
Marekani yaipa shavu Bongo kwa uhuru wa habari
Ubalozi wa Marekani umetoa pongezi za dhati kwa Tanzania kufanikiwa kupanda chati kwenye kiashiria cha uhuru wa vyombo vya habari duniani (World Press Freedom Index) cha hivi karibuni cha Waandishi Wasio na Mipaka (Reporters without Borders).
Kupanda huko kutoka nafasi ya 88 mpaka ya 55 mwaka huu, kwenye orodha hiyo, ni ishara ya juhudi za Rais Jakaya Kikwete kujenga mazingira bora ya uandishi wa habari kuhusu masuala yaliyo kwenye kiini cha jamii iliyo huru na wazi - ikiwa ni pamoja na masuala ya rushwa - bila ya kuhofu kuadhibiwa.
Taarifa ya ubalozi ilotolewa jana imemnukuu Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, Condoleezza Rice, pale alipotamka kwamba "vyombo vya habari vilivyo huru na hai ni nguzo muhimu sana ya demokrasia. Hii ni sauti ya wananchi wanaotoa maoni yao na dukuduku zao kwa uongozi wa taifa".
Taarifa hiyo pia ilimnukuu Rais Kikwete alivyosema hivi karibuni, "uhai wa vyombo vya habari na upana wa maoni yake – ukiwemo uwezo wa kukosoa sera za serikali – ni kipimo cha kupima nguvu za taasisi za kidemokrasia za nchi husika".
Imesema nchini Marekani, vyombo vya habari vimekuwa ni chombo muhimu katika kuendeleza majadiliano, kulinda uhuru, na kufichua vitendo vya rushwa katika mihimili yote ya serikali. Vyombo vya habari vya Tanzania vinafanya juhudi kutimiza wajibu huo hapa nchini, na Rais Kikwete anastahili pongezi kwa kuhamasisha mwelekeo huu.
"Marekani itaendelea kutoa misaada ya kiufundi, ikiwa ni pamoja na mafunzo katika uandishi wa habari za uchunguzi, ili kuunga mkono juhudi za Rais Kikwete kuimarisha zaidi uhuru wa vyombo vya habari nchini Tanzania.
"Bado kuna mambo mengi yanayoweza na yanayohitajika kufanywa ili kujenga mazingira huru kabisa ya uandishi wa habari za uchunguzi. Sheria mpya ya kupambana na kuzuia rushwa isitumiwe kuzuia vyombo vya habari kuchunguza vitendo vya rushwa.
"Taasisi ya Kupambana na Kuzuia Rushwa (TAKUKURU) haina budi kufanya kazi kama taasisi inayojitegemea, na maafisa wanaojihusisha na vitendo vya rushwa kubwa ni lazima wafikishwe mbele ya vyombo vya sheria.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...