuzitafsiri vizuri hizi kanuni kabla ya kuanza kuingia kwenye mambo mengine ya maendeleo.
Mheshimiwa Spika, tunao mpango hivi sasa labda tunataka soka la kulipwa, tunao mpango wa kuvifanya vilabu vyetu viwe kampuni lakini tunapingana na sheria na ndiyo maana wakati wa kuchangia hotuba ya Mheshimiwa Rais, aliyoitoa tarehe 30 Desemba, nilisema Serikali iangalie uwezekano wa kuzirekebisha kama si kufuta kabisa Sheria hizi za Baraza la Michezo.
Mheshimiwa Spika, lakini kanuni hizo hizo tena kwenye marekebisho ya Katiba, kwa sababu huwezi kusajili chama cha mchezo wa miguu pale, msajili ni lazima uwe na Katiba. Marekebisho ya Katiba unapotaka kuyafanya, kanuni inaelekeza, naomba kunukuu: �Chama chochote kitakachofanya mabadiliko ya jina, anuani, madhumuni au kifungu chochote cha Katiba yake, kitatakiwa kupata idhini kwa kupeleka maombi kwa msajili kupitia msajili msaidizi kwa kujaza fomu za maombi.� Zimetajwa hizo fomu. Sasa kuifanya Yanga iwe kampuni na itambulike, ni lazima hizi sheria tuzifuate. Lakini tukitaka kwenda tunavyokwenda hivi sasa, ndio maana tunazaa migogoro hii. Wizara imeshindwa kuwa wazi tangu mapema, kuelekeza ama kushauri kuhusu suala hili la Yanga, ndio tumefika hapa tulipo.
Mheshimiwa Spika, naiomba Wizara sasa, bahati nzuri nimeandika, wanieleze jitihada ambazo watazifanya kwa makusudi, kuhakikisha mgogoro huu wa Yanga Asili na Yanga Kampuni unakwisha.Mheshimiwa Spika, sambamba na hilo, upo mgogoro katika Club ya Simba, ambao nao pia umechangiwa kwa kiasi kikubwa na Watendaji wa Wizara. Mara baada ya Msajili kwenda kufanya uhakiki wa wachama wa Simba, kuanzia pale ndipo zogo lilipotokea. Sasa ili tuendane na kauli ya Mheshimiwa Rais ya kuhakikisha Tanzania inacheza Fainali za Afrika mwaka 2008, ili maendeleo yapatikane, ni lazima tuhakikishe migogoro hii, tunaiondoa.
Mheshimiwa Spika, nina hakika kabisa Mheshimiwa Waziri ni mtunzi mzuri wa nyimbo, lakini nina hakika pia ni mchezaji mzuri sana, alikuwa zamani akichezea Timu ya Kikwajuni. Centre Forward mzuri sana. Mheshimiwa Joel N. Bendera, amecheza Korogwe Nyota, anaujua mpira vizuri sana. Nina hakika mgogoro huu katika kipindi kifupi wataumaliza ili tuweze kwendana na ahadi ya Rais.
Mheshimiwa Spika, sambamba na kurudisha michezo shuleni, ningeiomba Wizara ihakikishe tunawapa angalau mafunzo ya awali, walimu wa shule za msingi na walimu wa shule za sekondari, angalau wajue kuwafundisha wale watoto wetu pale shuleni mchezo huu wa mpira wa miguu. Kuwe na kozi fupi fupi kwa walimu ili ziweze kuwasaidia.
Mheshimiwa Spika, nazungumzia vyombo vya habari. Nimekuwa nikisoma magazeti na kwa kweli sasa inabidi hata nisiyasome, yapo baadhi ya magazeti yamekuwa yakihoji na kueleza mgogoro wa suala la NSSF na Quality Group, juu ya mikataba ya ununuzi wa yale majengo. Hilo limezungumzwa sana kwenye vyombo vya habari na baadhi ya vyombo ndivyo ambavyo wamebebea bango suala hilo, yaani ndivyo ambavyo vinaandika habari hizo.
Magazeti yote ya IPP, huwa yanaandika habari hizo kila kukicha. Sasa ningependa katika majumuisho, mnifahamishe yanayoandikwa na magazeti yale, yako sawa sawa? Kama yako sawa sawa, Serikali inachukua hatua gani na kama yanayoandikwa siyo sawa sawa, basi pia nitaomba tamko la Wizara, ni hatua gani mnachukua kwa sababu kama yatakuwa siyo sahihi, ina maana wanatupotosha? Nitaomba maelezo hayo.
Mheshimiwa Spika, nimalizie kwa kuwapongeza wandaaji wa Mashindano ya Miss Tanzania, pamoja na wandaaji wa Mashindano ya Miss Utalii. Niwapongeze hasa wa Utalii na nichukue nafasi hii kuipongeza Serikali kwa kuhakikisha kwamba, mashindano yale ya Utalii Duniani yalifanyika hapa Tanzania na yalifanyika kwa ufanisi mkubwa sana, baada ya Serikali kuamua kuingilia na kusimamia Mashindano yale. Naipongeza sana Serikali kwa sababu kinyume cha hivyo, Tanzania tungeweza kupata aibu.
Mheshimiwa Spika, nizungumzie suala la makocha, tayari tunao makocha wa Kigeni ambao wataifundisha Timu yetu ya Taifa, lakini bado tunataka makocha kwa ajili ya timu zetu za mitaani. Naiomba Wizara iandae utaratibu wa makusudi kabisa wa kuhakikisha vijana wetu wanapata mafunzo ya ukocha hapa nyumbani au kwa kupelekwa nje.


Fide, get a job, this is too much in da blog.
ReplyDeleteWhat r u down for?
Katty.
What the Hell is he talking about?
ReplyDeleteNadhani hizi zitakuwa PUMBA za Idd Azan, ni mmoja kati ya wabunge mizigo katika Bunge la Jamhuri ya Muungano! How on earth can a man of Idd Azan manner become an MP? God rescue our country Tanzania!
ReplyDeletehuyu jamaa ameanza kujichomeka kwenye blogu yetu tukufu.bro najua huwezi kurusha comment zangu lakini kaa ukijua fide ni fitina!utanambia one day
ReplyDeleteAcheni uzandiki usiokuwa na msingi. Kuna suala la kujadiliwa humo. Nadhani Ndg. Fide ana jambo la muhmu sana katika waraka aliotuma, kwani kuna mgogoro mkubwa wa kisheria ambao wengine tunajaribu kutouangalia. Ebu jaribuni kusoma tena waraka wote harafu ndio mtoe comments.
ReplyDeleteBw. Londo na Tungaraza,
ReplyDeleteKwanza napenda kutoa shukrani zangu za dhati, walau kwa kutoa hizo ansard za Bunge. Tumejaribu leo kuongea na wahusika wizarani na kwenye baraza la michezo la Taifa (BMT), na wenyewe pia wameshtushwa sana na ansard hizo, wameniahidi kufuatilia majibu ya Waziri, lakini kubwa walilokiri wanakubaliana nanyi kuwa kuna mapungufu mengi ya kisheria kati ya usajili wa vyama/vilabu vya michezo vya hiyari na vilabu/vyama vya mpira wa kulipwa.
Wewe anony wa 4:19:00 ndiye mwenye FITNA. Huyo jamaa ametuwekea hizo ansard ambazo wengi hatukuziona, kimsingi ametusaidia kufungua macho, sasa hiyo fitna ipo wapi?
ReplyDeleteMtu mwenye fitna kwa kawaida hajibu hoja, ila anaangalia nani ametoa hoja...ni uvivu wa kufikiri tu.
Good boys for wonderful job. Most of us was unaware that some of you use our session ansard to build you arguments in the public discussion. This will make some of us even more careful...Thank you Michuzi and keep it up.
ReplyDeletemichu nisalimie huyo Fide na mwambie aendelee kutuletea habari ndio uhuru wa kutoa maoni wala hamna wasi wasi wa kuhujumiwa hapa wewe ni tarishi. Wenye mawazo mafupi ndio wanaona kila mtu akitoa habari yake hapo basi kakosea na ndio desturi ya watu wengi waliofirisika kimawazo dunia ya leo uhuru wa kutoa mawazo uko wazi na ndio maana ya blog zetu hizi acheni mwazo ya enzi hizo za giza . Nipe email ya Fide michu.
ReplyDeleteYANGA KUWA KAMPUNI: KWA MISINGI IPI NA MASLAHI YA NANI?
ReplyDeleteMgogoro wa Yanga ni moja ya mambo ambayo nimekuwa nikiyafuatilia kwa karibu sana tangu ulipoibuka wiki chache zilizopita. Sikuwa na sababu nyingine ya kufuatilia mgogoro huo, isipokuwa ni kuangalia kwa makini chanzo cha mgogoro huo hasa kwa kuwa ulikuwa ukimuhusisha Bw. Manji ambaye katika miaka ya karibuni amekuwa habari, mjadala, gumzo na soga kubwa katika vyombo vyetu vya habari.
Ikumbukwe kuwa Manji alisitisha ufadhili wake Septemba 20. Seke seke la mgogoro huo lilianza tarehe 8 Oktoba mwaka huu pale Bw. Yusuf Manji alipotangaza kuacha ufadhili wake Yanga kwa sababu kuu moja nayo ni kushauriwa na familia yake na marafiki zake. (Tanzania Daima, 11/10/2007)
La kushangaza hapa ni kuwa siku moja baada ya tamko lake Bw. Manji, Oktoba 9 alifunga safari mpaka kwenye makutano ya mtaa wa Twiga na Jangwani yalipo makao makuu ya klabu ya Yanga. Pengine hilo siyo tatizo kwani naye kama mwanachama mwingine yeyote wa Yanga ana haki ya kufika mahali hapo, tatizo ni Bw. Manji kuitisha mkutano wa wazee na kuanza kurusha shutuma dhidi ya uongozi na kubadilisha sababu mbali ya ile aliyouelezea UMMA awali kwa maandishi ikiwemo ucheleweshaji wa KATIBA mpya, na kutoa masharti ya nini kifanyike ili abadilishe maamuzi yake mojawapo ni kubadilisha timu kuwa kampuni, hili lilikuwa ni kosa. Pamoja na hilo, Bw. Manji kutoa dau la milioni 50, 10 kwa ajili ya 'wazee' (Ukipenda unaweza kuiita rushwa) na 40 kwa ajili ya maandalizi ya timu, huku akitoa sharti kuwa ni lazima ziwe chini ya katibu mkuu Bw. Kisasa bila ya kufuata utaratibu na katiba ya klabu na kanuni za masuala ya fedha za klabu, hili lilikuwa kosa jingine. Hali hii ndiyo iliyopelekea mmoja wa 'wazee' wa Yanga kuhoji uhalali wa Manji kuwapangia jinsi ya kuendesha klabu kama alivyonukuliwa "Manji hawezi kutuchagulia wanachama au viongozi anaowataka huku ni kuvuka mipaka, yeye mwisho wake ni ufadhili na siyo kuchagua viongozi". (Tanzania Daima, 12/10/2007)
Kwa mujibu wa uchambuzi, mgogoro mzima ni kati ya uongozi halali wa Bw. Madega na mfadhili wa timu Bw. Manji. Jambo linalovuta hisia zangu hapa ni kuwa wakati Bw. Manji anautuhumu uongozi kwa kuchelewesha "utekelezaji wa vitendo" juu ya rasimu ya muafaka ikiwemo katiba mpya ambayo ingepelekea Yanga kuwa kampuni; Bw. Madega anapinga wazo la Yanga kuwa kampuni bila ya kufanyia marekebisho kadhaa muhimu kwa kulinda maslahi ya wengi ambao ni wanachama wa klabu hiyo kongwe.
Kwa kuwa Bw. Madega alionyesha wasiwasi wake waziwazi kwa wahariri wa habari tarehe 11/10/2007 juu ya suala zima la ujio wa Bw. Manji Jangwani na uhamishaji wa timu ya Yanga kwenda kuwa kampuni, ambako kutapelekea moja kwa moja Bw. Manji kuwa ndiyo mmiliki mkuu. Nilitegemea magazeti mengi yangeonyesha umakini wa Bw. Madega na hoja zake za msingi kama alivyoainisha. Kinyume chake, ni gazeti moja tu la kila siku ambalo liliandika kwa kirefu hoja za msingi za uongozi kukataa masharti ya mfadhili Bw. Manji. Zaidi ya hapo vyombo vingi vya habari vilikuza zaidi kauli ya Madega kuwa wazee wa Yanga wanatumiwa kwa njaa zao.
Pengine suala la muhimu hapa ni kujadili wasiwasi wa Bw. Madega juu ya kuwekwa rehani kwa maslahi ya wanachama wengi, ambao pengine kwa kutojua sheria au kwa makusudi (Ikumbukwe Bw. Madega yeye ni mwanasheria na wa wakili wa mahakama kuu) Kwa mujibu wa Bw. Madega kupitisha rasimu na kuwa katiba bila maerekebisho ya msingi kungeweza kuhatarisha uhai wa klabu na maslahi ya wanachama wengi; ameahinisha haya kama alivyonukuliwa na Tanzania Daima la 11/10/2007 kama ifuatavyo:
(1) Katika kifungu cha 39(2) (d) cha Katiba ya Yanga kinauagiza Mkutano Mkuu wa Uchaguzi kuchagua wanachama wawili ambao si miongoni mwa viongozi wa klabu kuwa wajumbe wa bodi ya wakurugenzi wa kampuni kwa ajili ya kuwakilisha masilahi ya klabu kwenye kampuni.
(2) Kamati iligundua kifungu hiki kina makosa makubwa mawili, kwanza makosa yameshafanyika kuwa wanachama wawili hawakuchaguliwa kwenye mkutano wa uchaguzi, hivyo bodi ya kampuni hata kama itaundwa basi wawakilishi wa wanachama ndani ya kampuni hawatakuwepo, hivyo bodi ya kampuni kuifanya iwe batili.
Lakini kubwa naloliona hapa, ni kukosekana kwa uwakilishi wa dhahiri wa klabu katika bodi ya kampuni, kwani hisa ni mali ya mwanahisa na siyo mali ya klabu. Hivyo basi hata mwanahisa aliyepoteza sifa za kuwa mwanachama wa Yanga, bado anaweza kuendelea kumiliki hisa zake kimsingi. Hili huenda likapelekea wanachama wawili watakaoingia kwenye bodi ya wakurugenzi, kuwakilisha maslahi yao kama wanahisa na siyo maslahi ya klabu.
Ikumbukwe kuwa hisa zinarithishwa, lakini haki ya uanachama inapotea pale mtu anapopoteza sifa za kuwa mwanachama, ikiwemo kifo. Katika hili, kama katiba itaenda jinsi ilivyo tusishangae siku moja mwenye hisa nyingi akawa tajiri asiyependa michezo kabisa, achilia mbali kutokuwa mwanachama hata wa klabu hiyo. Kuiepusha Yanga na vilabu vingine na balaa hili, maslahi ya klabu katika kampuni iwayo yoyote ile, ni lazima yasimamiwe na viongozi waliochaguliwa na kimsingi ndio wasimamizi wakuu wa mali zote za klabu, ikiwemo maslahi ya wanachama. Na hili ni lazima litamkwe waziwazi kwenye katiba ya klabu kampuni, ni jinsi gani viongozi wa kuchaguliwa watashirikishwa kwenye bodi ya kampuni.
Pamoja na hayo wasiwasi mwingine ambao Bw. Madega ameuelezea waziwazi bila kificho ni kuwa:
(3) Kifungu cha 39 (2) (f) cha katiba kinataka klabu na kampuni kuingia katika makubaliano ya kimaandishi ya uendeshaji wa timu na kwa niaba ya klabu makubaliano hayo yatasainiwa na Katibu Mkuu wa klabu.
Udhaifu wa kipengele hiki ni pale katibu mkuu pekee ndiye anayetakiwa kusaini makubaliano. Swali, je, ni kwa nini kwa taasisi kubwa kama Yanga mikataba yake isainiwe na katibu mkuu peke yake?
(4) Kifungu cha 39(2)(b) kinamtambua mfadhili wa klabu kwa mujibu wa rasimu ya muafaka wa Yanga uliofikiwa na wanaYanga tarehe 22/06/2006 na ukiangalia rasimu ya muafaka, mfadhili ametambuliwa kama Yusuph Manji na si kampuni.
Hapa pia kuna kasoro kubwa ya kikatiba kwani haipaswi kwa jina la mtu binafsi (natural person) kuingia katika katiba kwani katiba inaundwa ili iishi muda mrefu, hivyo unapotambua jina la mtu binafsi kwenye katiba, maana yake umetengeneza katiba ya kuishi chini ya saa moja, kwani wakati wowote mwanadamu anaweza kupoteza uhai.
(5) Kifungu cha (39)(2)(c) ni kuwa klabu itamiliki hisa zilizo sawa na asilimia hamsini na moja (51%). Kama ni kweli klabu inamiliki hisa 51%, maana yake klabu ndiyo yenye hisa kubwa ndani ya kampuni, hivyo ni wazi kuwa kiongozi wa kampuni anapaswa kuwa kiongozi wa klabu ili kulinda masilahi ya hisa zake nyingi.
(6) Tofauti na mfumo uliopo sasa, klabu haina mwakilishi kwenye bodi ya kampuni. Hivyo hapo mbele utakuja kuona si kweli kwamba klabu inamiliki hisa 51% za kampuni.
Hayo ndiyo mapungufu ambayo uongozi wa Yanga umeyaona kwenye katiba na hivyo kufanya utekelezaji wa suala zima kuwa linataka muda.
(a) Muafaka.
Baada ya kupitia hati ya muafaka kwa kina, kamati iligundua yafuatayo:
(1) Kampuni ya Yanga itakuwa na hisa ya sh 6,000,000 (milioni sita).
- Hisa moja itauzwa kwa sh 1,000 (elfu moja) tu, hivyo kufanya mtaji wa kampuni kuwa ni sh 6,000,000,000 (bilioni sita) endapo hisa zote zitauzwa.
- Kifungu cha 3.2.2 cha rasimu ya muafaka kinaipa klabu hisa saba tu kati ya hisa 6,000,000. Thamani ya hisa saba ni sawa na shilingi 7,000. Hii ndiyo thamani ya kampuni kwenye klabu.
Hisa 3,059,993 zenye thamani ya shilingi 3,09,993,000 zitatengwa pembeni, zitatakiwa klabu kuzinunua ndani ya miaka miwili na klabu ikishindwa, basi hisa hizo zitauzwa kwa watu wengine.
Hivi tujiulize, klabu itapata wapi shilingi bilioni tatu ndani ya miaka miwili ili iweze kununua hisa?
Na asilimia 51 ya hisa zote za kampuni bali itakuwa na hisa saba tu zenye thamani ya shilingi 7000. Rasimu ya muafaka inasema kwamba mfadhili atamnunulia kila mwanachama hisa 10 zenye thamani ya shilingi 10,000.
Kutokana na mgawanyiko wa hisa ulivyo kwenye rasimu (7) tu, wakati mwanachama ana hisa 10 zenye thamani ya shilingi 10,000 kwa maana hiyo mwanachama mmoja ana thamani kubwa ndani ya kampuni kuliko ndani ya klabu yenyewe, ambayo thamani yake ni shilingi 7,000 na ndiyo maana klabu haikutakiwa kuwa na mwakilishi kwenye bodi ya kampuni kwa kuwa haina hisa nyingi kwenye kampuni.
Tujaribu kuangalia lengo la kununulia wanachama hisa, je ni kuwa anawapenda?, kitendo cha kuwahamisha kutoka klabu kwenda kampuni pamoja na timu si kuiua klabu? hapa suala la kuzingatiwa ni kuwa hakutakuwa na demokrasia nyingine ya kura moja mtu mmoja bali ni HISA MOJA KURA MOJA.
Na hili likifanyika mwenye hisa nyingi ndio mwenye maamuzi yote...hivi huko ndiko wanachama wa Yanga wanakotaka kwenda?
Vyombo vya habari
Vyombo vya habari vina dhamana kubwa ya kuhabarisha umma juu ya nini kinajiri, kama wengi wanavyopenda kusema habari ni haki ya kila msomaji. Pamoja na majukumu makubwa na heshima iliyoshiba juu ya vyombo vyetu vya habari, lakini inasikitisha kuwa vyombo vya habari vingi (si vyote) vinapoamua kuuza haki hiyo kwa wenye 'dau' zito. Migogoro katika vilabu vyetu kwa kiasi kikubwa inachochewa na ubinafsi wa wananchama wanaoendekeza njaa zao lakini pia imekuwa ikishadidiwa kwa kiwango kikubwa na vyombo vyetu vya habari. Sikemei umuhimu wa vyombo vya habari kutangaza kauli za uchochezi kama zilivyo, la hasha! nalotaka kusema hapa ni kuwa viripoti kwa nia ya kuujulisha umma, kuuonesha nini kinafanyika na kuutahadharisha na sio kuunga mkono uchochezi huo.
Aidha vyombo vyetu vya habari havina ruhusa ya kutetea uozo, maovu na uvunjifu wa amani katika vilabu vya michezo. Kutoa habari nusu nusu sio tu kunamnyima msomaji haki yake ya msingi, lakini pia kunakuwa kumesaidia kuchochea fujo zisizo na msingi. Ni ombi langu kuwa wakati umefika, kuanza kuheshimu wasomaji wetu/wenu kwa kuwapa kile kinachojiri kukiwa na habari ambazo zina uwiano, badala ya kuangalia nani mwenye dau, au habari gani itauza.
Dennis Londo
Japo kuwa mimi nashabikia klabu ya Yanga iwe kampuni, lakini nimefarijika na jinsi ya ujengaji hoja kwa mtundiko wa Fide. Kwa maelezo kutoka kwa Mbunge wa Kinondoni kama ambavyo yamepatikana katika Hansards za Bunge ni kweli kuna haja ya sisi wanamichezo na wapenda maendeleo tuangalie kwa kina ni wapi sheria zinagongana na kusababisha kuwepo kwa migogoro isiyokwisha kila siku.
ReplyDeleteKwa haraka haraka, kama kwa mujibu wa Mh. Azzan tatizo lililopo kwenye sheria nadhani ni vema hatua zifaazo zichukuliwe kuepusha migogoro isijitokeze tena au kuipunguza.
Lakini hata hivyo, kwa Vilabu kama Yanga au Simba, kwa vyovyote vile havina budi fast track process ya kuanzisha kampuni ili viendelee mbele. Ulimwengu wa sasa Football ni biashara na wala asikudanye mtu. Leo matajiri wengi duniani wanapigana vikumbo kununua vilabu vilivyoko katika Premier League ya Uingereza, kwa sababu ni biashara inayolipa.
Ninaimani kuwa mabadiliko katika michezo inaweza kuleta pia impact katika uchumi wa nchi. Fikiria, endapo klabu zote za Ligi ziwe na rasilimali ikiwemo viwanja vyao binasfi itakuwaje?
Vyovyote itakavyo kuwa ni lazima tubadilike ili tupate maendeleo.
'UCHUMI TUNAO LAKINI TUMEUKALIA'