HOTUBA YA RAIS WA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA, MHESHIMIWA JAKAYA MRISHO KIKWETE KATIKA MKUTANO WA WATANZANIA WAISHIO UINGEREZA SAVOY PLACE,LONDON 18 APRILI, 2008
(Hotuba hii ilisomwa na Makamu wa Rais Dk. Ali Mohamed Shein kwa niaba ya Rais)
Awali ya yote napenda kuelezea furaha kubwa niliyonayo kwa kushirikishwa katika mkutano wenu huu wa kihistoria hapa London.
Nawashukuru wale wote miongoni mwenu walioibua wazo la kuandaa mkutano huu. Ni wazo zuri na la kimaendeleo linalostahili kupongezwa na kuungwa mkono na sisi sote.
Nakushukuru pia wewe Mheshimiwa Balozi na wafanyakazi wote wa Ubalozi wetu hapa London kwa kusimamia vizuri maandalizi ya mkutano huu. Tunawapongeza sana kwa kazi yenu nzuri ambayo hakika sote tumeishuhudia.
Mkutano huu umeandaliwa vizuri; taarifa zake zimetayarishwa kwa uhodari na kusambazwa mapema kwa wahusika na mandhari ya ukumbi huu wa mkutano yanapendeza machoni. Hongereni sana.
Nimeambiwa kuwa mkutano huu unajumuisha Watanzania muishio Uingereza na Ireland. Lakini pia nimeambiwa wapo wengine mliotokea Finland na Ubelgiji. Hii inaonyesha dhahiri jinsi gani mnavyothamini mkutano huu na mambo unayoyasimamia.
Hiki ni kielelezo cha wazi cha dhamiri yenu ya kutaka kuchangia kwa namna moja au nyingine katika maendeleo ya nchi yetu. Huu, ndugu zangu, ndio moyo wa uzalendo tunaoutegemea kutoka kwenu. Napenda kuwashukuru nyote kwa mapenzi yenu makubwa kwa nchi yetu.
Kwa kweli lazima nikiri kwamba mimi nimefurahishwa sana na kutiwa moyo na uamuzi wenu wa kuwa na mkutano huu. Kwani katika safari zangu zote za nje nimekuwa nikiwasihi sana Watanzania wenzetu waishio ughaibuni kutokusahau nyumbani walikotoka.
Kila mara nimekuwa nikisisitiza kwao kuwa moja ya mambo wanayoweza kuyafanya ni kuendeleza maeneo waliyotoka au kuzaliwa kwa kujenga nyumba bora za kuishi. Nimekuwa nikisema hayo kwa kuamini kuwa kwa kufanya hivyo watakuwa wanasaidia kuboresha hali ya maisha ya wananchi wetu vijijini kwani nyumba ni moja ya mahitaji muhimu katika maisha ya mwanadamu.
Aidha, nimekuwa nikiwaeleza kuwa jukumu la serikali ni kuandaa mazingira mazuri ya uwekezaji yatakayowawezesha kuleta mitaji yao nyumbani kwenye miradi ya kiuchumi na kijamii bila ya usumbufu wowote. Nafurahi kwamba leo wito wangu huo hatimaye umepata sikio sikivu. Naamini mkutano wenu ni mwanzo wa ushirikiano baina ya serikali na Watanzania waishio ughaibuni (Diaspora).
Ushirikiano utakaojenga mazingira bora ya kuwashirikisha Watanzania waishio nje ya nchi yetu katika ujenzi wa taifa lao kama inavyofanyika katika mataifa mengine duniani.
Mheshimiwa Balozi na Ndugu Watanzania wenzangu,
Nimeelezwa kuwa idadi ya Watanzania waliohamia ughaibuni kwa ajili ya kutafuta maslahi bora na sababu nyinginezo imeendelea kuongezeka na kukua mwaka hadi mwaka. Hali hii inatoa changamoto kubwa kwetu sisi tulioko serikalini katika kubuni na kuandaa mikakati na sera za kuwatambua Watanzania hao na hatimaye kuweka utaratibu wa kuwahamasisha ili waweze kuchangia kwa ukamilifu katika maendeleo ya taifa lao.
Napenda kusema kuwa serikali inatambua wazi hazina kubwa ya uwezo wa kitaaluma, nguvu kazi na hata uwezo wa kuwekeza nyumbani iliyo ughaibuni.
Umoja wa Afrika (AU) ambao kwa sasa mimi ndiye Mwenyekiti wake, ulitangaza tangu mwaka 2003 kutambua Waafrika waishio nje ya Bara letu yaani “African Diaspora”, kuwa jimbo rasmi.
Uamuzi huo ulitokana na mchango mkubwa wa Waafrika waishio ughaibuni katika chumi za nchi zao. Kwa mantiki hiyo basi, nasi kuanzia sasa tutawahesabu na kuwatambua Watanzania waishio ughaibuni kama ni Mkoa rasmi wa nchi yetu na tutaandaa mipango yetu ya maendeleo kwa kuzingatia hilo.
Sote tunafahamu kuwa marejesho ya fedha kutoka watu waishio nje ya nchi zao kote duniani yanakua kwa kasi kubwa na huleta mafanikio ya kiuchumi katika nchi zinazopokea marejesho hayo.
Kwa mfano, taarifa za Benki ya Dunia zinaonyesha kuwa Diaspora milioni 150 duniani kote walirejesha kiasi cha dola za Kimarekani bilioni 300 kwa nchi 162 mwaka jana. Kiasi hicho inasemekana ni kikubwa kuliko misaada yote ya maendeleo (ODA) kwa nchi zinazoendelea.
Ni dhahiri kuwa hizi ni pesa nyingi sana ambazo zinaweza kufanya mambo makubwa ya kimaendeleo katika nchi zetu. Hata majirani zetu wa Kenya hupata mapato ya kutosha yatokanayo na raia wao waishio nje.
Kwa mujibu wa Benki ya Dunia, Kenya mwaka 2006 iliingiza dola bilioni moja kwa njia hii ikilinganishwa na dola milioni moja tu zilizorejeshwa Tanzania katika kipindi hicho na Watanzania waishio ughaibuni. Hii inaonyesha kwamba Tanzania bado tuko nyuma sana katika eneo hili.
Nimemsikia Balozi katika hotuba yake, akisema kuwa kwa upande wa Tanzania marejesho mengi hupitia njia zisizo rasmi au njia za panya kama zinavyofahamika kule nyumbani. Sina hakika kama hili ni kweli. Lakini Gavana wa Benki Kuu, Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB na Benki ya Posta wapo hapa. Wao wanaweza kulifafanua vizuri jambo hili kuliko mie.
Naamini watakapopata fursa watafanya hivyo ili sote tupate picha kamili ya hali ilivyo.
Hata hivyo, ninachofahamu mimi ni kuwa CRDB wana akaunti yao ya Tanzanite ambayo wengi wenu mnaitumia. Pengine tuwaachie Benki Kuu na benki za biashara watizame jinsi gani ya kuboresha njia za marejesho ya fedha kutoka ughaibuni.
Tuwaombe wabuni njia rahisi zaidi na za nafuu za kutuma fedha ili kuchochea marejesho, kwa manufaa ya wale wanaopokea na pia kwa manufaa ya uchumi wa taifa letu. Mimi naamini hili linawezekana kabisa na kamwe haliwezi kutushinda kutekeleza.
Tunachohitaji kujua ni tatizo liko wapi ili tuweze kulirekebisha. Maana matatizo yapo ili yashughulikiwe.
Ndugu Watanzania wenzangu;
Serikali yenu inatambua kuwa Watanzania wengi mliosomea ughaibuni kisomo chenu ni kizuri, mnao ujuzi na uzoefu wa kutosha na baadhi yenu kipato chenu pia ni kizuri. Naamini mkiwezeshwa kidogo, mkawa ni wawekezaji kule nyumban, mnao uwezo mkubwa wa kuchochea ukuaji wa uchumi wa nchi yetu.
Nilipofika hapa nimebahatika kuona taarifa iliyotayarishwa na waandaaji wa mkutano huu inayotokana na majibu mliyotoa wakati wa kujiandikisha. Inaonekana kuwa wengi wenu ni wasomi mahiri wenye taaluma mbali mbali. Pia, wengi wenu mmesema kuwa mko tayari kurejea nyumbani na kuajiriwa au kujiajiri katika sekta mbali mbali.
Napenda kutumia fursa hii kuwakaribisha wale wote mnaotaka kurudi nyumbani. Karibuni sana nyumbani. Kazi za kufanya zipo. Naamini hamtakosa cha kufanya.
Kwa wale wanaotaka kujiajiri tunao mkakati wa kuwawezesha. Hivyo msiogope kurejea nyumbani. Mbona sisi tupo huko. Njooni tushirikiane kwa pamoja kuijenga nchi yetu. Aidha, nimefarijika kuona katika agenda yenu kuwa zipo kampuni kutoka nyumbani zinazozungumzia nafasi za ajira.
Huu ni ushahidi tosha kwamba kazi zipo kwa wale wenye ujuzi na sifa stahiki. Nina hakika mishahara mtakayolipwa nayo itakuwa mizuri kwani hivi sasa kuna ushindani mkali miongoni mwa waajiri katika kupata wafanyakazi bora wenye sifa na ujuzi unaoendana na mahitaji ya soko la ajira nchini na duniani. Hivyo msiwe na wasiwasi wa kupata ajira. Njooni.
Mheshimiwa Balozi na Watanzania wenzangu,
Katika majibu yenu mmetaja ukosefu wa vivutio vya kuwahamasisha kuwekeza nyumbani, ukosefu wa mitaji kutokana na ukosefu wa taasisi za fedha zenye kulenga Diaspora kule nyumbani.
Vile vile mmetaja ukosefu wa taarifa kuhusu fursa za uwekezaji kwa Diaspora. Mie nawapa changamoto. Andaeni mapendekezo yenu kuhusu vivutio mnavyodhani vinafaa. Serikali itayafanyia kazi mapendekezo yenu haraka iwezekanavyo.
Pengine mtapenda kufahamu kuwa tayari Serikali imekwishaunda kamati maalum inayozishirikisha Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Wizara ya Mambo ya Ndani, Idara ya Uwekezaji na Uwezeshaji na Wizara ya Ajira na Maendeleo ya Vijana pamoja na Ofisi ya Rais kuangalia mambo yafuatayo:
Kwanza, kuwashirikisha Watanzania waliopo nje ya nchi katika kujenga na kuendeleza uchumi wa nchi yetu katika mfumo rasmi. Mpango huo kwa lugha ya kiingereza unajulikana kama “The National Institutional Framework for Engaging Diaspora for Economic Development”.
Pili, kufanya mchakato wa marekebisho ya sheria zinazohusiana na marejesho ya fedha na mikopo kwa watu waishio nje ya nchi ili kuweka utaratibu wa Watanzania hao kufungua akaunti maalum zitakazorahisisha utumaji wa fedha nyumbani kwa kutumia mfumo rasmi.
Tatu, kupitia upya Sheria ya Uraia ili kuona uwezekano wa kuruhusu uraia wa nchi mbili. Kamati hiyo itapitia pia mapendekezo yatakayotokana na mkutano wenu hapa leo. Kwa hiyo nawashauri muwe makini na mtoe mapendekezo yanayoweza kutekelezeka.
Napenda kuwahakikishia kuwa Serikali yenu ni sikivu na pale mtakapotoa mapendekezo ya kujenga na si kubomoa, tutayafanyia kazi mapema iwezekanavyo na matokeo mtayaona. Nataka pia niwatoe wasiwasi kuhusu hali ya uchumi wa nchi yetu.
Najua Gavana wa Benki Kuu yupo hapa, naamini atawapa taarifa ya kina kuhusu mwenendo wa uchumi wetu.
Lazima niseme tu kuwa hali ni nzuri. Uchumi wetu mwaka jana (2007) ulikua kwa asilimia 7.3 ikilinganishwa na asilimia 6.7 mwaka 2006. Tumeendelea pia na kazi ya uboreshaji wa mazingira ya uwekezaji nchini kwa kurekebisha baadhi ya sheria na miundo ya uendeshaji iliyokuwa ni kikwazo cha ufanisi. Hatua hizi na nyinginezo zimesaidia sana katika kuboresha mazingira ya uwekezaji nchini.
Hivyo hali ni nzuri na nyote mnakaribishwa kuwekeza nchini.
Ndugu Watanzania wenzangu,
Katika kupitia ratiba yenu nimeona mambo ambayo yananipa matumaini makubwa katika kuwashirikisha Watanzania mlio ughaibuni.
Kwa mfano nimeona kuwa Shirika la Taifa la Nyumba lina mpango wa kuwapa fursa ya kuwajengea nyumba wale wanaopenda kujenga kwa mtindo wa kulipa kwa awamu. Hii ni fursa nzuri. Nawashauri wale wote kati yenu wenye nia ya kufanya hivyo muitumie kwa ukamilifu fursa hiyo.
Nimeona pia kuwa mtapewa maelezo ya ziada kuhusu fursa za kuwekeza katika soko la hisa la nyumbani na mtaelezwa utaratibu wa kuweza kujiajiri kwa kuanzisha biashara aidha nyumbani au huku ughaibuni.
Bila shaka mwisho wa siku ya leo mtatoka hapa mkiwa mmeelimika vya kutosha kuhusu fursa za kuwekeza zilizopo nyumbani ili muweze kujipanga vizuri katika kuzitumia. Nimefurahi pia nilipomsikia Balozi hapa akisema kuwa wengi wenu tayari mmewekeza nyumbani.
Hili ni jambo jema sana. Nawapongezeni kwa uamuzi wenu huo wa busara. Serikali itafanya kila iwezalo kuwasaidia katika jitihada zenu za kuwekeza zaidi kwani jinsi mnavyozidi kuwekeza nyumbani ndivyo na uchumi wetu unavyonufaika zaidi na uwekezaji wenu.
Napenda kuwakumbusha usemi usemao kuwa nchi hujengwa na wenye nchi. Nyinyi kama Watanzania ni sehemu ya wenye nchi, hivyo mnayo dhamana kubwa ya kuijenga nchi yenu ili iwe mahali pazuri pa kuishi kwa kila mmoja wetu.
Hatuna mjomba atakayetujengea nchi yetu bali tutaijenga sisi wenyewe. Ni vyema sote tukalitambua na kulizingatia hili.
Dhamana ya kuijenga na kuiendeleza nchi yetu ni yetu sote. Kila mmoja wetu kwa nafasi aliyonayo. Ndugu zangu Watanzania wenzangu,Nimesema sana. Lakini kabla ya kumaliza hotuba yangu naomba niseme jambo moja zaidi.
Nimeona katika taarifa ya maandalizi ya Mkutano wenu kuwa ni kiasi cha asilimia 13 tu ya Watanzania waishio katika nchi mnakokaa ndiyo pekee wamejiunga katika Jumuiya yenu. Hali hii si nzuri hata kidogo. Nawashauri wale wote ambao hamjajiunga na umoja wenu mfanye hivyo.
Pia wale ambao hamjajiandikisha Ubalozini nendeni mkajiandikishe. Hili ni jambo muhimu sana kwani Serikali inaweza kuwafikia tu kupitia jumuia zenu au ofisi ya Ubalozi. Nawaomba sote daima tukumbuke kuwa umoja ni nguvu, utengano ni udhaifu.
Huku ughaibuni familia yako na ukoo wako ni Watanzania wenzio. Jumuiya yenu ndiyo jukwaa la Watanzania kuweza kukutana, kubadilishana mawazo na kupashana habari. Jumuia zenu pia ni jukwaa la kuweza kufuatilia mambo yanavyokwenda nyumbani na kutoa kauli zenu au kufuatilia mambo yanayowahusu ambayo mngependa serikali iyajue na kuyatilia maanani.
Hivyo jumuia zenu ni chombo muhimu sana cha kuwaunganisha na kuwahudumia.
Nawaomba mkitumie chombo hiki kikamilifu. Mheshimiwa Balozi na Ndugu Wajumbe wa Mkutano huu,Mwisho kabisa napenda kurudia yale niliyoyasema.
Kwanza, nimepongeza na kukaribisha wazo la kuandaa mkutano huu. Nimesema mkutano wenu ni wa kihistoria kwa vile ni mkutano wa kwanza kuwakutanisha Watanzania waishio ughaibuni kuzungumzia agenda ya jinsi ya kushiriki katika ujenzi wa nchi yetu na uchumi wake.
Pili, nimesema kuwa mkutano huu ni mwanzo wa ushirikiano wa karibu baina ya serikali na Watanzania mlioko ughaibuni. Ushirikiano wenye lengo la kuwawezesha kurejesha fedha nyumbani kupitia utaratibu rasmi na kuwajengea mazingira mazuri ya kuwekeza mitaji kwenye uchumi wa nchi yetu. Tatu, nimeeleza nia ya serikali ya kufanya kazi pamoja nanyi katika kuondoa kasoro zilizopo zinazowazuia kurejesha fedha nyumbani kihalali na kuzitumia kama mitaji ya kuanzishia miradi ya kiuchumi na kijamii. Nne, nimesema kuwa serikali tayari imeanza kuchukua hatua za kuweka mazingira mazuri yatakayowawezesha Watanzania mlioko ughaibuni kushiriki kwa ukamilifu katika harakati za kuinua uchumi wa nchi yetu.
Hatua hizo ni pamoja na kuunda kamati maalum inayoshughulikia suala hili. Tano, nimewakaribisha wale wote miongoni mwenu mnaojisikia kutaka kurudi nyumbani kufanya hivyo.
Nimesema kwa wale wenye ujuzi na sifa stahiki kazi zipo. Msiogope kurudi nyumbani. Njooni tuijenge nchi yetu kwa pamoja. Sita, nimesisitiza umuhimu wa jumuia zenu huku nje na kuwaomba wale wote ambao hawajajiunga na jumuia yenu hapa London kufanya hivyo.
Aidha, nimeomba tujenge utamaduni wa kujisajili kwenye Balozi zetu kwavile Balozi ndizo kiungo baina yenu na Serikali yenu. Na saba, nimewahakikishia kuwa serikali itayafanyia kazi maoni au ushauri mtakaotoa kwenye mkutano huu kwa lengo la kuondoa kero au kasoro zinazokwamisha nia yenu njema ya kuwekeza nyumbani.
Mheshimiwa Balozi, Ndugu Watanzania wenzangu na wageni waalikwa,
Baada ya kusema hayo, sasa natamka rasmi kwamba mkutano wenu umefunguliwa. Nawatakia nyote mkutano mwema wenye mafanikio. Ahsanteni kwa kunisikiliza.
Naam, hawa ndio wawakilishi wa Tanzania Bara walioko London au UK. Nadhani ipo haja kwa Wanzibari pia kuwa na diaspora yao.
ReplyDeleteWabongo acheni wivu!! hebu kumbukeni ule msemo wetu wa kwamba ''mbuzi hula urefu wa kamba yake''. Chenge alikuwa mwanasheria mkuu wa serikali kwa miaka kumi na katika kipindo hicho nchi imeingia mikataba mibovu mingi sana, sasa unategemea yeye chengye awe fala kwa kuwaachia wenzake wajikombee mihela wakati yeye ndiyo muuandaji wa hiyo mikataba inayoleta dili. Hivi si mtakuwa mnakumbuka wazee walivyokuwa wakishindana kuuza mashirika na wafanyakazi wake ili wajipatie 10% zao na kama nchi ilikuwa na lukuki wa mashirika na fikiria katika kila mkataba chenge apate 2% ya 10% atakuwa amekusanya ngapi mpaka sasa. Actually msikonde sana kwani hivyo ni vijisenti tu ukilinganisha na ukwasi waliojilimbikizia wakati wananchi hawajaanza kuchonga sana. Na pia kumbukeni ya kwamba kila mtu ana viwango vyake!! tehee!! teheee!!!duh! hi nayo Chenge katoa kali, maana viwango kwenye kutafuta wachumba, kwenye umasikini, utajiri n.k. Lets do something agaisnt mafisadi na haya mambo tusimuachie JK peke yake kwani wapo wengi na mtamchukua muda kuwamaliza kwa staili ya kuunda tume.
ReplyDeleteMlalahoi
Mzee wa kuperemba naona uko juxtaposed...
ReplyDeleteNatumai kuwa swala langu umelifikisha kwa kingalu.
Weekend njema...
Hawa wote wanapiga boksi?
ReplyDeleteMbona asilimia sabini wote wako nyumbani na asilimia ishirini wa ubalozi? Hiyo diaspora iwapi?
ReplyDeleteWe annon wa kwanza una matatizo sasa hao wanzanzibari wakwavutwe na kamba, mnajibagua kama nini, matatizo ya kutawaliwa sijui ni lini mtayaacha.
ReplyDeleteopen letter ya mheshimiwa raisi wa tanzania:
ReplyDeletemheshimiwa raisi kwa kifupi kila ulicho nacho ni MUNGU kakupa kwa kifupi kazi yako ina jukumu kubwa sana mbele ya kwanza MUNGU na taifa la tanzania na watu wake.
hivyo kwa kifupi mheshimwa raisi yote tuliyonayo binadamu ni uwezo wake MUNGU hivyo ukijiuliza umri ulio nao ni mkubwa kulinganisha na muda unaoweza kuishi.chukulia uishi miaka 70 na mara nyingi 70 unakuwa katika hali ya kuwa nyumba ya magonjwa.hivyo cha kufanya mheshimiwa raisi ni mema uliyoyafanya katika kuapa bila kujali mama, baba, ndugu au rafiki.pa kudumu ni akhera tulikuja bila nguo na tutarudi tukiwa mizigo kwenye shimo.hii mheshimiwa raisi na kukumbusha ikiwa leo tunamuogopa binadamu je MUNGU itakuwaje nakuombea kwa MOLA uchukulia haki ya kila raia kwa ukaribu na hasa rushwa na ufisadi ambao ukiachia itakuwa wewe umeruhusu na umeshirikiana na hao unahisi wazuri wako kumbe ni wabaya wako mbele ya MUNGU.MUNGU TUNAKUOMBA TUJALIE KILA KIUMBE TUFUATE MAAGIZO YAKO ILI TUWEZE KUPATA RADHI YAKO AMEN