Ndugu Watanzania wenzangu,

Yanga imo njiani kuuzwa. Bei ya yanga imeshapangwa ni shilingi bilioni 3 na wanunuzi wa Yanga washajulikana. nani anajua pengine kesho zamu ya Simba kuuzwa.

Cha msingi hapa si kuuzwa kwa timu tu. Cha msingi ni kwa nini timu inataka kuuzwa? jinsi gani timu inataka kuuzwa? na kwa faida ya nani?

Serikali na Bunge la Awamu ya Nne imeonyesha ushabiki wake katika fani ya michezo. Imeonyesha hivyo kwa Rais na watendaji wengine wa Serikali walivyoshiriki katika kuiimarisha timu ya taifa. Bunge limeonyesha jinsi linavyothamini kandanda kwa kuruhusu kwa mara ya kwanza timu kuingilia kikao cha Bunge. Pia kwa mchango wa mamilioni ya shilingi iliyochangwa na wabunge kama motisha kwa wachezaji wa timu ya taifa.

Yanga na Simba siyo tu ni timu za kandanda bali pia ni moja ya vitambulisho vya taifa letu. Yanga pia ni ina asili ya kisiasa ya Tanzania. Kama hili limesahaulika basi yapasa likumbukwe na kutiliwa maanani.

Muhidin na wengine wote ambao mna nafasi ya kuweza kuwafikia wenye nguvu ya kuweza kuisitisha nia hii dhalimu nawaombeni mfanye hivyo haraka kabla mambo hayajaharibika.
Namuomba Waziri wa Habari, Utamaduni na Michezo, Muheshimiwa Mohamed Seif Hatibu achukue hatua za haraka kusitisha mizengwe ya nia ya kuiuza timu ya Yanga.

Mtanzania mwenzenu katika michezo,

Fidelis M Tungaraza.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

Kuna Maoni 23 mpaka sasa

  1. Tungaraza na watanzania wenzangu,
    Hii dhambi ya kuuza kila kitu tutauza mpaka mama na watoto wetu.

    Biashara ya utumwa ilianza kirahisi sana kwa watawala kuuza mateka wa vita na wahalifu. Walipokwisha na biashara imenoga, kilichotokeaa ndo tunacholia mpaka leo. Historia ni rahisi sana kujirudia.

    Kuna kibepari sijui hiki ni kikabaila kinainunua Tanzania sasa hivi huku tukimwangalia. Huyu jamaa ni mwaribifu wala si mtakia mema watanzania. Pesa anazonunulia ni alizoiba toka katika majasho ya watanzania.

    Sipingi wawekezaji ila huyu maslahi ya wawekwezwaji hayapo. Bilioni 3 ni nini wakati serikali imeshamjengea uwanja mpya?

    ReplyDelete
  2. Kaka Fidee!! Noana chozi na damu ya kijani inakububujika, pole! Maoni yangu ni kama hivi: Timu kuuzwa siyo mbaya-imeshaonekana miaka ya nyuma pale kila mtu mwenye hela ndio alimiliki hiyo timu. Vurugu za wanachama ndizo zilizowakimbiza 'wahisani' Hii ilidhihirisha jinsi gani kulivyokuwa na Menejiment isiyo yakinifu na miundombinu. Mda wa kuweka menejimenti ya kisasa ambayo Wanachama wa yanga watabakia na haki Kwa kufanya yafuatayo
    Yanga iwe incoporated as a public company with shares derived from Long time members!
    Wawe na Share mfano...51%Wanachama wa zamani miaka 20+ 20 shares @ TShs.1000.00 and consequently miaka 10,5,2,1 all @ TShs.1000.00
    Vilevile waunde baraza mbili za mashare holders wanachama na sio wanachama ambazo zitakuwa na madaraka kwenye bodi ya menejiment,
    wanachama wakiwa na usemi mkuu.
    Halafu wauze share zilizobaki asilimia 49% kwa watu binafsi au makampuni au kampuni ambazo zitaweka miundombinu zitakazo endeleza soka na 'KANDAMBILI"

    ReplyDelete
  3. kusema kuwa Yanga na Simba ni "vitambulisho vya taifa letu" nafikiri ni ushabiki uliovuka mpaka.
    Mimi sikubaliani kuwa eti yanga na simba ni alama za Taifa-bali ni kampuni za michezo, kama vile Manchester, au Arsenal-sasa kama inata kuuzwa wacha iuzwe, jamani serikali mnataka ianze kuingilia timu moja moja moja?? Kuna timu ngapi zimekufa hamjawahi kuomba serikali ingilie kati??Ingekuwa Taifa Stars inauzwa, basi hapo ningekuunga mkono. acha wauze tu.........

    ReplyDelete
  4. Ndugu Tungaraza suala la Yanga kuuzwa lisikuumize kichwa,jua ni jambo la maendeleo.Tena ikiuzwa hakika italeta mapinduzi ya hali ya juu kisoka nchini kwani nina uhakika timu itapata faida kubwa sana kwani itakua inajiendesha kibiashara zaidi kuliko ilivyo sasa kama shamba la bibi kila anayetaka hela ya kula au umaarufu basi anazikimbilia timu hizi,fikiria wakitengeneza fulana,jezi,kofia,chupi,kanga,vitenge,majarida,picha za wachezaji,kalenda,'diary' mataulo,'tracksuits', uwanja wao wenyewe ukiboreshwa,bar na cafee,pia kandambili,mifuko ya aina mbalimbali vikatengenezwa,ndugu hivi vyote vitauzika hapa Tanzania hapo hujajumuisha wadhamini wengine.Ilivyo sasa kamwe haya mapinduzi ya kibiashara hayawezi kufanikiwa. Mtaishia kugombana tu.Tubadilike jamani,hawa kina Mzimba na shikamoo wengine hawana jipya katika zama hizi.Huyo mtu kama ni kweli atawekeza huo mshiko ni kwamba amechungulia soko vizuri sana na baada ya miaka 3 au 4 ataanza kuogelea kwenye faida tu,hapo sasa anaipeleka Yanga DSE. We utaki kina Kiemba,Nsajigwa,Mwaikimba, Haroub Canna,watembelee ma 'convertable' mjini? Kama Michu naombea litokee hilo japo wengine watapinga lakini kwa hili kwangu ni kheri tu.Ila atarogwa mtu hapo jamaa hao wajiadhari ze wazees ni wabayaz nduju Tungaraza(mwalimu wangu mmoja enzi hizo nasoma shule ya msingi Mlimani sijui yungalipo? We ni nduguye msalimie sana... Rui frm Kansas

    ReplyDelete
  5. Kwa maoni yangu hili wala haliitaji waziri au kiongozi yoyote yule kuingilia kati, bali linahitaji washabiki na wachezaji kusema hapana. Kwa sababu hao viongozi tayari wameshashikwa mashati. Nafikiri nyie wote mnafahamu kwa jinsi serikali yetu na watawala wetu wanavyofanya mambo kwa hiyo tusitegemee kupata nafuu kutoka kwao sana sana tutakuwa tumewapa deal ya kuchukua 10%. Cha muhimu narudia tena ni washabiki na wachezaji kusema hapana, hili linawezekana kwa sababu timu sio jina tu bali ni wachezaji na ushindi. Na yeyote anayenunua timu anahitaji wachezaji wazuri na kocha mzuri bila kusahau washabiki ambao ndio wateja wenyenyewe kwa sababu mpira ni biashara. Sasa kama washabiki wakisema wao basi na yanga basi hakuna tena biashara hapo.
    Naomba kuwakilisha.
    Halifa

    ReplyDelete
  6. Tungaraza hayo mawazo yako ndo yanaitwa mawazo mgando! Yaani huwezi kufikiria mbali ya Yanga ya miaka ya 40 na 50. Ile ya Mzee Tabu Mangara? Mabadiliko makubwa yanatakiwa Yanga na soka la bongo kwa ujumla. Tufike mahali kuwe na tofauti kati ya klabu (mahali ambapo wapenzi na wanachama wanakwenda kunywa kahawa, kupiga soga, nk) na professional timu inayojiendesha kibiashara.

    Bila kutenga hivi vitu viwili, daima tutabaki kwenye kucheza makida*2, migogoro kila leo.

    Hapa simaanishi kuwa timu lazima iuzwe kwa Manji (hakuna kitu kama hicho anyway), ila tujiulize, kwa mfano: Umiliki wa Abramovic pale Chelsea unawazuia wanachama wa Chelsea kunywa gahawa zao na kufurahia mabao ya Drogba na wengine?

    What if kila the so called mwanachama wa Chelsea (at timu ingine) angekuwa na mamlaka ya kusema nani aongoze timu, mchezaji gani asajiliwe, soka la Uingereza lingekuwa hapo lilipo?

    ReplyDelete
  7. Watanzania ndio maana hatuendelei hivihivi halafu tunaishia kulalamika tu kila siku.
    Hivi ni kweli kabisa hatuna jambo lingine la maendleo la kuzungumzia mpaka kila siku ni Yangaaa Yangaa! Hee!
    Kweli hatuna issue nzito za maendeleo za kujadiliana humu kila siku tusikie mambo ya yanga tu?
    Come on! wake up you people! Misaada inayotoka nchi za nje ni kodi hizo za wananchi wao ambao wanafanya kazi na sio saa zote ku-diskas mambo ya kijiweni ya mpira tu.
    Hivi waTanzania wenzangu tutazinduka lini jamai?
    Na we Michuzi kwenda kutuwekea mapicha yote kwenye page moja katika hii blog yako ndo nini mpaka inachukua dakika 20 nzima tunasupiri tu bulogi yako kufunguka.
    Unafikiri hatuna kazi nyingine za kufanya? huo muda tunaosubiri bulogi yako mpaka ifunguke utaulipa wewe?
    Eboo!

    ReplyDelete
  8. NAUNGA MKONO 100% KUUZWA TIMU YA YANGA. NI HATUA YA MAENDELEO AMBAPO TIMU ITAENDESHWA KAMA KAMPUNI SASA. KUMBUKA TIMU ZOTE ZINAZOFANYA VIZURI DUNIANI KAMA MAN UTD, CHELSEA, N.K. NI KAMPUNI. KAMA VIPI BAADHI YA HISA ZA YANGA ZILETENI DAR ES SALAAM STOCK EXCHANGE WAHAFIDHINA WA YANGA TUTAZINUNUA KWA WINGI TU. AISEE MTAPETA SANA MKIIGEUZA HIYO TIMU KUWA KAMPUNI SIO SASA HIVI ETI MNADHALILIKA KWA SABABU MFADHILI KAONDOKA.

    ReplyDelete
  9. Tungaraza tunaelewa kuwa yanga ina historia katika tanzania hata Nyerere alikuwa mwanachama well by then ilikuwa katika harakati za kugombea uhuru. Lakini kwa sasa tulishapata uhuru hivyo jukumu lake kwa wakati huo ishakuwa historia. kwa sasa timu inabidi iendeshwe kibiashara kwani sio ridhaa tena kama ilivyokuwa miaka ya nyuma. Hebu fikiria hao wachezaji wanakuwa camp kwa mwaka mzima mapato yao yanatemea viingilio kibaya zaidi wachezaji hao hawana social security wakiizeka hamna tena source of income. wanabaki na majina makubwa lakini hamna walichostahiri kuwanacho.
    Kwa mfumo tulionao naona hautusaidii kwani tangu niwe mpenzi wa yanga hadi hii leo nachosikia ni migogoro tu yanga asili kandambili mara kampuni for real am sick to death of hearing those claims so its better to get another direction. Am sure its gonna be the motive to other clubs too.

    ReplyDelete
  10. Yanga imeuzwa? Lini tena? Najua kuwa kuna mazungumzo ya kuifanya iwe kampuni na hiyo naiunga mkono. Lakini kuuzwa bado hatujaona hapa kilabuni.

    ReplyDelete
  11. MKATABA WA BILIONI MOJA KWA MWAKA SAWA NAKUBALI HALAFU WAPENI WAPENI MKATABA WA MIAKA MITANO TU BASI. KWA TAARIFA YAKO SIMBA NA YANGA ZINALIPA.

    ReplyDelete
  12. Najua wengi mtanimaindi lakini sijali hata kidogo.
    I am not a fan of either of the two teams,never will.
    Hizi ndizo timu zinazodumaza soka la bongo.Chembechembe za U-Simba na Yanga zimetapakaa nchi nzima kiasi cha kuathiri mechi nyingine kupitia kwa marefa au hata wachezaji hapa nchini.
    Viongozi wa timu wamefanya timu mitaji yao binafsi.Hujiulizi kwa nini wanagombania uongozi hadi mahakamani,kwani kuna raha gani ya kuongoza timu wakati unapata adha ya washabiki wake kwa matusi na kurushiwa mawe?
    Muda mwingi unatumika kutatua migogoro kuliko kuendeleza timu.Kila mgogoro wanataka serikali iingilie kati.TFF yenyewe inasalimu amri kwa hizi timu kwani viongozi wake nao ni fans of either of the teams.Wanabadilisha msimamo wao kila kukicha just to accomodate Simba and Yanga.Najua ni timu zenye majina makubwa but ligi haichezwi na timu mbili tu.
    So whatever happens,may be a change will make a diferrence we ought to see in club level as in National level.
    ~Sam.

    ReplyDelete
  13. These teams have great potential. Mengi advised them to put their shares on DSE years ago but they didnt.
    If Liverpool could be sold to Americans lord forbid what chance does Yanga stand(If you are living in UK you will appreciate this ).
    It is crussial that the people dealing with this negotiate good deal because there is no turning back now .

    ReplyDelete
  14. Fide..hujawahi kujiuliza unachopenda

    1.je club ya yanga leoikibadilisha jina ikawa MAJAMBOZ CLUB, bado utaipenda

    2.Je wachezaji wote,makocha na viongozi wakihama Yanga leo nakujiunga na NJAGU club,bado utaipenda?

    3. kama ni rangi...Je Yanga ikibadilisha rangi zake kutoka kijani na njano hadi blue na grey,je bado utaipenda?

    Fide usikubalikuishi kwenye fantasy,hamna kitu tangible unachopenda kuhusiana na YANGA, Acha wanaopenda ILLUSIONS wainunue.Tuongelee mambo muhimu yatakayo add value kwenye maisha ya wake, waume, watoto wetu

    ReplyDelete
  15. kaka, khabari ya yanga unaandika kwa maandishi ya rangi ya mahasimu wao, unategemea nini??

    ReplyDelete
  16. Ndugu zangu kuuza timu kwa manufaa ya walio wengi nadhani ni jambo jema tatizo ni je hawa wanaotaka kununua wanapanga kuwapa manufaa walio wengi? Ningeshauri kuwa mtu kama Manji angengojea msimu mpya wa usajili ili anunue wachezaji anaowataka toka ktk timu yoyote na awalipe mishahara mikubwa kisha aanzishe timu yake na kuacha timu hizi kongwe zijipangie mipango yake. Kwa kufanya hivyo hawezi kugombana na mtu yeyote na atatumia fedha kidogo na zinazoelezeka na nadhani atafanya vizuri zaidi na kuwa na timu yenye uwezo hapa Afrika kuliko ilivyo sasa maana inabidi atoe fedha za kuwapa wanachama ili wakubaliane naye na kupinga mawazo mengine toka kwa viongozi. Timu za Yanga na Simba haziwezi kukwepa mabadiliko ila inabidi yafanyike kwa kuzingatia hali halisi na historia sio mabavu ya pesa tu!!

    ReplyDelete
  17. Michuzi,

    Hii blogu yako inaelimisha au inatia ujinga zaidi?

    Mwandishi wa habari iliyotolewa maoni amejitahidi sana kueleza habari nzima kwa lugha ya kiswahili tangu mwanzo hadi mwisho.

    Nimesoma maoni yote hapo juu uliyotundika lakini sijaelewa kwa kweli lugha iliyotumika, labda mmoja tu amejitahidi kuandika Kiingereza tangu mwanzo mpaka mwisho ambacho vile vile hakivutii!

    Najua lugha yoyote ile huwa inakua, lakini kama ndio ukuaji wa lugha namna hii inabidi turudi shuleni!....Ukute ndiyo sababu labda hata viongozi wetu hawawezi kujieleza kwa lugha tunayielewa wote.

    Endelea libeneke bwana!

    ReplyDelete
  18. Tungaraza,
    how much in the form of bank notes have you contributed to the club? If at all you have contributed do you think its enough for the players and coaches?
    There are a lot of serious issues that requires government's attention and this isnt among those issues. Forget Yanga & Simba what about hospitals and school? I dont know you but from what you have read you seem to be very juvenile. Words of advise: grow up.

    ReplyDelete
  19. Zifuatazo ni ansadi za bunge zilizotafitiwa na Ndugu Dennis Londo na kuletwa hapa na Fidelis M Tungaraza.

    Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi hii. Natumia nafasi hii pamoja na kwamba nilishawashukuru wananchi wangu wa Kinondoni, lakini naendelea kuwashukuru tena. Ninawashukuru kwa mara ya kwanza kabisa, wanamichezo wote wa Wilaya ya Kinondoni na Mkoa wa Dar es salaam, kwa jitihada zao walizofanya na kuhakikisha ninakuwa Mbunge wa Jimbo la Kinondoni.

    Mheshimiwa Spika, nachukua nafasi hii tena, kumshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kwa kuanzisha au kuunda Wizara hii muhimu sana ya Habari, Utamaduni na Michezo.

    Mheshimiwa Spika, nitakuwa mchoyo wa fadhila kama sitatoa shukrani ama kumpongeza Rais wetu wa Awamu ya Tatu, Mheshimiwa Benjamin William Mkapa na uongozi wote wa Awamu ya Tatu, kwa kitendo cha kuamua kujenga Uwanja Mkubwa na wa Kisasa Tanzania na ninafikiri katika Afrika, pale Dar es Salaam.

    Mheshimiwa Spika, nachukua nafasi hii pia, kumpongeza tena Rais wetu Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete, kwa uamuzi wake wa kutuletea Makocha kwa ajili ya kuifundisha Timu yetu ya Taifa ya Mpira wa Miguu, tena wametoka katika nchi ambayo imeendelea sana katika mchezo wa mpira wa miguu.

    Mheshimiwa Spika, hii inaonesha ni jinsi gani Serikali ya Awamu ya Nne, inavyopenda maendeleo ya michezo. Nina hakika ile azma ya Rais wetu kwamba, ifikapo mwaka 2008, basi angalau tucheze Fainali za Mataifa ya Afrika ambazo zitafanyika Ghana. Kitendo cha kumleta Kocha huyu, nina hakika kabisa, kitasaidia na kitaiwezesha Tanzania kucheza Fainali hizo.

    Mheshimiwa Spika, pamoja na azma hiyo nzuri ya Serikali yetu, pamoja na azma nzuri ya Rais wetu, lakini mchezo wa mpira umekumbwa na migogoro mingi sana na kama Wizara hii haitakuwa makini, nina hakika azma ya Rais, haiwezi kufikiwa. Migogoro katika vyama vya michezo, migogoro katika vilabu imekuwa ni mikubwa sana.

    Mheshimiwa Spika, chanzo kikubwa cha migogoro hiyo, watendaji wa Wizara yetu wanahusika sana. Nampongeza sana Waziri wa Wizara hiyo aliyepita, Mheshimiwa Prof. Juma A. Kapuya na Naibu wake, Mheshimiwa Mudhihir M. Mudhihir, kwa kazi nzuri waliyoifanya kipindi kile, lakini walikwamishwa sana na watendaji katika Wizara ile.

    Mheshimiwa Spika, mahali ambapo kuna migogoro, hapawezi kuwa na maendeleo. Hiyo migogoro ndiyo ilitufikisha hapa tulipo hivi sasa. Mheshimiwa Capt. John D. Komba, alizungumzia miaka ya 1970 na alionesha jinsi gani Tanzania tulipiga hatua katika michezo, mchezo wa mpira wa miguu lakini hata michezo mingine. Lakini kuanzia miaka ya 1990 � 1995 mpaka hivi sasa, kwa kweli tumerudi nyuma sana katika michezo, lakini kubwa ni migogoro. Migogoro hii, watendaji wetu wamekuwa wakihusika kwa namna moja ama nyingine, kuisababisha itokee ama kuifanya iendelee kuwepo.

    Mheshimiwa Spika, huwezi kuzungumza maendeleo ya mchezo wa mpira wa miguu Tanzania, ukakosa kuitaja Simba ama ukakosa kuitaja Yanga. Panapotokea matatizo ama migogoro katika vyama hivyo viwili, basi ujue hata Timu ya Taifa, haitafanya vizuri kwa sababu asilimia kubwa ya wachezaji ambao tunawatumia wanatoka katika vilabu hivyo.

    Mheshimiwa Spika, lakini migogoro imeendelea kuwepo na naomba ninukuu baadhi ya Kanuni zilizounda Baraza la Michezo la Taifa na nina hakika kama kweli watendaji wetu wangekuwa wanazifuata, sidhani kama tungefika hapa tulipo. Tunataka maendeleo, tunataka mabadiliko, lakini mabadiliko ni lazima yaendane na sheria, taratibu na kanuni zilizopo. Leo katika Klabu ya Yanga, kuna mvutano mkubwa sana kati ya pande mbili na bahati nzuri na tunamshukuru Mwenyezi Mungu kwamba, Watanzania wote tunaongea Kiswahili. Lakini kama tungekuwa tunaongea lugha tofauti tofauti, basi sasa hivi nafikiri tungekuwa tunasema mengine katika Vilabu hivyo, tungeuwana au kutwa tungekuwa tunapigana.

    Mheshimiwa Spika, Yanga wana mgogoro katika kuboresha Young African Sports Club, lipo kundi liliamua kwamba, hapana twende kibiashara kwa maana ya kuanzisha Kampuni. Sasa Young Sports Club iwe Kampuni. Lakini kwa mujibu wa Kanuni zetu za Baraza, zinapingana na hilo.

    Mheshimiwa Spika, ninukuu Kanuni za Baraza la Michezo, Sheria ya Baraza la Michezo ya mwaka 1967, ikafanyiwa marekebisho mwaka 1971. Utaratibu wa kusajili vyama vya michezo, kipengele cha sita. Naomba kunukuu �Chama cha Mchezo wowote, hakitaruhusiwa kuendesha shughuli za michezo bila kusajiliwa na Msajili wa Vyama vya Michezo. Aidha, chama kilichosajiliwa, hakiruhusiwi kuwa na ushirikiano wa kimichezo na chama chochote, ambacho hakijasajiliwa.�

    Mheshimiwa Spika, juzi niliuliza swali kati ya Yanga mbili hizi, Yanga Kampuni na Young African Sports Club, Naibu Waziri alinijibu kwamba, Yanga Kampuni imesajiliwa chini ya Sheria Na. 212 ya Msajili wa Makampuni. Yanga Sports Club imesajiliwa chini ya Sheria ya Msajili wa Vyama vya Michezo. Kwa mujibu wa kanini hizi za Baraza ni kwamba, ndiyo ambayo inatambulika. Lakini kwa sababu ni mpango mzuri wa kuiondoa Yanga pale ilipo, kuipeleka sasa kwenye mahali ambapo watajipatia kipato kizuri, kuifanya iwe kampuni, kuiendesha kisasa. Hapa tunakingana sasa na kanuni ya Baraza. Nawaomba viongozi wa Baraza, wazipitie na kuzitafsiri vizuri hizi kanuni kabla ya kuanza kuingia kwenye mambo mengine ya maendeleo.

    Mheshimiwa Spika, tunao mpango hivi sasa labda tunataka soka la kulipwa, tunao mpango wa kuvifanya vilabu vyetu viwe kampuni lakini tunapingana na sheria na ndiyo maana wakati wa kuchangia hotuba ya Mheshimiwa Rais, aliyoitoa tarehe 30 Desemba, nilisema Serikali iangalie uwezekano wa kuzirekebisha kama si kufuta kabisa Sheria hizi za Baraza la Michezo.

    Mheshimiwa Spika, lakini kanuni hizo hizo tena kwenye marekebisho ya Katiba, kwa sababu huwezi kusajili chama cha mchezo wa miguu pale, msajili ni lazima uwe na Katiba. Marekebisho ya Katiba unapotaka kuyafanya, kanuni inaelekeza, naomba kunukuu: �Chama chochote kitakachofanya mabadiliko ya jina, anuani, madhumuni au kifungu chochote cha Katiba yake, kitatakiwa kupata idhini kwa kupeleka maombi kwa msajili kupitia msajili msaidizi kwa kujaza fomu za maombi.� Zimetajwa hizo fomu. Sasa kuifanya Yanga iwe kampuni na itambulike, ni lazima hizi sheria tuzifuate. Lakini tukitaka kwenda tunavyokwenda hivi sasa, ndio maana tunazaa migogoro hii. Wizara imeshindwa kuwa wazi tangu mapema, kuelekeza ama kushauri kuhusu suala hili la Yanga, ndio tumefika hapa tulipo.

    Mheshimiwa Spika, naiomba Wizara sasa, bahati nzuri nimeandika, wanieleze jitihada ambazo watazifanya kwa makusudi, kuhakikisha mgogoro huu wa Yanga Asili na Yanga Kampuni unakwisha.
    Mheshimiwa Spika, sambamba na hilo, upo mgogoro katika Club ya Simba, ambao nao pia umechangiwa kwa kiasi kikubwa na Watendaji wa Wizara. Mara baada ya Msajili kwenda kufanya uhakiki wa wachama wa Simba, kuanzia pale ndipo zogo lilipotokea. Sasa ili tuendane na kauli ya Mheshimiwa Rais ya kuhakikisha Tanzania inacheza Fainali za Afrika mwaka 2008, ili maendeleo yapatikane, ni lazima tuhakikishe migogoro hii, tunaiondoa.

    Mheshimiwa Spika, nina hakika kabisa Mheshimiwa Waziri ni mtunzi mzuri wa nyimbo, lakini nina hakika pia ni mchezaji mzuri sana, alikuwa zamani akichezea Timu ya Kikwajuni. Centre Forward mzuri sana. Mheshimiwa Joel N. Bendera, amecheza Korogwe Nyota, anaujua mpira vizuri sana. Nina hakika mgogoro huu katika kipindi kifupi wataumaliza ili tuweze kwendana na ahadi ya Rais.

    Mheshimiwa Spika, sambamba na kurudisha michezo shuleni, ningeiomba Wizara ihakikishe tunawapa angalau mafunzo ya awali, walimu wa shule za msingi na walimu wa shule za sekondari, angalau wajue kuwafundisha wale watoto wetu pale shuleni mchezo huu wa mpira wa miguu. Kuwe na kozi fupi fupi kwa walimu ili ziweze kuwasaidia.

    Mheshimiwa Spika, nazungumzia vyombo vya habari. Nimekuwa nikisoma magazeti na kwa kweli sasa inabidi hata nisiyasome, yapo baadhi ya magazeti yamekuwa yakihoji na kueleza mgogoro wa suala la NSSF na Quality Group, juu ya mikataba ya ununuzi wa yale majengo. Hilo limezungumzwa sana kwenye vyombo vya habari na baadhi ya vyombo ndivyo ambavyo wamebebea bango suala hilo, yaani ndivyo ambavyo vinaandika habari hizo.

    Magazeti yote ya IPP, huwa yanaandika habari hizo kila kukicha. Sasa ningependa katika majumuisho, mnifahamishe yanayoandikwa na magazeti yale, yako sawa sawa? Kama yako sawa sawa, Serikali inachukua hatua gani na kama yanayoandikwa siyo sawa sawa, basi pia nitaomba tamko la Wizara, ni hatua gani mnachukua kwa sababu kama yatakuwa siyo sahihi, ina maana wanatupotosha? Nitaomba maelezo hayo.

    Mheshimiwa Spika, nimalizie kwa kuwapongeza wandaaji wa Mashindano ya Miss Tanzania, pamoja na wandaaji wa Mashindano ya Miss Utalii. Niwapongeze hasa wa Utalii na nichukue nafasi hii kuipongeza Serikali kwa kuhakikisha kwamba, mashindano yale ya Utalii Duniani yalifanyika hapa Tanzania na yalifanyika kwa ufanisi mkubwa sana, baada ya Serikali kuamua kuingilia na kusimamia Mashindano yale. Naipongeza sana Serikali kwa sababu kinyume cha hivyo, Tanzania tungeweza kupata aibu.

    Mheshimiwa Spika, nizungumzie suala la makocha, tayari tunao makocha wa Kigeni ambao wataifundisha Timu yetu ya Taifa, lakini bado tunataka makocha kwa ajili ya timu zetu za mitaani. Naiomba Wizara iandae utaratibu wa makusudi kabisa wa kuhakikisha vijana wetu wanapata mafunzo ya ukocha hapa nyumbani au kwa kupelekwa nje.

    ReplyDelete
  20. Majadiliano mengine toka katika ansadi za Bunge la Tanzania iliyotafitiwa na Ndugu Dennis Londo na kunukuliwa hapa Ndugu Fidelis M Tungaraza.

    Session number 16 (20 July 2004)

    Swali kutoka kwa Mohd Hamis Misanga (Singida kusini)

    Kwa kuwa imedhihirika wazi kuwa kiwango cha mpira wa miguu hapa nchini kimezidi kushuka na hakipandi na kwa kuwa Serikali imeshakubali kimsingi kuanzisha mpira wa miguu wa kulipwa kama njia mojawapo ya kuinua kiwango hicho:-

    (a) Je, suala la kuanzishwa kwa mpira wa miguu wa kulipwa (Professional Football) limefikia wapi?

    (b) Je, Serikali imeandaa mazingira gani mazuri yatakayowezesha kuanzishwa kwa mpira wa miguu wa kulipwa nchini?

    Jibu kutokwa kwa Mudhihil.

    Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Kazi, Maendeleo ya Vijana na Michezo, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Mohamed Missanga, Mbunge wa Singida Kusini, lenye sehemu (a) na (b) kama ifuatavyo:-

    (a) Mheshimiwa Spika, Serikali imesharuhusu uanzishaji wa mpira wa miguu wa kulipwa. Suala la uanzishwaji wa vilabu vya mpira wa kulipwa au kuwa na wachezaji wa kulipwa ni suala la wadau wenyewe wenye mahitaji ya namna hiyo. Hivyo, hivi sasa milango iko wazi kwa yeyote anayetaka kumiliki timu au wachezaji wa kulipwa ili mradi masharti ya sheria nyingine za nchi yanazingatiwa.

    (b) Mheshimiwa Spika, Serikali kuridhia uanzishaji wa michezo ya kulipwa ni mazingira tosha ya kuwawezesha Wananchi wake kutekeleza azma yao ya kuwa na wachezaji wa soka ya kulipwa. Kuanzisha michezo ya kulipwa sio suala la mazingira pekee, linahitaji pia mtaji wa kutosha kumudu maendeleo ya timu, miradi endelevu, uongozi thabiti usioyumba, wachezaji wenye elimu ya mchezo na uwezo wa kucheza kwa mujibu wa mkataba na chama cha mchezo chenye uwezo wa kuendesha mashindano ya michezo ya kulipwa. Hata hivyo, endapo liko tatizo lolote linalokwaza nia hiyo, basi Wizara yangu ipo tayari wakati wowote kusaidia kwa yale yaliyo ndani ya uwezo wetu.

    ReplyDelete
  21. kaka Michuzi ubarikiwe kwa kuwa msikivu kwa maoni ya wadau.
    Picha zimepungua kwenye page moja katika bulogi yako, na sasa zinafunguka haraka sana kama zamani.
    Asante and Big up!

    ReplyDelete
  22. Huyu Tungaraza lazima atakuwa ni Komandoo, hawa ndio wanaoifilisi YANGA, anajua timu ikibadilishwa mfumo wa uendeshaji makomandoo wote KWISHA KAZI itabidi warudi MSATA na KIBADA wakalime nanasi na embe

    ReplyDelete
  23. YANGA KUWA KAMPUNI: KWA MISINGI IPI NA MASLAHI YA NANI?

    Mgogoro wa Yanga ni moja ya mambo ambayo nimekuwa nikiyafuatilia kwa karibu sana tangu ulipoibuka wiki chache zilizopita. Sikuwa na sababu nyingine ya kufuatilia mgogoro huo, isipokuwa ni kuangalia kwa makini chanzo cha mgogoro huo hasa kwa kuwa ulikuwa ukimuhusisha Bw. Manji ambaye katika miaka ya karibuni amekuwa habari, mjadala, gumzo na soga kubwa katika vyombo vyetu vya habari.

    Ikumbukwe kuwa Manji alisitisha ufadhili wake Septemba 20. Seke seke la mgogoro huo lilianza tarehe 8 Oktoba mwaka huu pale Bw. Yusuf Manji alipotangaza kuacha ufadhili wake Yanga kwa sababu kuu moja nayo ni kushauriwa na familia yake na marafiki zake. (Tanzania Daima, 11/10/2007)

    La kushangaza hapa ni kuwa siku moja baada ya tamko lake Bw. Manji, Oktoba 9 alifunga safari mpaka kwenye makutano ya mtaa wa Twiga na Jangwani yalipo makao makuu ya klabu ya Yanga. Pengine hilo siyo tatizo kwani naye kama mwanachama mwingine yeyote wa Yanga ana haki ya kufika mahali hapo, tatizo ni Bw. Manji kuitisha mkutano wa wazee na kuanza kurusha shutuma dhidi ya uongozi na kubadilisha sababu mbali ya ile aliyouelezea UMMA awali kwa maandishi ikiwemo ucheleweshaji wa KATIBA mpya, na kutoa masharti ya nini kifanyike ili abadilishe maamuzi yake mojawapo ni kubadilisha timu kuwa kampuni, hili lilikuwa ni kosa. Pamoja na hilo, Bw. Manji kutoa dau la milioni 50, 10 kwa ajili ya 'wazee' (Ukipenda unaweza kuiita rushwa) na 40 kwa ajili ya maandalizi ya timu, huku akitoa sharti kuwa ni lazima ziwe chini ya katibu mkuu Bw. Kisasa bila ya kufuata utaratibu na katiba ya klabu na kanuni za masuala ya fedha za klabu, hili lilikuwa kosa jingine. Hali hii ndiyo iliyopelekea mmoja wa 'wazee' wa Yanga kuhoji uhalali wa Manji kuwapangia jinsi ya kuendesha klabu kama alivyonukuliwa "Manji hawezi kutuchagulia wanachama au viongozi anaowataka huku ni kuvuka mipaka, yeye mwisho wake ni ufadhili na siyo kuchagua viongozi". (Tanzania Daima, 12/10/2007)

    Kwa mujibu wa uchambuzi, mgogoro mzima ni kati ya uongozi halali wa Bw. Madega na mfadhili wa timu Bw. Manji. Jambo linalovuta hisia zangu hapa ni kuwa wakati Bw. Manji anautuhumu uongozi kwa kuchelewesha "utekelezaji wa vitendo" juu ya rasimu ya muafaka ikiwemo katiba mpya ambayo ingepelekea Yanga kuwa kampuni; Bw. Madega anapinga wazo la Yanga kuwa kampuni bila ya kufanyia marekebisho kadhaa muhimu kwa kulinda maslahi ya wengi ambao ni wanachama wa klabu hiyo kongwe.

    Kwa kuwa Bw. Madega alionyesha wasiwasi wake waziwazi kwa wahariri wa habari tarehe 11/10/2007 juu ya suala zima la ujio wa Bw. Manji Jangwani na uhamishaji wa timu ya Yanga kwenda kuwa kampuni, ambako kutapelekea moja kwa moja Bw. Manji kuwa ndiyo mmiliki mkuu. Nilitegemea magazeti mengi yangeonyesha umakini wa Bw. Madega na hoja zake za msingi kama alivyoainisha. Kinyume chake, ni gazeti moja tu la kila siku ambalo liliandika kwa kirefu hoja za msingi za uongozi kukataa masharti ya mfadhili Bw. Manji. Zaidi ya hapo vyombo vingi vya habari vilikuza zaidi kauli ya Madega kuwa wazee wa Yanga wanatumiwa kwa njaa zao.

    Pengine suala la muhimu hapa ni kujadili wasiwasi wa Bw. Madega juu ya kuwekwa rehani kwa maslahi ya wanachama wengi, ambao pengine kwa kutojua sheria au kwa makusudi (Ikumbukwe Bw. Madega yeye ni mwanasheria na wa wakili wa mahakama kuu) Kwa mujibu wa Bw. Madega kupitisha rasimu na kuwa katiba bila maerekebisho ya msingi kungeweza kuhatarisha uhai wa klabu na maslahi ya wanachama wengi; ameahinisha haya kama alivyonukuliwa na Tanzania Daima la 11/10/2007 kama ifuatavyo:

    (1) Katika kifungu cha 39(2) (d) cha Katiba ya Yanga kinauagiza Mkutano Mkuu wa Uchaguzi kuchagua wanachama wawili ambao si miongoni mwa viongozi wa klabu kuwa wajumbe wa bodi ya wakurugenzi wa kampuni kwa ajili ya kuwakilisha masilahi ya klabu kwenye kampuni.

    (2) Kamati iligundua kifungu hiki kina makosa makubwa mawili, kwanza makosa yameshafanyika kuwa wanachama wawili hawakuchaguliwa kwenye mkutano wa uchaguzi, hivyo bodi ya kampuni hata kama itaundwa basi wawakilishi wa wanachama ndani ya kampuni hawatakuwepo, hivyo bodi ya kampuni kuifanya iwe batili.

    Lakini kubwa naloliona hapa, ni kukosekana kwa uwakilishi wa dhahiri wa klabu katika bodi ya kampuni, kwani hisa ni mali ya mwanahisa na siyo mali ya klabu. Hivyo basi hata mwanahisa aliyepoteza sifa za kuwa mwanachama wa Yanga, bado anaweza kuendelea kumiliki hisa zake kimsingi. Hili huenda likapelekea wanachama wawili watakaoingia kwenye bodi ya wakurugenzi, kuwakilisha maslahi yao kama wanahisa na siyo maslahi ya klabu.


    Ikumbukwe kuwa hisa zinarithishwa, lakini haki ya uanachama inapotea pale mtu anapopoteza sifa za kuwa mwanachama, ikiwemo kifo. Katika hili, kama katiba itaenda jinsi ilivyo tusishangae siku moja mwenye hisa nyingi akawa tajiri asiyependa michezo kabisa, achilia mbali kutokuwa mwanachama hata wa klabu hiyo. Kuiepusha Yanga na vilabu vingine na balaa hili, maslahi ya klabu katika kampuni iwayo yoyote ile, ni lazima yasimamiwe na viongozi waliochaguliwa na kimsingi ndio wasimamizi wakuu wa mali zote za klabu, ikiwemo maslahi ya wanachama. Na hili ni lazima litamkwe waziwazi kwenye katiba ya klabu kampuni, ni jinsi gani viongozi wa kuchaguliwa watashirikishwa kwenye bodi ya kampuni.

    Pamoja na hayo wasiwasi mwingine ambao Bw. Madega ameuelezea waziwazi bila kificho ni kuwa:

    (3) Kifungu cha 39 (2) (f) cha katiba kinataka klabu na kampuni kuingia katika makubaliano ya kimaandishi ya uendeshaji wa timu na kwa niaba ya klabu makubaliano hayo yatasainiwa na Katibu Mkuu wa klabu.

    Udhaifu wa kipengele hiki ni pale katibu mkuu pekee ndiye anayetakiwa kusaini makubaliano. Swali, je, ni kwa nini kwa taasisi kubwa kama Yanga mikataba yake isainiwe na katibu mkuu peke yake?

    (4) Kifungu cha 39(2)(b) kinamtambua mfadhili wa klabu kwa mujibu wa rasimu ya muafaka wa Yanga uliofikiwa na wanaYanga tarehe 22/06/2006 na ukiangalia rasimu ya muafaka, mfadhili ametambuliwa kama Yusuph Manji na si kampuni.

    Hapa pia kuna kasoro kubwa ya kikatiba kwani haipaswi kwa jina la mtu binafsi (natural person) kuingia katika katiba kwani katiba inaundwa ili iishi muda mrefu, hivyo unapotambua jina la mtu binafsi kwenye katiba, maana yake umetengeneza katiba ya kuishi chini ya saa moja, kwani wakati wowote mwanadamu anaweza kupoteza uhai.

    (5) Kifungu cha (39)(2)(c) ni kuwa klabu itamiliki hisa zilizo sawa na asilimia hamsini na moja (51%). Kama ni kweli klabu inamiliki hisa 51%, maana yake klabu ndiyo yenye hisa kubwa ndani ya kampuni, hivyo ni wazi kuwa kiongozi wa kampuni anapaswa kuwa kiongozi wa klabu ili kulinda masilahi ya hisa zake nyingi.

    (6) Tofauti na mfumo uliopo sasa, klabu haina mwakilishi kwenye bodi ya kampuni. Hivyo hapo mbele utakuja kuona si kweli kwamba klabu inamiliki hisa 51% za kampuni.

    Hayo ndiyo mapungufu ambayo uongozi wa Yanga umeyaona kwenye katiba na hivyo kufanya utekelezaji wa suala zima kuwa linataka muda.

    (a) Muafaka.

    Baada ya kupitia hati ya muafaka kwa kina, kamati iligundua yafuatayo:

    (1) Kampuni ya Yanga itakuwa na hisa ya sh 6,000,000 (milioni sita).

    - Hisa moja itauzwa kwa sh 1,000 (elfu moja) tu, hivyo kufanya mtaji wa kampuni kuwa ni sh 6,000,000,000 (bilioni sita) endapo hisa zote zitauzwa.

    - Kifungu cha 3.2.2 cha rasimu ya muafaka kinaipa klabu hisa saba tu kati ya hisa 6,000,000. Thamani ya hisa saba ni sawa na shilingi 7,000. Hii ndiyo thamani ya kampuni kwenye klabu.

    Hisa 3,059,993 zenye thamani ya shilingi 3,09,993,000 zitatengwa pembeni, zitatakiwa klabu kuzinunua ndani ya miaka miwili na klabu ikishindwa, basi hisa hizo zitauzwa kwa watu wengine.

    Hivi tujiulize, klabu itapata wapi shilingi bilioni tatu ndani ya miaka miwili ili iweze kununua hisa?

    Na asilimia 51 ya hisa zote za kampuni bali itakuwa na hisa saba tu zenye thamani ya shilingi 7000. Rasimu ya muafaka inasema kwamba mfadhili atamnunulia kila mwanachama hisa 10 zenye thamani ya shilingi 10,000.

    Kutokana na mgawanyiko wa hisa ulivyo kwenye rasimu (7) tu, wakati mwanachama ana hisa 10 zenye thamani ya shilingi 10,000 kwa maana hiyo mwanachama mmoja ana thamani kubwa ndani ya kampuni kuliko ndani ya klabu yenyewe, ambayo thamani yake ni shilingi 7,000 na ndiyo maana klabu haikutakiwa kuwa na mwakilishi kwenye bodi ya kampuni kwa kuwa haina hisa nyingi kwenye kampuni.


    Tujaribu kuangalia lengo la kununulia wanachama hisa, je ni kuwa anawapenda?, kitendo cha kuwahamisha kutoka klabu kwenda kampuni pamoja na timu si kuiua klabu? hapa suala la kuzingatiwa ni kuwa hakutakuwa na demokrasia nyingine ya kura moja mtu mmoja bali ni HISA MOJA KURA MOJA.

    Na hili likifanyika mwenye hisa nyingi ndio mwenye maamuzi yote...hivi huko ndiko wanachama wa Yanga wanakotaka kwenda?


    Vyombo vya habari

    Vyombo vya habari vina dhamana kubwa ya kuhabarisha umma juu ya nini kinajiri, kama wengi wanavyopenda kusema habari ni haki ya kila msomaji. Pamoja na majukumu makubwa na heshima iliyoshiba juu ya vyombo vyetu vya habari, lakini inasikitisha kuwa vyombo vya habari vingi (si vyote) vinapoamua kuuza haki hiyo kwa wenye 'dau' zito. Migogoro katika vilabu vyetu kwa kiasi kikubwa inachochewa na ubinafsi wa wananchama wanaoendekeza njaa zao lakini pia imekuwa ikishadidiwa kwa kiwango kikubwa na vyombo vyetu vya habari. Sikemei umuhimu wa vyombo vya habari kutangaza kauli za uchochezi kama zilivyo, la hasha! nalotaka kusema hapa ni kuwa viripoti kwa nia ya kuujulisha umma, kuuonesha nini kinafanyika na kuutahadharisha na sio kuunga mkono uchochezi huo.

    Aidha vyombo vyetu vya habari havina ruhusa ya kutetea uozo, maovu na uvunjifu wa amani katika vilabu vya michezo. Kutoa habari nusu nusu sio tu kunamnyima msomaji haki yake ya msingi, lakini pia kunakuwa kumesaidia kuchochea fujo zisizo na msingi. Ni ombi langu kuwa wakati umefika, kuanza kuheshimu wasomaji wetu/wenu kwa kuwapa kile kinachojiri kukiwa na habari ambazo zina uwiano, badala ya kuangalia nani mwenye dau, au habari gani itauza.

    Dennis Londo

    ReplyDelete

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...