Serikali za Tanzania na Marekani Jumapili ilopita zimetiliana saini mkataba wa msaada wenye thamani ya mabilioni ya fedha ambao utatekelezwa chini ya makubaliano ya Millenium Challenge Compact (MCC).
Sherehe ya kuvutia ya utiaji saini wa makubaliano haya zilifanyika katika viwanja vya Ikulu ya Dar Es Salaam. Rais George W Bush, aliyetembelea Tanzania, alitia saini kwa niaba ya Marekani wakati Mheshimiwa Rais Jakaya Kikwete alitia saini kwa niaba ya Tanzania.
Msaada huu unatolewa na Serikali ya Marekani kupitia shirika lake la Millennium Challenge Corporation. Utatekelezwa chini ya akaunti iitwayo Millennium Challenge Account (Tanzania) na mkataba wa utekelezaji huu ndiyo unaitwa Millennium Challenge Compact (MCC).
2.Lengo Kuu la MCC
Lengo kuu la MCC ni kuchochea ukuaji wa uchumi, kuinua kipato cha wananchi, na kuwaletea maisha bora kupitia uimarishaji wa njia za usafiri na usafirishaji, pia kupitia katika uboreshaji wa miundombinu ya nishati na maji.
3. Thamani ya MCC
Thamani ya msaada utakaotolewa chini ya mkataba huu wa MCC ni dola za Marekani milioni 698. Sehemu kubwa ya kiasi hiki itaingizwa katika miradi ya usafirishaji kwa maana ya ujenzi wa barabara, ikifuatiwa na sekta ya nishati, na hatimaye sekta ya maji.
4. Miradi itakayotekelezwa chini ya MCC
(a) Barabara zitakazojengwa ni:
(i) Tanga-Horohoro (kilomita 68)
(ii) Tunduma-Sumbawanga (kilomita 224)
(iii) Songea-Namtumbo (kilomita 61)
(iv) Peramiho-Mbinga (kilomita 78)
(v) Kilomita 35 za barabara mbali mbali za Pemba
(vi) Uwanja wa ndege wa Mafia
(b) Nishati (Umeme)
(i) Kutandaza nyaya za umeme baharini kutoka Dar Es Salaam hadi Zanzibar
(ii) Ujenzi wa chanzo cha umeme wa maji kwenye Mto Malagarasi kwa ajili ya miji ya Kigoma, Uvinza na Kasulu
(iii) Ukarabati za vituo vya umeme na usambazaji umeme katika mji ya Mbeya, Iringa, Dodoma, Morogoro, Tanga na Mwanza
(c) Maji
(i) Upanuzi wa mitambo ya kusukuma maji Ruvu Chini kwa ajili ya jiji la Dar Es Salaam
(ii)Udhibiti wa upotevu wa maji katika jiji la Dar Es Salaam (inakadiriwa kuwa kiasi cha asilimia 60 ya maji yanayoingia katika jiji la Dar Es Salaam yanavuja na hivyo kupotea)
(iii) Kuongeza upatikanaji wa maji katika mji wa Morogoro
5. Usimamizi wa Utekelezaji wa Mkataba wa MCC
Chombo maalum tayari kimeundwa na Rais kwa ajili ya kusimamia utekelezaji wa MCC. Chombo hiki kinachojitegemea kitajulikana kama MCA-T. Chombo hiki kiliundwa rasmi na Rais kupitia GN Na. 202 ya Septemba 21, mwaka jana, 2007. Chombo hiki tayari kimeanza kazi. Ajira katika ngazi ya wakurugenzi na baadhi ya maofisa waandamizi imekwishakukamilika na zoezi linaendelea. Mtendaji mkuu wa MCA-T ni B.S. Mchomvu.
6. Ratiba ya Utekelezaji wa MCC
Baada ya kutiwa saini kwa MCC sasa unafuata utekelezaji. Kazi inayofanyika sasa, kama itakavyokuwa kwa sehemu kubwa ya mwaka huu wa 2008, ni maandalizi ya utekelezaji. Itaandaliwa michoro (designs) ya miradi, zitaandaliwa taarifa za mazingira, zitaadaliwa nyaraka za kuwania kazi zitakazofanyika chini ya mkataba huo, zitatengenezwa tenda na zitachambuliwa, kabla ya hatimaye kuteua wakandarasi.
Bila shaka, juhudi zitafanyika ili kuweza kuzikamilisha kazi hii ya maandalizi katika kipindi kifupi iwezekanavyo. Hata hivyo, imepangwa kuwa tarehe rasmi ya MCC kuanza kipindi cha miaka mitano ya utekelezaji wa miradi iwe Septemba, mwaka huu, 2008 na utekelezaji rasmi wa miradi uanze mwishoni mwa mwaka 2008 ama mwanzoni mwa 2009.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

Kuna Maoni 12 mpaka sasa

  1. VYOVYOTE ITAKAVYOKUWA KUPITIA MSAADA HUO AU FUNGU LOLOTE, SERIKALI KUPITIA TANESCO NA EURA(INGAWA SIJAONA UTETETEZI WAO KWA WATEJA)IHAKIKISHE KUWA GHARAMA ZA KUUNGANISHIWA UMEME NA KUTUMIA UMEME ZINATEREMSHWA.

    NI KICHAA TU ANAYEWEZA KUPANDISHA GHARAMA KUFIKIA KIWANGO CHA SASA WAKATI MAISHA AU HATA TUSEME MISHAHARA YA WATU HAIJAPANDA HIVYO!!
    VINGINEVYO RUHUSUNI MAKAMPUNI YA UGAVI WA UMEME YAMWAGIKE KAMA YA SIMU ZA MKONONI MUONE NI JINSI TANESCO WATAKAVYOPIGA MIAYO OFISINI KUSUBIRI BILL ZA IKULU NA ZA KWAO WENYEWE!

    YAANI KURA YANGU NA FAMILIA YANGU WOTE HATA KAMA NI 0.00003 YA KURA ZOTE TUTAWAPA CHAMA CHOCHOTE NA SIO CCM KUTOKANA NA HILI SUALA LA UMEME!

    NO FREE MARKET SYSTEM IN SUCH A MONOPOLISTIC MARKET OF TANESCO!

    ReplyDelete
  2. hmmm,kweli baniani mbaya kiatu chake dawa.

    ReplyDelete
  3. Maendeleo ya sehemu yoyote ile huhitaji Miundo mbinu imara kama barabara, nishati thabiti na watu makini. Serikali ya Marekani imelenga katika kuendeleza hizo sekta japo ya kujenga watu makini haipo hapo kwa hiyo inabidi tupeane discipline sisi kwa sisi. Watanzania tuwe wakali hizi fedha zisijeishia matumboni mwa watu, tuwafanye woote wanaohusika na hizi fedha wawe accountable for their actions. kwa hili tutafika tunapotaka kufika.
    Wahandisi na wadau wa uhandisi jiandaeni kwa kazi zijazo mbele yenu,muwe makini katika utekelezaji wa huu mradi maana nyie ndio mna dhamana ya barabara bora, mifumo ya maji bora zaidi, na mifumo ya umeme bora zaidi. Nyinyi ndio mnawabeba watanzania kwa uzembe wenu mtalaumiwa na watanzania tafadhali kuweni makini katika hili. Simameni Imara katika hili kuonyesha tofauti na huko tuliko toka.Tambueni kwamba unapopokea rushwa ili kupunguza ubora wa barabara and kukubalisub standard equipments unawahujumu watanzania na kuwaneemesha watu wachache wenye uchu wa fedha wasio na uchungu wala kupenda maendeleo ya watanzania. Mmeyaona ya Richmond kuweni makini.
    Mwisho naishukuru serekali ya marekani kwa msaada huu(japo sijafahamu kwa hakika nini watapata as return) na focus ya Bush kwenye malaria and ARVs.

    ReplyDelete
  4. Raisi Bush kama kweli anatujali pesa hizi asingetupa sisi bali angewalipa makontrakita hukohuko na sisi kutukabithi miradi iliyokamilika, vinginevyo yatakuwa ya barabara ya Sam Nujoma, pesa zililiwa na pande mbili husika sasa hakuna wa kumdhibiti mjenzi, pamoja na akina Masanja kuiombea lakini imeshindikana.

    ReplyDelete
  5. Du bro Michu jamani, Mbona wanatusahau sana watu wa Kilimanjaro? Barabara za kilimanjaro hazifai jamani Vumbi kila kona ukitoka ugaibuni kama hivi ni noma tupu yani kwani ukifika maeneo ya Himo kuna barabara Moja inaelekea huko kilema Juu kuliko na Chuo cha Ualimu Mandaka pamoja na St. James seminari Hadi Kilema Hospital hiyo barabara Bro michu huwa ni mbaya sana jamani wangetufikiria angala hata kalami kidogo ili kupunguza tu vumbi.

    Umetusifia kwa usafi Bro michu ni kweli na hiyo barabara huwa ni safi sana ila wakati wa kiangazi wakina dada hatuna haja ya kutumia poda kwani vumbi ni poda tosha. Wakati wa tope ndio balaa nyingine kwani du gari zinayumba bro unatamani kushuka utembee kwa miguu.

    Dada kutoka ughaibuni.

    ReplyDelete
  6. Asante Sana Kaka Milaikomchuzimix Kwakweli Hapo Ndio Ninapokupigia Deki aka Kukufagilia Kwa Kuweza Kutuanikia Ni Jinsi Gani Hio Mchovumond Itakavotafuna Hizo Hela.Kwa Ujumla Kama Kawaida Yetu Tunaishia Kuona Maandishi Tu Hivo Tunaitakia Hio Mchovumond Utafunaji Mzuri Wa Hizo Pesa Huku Sisi Kama Kawaida Tuko Pembeni Tunaangalia.Endelea Na Kazi Nzuri Unazofanya Kwa Niaba Ya Watanzani kaka Laikomchuzimix

    ReplyDelete
  7. HAYA ANDAMANENI SASA!!

    ReplyDelete
  8. NDUGU ZANGU WATANZANIA JE TUFANYE NINI HILI VIONGOZI WETU WA SERIKALI WATUONEE HURUMA SISI RAIA NA MAISHA MAGUMU TUNAYOPATA ? HIZI PESA TUNAOMBA ZITUMIKE INAVYOTAKIWA KWA MARA YA KWANZA TUPENI MISAADA MNAYOPEWA.WATTO MASHULENI WANAKAA CHINI,VIJIJINI MAJI MASAFI HAKUNA TUSAIDIENI SERIKALI SISIS NDIO TUNAOJENGA NCHI.

    ReplyDelete
  9. tatizo bongo ni utekelezaji mfano kama huyo mch**vu ni mchovu kweli kweli sijui nani anawapendekeza hawa watu wamezoea copy n paste miradi hii haitekelezeki na speed yao huwa ndogo sana?sina hakika kama changes za utawala wa mawizara za maana zitatokea bongo hivi karibuni tuombe Mungu,hivi hawa vijana wengi wasomi kwa nini hawawekwi huku?walioenda MCA wametoka huku huku mawizarani watu wale wale.nasikia uchungu sana nisije nikajifungua bure ngoja nikashue bia mbili pale breakpoint niupunguze kidogo,phd yangu hainisaidii niliyoipata kwa kupiga box la nguvu.

    ReplyDelete
  10. ...Jamani muda mwingine tuache kukariri habari manake sasa hakuna ambacho kitaendelea!kwa sasa ni mapema sana kusema lolote la msingi ni kuipa muda MCA-T kwani kila kitu kipo hadhari then matokea yake tuje kuyaona baada ya miaka mitano hapo ndo tunaweza kusema lolote tunalotaka!tukumbuke kuwa kamati hiyo ndo ambayo imetufikisha hapo mpaka leo mkataba umesainiwa!kazi sasa ipo mbele yao la msingi ni kuwapa muda tusije kuchonga sana sasa then baadae tukakosa la kuongea. Nina imani wote ni wajenga nchi na wote basi tuungane kujenga nchi yetu na nina imani nao MCA-T wataungana nasi katika hili.

    ReplyDelete
  11. Kwa anon hapo juu uliyeongelea kwa nini vijana wengi hawaweki huko!naona labda hukupata kusoma vizuri hapo nyuma jinsi utaratibu wa MCA-T ulivyokwenda na mpaka kuajiri safu nzima ya utekelezaji wa mradi huu. Ukiachilia mtendaji mkuu wa MCA-T ambaye aliteuliwa na Raisi nafasi zingine za kazi zilitangazwa nchi nzima wakati mradi unataka kuanza rasmi baada ya kupitishwa na serikali ya Marekani na kila mwananchi mwenye sifa alikuwa huru kuomba kazi( http://www.mca-t.go.tz ) ila kwa kigezo kikubwa kuwa uzoefu wa kazi ilikuwa ni muhimu sana kwani kumbuka huu ni mradi ambao unatakiwa kukamilika kwa kipindi ambacho kimepangwa na hivyo inakuwa ngumu kwenda na watu ambao akiingia ofisini afundishwa kazi halafu ndo akae sawa. Ni suala ambalo hata mimi wakati mwingine huwa sielewi kuwa wale ambao hatuna uzoefu tutaanzia wapi??ila ndo kama ilivyo kila nafasi ya kazi na taratibu zake!ila nina imani kuwa wapo vijana ambao walikuwa na sifa ambazo zilihitajika na sasa wanachapa mzigo na MCA-T. Basi tusubiri matokeo tu sasa.

    ReplyDelete
  12. Mkuu,
    Huwezi kumpa fedha jamaa yako ambaye unafahamu ni mtumiaji wa madawa ya kulevya yaani Kijigu kwa kiswahili cha mtaani. Serikali ya Tanzania ni kijugu walevi wa Utajiri.. wametuibia fedha nyingi sana za Misaada kwani toka Ujenzi wa Benki Kuu, Mabarabara, Richmond na miradi kibao yote ni fedha za misaada..Hapatakuwepo na tofauti yoyote ktk fedha hizi na kibaya zaidi wao Waamerika sio Wajinga. Kiasi cha dollar Billioni 5 kaziomba Bush kwa ajili ya Millenium Challenge, hivyo fedha hizi zimeombwa kwa mataifa mengi sisi tukiwa moja ya nchi hizo lakini sidhani kama tuta qualify..Kama tumeisha qualify basi wamejidanganya wenyewe..

    Mzee Bush mwaka kesho hana kazi hivyo katafuta Ulaji wake ktk kuweka makoloni yao..Kifupi ni kwamba Millenium Challenge wanajishughulisha na mengi sana.

    Kwa habari zaidi someni hapa:-

    http://www.whitehouse.gov/infocus/developingnations/millennium.html

    ReplyDelete

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...