
UJENZI WA NYUMBA ZA ASKARI POLISI WATIWA SAINI
Na Anna Nkinda & Majaliwa Mbogellah,
Mradi wa ujenzi wa nyumba za Polisi Kilwa Road jijini Dar es Salaam, Ziwani-Unguja na Wete –Pemba umetiwa saini leo jijini Dar es Salaam katika eneo la Kituo cha Polisi Kilwa Road mbele ya Mkuu wa Jeshi hilo Said Mwema , Mkurugenzi wa Mfuko wa Hifadhi ya Taifa (NSSF) Dr. Ramadhani Dau na Makandarasi walioshinda tenda ya ujenzi wa nyumba hizo.
Dr. Huba Nguluma, ambaye ndie kiongozi wa mradi huo, akisoma taarifa fupi iliyoandaliwa kwa ajili ya utiaji saini na ukabidhi wa ujenzi kwa makandarasi hao, alisema tatizo kubwa linalowapata watu wanaoishi katika nchi zinazoendelea ni upatikanaji wa makazi bora hivyo tatizo hilo haliwezi kubadilika kama hakutakuwa na ushirikishaji wa kuhakikisha kuwa makazi ya wananchi yanaboreshwa.
Dr. Nguluma aliongeza kusema kuwa chuo Kikuu cha Ardhi Dar es Salaam kilifanya kazi ya kubuni michoro ya majengo ya nyumba za Askari Polisi ambayo ilipitiwa na Jeshi hilo na kufanyiwa mapendekezo,Jeshi la Polisi lilichukua jukumu la kutafuta fedha kupitia Mfuko wa hifadhi ya Jamii (NSSF) ambao umekubali kugharamia awamu ya kwanza kwa kufadhili ujenzi wa nyumba za maghorofa 24 Kilwa Road Barracks Dar es Salaam kwa ajili ya familia 96, maghorofa 3 Ziwani Barracks Unguja kwa ajili ya familia 12 na Maghorofa 3 Wete Pemba kwa ajili ya familia 12 .
Aidha Nguluma aliendelea kusema kuwa mradi huo umegawanywa kwenye lots tano ili kurahisisha ujenzi kwa kutumia makandarasi tofauti ambao walileta ushindani katika gharama , katika kufanikisha ujenzi wa nyumba hizo kwa muda mfupi na ufanisi zaidi alisema lot moja itajengwa Pemba , lot mbili zitajengwa Ziwani Barracks Unguja na lot tatu, nne, na tano zitajengwa Kilwa Road Barracks Dar es Salaam.
Hivyo ufanisi huo utategemea ushirikiano mkubwa kutoka Mfuko wa Hifadhi ya Jamii, Polisi na Makandarasi waliopewa tenda hizo.
Mkurugenzi wa Mfuko wa Hifadhi ya Taifa Dr. Ramadhani Dau alisema ujenzi wa nyumba hizo unazingatia mkataba wa kujenga nyumba za Askari Polisi uliosainiwa na Mkuu wa Jeshi la Polisi Saidi Mwema ofisini kwake na kuwa NSSF itagharamia ujenzi wa nyumba hizo kwa awamu ya kwanza na pia itagharamia kwa awamu ya pili pindi taratibu za kiofisi zitakapokamilika.
Dr. Dau aliongeza kusema kuwa makandarasi waliopewa tenda ya kujenga nyumba hizo za Askari wamepatikana kupitia ushindani uliozingatia uwezo wa kazi na ufanisi wa makandarasi hao hivyo hapatakuwepo ucheleweshaji wa malipo kwa makandarasi wataofanya kazi hiyo kwa kuzingatia mikataba waliotiliana sahihi leo.
Dr. Dau aliwataja makandarasi waliopewa tenda ya ujenzi wa nyumba hizo za Askari kuwa ni MCC20 ambao watajenga majengo sita Kilwa Road Barracks Dar es Salaam, Kampuni ya Ujenzi Aleco ambao watajenga ghorofa 9 Kilwa Road Barracks, na Group International itajenga block 9 ambapo kila block zitakaa familia nne.
Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini Said Mwema akiushukuru uongozi wa Mfuko wa Hifadhi ya Taifa , Mkuu wa chuo Kiuu cha Ardhi Dar es Salaam zamani kikiitwa UCLAS, Makamisha na makandarasi alisema jumla ya maghorofa 282 yatajengwa kufuatia kauli ya Mh. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Zanzibar Jakaya Kikwete kwa Jeshi la Polisi nchini.
Saidi Mwema alisema kuna mwingiliano mkubwa kati ya maendeleo ya kiuchumi, kijamii na na kuwa mahusiano hayo yanawewza kuboresha huduma za kijamii bila hata kutumia bunduki kama Askari Polisi wanaweza kuboreshwa kwa kupatiwa huduma mhimu katika maisha yao ikiwa ni pamoja na sehemu nzuri za kuishi.
IGP Mwema alisema ujenzi wa nyumba hizo utawapa moyo Askari Polisi kufanya kazi kwa bidii na maarifa na utawahakikishia usalama wa maisha yao kwani ni kipindi kirefu Askari Polisi wamekuwa wakiishi nyumba zisizo na hadhi hivyo amewaomba makandarasi waliopewa tenda hizo kujenga nyumba hizo kwa kiwango kinachostahili na kuzingatia mkataba uliowekwa wa kuhakikisha kuwa ndani ya mwaka moja wawe wamemaliza ujenzi wa nyumba hizo.
Aidha, askari Polisi waliohudhuria sherehe hizo walilishukuru Jeshi hilo na serikali ya awamu ya nne kwa kuwakumbuka na kuamua kuwajengea nyumba bora za kuishi jambo ambalo litaimarisha maisha yao na familia zao. Nao baadhi ya wananchi waliokusanyika kujionea utiaji saini wa ujenzi huo walifurahia ujenzi wa nyumba hizo na kusema kuwa wanaamini askari wengi wanaoishi uraiani watapata makazi katika nyumba hizo jambo ambalo litaimarisha usalama wao na familia zao.
Ujenzi wa maghorofa ya Polisi unafuatia utafiti uliofanywa mwezi wa tano mwaka 2006 uliozingatia hali halisi ya makazi ya Polisi na kutoa mapendekezo ya namna ya kuboresha makazi hayo kama kigezo mojawapo cha uboreshaji wa utendaji wa Jeshi la Polisi.
Ujenzi huo utagharimu bilioni 20 za kitanzania kwa awamu zote mbili kwa maghorofa 60.


Hilo ni jambo zuri na la kufurahisha ila tu jee polisi hawa watawajibika wakishalala katika nyumba nzuri au ni yaleyale ya rushwa kuendelea.Labda hizo nyumba zitawapa moyo wa kazi.Ulaya hakuna kota za polisi hilo walijuwe.Wenzao wanajikodia wenyewe na wanawajibika.Wawajibike mwaka mpya.
ReplyDeleteMmmh...!Wataishi kwenye nyumba za bure,watataka rushwa,watanyanyasa wafanyabiashara wadogowadogo(wale wanaotafuta hela ya siku tu)watanyanyasa kina mama ntilie,watawadai vitambulisho kwa viboko wazalendo na hapo pembeni anapita mgeni na haulizwi kitu na orodha haiishii hapa...!
ReplyDelete