Jk na Mama Salma Kikwete wakimfariji mjane wa aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Tabora Marehemu Ukiwaona Ditopile Mzuzuri huko nyumbani kwake Upanga. Kulia ni Mariam Ditopile mtoto wa marehemu na nyuma ya Rais ni mtoto wa Rais, Rashid Chodo Kikwete. Aliyesimama karibu na Mama Salma Kikwete ni ndugu wa marehemu ambaye jina lake halikuweza kutambulika mara moja
Marehemu Ukiwaona Ditopile Mzuzuri enzi za uhai wake. Chini ni maombolezo nyumbani kwake mtaa wa Mindu, Upanga,l Dar.


ALIYEKUWA Mkuu wa Mkoa wa Tabora Kepteni Mstaafu Ukiwaona Ditopile Mzuzuri aliyefariki jana Aprili 20,2008 majira ya saa 3:00 katika Hotel ya Hilux iliyopo Mkoani Morogoro anatarajiwa kuzikwa kesho huko Kinyerezi, pembezoni mwa jiji la Dar, maeneo ya Segerea.


Mamia ya waombolezaji wamefurika nyumbani kwa mareehemu mtaa wa Mindu, Upanga, Dar, kujiunga na familia ya marehemu katika kuomboleza kifo hicho ambacho kimeacha watu wengi midomo wazi



Marehemu Ditopile alifikia katika hoteli ya Hilux ,Morogoro akitokea Tabora akiwa safarini kuelekea Dar es Salaam kwa mapumziko akiwa ameambatana na mkewe mdogo,Tabia.



Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Mkurugenzi wa hoteli hiyo Joseph Kitambi, Ditopile alifika hotelini hapo Aprili 18, majira ya saa 5:30 usiku,ambapo alipatiwa chumba No.106.



Kitambi alisema Aprili 19,majira ya saa 5:00 usiku watumishi wa hoteli hiyo wakati wakifunga shughuli zao za huduma, Ditopile alikuwa bado hajarudi hotelini kutoka kwenye shughuli zake ambazo amekuwa akizifanya kwa muda wote tangu kufika hotelini hapo.



Akifafanua zaidi Mkurugenzi huyo alisema, Aprili 20 majira ya saa 2:30 asubuhi mkewe Tabia alitoa taarifa ya kuzidiwa kwa mumewe na kuomba msaada ambapo wahudumu walifika katika chumba chake na kumwangalia na kukuta akiwa amelala kwenye kochi,na alionekana kuwa ni mtu asiyejitambua,na kutoa taarifa kwenye hospitali kuu ya Mkoa kwa msaada zaidi.



Mkurugenzi huyo aliiambia habari leo kuwa marehemu alifariki kabla ya kupata kifungua kinywa cha asubuhi ambacho hutolewa na hoteli hiyo kuanzia saa 12:30 asubuhi hadi majira ya saa 4:30.



Alisema kuwa wauguzi wa hospital walifika katika hoteli hiyo,na kumchukua kwenye gari,akionekana kama mtu ambaye ameshafariki,na kumpeleka hospitalini kwa ajili ya kufanya uchunguzi zaidi.



Hata hivyo Mkurugenzi huyo alidai kwa kipindi chote ambacho Ditopile amekuwa katika hoteli hiyo,alionekana kuwa ni mtu aliyekuwa akisumbuliwa na maradhi,kutokana na mwili wake kudhoofu na nyuso kutokuwa na uchangamfu.



Aidha alidai kuwa wakati wafanyakazi hao wanautoa mwili wake nje kwa kushirikiana na madaktari waliofika kutoka hospitalini,walikuta mswala wa kuswalia,ambapo mkewe alidai kuwa mumewe aliamka alfajiri na kuswali swala ya asubuhi,kabla ya mauti kumkuta.

Baada ya mwili huo kufikishwa hospitalini Mganga Mkuu wa Hospitali ya Mkoa Dkt.Meshack Masi alisema alipokea taarifa kutoka kwenye uongozi wa hoteli hiyo,iliyoeleza kuwa Ditopile amezidiwa hivyo wanahitaji msaada haraka.



'Kweli tulipokea taarifa hizo…walikuwa wakiomba msaada haraka…na sisi tulituma gari pamoja na wauguzi mara moja kwenda pale Hilux hoteli na kumleta hapa hospitalini'alisema Daktari Masi.



Hata hivyo Dkt.Masi alisema baada ya wauguzi kufika hotelini hapo,na kuuona mwili wake waligundua kuwa ameshafariki na kuubeba mwili wake na kuupeleka hospitalini hapo na kuulaza wodini grade 1, kwa ajili ya kuudhibitisha,kabla ya kuupeleka kwenye chumba cha kuhifadhia maiti.



Kamanda wa Polisi mkoa wa Morogoro Thobias Andengenye alisema kuwa marehemu alipotoka mkoani Tabora alifika Mkoani Morogoro na kwenda Wilaya ya Mvomero kwa ajili ya kukagua mashamba yake yaliyopo kwenye eneo la Mgongola akiwa na mkewe mdogo Tabia kabla ya kufika Morogoro Mjini ambapo alipata malazi.



Aliongeza kuwa baada ya kukagua mashamba yake marehemu aliondoka Wilayani Mvomero na kuja Morogoro Mjini ambapo alifika majira ya saa 3 usiku na kufikia kwenye hotel ya Hilux iliyopo Mjini hapo kwa ajili ya kupata malazi ambapo alipewa chumba No.106.



Alisema marehemu aliitumia siku ya Aprili 19,kutembelea ndugu na jamaa zake kabla ya kurudi nyumbani kwake Jijini Dar es Salaam,na kudai kuwa alirudi hotelini hapo majira ya saa 12 jioni,ambapo alitarajia kuondoka Aprili 20 kurudi nyumbani kwake.



Katika ziara ya marehemu ya kutembelea na kusalimiana na ndugu zake,pia alipata wasaa wa kumtembelea Chifu Kingalu Mwana Banzi wa 14 wa kabila la waluguru.



Kwa upande mwingine mdogo wake na Marehemu, Selemani Mzuzuri,alipohojiwa alisema hana lolote la kuzungumza na kueleza kuwa bado ana majonzi mazito ya kifo cha kaka yake,hivyo hataweza kuzungumzia jambo lolote.



Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Meja Jeneral mstaafu Said Kalembo ambaye alifika hospitali ya mkoa wa Morogoro akizungumza na waandishi wa habari alisema kwamba mwili wa marehemu unatarajiwa kuchukuliwa na gari la jeshi na kusafirishwa kuupeleka kwenye chumba cha kuhifadhia maiti kwenye hospitali ya Jeshi ya Lugalo iliyopo Dar es salaam.



Marehemu Ditopile, ambaye pia aliwahi kuwa Naibu Waziri wa Ulinzi na Jeshi la kujenga Taifa na Naibu Katibu Mkuu wa CCM, amewahi pia kuwa Mkuu wa Mkoa wa Kigoma,Lindi na Tabora kabla ya kukabiliwa na kesi ya Mauaji bila kukusudia.


Habari kama hii na picha nenda pia: lukwangule.blogspot.com

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

Kuna Maoni 12 mpaka sasa

  1. RIP and may the family be encouraged in this trying period. They are all God's plans, us as human beings must do according to his will.

    We pray for the family and they will be strengthen at this time.

    Poleni sana wafiwa.

    mdau Sverige

    ReplyDelete
  2. Familia ya marehemu tunaipa pole sana. Mungu alitoa na Mungu ametwaa, jina lake lishukuriwe.

    Lakini nina swali moja: Hiyo tarehe 19, alirudi hotelini saa 12 jioni au baada ya 5 usiku?? I quote: "Kitambi alisema Aprili 19,majira ya saa 5:00 usiku watumishi wa hoteli hiyo wakati wakifunga shughuli zao za huduma, Ditopile alikuwa BADO hajarudi hotelini..." NA "Alisema (Kamanda wa Polisi mkoa wa Morogoro Thobias Andengenye) marehemu aliitumia siku ya Aprili 19,kutembelea ndugu na jamaa zake kabla ya kurudi nyumbani kwake Jijini Dar es Salaam,na kudai kuwa alirudi hotelini hapo majira ya saa 12 jioni...". Hapo MMENIKONFYUZI!!

    ReplyDelete
  3. RIP Ditopile Mzuzuri!
    Hot Pilipili... true dat!! true dat!! Coz I am confused too!

    Bwana Ametoa na Bwana Ametwaa!

    Poleni sana familia na wana ndugu wote!

    ReplyDelete
  4. Poleni sana familia ya marehemu
    Kaka!brother Ditopile,mwenyezi mungu atampuzisha mahala pema peponi,
    Marehemu Kaka!brother Dito atakumbukwa kwa mengi,alikuwa mtani wa jadi wa wanahabari,kipenzi cha watoto wa mjini,mtu wa watu,
    Mungu mlaze mahala pema peponi

    ReplyDelete
  5. A very sad ending indeed!For some us who value human life this is yet another tragic loss of life which could have been averted!To some he may have committed a murderous sin BUT it is only GOD THE ALMIGHTY and him only who has the authourity to pass a judgement.He is the only one who knows what had happened why it had happened the way it did happen!TWO WRONGS DO NOT MAKE A RIGHT.Ditopile should have been kept under special care,for he must have gone thru very agonising moments during the last days of his life!He needed all the support he could get morally and psychologically.He was never to be castigated into oblivion pr insignificance while he was still alive.Huu ni mtihani mwingine mkubwa aliotupatia Mwenyezi Mungu.Ikiwa Mungu yuko tayari kusamahe kwa nini sisi binadamu tunakuwa wagumu kusamehe?Fikiria ni wahalifu wangapi wanao ozea jela ambao wangeweza kurejea maisha yao ya kawaida iwapo wangeachiliwa huru LEO?Kwa nini binadamu afungwe Maisha ikiwa siyo tishio kwa usalama na maisha ya binadamu wengine bali ni mhalifu kutokana na udhaifu wa kibinadamu tu?YALIYO SAMEHEWA DUNIANI HATA MBINGUNI AU PEPONI YATASAMEHEWA PIA.Bado tunayo nafasi ya kubadilisha Mioyo yetu.Mwenyezi Mungu anatuangalia nyakati zote.Wenye dhamana ya kuleta mabadiliko ndiyo watakao beba Msalaba!-tonny

    ReplyDelete
  6. Qallu Inna Lillah Wa Inna Illayhi Rajioon .nakumbuka mimi nilipokuwa primary miak ya 87 huyu ndio kiongozi wa kwanza wa serikali kuja kututembelea alituchekesha sana na kusema tukitaka kumkumbuka yeye tukumbuke kiongozi wa Tanzania mwenye jina refu kuliko woote ndio yeye Mzuzuri akatulistia majina yake yoote..... Naiombea familia yake kina mama na watoto Mwenyezi Mungu awape nyoyo za subira katika kipindi hiki cha mtihani mgumu kwa binadamu. Vilevile pole kwa nduguze. jamaa na rafiki zake woote wa karibu akiwepo Mheshimiwa Rais wetu kwa kuondokewa na kipenzi chao.Kwani mara nyingi huwa tunaikumbuka familia ya marehemu tuu ambayo ndio inabaki katika wakati mgumu zaidi hasa ukiondokewa na kiongozi wa family lakini mtu huwa ana maswahiba wake wa karibu ambao nao wana uchungu sawa na familia yake lakini inabidi wajikaze kwa ajili ya kuifikiria family.Hivyo tunawaombea Mwenyezi Mungu awatilie wepesi kwa hili inshallah. Inshallah Mwenyezi Mungu awape imani wahusika woote.

    Haya narudi kwa wee Hot Pilipili kulikoni ? kwani wewe umekuwa shushushu bin detective mchunguza chanzo cha hiki kifo ama ? sasa kwa nini uchanganywe kwa hizo habari kutofautiana ? ndio habari zimetofautia lakini kwa nini unataka uanzishe mjadala humu na unawajua wadau wa Michuzi wengine huwa wanasubiri mwanzo tuu. tafadhali acha chokochoko yasije yakakushinda, binadamu mwenzio mchokoe akiwa hai utakavyo , lakini umauti ukishamfika ni kuombeana maghfira tuu kwa Mwenyezi Mungu kwani na sisi soote ndio tuendako hatujui saa wala siku ugumu ni kutangulia tuu.

    ReplyDelete
  7. Poleni wanafamilia na wote waliokuwa na upendo naye wa kweli. Dito alikuwa na sura nzuri sana (handsome) na tabia zake zilionyesha ya kuwa ni mzee wa mjini. I will miss you kaka Dito. Rest in peace.

    ReplyDelete
  8. inna lillah wanain irah rajiuon.
    Kaka Dito umetutoka hili ni pigo kubwa sana sisi watoto wa mjini.pengo lako halizibiki kwa sasa.

    umatusaidia sana timu yetu ya Ashanti hadi kupanda daraja kwa hali na mali bila kusahau nasaha zako na ushauri kila wakati kwenu sisi.bila kuwasahau BOOM FC.

    hukuona kinyaa kukaa kijiweni na sisi tusio na ajira au elimu. nani anaweza kukubali kuwa down to the Earth kama wewe? leo hii kumekuwa na vijiwe au mitandao kadhaa wa kadhaa ambayo kila nukta lazima kuwe na msisitizo kuwa 'sisi ni wasomi'

    sisi watoto wa Ilala hatukujua kama una digrii na wala hukuwahi kujikweza kuwa wewe ni msomi.

    umetuachia Historia ambayo ni taabu sana kupata mtu wa kuirithi.

    kalale pema peponi dua zetu na nyiradi zetu utakuwa unazipata kila tukikutana na kila tumalizapo swala zetu.

    ni mimi mwana Ilala toka mtaaa wa Moshi Ilala.

    ReplyDelete
  9. MUNGU AMLAZE KWA AMANI KATIKA MAKAO ALIYOMUANDALIA MPENDWA WETU.POLENI NDUGU NA JAMAA NA MARAFIKI.POLE KWA WANA HABARI WOTE, ALIKUWA RAFIKI MKUBWA.PEACE.

    ReplyDelete
  10. Kushtakiwa Mafisadi...Tatizo ni utajiri au uhusiano na dola?

    2008-04-21 10:50:15
    Na Ani Jozeni


    Katika mkutano wake wa kwanza wa Bunge kama Waziri Mkuu, Mizengo Kayanza Peter Pinda, amepewa mtihani mgumu wa kutangua, au kutawala bungeni, jinsi suala nyeti la `ufisadi` Benki Kuu litakavyojadiliwa na kufanyiwa kazi.

    Tofauti na suala la Richmond Development Company, hapa wabunge wanaonekana kuwa waangalifu kwa kiwango fulani, na hata wale `wakali` wa vyombo vya habari wanagwaya kwa kiasi ambacho si haba wakiongelea suala la `ufisadi,` na ni wazi ujasiri wa kulishupalia kama lile la Richmond ni mashakani.

    Ni katika mazingira hayo ambako vikwazo vya kufungua mashitaka vimetolewa.

    Moja ya kauli tangulizi alizotoa Waziri Mkuu Pinda ni kuwa ``utajiri wa mafisadi ni kikwazo kushitakiwa,`` kwa mujibu wa kichwa cha habari cha mojawapo ya magazeti siku iliyofuata, akisema ukimpeleka mahakamani mtu mwenye fedha huku una ushahidi kidogo hufiki mbali.

    Ilielekea vile vile kuwa alilenga ``mapungufu`` kadhaa katika Ofisi ya Mwanasheria Mkuu, licha ya kuwa suala hapa ni utaratibu na siyo uwezo wa ofisi kumudu.

    Na kwa hali yoyote ile, hivi tatizo la kushitaki ni wasiwasi wahusika kushinda, au ni uthabiti wa dola?

    Ingekuwa suala ni uwezo wao wa kushinda, labda ingeathiri tu idadi ya wale wanaofikishwa mahakamani, ngazi zao au jinsi makampuni haya au yale kwa wakati fulani yalivyohusika.

    Siyo jambo la kushindwa kufikiria kupeleka huyu au yule mahakamani, kwani kinachozungumziwa ni fedha zilizotolewa kwa watu kadhaa, inasemekana kwa udanganyifu, kuwa makampuni yao hayakuwa tayari yamesajiliwa, na katika Richmond, inasemekana hata kampuni yenyewe haina uhalisi kamili wa kuwepo. Ina maana fedha ilitoka bila kazi yoyote ya maana.

    Kwa vile lugha ya serikali kuhusu masuala ya Richmond na yale ya malipo ya Benki Kuu, iwe ni EPA, minara miwili, Meremeta Gold, Mwananchi Gold, Kagoda Agriculture Co., na bado haijaanza kujadili Millennium Business Park kwa undani, sasa kote huko kuna wakubwa wenye fedha nyingi ambao ile kamati ya wakuu watatu wa ulinzi na usalama hawawezi kuwagusa?

    Sasa kama serikali inaongea lugha kama hiyo, kuwa hawa ni maofisa wakubwa wana fedha na hivyo hatuwezi kuwapeleka polisi, si sawa na kukaribisha maandamano ili watu watake kuwa hawa wahusika wakamatwe, hata wangekuwa kina nani?

    Hivi kauli hii ya Bw. Pinda inaendana na ile ya Mkuu wa Jeshi la Polisi kuwa 'mtumbwi ukipinduka (kutokana na suala la malipo ya EPA) tutazama wote'? Hivi hatari hiyo ya ``mtumbwi kuzama`` ni wahusika hao kushinda kesi kwa ushahidi haba?

    Kimsingi ni kuwa serikali bado inaendelea kukimbia kivuli chake, wakati kivuli hicho sasa kinaanza kugeuka jini, na kuichongea serikali, hawa watawala (au mtawala) wa awamu iliyopita, na wananchi, katika njia ambayo 'suluhisho la Richmond\' siyo rahisi kufikiwa.

    Iliwezekana kwa aliyekuwa Waziri Mkuu kubeba mzigo wa Richmond kupata tenda (licha la ubora wa tenda yenyewe, kulipa umeme wa Megawati 100 kwa miaka miwili ya malipo kamili, na siyo miaka 20 kama IPTL, ambao nao ni Megawati 100).

    Imeshindikana kwa mbunge yeyote au wahusika wa sakata la Richmond kutaja kuwa mradi huo una tija na faida kubwa kwa nchi; basi kivuli hicho kinawakimbiza, wanaangalia ``hatua za kinidhamu`` za kuchukuliwa kwa wahusika waliokwepesha mkataba wa miaka 20.

    Imetajwa kwa mfano kuwa makampuni yaliyohusika na EPA ni 22, na kwa vile inaonekana katika suala la Meremeta Gold kuwa idhini au amri ya malipo ilitoka kwa Katibu Mkuu Kiongozi M.Y.C. Lumbanga, kwa mujibu wa barua iliyochapishwa `Raia Mwema` wiki iliyopita (toleo la Aprili 9-15), basi ni aina hiyo hiyo ya uhusika inahitaji kuainishwa.

    Tatizo la kukimbia kivuli ni lile la kushindwa kusema kwa nini Katibu Mkuu Kiongozi alitoa amri kama zile, na ni nini katika sera zinaendana na amri zile, kwani haiwezekani kuwa alitoa amri hiyo kwa manufaa binafsi, au kuwaridhisha marafiki zake binafsi.

    Sasa kama yapo masuala ya sera - kama Waziri Dk. Ibrahim Msabaha alivyosema katika utetezi mfupi Bungeni siku ya kutoa rai au tangazo la kujiuzulu - kwa nini iwe taabu kwa serikali kulenga huko, na badala yake inasema ni fedha ndiyo suala?

    Suala hapa ni la kimantiki badala ya kuwa la kisiasa, la uwezekano wa kutatua tatizo la malipo ya fedha nyingi Benki Kuu kwa kulikwepa, kutafuta visingizio kama utajiri wa wahusika, na kutazamia kuwa kwa sababu hiyo suala hilo basi litaisha lenyewe.

    Kama serikali haitazamii kuwa litakwisha kwa namna hiyo, basi inajaribu kulichochea kwa kauli za kebehi kuwa haiwezi kuwapeleka watu wenye fedha zao mahakamani, na watu wakikasirika, labda ndipo ithubutu.

    Kama suala halitakuwa ni kuwapeleka mahakamani, jawabu lingine sasa ni lipi?

    Kimsingi ni wazi kuwa, upo udhaifu wa wazi wa jinsi serikali inavyolea suala la `ufisadi` likawa ni lugha ya kawaida, na chanzo cha mivutano isiyoisha katika vyombo vya habari na Bunge, na hasa kutokana na mfano wa Richmond ambao kwa sababu za `makundi` liliachwa likaota mbawa, lisishikike tena, na likaota meno, likang\'ata.

    Sasa kuanza kurudi kinyumenyume na kuanza kusema ``hivi unafahamu tulikosea hata kule Richmond; ule mradi ni mzuri tu ingawa ile kamati iliangalia suala la nani anahusika na kampuni ndogo kiasi kile`` itakuwa vigumu.

    Kwa sababu za kisiasa za muda mfupi, serikali inajilazimisha kufunga mdomo, wananchi waambiwe chochote kile, waamue chochote kile, alimradi tu inyamaze, kwani kufahamu serikali ilichukua maamuzi gani ni kuvuruga furaha; wote tunapinga `mafisadi,` ni wale waliokabidhiwa pesa kufanya kazi ya nchi.

    Wakati ambapo kinachozungumzwa sasa hivi ni `ufisadi,` na hata Waziri Mkuu anachelea kutaja masuala husika na kuwa ni kazi halisi, na halali za nchi kwa mujibu wa kutumia utashi wa kizalendo, hali hii itaendelea hadi lini?

    Serikali inaona ni bora amani ianze kuvunjika kwa hatua, kuanzia Richmond (iweje ikiri kuwa viongozi wakuu wanaweza kufanya biashara pamoja na wageni?) au EPA, Meremeta Gold n.k.? Kwa nini serikali iendelee kuongozwa na dhana ya kuhofia kusema kuwa eti siku moja serikali ilikiuka sera ya Mahakama Kuu ya kufuta takrima katika uchaguzi mkuu, yaani kutotosheka na ruzuku?

    Hivi ruzuku peke yake ingetosha kufanya uchaguzi mgombea afahamike kote, na apendwe kote?

    Wakati wahojaji lukuki wanalalamikia ``ufisadi`` kutokana na unafiki wa kawaida ambao ndiyo hasa msingi wa Injili kuwa wasio wasafi wanatangulia kuokota mawe kuua mwanamke maskini `mzinzi,` kama ilivyokuwa kule Nigeria, kama si kelele za wanaharakati wa Haki za Binadamu, tunasahau suala zima la uhuru wetu.

    Rais Mstaafu Benjamin Mkapa alihakikisha kuwa wagombea wanapata fedha za ndani kujinadi kwa wanachama wa CCM, na baada ya hapo mgombea wa CCM anafahamika kote, na kupendwa kote.

    Wapinzani waliruhusiwa pia kupata fedha kutoka nje, au vifaa kama helikopta, lakini chama tawala siyo haki kitafute fedha nje, badala ya miundombinu, wakati ``uwezeshaji`` ni sera ya kawaida kwa mikopo - iwe ni jeshi livune dhahabu, au chama kivune kura.

    ReplyDelete
  11. kumbe huyu mtu bado yankie hivi. mbona hili jina lake nimeanza kulisikia toka nikiwa mdogo saana? lilikua unique refu na ukilisikia hutalisahau. nilizania atakua amelingana na kina kawawa, nyerere etc...naona mwanae mdogo tu hapo. jamani bado mdogo labda aliingia kwenye chama akiwa in his 20's

    ReplyDelete
  12. Rest in Peace. Never met or knew you Brother DITO. You had your misfortunes but I still feel it is what they call 'accident'. From what I have read about you (handsome dude) and your body language in the photos - you seem to have had a beautiful soul. Poleni sana wafiwa and May his Soul rest in Eternal Peace.Amen.

    ReplyDelete

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...