TAMKO LA SERIKALI KUHUSU TAARIFA YA UKAGUZI WA HESABU KATIKA AKAUNTI YA MALIPO YA MADENI YA NJE (EXTERNAL PAYMENT ARREARS ACCOUNT – EPA) ILIYOKO BENKI KUU YA TANZANIA

Nafurahi kuwaarifu kuwa, kazi ya Ukaguzi wa Hesabu za mwaka wa fedha 2005/06 za Akaunti ya Madeni ya Malipo ya Nje yaani External Payment Arrears (EPA) katika Benki Kuu ya Tanzania imekamilika. Kazi hiyo ilifanywa na Wakaguzi wa Kampuni ya Ernst and Young kwa niaba ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali. Ilianza Septemba, 2007 na kukamilika Desemba, 2007. Juzi tarehe 07 Januari, 2008 Rais Jakaya Mrisho Kikwete alikabidhiwa Taarifa hiyo na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Serikali. Rais ameisoma, ameifanyia kazi na kuitolea maamuzi.

Historia ya EPA


Katika miaka ya 1970 mpaka 1990 nchi yetu ilikuwa inakabiliwa na tatizo kubwa la upungufu wa fedha za kigeni. Benki Kuu ya Tanzania ilipewa jukumu la kusimamia matumizi ya fedha za kigeni kwa niaba ya Serikali. Benki Kuu ndiyo iliyokuwa na mamlaka ya kupanga na kuamua nani agawiwe fedha za kigeni na kiasi gani!

Kwa ajili ya kuwahudumia wafanyabiashara, mashirika na makampuni yanayoagiza bidhaa na huduma kutoka nje, Akaunti maalum ilifunguliwa katika Benki ya Taifa ya Biashara kwa wakati huo. Akaunti hiyo ilijulikana kwa jina la External Payment Arrears (EPA) au Akaunti ya malipo ya Madeni ya Nje, kwa tafsiri ya Kiswahili.

Waagizaji wa bidhaa au huduma kutoka nje waliwajibika kulipa kwenye Akaunti hiyo, fedha ya Tanzania yenye thamani inayolingana na fedha za kigeni zinazotakiwa kulipia bidhaa au huduma hiyo huko nje. Baada ya waagizaji wa ndani kufanya hivyo, kutegemeana na upatikanaji wa fedha za kigeni, wauzaji au watoaji huduma wa nje walilipwa. Benki Kuu iliamua nani alipwe na Benki ya Biashara ilifanya malipo.

Juni, 1985 iliamuliwa kuwa shughuli za akaunti hiyo zihamishiwe Benki Kuu kutoka Benki ya Taifa ya Biashara na zimeendelea kuwepo hapo mpaka sasa. Katika Benki Kuu kikaundwa kitengo maalum cha kusimamia na kuendesha shughuli za akaunti hiyo kilichojulikana kama Debt Management Unit chini ya Kurugenzi ya Sera (Directorate of Economic Policy).

Kwa sababu ya tatizo la upungufu wa fedha za kigeni kuendelea, malimbikizo ya madeni hayo yalizidi kukua mwaka hadi mwaka. Kwa mfano, mwaka 1999 deni hilo lilifikia dola za Kimarekani 623 milioni. Kati ya fedha hizo, dola 325 milioni ndilo deni la msingi na dola 298 milioni ni riba yake. Baadae likaongezeka kufikia dola 677 milioni.




Juhudi za Kulipa Madeni

Juhudi za kulipa malimbikizo ya madeni hayo ziliendelea kadri fedha za kigeni zilipopatikana. Kwa nia ya kutaka kutafutia ufumbuzi wa haraka tatizo hilo na kupunguza mzigo wa madeni, Serikali ilianza kutafuta njia nyingine mbalimbali. Mwaka 1994, Serikali kwa kushirikiana na Benki ya Dunia ilianzisha Mpango wa Kununua Madeni (Debt Buy Back Scheme). Yaani waliokuwa wanaidai BoT waliombwa wakubali kulipwa sehemu tu ya madeni wanayodai. Wapo wadai kadhaa walikubali na madeni yao yakauzwa chini ya mpango huo. Taarifa za mwaka 2004 zinaonyesha kuwa madeni ya thamani ya dola 228 milioni yalilipwa chini ya mpango huu.
Pili, Serikali ilifanya juhudi ya kupata msamaha wa madeni hayo kutoka nchi wanachama wa Paris Club. Serikali iliomba kuwa pamoja na kutusamehe madeni ya kiserikali toka nchi zao wasaidie tusamehe na madeni ya makampuni yao kwetu. Yapo pia madeni ambayo yamelipwa na makampuni ya Bima baada ya makampuni yaliyouza bidhaa na huduma Tanzania kushindwa kulipwa. Madeni ya dola 216 milioni yalihusika chini ya michakato hii. Hivyo basi, deni la dola 444 milioni lilipungua katika ile jumla ya dola 677 milioni. Kwa hiyo mwaka 2004 deni katika Akaunti ya Malipo ya Nje lilikuwa dola 233 milioni. Yalikuwepo mawazo ya baadhi ya watu kuwa pengine deni hilo lisilipwe au tulikatae. Walikuwepo waliokubali madeni yao yafutwe na wengine waliagiza fedha zao zipewe NGO. Lakini, baadhi ya wadai waliendelea kudai na wengine hata kushitaki mahakamani. Hivyo BoT ililazimika kuendelea kulipa kadri wadai walipojitokeza.


Ulipaji kwa Idhini


Katika utaratibu wa malipo ya madeni ya EPA kanuni zinaruhusu mdai kuamua deni lake kulipwa kwa mtu au kampuni nyingine. Kanuni zinamtaka mdai kutoa hati iliyothibitika kisheria ya yeye kuidhinisha malipo hayo yafanywe (Notarised Deeds of Assignments) hivyo. Pia yapo masharti ya kutimizwa na kampuni au mtu aliyeidhinishwa kulipwa hilo deni. Utaratibu umetumika kufanya malipo kadhaa ya madeni katika Akaunti ya EPA.

Matatizo ya Mwaka 2005/6

Katika ukaguzi wa Hesabu za BoT za mwaka wa fedha 2005/6, Agosti, 2005 kuligundulika matatizo katika ulipaji wa madeni kwa utaratibu wa idhini ya kulipwa wakala wa mdai katika akaunti ya EPA. Kukajitokeza kutokuelewana kati ya Benki Kuu na Mkaguzi Deloitte and Touche’ aliyegundua tatizo hilo. Baadaye mkaguzi huyo alisitishwa kuendelea na kazi. Serikali ikaingilia kati na tarehe o4 Desemba, 2006 ilimuagiza Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kuhakikisha kuwa ukaguzi wa akaunti hiyo unafanyika kwa kina. Aidha, ilimuagiza atafute kampuni ya kimataifa ya ukaguzi ifanye kazi hiyo kwa niaba yake. Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabau za Serikali, ndiye kwa mujibu wa Sheria ya BoT mkaguzi wa Hesabu za Benki Kuu. Hata hivyo kwa mazingira hayo maalum Serikali ilimtaka CAG atafute mkaguzi mwingine wa nje.



Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) alifanya hivyo na matokeo ya mchakato wa kutafuta kampuni hiyo uliochukua miezi mitano (Januari hadi Mei, 2007) ndipo ikapatikana kampuni ya Ernst and Young.
UKAGUZI

Wakaguzi wa Kampuni ya Ernst and Young wakaanza kazi hiyo Septemba, 2007 na kuikamilisha Desemba, 2007. Wakaguzi hao wamefanya kazi nzuri iliyothibitisha kiwango cha juu cha weledi (Professionalism) cha wakaguzi hao. Tunawapongeza, tunawashukuru. Tunatambua kuwa walipata matatizo mengi hasa ya kupata taarifa zilizo sahihi kwa sababu ya matatizo ya utunzaji wa kumbukumbu. Madeni haya ni ya miaka 27 na zaidi iliyopita. Kumbukumbu zimehamishwa kutoka NBC kwenda BoT. Hata huko NBC shughuli zilikuwa zinafanywa katika matawi mbalimbali nchini tena miaka hiyo hapakuwa na kompyuta hivyo kumbukumbu zote ziliwekwa kwenye majalada. Pamoja na matatizo hayo ukaguzi wa hesabu za mwaka 2005/6 ulikamilika kwa kiwango cha kuridhisha.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo ya Ukaguzi katika mwaka wa fedha wa 2005/2006 uliochunguzwa, katika mwaka 2005 yalifanywa malipo ya jumla ya Shilingi 133,015,186,220.74 kwa Makampuni 22 ya hapa nchini. Makampuni hayo ni: Bencon International Ltd. of Tanzania, VB & Associates Company Ltd. of Tanzania, Bina Resorts Ltd. of Tanzania, Venus Hotel Ltd. of Tanzania, Njake Hotel & Tours Ltd., Maltan Mining Company Ltd. of Tanzania, Money Planners & Consultants, Bora Hotels & Apartment Ltd., B. V. Holdings Ltd., Ndovu Soaps Ltd., Navy Cut Tobacco (T) Ltd. of Tanzania, Changanyikeni Residential Complex Ltd., Kagoda Agriculture Ltd., G&T International Ltd., Excellent Services Ltd., Mibale Farm, Liquidity Service Ltd., Clayton Marketing Ltd., M/S Rashtas (T) Ltd., Malegesi Law Chambers (Advocates), Kiloloma and Brothers na KARNEL Ltd.

Aidha, ukaguzi umebaini kwamba kati ya fedha hizo, kiasi cha Shilingi 90,359,078,804.00 zililipwa kwa makampuni kumi na tatu (13) ambayo yalitumia kumbukumbu, nyaraka na hati zilizo batili na za kugushi. Hivyo, Makampuni hayo hayakustahili kulipwa chochote. Makampuni hayo ni: Bencon International Ltd. of Tanzania, VB & Associates Company Ltd. of Tanzania, Bina Resorts Ltd. of Tanzania, Venus Hotel Ltd. of Tanzania, Njake Hotel & Tours Ltd., Maltan Mining Company Ltd. of Tanzania, Money Planners & Consultants, Bora Hotels & Apartment Ltd., B. V. Holdings Ltd., Ndovu Soaps Ltd., Navy Cut Tobacco (T) Ltd. of Tanzania, Changanyikeni Residential Complex Ltd., Kagoda Agriculture Ltd.

Aidha, ukaguzi umeendelea kubaini kuwa Makampuni tisa (9) ambayo yalilipwa jumla ya Shilingi 42,656,107,417.00 hayakuwa na nyaraka za kuonyesha stahili ya malipo na hivyo kuwafanya wakaguzi washindwe kuhakiki uhalali wa malipo hayo. Makampuni hayo ni: G&T International Ltd., Excellent Services Ltd., Mibale Farm, Liquidity Service Ltd., Clayton Marketing Ltd., M/S Rashtas (T) Ltd., Malegesi Law Chambers (Advocates), Kiloloma and Brothers na KERNEL Ltd.

Wakati huo huo Makampuni mawili, yaani, Rashtas (T) Ltd na G&T International Ltd., kumbukumbu zake za usajili katika daftari la Msajili wa Makampuni nchini hazikuweza kupatikana.

Uamuzi wa Rais

Baada ya kuipitia Taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Serikali na ya Mkaguzi wa Nje, yaani, Kampuni ya Ernst and Young, Mhe. Rais amesikitishwa na kukasirishwa na taarifa ya kuwepo vitendo vya ukiukwaji wa makusudi wa sheria, kanuni na taratibu za uuzaji wa madeni ya nje vilivyofanywa katika taasisi muhimu na nyeti kama vile Benki Kuu. Kwa hiyo, ameamua kuwa hatua za kisheria na kiutawala zichukuliwe dhidi ya makampuni na watu waliohusika na vitendo hivyo viovu.


Kwa ajili hiyo Rais ameamua yafuatayo:-

1. Ametengua uteuzi wa Dkt. Daudi A. Balali kuwa Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania.

2. Ameagiza Bodi ya Wakurugenzi ya Benki Kuu ikutane mara moja kujadili taarifa ya ukaguzi na kuchukua hatua zipasazo za kinidhamu dhidi ya Maofisa wote wa benki, walio chini ya mamlaka yake waliohusika na kusababisha hasara hii kwa taifa.

3. Shughuli za ulipaji wa madeni katika Akaunti ya EPA zisimamishwe mara moja mpaka hapo taratibu za uhakiki na utaratibu mpya utakapotengenezwa.

4. Rais amewaagiza; Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Inspekta Jenerali wa Polisi na Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa, kuchunguza na kuchukua hatua zipasazo za kisheria kwa makampuni na watu waliohusika na uhalifu huu. Rais amewataka watumie ipasavyo mamlaka na madaraka waliyo nayo kwa mujibu wa sheria. Aidha, amewataka wakamilishe kazi hiyo katika kipindi cha miezi sita. Amemuagiza Mwanasheria Mkuu wa Serikali awe kiongozi wa kazi hii. Amewataka wahakikishe kuwa fedha zilizolipwa isivyo halali zinarudishwa.

5. Rais pia amemtaka Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kushirikiana na kuwasaidia watendaji wakuu hao wa vyombo vya dola katika kufanikisha jukumu lao hilo. “Watu wengine wenye taarifa za ziada pia wazitoe kwa Timu ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG) na wenzake”.

6. Kutokana na hatua ya kutengua uteuzi wa Bwana BALALI, Mhe. Rais amemteua Prof. BENNO T. NDULU (Naibu Gavana) kuwa Gavana Mpya wa Benki Kuu. Halikadhalika, amemteua Dkt. ENOS S. BUKUKU (Katibu Mkuu – Miundombinu) kuwa Naibu Gavana wa Benki Kuu (Fedha na Uchumi). Pia amemteua Ndugu Omari Chambo kuwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Miundombinu. Uteuzi huu unaanza mara moja.
(Phillemon L. Luhanjo)
KATIBU MKUU KIONGOZI

IKULU,
DAR ES SALAAM
09 Januari 2008

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

Kuna Maoni 36 mpaka sasa

  1. Ooooohhhh.... Sijui uanzie wapi....Milioni tisini alfu, na kadhaa, pesa za kitanzania sawa na dola za kimarekani, milioni sabini na tano, kama sijakosea zimelipwa kinyume na Sheria.
    quote
    idha, ukaguzi umebaini kwamba kati ya fedha hizo, kiasi cha Shilingi 90,359,078,804.00 zililipwa kwa makampuni kumi na tatu (13) ambayo yalitumia kumbukumbu, nyaraka na hati zilizo batili na za kugushi.
    unquote


    Shule ngapi zingejeka kwa fedha hizo ?
    Hospitali ngapi zingejengeka kwa fedha hizo ?
    Bara bara ngapi zingejengeka kwa fedha hizo ?
    Na mengine mengi tu ?
    Tunategemea sheria kali kuchukuliwa dhidi ya huu ubadhirifu wa mali ya umma, unprecedented Crimes in History of Tanzanian....


    By Mchangiaji

    ReplyDelete
  2. Wapendwa
    Ninachoshangaa ni kuwa mbona wale watuhumiwa nambari moja hawakutajwa?, au tayari wameshafanya namna?

    Nimeshangaa sana kuona wale key suspects waliosababisha hofu na malalamiko makubwa kutoka kwa watanzania, ingawaje tuna imani kuwa wao ni wahusika wakuu,hawajatajwa bwana
    Sounds funny and ridiculous

    ReplyDelete
  3. Sasa kama kuna ukikwaji wa mambo hapo benki kuu mboni manaibu gavana wao hawajaondolewa? ama hawa ndio walioteuliwa juzi juzi ili kuandaliwa kuchukua nafasi ya bilali? kama hivyo ndivyo basi hiki ni kiini macho kwani Rais alikuwa anajua anafanya nini hata kabla ya ukaguzi wa mahesabu haujaisha.

    Mwisho kabisa mbona taarifa hii ni ya EPA tu Twini tawa ni aje? walivuta pia kina Bilali?

    na Je kwa akina bilali ndio mwisho? kwenye madini je mbona hajawachukulia hatua wale waliongia mikataba mibaya kuusu madini?

    ReplyDelete
  4. Mhhh!! Long overdue...Sasa tuone hao 22 companies kama watakamatwa...Mungu Ibariki Tanzania!

    ReplyDelete
  5. huo mshiko walio KWIBA unakuaje? utarudi au ndio CHANGA???

    ReplyDelete
  6. Changa la macho

    ReplyDelete
  7. Changa la macho hilo mwanawane........

    ReplyDelete
  8. Hongera JK, lakini naona kuna watu wanatolewa chambo humu... this issue goes higher to the last gov. top leaders...

    ReplyDelete
  9. Ya Balali kuachishwa kazi: Mpaka ripoti hii inatayarishwa na Ofisi ya Rais, Ofisi hiyo hiyo haikuwa na uhakia kuwa Balali kajiuzulu (Maura Mwingira na Salva Rweyemamu na hata Waziri Meghji hwakuwa na taarifa ya kujiuzulu kwa Balali…eti walikuwa wanakusikia tu kutoka vyombo vya habari!

    Balali alijiuzulu kitambo. Kwa nini Rais angoje ripoti yake itoke ndipo amwachishe kazi Balali?

    The ripoti smells fishy!

    Ni nani kamchagua Mkaguzi Deloitte and Touche aliyegundua tatizo hilo?

    Ripoti haisemi kwa nini kulikuwepo na kutoelewana baina ya Benki Kuu na Mkaguzi Deloitte and Touche?

    Serikali ilimuagiza Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) atafute kampuni ya kimataifa ya ukaguzi ifanye kazi hiyo kwa niaba yake.

    Ikiwa Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali alishindwa kuifanya kazi hiyo, kwa nini baada ya kuipata kampuni ya Ernst and Young, kampuni hiyo hiyo ilimpelekea ripoti huyo aliyeshindwa eti aipitie kabla ya kuiwasilisha kwa Rais?

    Makampuni yaliyogusha services na kulipwa, na kadhalika, yametanjwaWatuhumiwa wametajwa. Ni nani atakayetuhakikishia kuwa ripoti ya Rais aliyotoa ni sahihi kulingana na ugunduzi wa kampuni ya Ernst and Young?

    Isije Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali au Ikulu au wote pamoja wame-sex up the report ionekane nzuri by doctoring it!

    ReplyDelete
  10. sisi watu wa ulaya hatuna muda wa kusoma uzushi kibao kama huu,michuzi usituweke mambo marefu kama haya kwani hatuna muda wa kusoma...yote katakata.

    ReplyDelete
  11. Hiyo taarifa imetolewa ofisi ya Rais baada ya kusoma ripoti ya mkaguzi wa nje, na Rais ametoa maamuzi kwa wote waliohusika warudishe na wachukuliwe hatua za kisheria. Bado mnasema changa la macho? Sasa nyie mnaojua zaidi ya huyo mkaguzi alichosema pelekeni taarifa zenu kwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali kama taarifa inavyosema ili hatua zichukuliwe. Au zitoeni humu kwenye blogu mkiwa na ushahidi tuzifikishe kwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali ili sheria ifate mkondo wake.

    Mnataka nini sasa?

    ReplyDelete
  12. jamani tusubiri tuone, angalau kuna kitu kinafanyika.

    Haya maelezo kuwekwa hadhari peke yake si kazi ndogo, anaweza toka mtu roho hapa!

    JK jitahidi pole pole utafika usiogope maana wizi umezidi, unaona mpaka ughaibuni watu wanang'ang'aniwa na wazee kwa madili ya ajabu ajabu.

    Watanzania tujifunze kuacha wizi jamani tunatia aibu!

    Bora kuuza mihadarati kuliko wizi wa mali ya umma, mwishoni taifa zima linaumia.

    ReplyDelete
  13. Nadhani hii ni hatua nzuri kwa namna fulani. Lakini nina hofu kubwa kwamba yawezekana ni hatua iliyozungukwa na wingu la kisiasa kwa kiwango kikubwa. Kwani kuna mashaka yatokanayo na mambo mengi hapa:
    1. Balali amekuwa kwenye wadhifu huo kwa muda mrefu kuliko utaratibu wa BoT (ingawa labda si utaratibu wa kesheria). Lakini swali ni kwamba kwa nini mtu ambaye inawezekana ni Gavana mbovu kuliko watu wote waliowahi kushika nafasi hiyo ashike nafasi hiyo kwa muda mrefu kuliko mtu yeyote? Namna pekee mbavyo ingewezekana ni kama utendaji wake ungeshabihiana na hali halisis. Haikuwa hivyo.

    2.Uozo wa Balali ulienea mpaka mitaani Manzese. Kwa nini Mheshimiwa Rais anakuja kukasirishwa leo baada ya uozo huo kumfikia kila mtu. Uozo wa Balali haukuhitaji serikali kuhangaika hivyo ili kumvua madaraka. La hasha!

    3. Utendaji kwenye serikali yetu na kwenye mashirika ya umma unanipa wasi wasi sana. Kwa sababu inaelekea hakuna utaratibu wa usimamiaji mambo vizuri. Bado tunafanya kazi kama zima mote. Mpaka janga litokee na madhara makubwa yapatikane ndio magari ya zima moto yanaanza kupiga kelele mitaani!!! Inakuaje matatizo yanatokea kwenye serikali yanaingia kwenye kumbi za siasa na majukwaa mitaani na yanazunguka mpaka Manzese kabla msimamiaji mkuu wa maswala hayo hajapata habari??? Hii ni hatari kwetu na hata hao tunaowateua bado ni hatari tu kwani inaonyesha Tanzania kila mtu anajifanyia atakavyo tu bila usimamizi - kwa maana nyingine mfumo ndio una matatizo. Mtu yeyote akiwekwa hapo atajaribiwa tu na mfumo ulio huru bila usimamizi.

    4. Je maswala haya ya hawa watendaji wa Mkapa kama akina Pr. Mahalu waliovurunda kwa wazi hivi yataishia wapi. Watu hawa wasingeweza kufanya uozo huu bila ofisi kubwa kuhusika. Tunahitaji kusikia malelezo ya uozo huu kutoka kwa Mkapa. Balali ni mtu wa Mkapa. Mahalu ni mtu wa Mkapa. Wajinga wajinga wengi tu wanfanya uozo kwa kofia ya Mkapa chini ya maelezo ya Rais Kikwete kwamba hatafuatilia mambo ya Mkapa.

    ReplyDelete
  14. Mbona hela ndogo hizo... Nyingine ziko wapi? Anaye wapongeza Ernst and Young ni tahiri, ukweli wa mambo ni kwamba consultancies kama hizo zikiletwa ni kuja kufanya "damage control" Kuna kitu zaidi kinahitajika hapa zaidi ya ripoti ya uongo na kweli hii...

    ReplyDelete
  15. NAOMBA BABU SEYA AFUNGULIWE ... HAKUFANYA MAKOSA WALIOFANYA MAKOSA NI HAWA NA WAFUNGWE MILELE

    ReplyDelete
  16. MKAPA MBONA HAYUMO????????

    ReplyDelete
  17. HUUUUUUUUUUU NDIYO UMUHIMU WA WAPINZANI

    NA TWIN TOWERS VIPI??

    ILA KUNA MENGI HAYAJASEMWA KATIKA REPORT HIII

    NA KUNA WATU WENGI WANAHUSIKA

    ReplyDelete
  18. Hamna Jipya mnalosema kazi kulalama tu, humu ndani pia wako wasiolipa kodi, wezi wa mali ya umma na wazembe wanaotumia muda wa kazi kublog zaidi ya masaa 2. Sasa mnanalalama nini? Kama mnayo ripoti yenu yenye ushahidi zaidi ya huo na nyie itoeni na mtuambie mtachukua hatua gani.

    Mlitaka Raisi afanyaje? Semeni!
    Mlikuwa mnaingojea kwa hamu hiyo ripoti na imetoka bado mnalalamika. Hivi mmeshafanya jambo gani kubwa zaidi ya kulalamika kila siku.

    MVUA IKINYESHA MNALALAMIKA, JUA LIKIWAKA MNALALAMIKA! Mnatakaje sasa, ingieni nyie mkaifanye hiyo kazi. Waswahili kwa maneno kudadadek!

    Kazi kuchonga tu, tunataka hiki tunataka kile, wengine hamna lolote mnalochangia kwenye uchumi wa nchi si kwa kodi ya mshahara wala ya biashara!

    ReplyDelete
  19. Haya sasa wanadai mambo yako nje . watuhumiwa wako wapi ? watajwe na hatua zichukuliwe kama JK kakasirishwa sana na hicho kitendo . Tumechoka na maripoti marefu na maneno ya sio kuwa na mwisho . Action speak louder than words... JK ukumbi ndio huu Shine! Shine !Shine !

    ReplyDelete
  20. Ok vizuri hata kama ni kiini macho it is a start sasa bado twin towers vp? na madini?

    ReplyDelete
  21. jamani wadanganyika! hata report, wewe utamletaje mtu kutoka nje anayekudai kuja kukukagua wewe? Kwani lazima uwe taahira kushindwa kuelewa haya? Au kwa vile vingunge wa sasa wa bot ni watoto wa ex-vingunge wa bot wa zamani ambao wameiba sasa inabidi waendelee kufichwa! this is just bullshit

    ReplyDelete
  22. Hapo imebidi Balali ajitoe sadaka. Kwa ufupi huu ni UZUSHI mtupu

    ReplyDelete
  23. Hii si aibu ya BOT.ni aibu ya watanzania wote mbele ya dunia.wajameni sipati picha kazi inafanywa baada ya watu wa kawaida kupiga kelele na shinikizo hivi serikali inafanya kazi kweli?miaka yote hiyo wakaguzi wa hesabu wanajizungusha KWENYE VIYOYOZI TU.Watanzania!!!!!!

    ReplyDelete
  24. Haya sasa PCB kazi kwenu. Mmeletewa hadi mlangoni. Majina ya makampuni yaliyochukua pesa hayo hapo. Na mmeambiwa wazi kuwa walighushi (navyoelewa mimi hii ni fraud and fraud is a criminal offence). Tunasubiri kuona jinsi wenye makampuni hayo watakavyokamatwa na kuwa prosecuted na jinsi watakavyofilisiwa kurudisha hela ya kujengea shule, hospitali na barabara za walalahoi. Mkishindwa tena hapa basi mfunge tu hizo ofisi.

    ReplyDelete
  25. WANAOKULA WALE TU.KAMA WANAONA HALI ZA WATANZANIA WALIO WENGI NAAMINI HII HAKI WATAILIPA MACHONI PA MUNGU.NA BADO MAENEO NI MENGI SANA.

    ReplyDelete
  26. HAINIINGII AKILINI KWA NCHI MASKINI KAMA HII BILIONI 90 ZIYEYUKE NA RAIS WA WAKATI HUO HANA HABARI. LAZIMA ALIHUSIKA KWA NJIA MOJA AMA NYINGINE!!!

    ReplyDelete
  27. They say u can lead horse to the water but you cant get them to drink it, he sure has shown resilience to the ungrateful Tanzanians, I will remember his reign by the history on our economic growth which has never been as high before since independence but disgustingly we let the real Wafisadi sit on it, and blame to the dignified and hardworking one? But hey time will soon tell how down hill our economy will go and then we can have a real thing to blame on , to not even be able to afford a little maharage, and fuel prices keeps on souring high with no rain in sight , then will think about how unfair to Ballali people have been. To be honest that’s not even an office to worth his time, it’s like a market – you worth more, enjoy your retirement, I dare to say a proper office, and I salute you!!!

    ReplyDelete
  28. Du inasikitisha sana, tusubiri tusikie kama kuna kitu kitaendelea . Labda upinzani washikilie bango tena , maana kwahili ni upinzani ndio wametusaidia , Serikali ilibisha kabisa.
    Mimi sijui mwisho wetu watanzania kwani tunashindwa kabisa kujisimamia wenyewe kwenye shughuli zetu, kila mahali ni wizi na rushwa na serikali inajua fika ila inakaa kimya hadi waone funza watoka ndio wanashituka , wapinza endelea kuisaidia Serikali labda kwa kelele zenu tutafika.

    ReplyDelete
  29. Watanzania tunabebeshwa mizigo ya kulipa kodi kubwa , kumbe watu wanachota kiulaini.
    Tunasubiri Madini na Richmond.

    ReplyDelete
  30. Mimi naona Raisi hakuwa na haja ya kuwaachia PCB, IGP..... angeamuru mara moja waharifu kukamatwa kwani wanajulikana, na yeye anawajua kama yeye hausiki.
    Hili ni changa la macho.
    Subiri muone.

    ReplyDelete
  31. Nashangaa watu mnalaumu hizo hela zenyewe zote kwanza hazikutoka tanzania. Baada ya TZ kuonyesha kusikitishwa na uamuzi wa kutofutiwa madeni yote UK iliisaidia kwa kuipa extra £5 million a month kwenye annual aid yake mpaka deni hili lilivyoisha.

    Ukweli ni kuwa Bongo imejaa na hela za misaada na inaonekana ndio maana hizi hela zililiwa maana walichoitaji kuonyesha ni uthibitisho kuwa bado nchi inadaiwa kupewa msaada toka UK.

    Na FYI hii ripoti ilifanywa kwa sababu ya pressure kubwa TZ iliyopata toka UK kwaiyo msitegemee ripoti za Twin towers wala madini. Ukweli ni kuwa kila mtu bongo mwizi na mimi nikienda ntaiba vilevile.

    ReplyDelete
  32. Habari kutoka ndani kabisa zinasema wengi wa watuhumiwa hawa walikuwa wanafahamu kitakakchotokea na tayari walishahamisha mali na fedha zao hapa nchini na wako ughaibuni sasa hivi kwa 'matibabu' mpaka hapo joto litakavyotulia kama lile la Ditopile na wengine wengi

    ReplyDelete
  33. Huu ni upuuzi mtupu, ndio maana Tanzania haiendelei, hizi pesa zingefanya mambo mengi sana kwa manufaa ya wananchi wote lakini kutokana na tamaa ya wachache nchi yetu itazidi kurudi nyuma kila siku, anayetegemea kuwa Balali atakamatwa aendelee kuomba, wahusika ni wengi na wengineo bado wapo serekalini, wanyonge walie tu na wenye nafasi waendelee kuiba...

    ReplyDelete
  34. Fungueni macho watanzania muone...
    account iliyochotwa ni ya serekali, hata Governor mwenyewe haigusi bila mkono wa serekali yenyewe... fungueni macho...

    ReplyDelete
  35. Hilo changa la macho. balali amejiuzulu muda mrefu. kikwete anasema amemfukuza kujipatia umaarufu wa kisiasa

    ReplyDelete
  36. MIE NILIFKIRI RAIS ANGETEUA TEAM MPYA NA GAVANA MPYA,sasa KAma Gavana alichota pesa si inamaana hata NAIBU GAVANA CHEZO ANALIJUA.NA maana kwamba nae yupo ktk uchotaji.VIPI KUHUSU yale MAJENGO MAWILI MBONA HATUJAONA MATOKEO YAKE???? AU REPORT PAPER ZAKE ZIMEUNGUA???? AU ZIMECHAMBIWA?

    ReplyDelete

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...