gari ambalo marehemu chacha wangwe alipata nalo ajali
deus mallya, aliyekuwa na marehemu chacha wangwe wakati wa ajali hiyo
mdau jacob mugini katuletea picha hizi sasa hivi kuonesha hali ilivyokuwa huko tarime kwenye mazishi ya hayti chacha wangwe. juu ni meza kuu ambapo viongozi wa vyama vya siasa wakiwa wameketi, na chini ni baadhi ya waombolezaji


Hayati Chacha Wangwe

Na Mwandishi wa Globu ya Jamii, Tarime

Mazishi ya Mh. Chacha Wangwe, aliyekuwa Mbunge wa Tarime aliyefariki dunia kwa ajali ya gari majuzi huko Dodoma, yameshindwa kufanyika leo kijijini kwake Kamokorere baada ya kufumuka kwa vurugu kubwa ambapo wabunge na viongozi wa serikali na vyama vya siasa walohudhurian ilibidi watoke bomba kusalimisha maisha yao.

Vurugu hiyo ilianza dakika chache baada ya kuwasili kilioni hapo kwa Mwenyekiti wa Taifa wa CHADEMA, Mh. Freeman Mbowe, katika kijiji cha Kemokorere kiasi cha kilomita 20 hivi toka mjini Tarime.

Hali ilipokuwa mbaya, ilibidi Mh. Mbowe na viongozi wote waliohudhuria mazishini waondolewe kilioni chini ya ulinzi mkali wa FFU ukiongozwa na Kamanda wa Polisi wa mkoa wa Mara Afande Leberatus Barlow ambao walifanya kazi ya ziada kuepusha balaa.

Viongozi wengine waliohudhuria walikuwa ni pamoja na wenyeviti wa vyama vya upinzani Profesa Ibrahim Lipumba (CUF), Augustino Lyatonga Mrema (TLP), John Cheyo (UDP) James Mbatia (NCCR-Mageuzi) na Mbunge wa Karatu Mh. Wilbroad Slaa pamoja na kiongozi wa upinzani bungeni, Mh. Hamad Rashid.

Wote hao walisindikizwa chini ya ulinzi mkali wa FFU kuondoka mahali hapo na kuelekea Musoma. Waziri wa Kilimo na Umwagiliaji, Mh. Steven Wassira, na Manaibu Mawaziri ambao ni wabunge wa Kanda ya Ziwa, Dr. James Wanyacha na Gaudensia Kabaka nao ilibidi waondoke.

Ujumbe toka Kenya ulioongozwa na Dr Wilfred Machage ambaye ni mbunge wa jimbo la Kurya na pia Naibu Waziri katika serikali ya mseto ya Kenya pamoja na wakuu wa wilaya wawili nao walikuwepo na ilibidi waondoke kwa kuruka ukuta.

Tofauti na walivyoingia, itifaki haikuweza kufuata kama walipowasili wabunge 20 wakiongozwa na mbunge wa Bumburi Mh. William Lukindo vurugu hilo lilipoanza na ilibidi kila mmoja aondoke chini ya ulinzi mkali.

Maelfu ya waombolezaji, wengi wao wakiwa vijana waliobeba mabango yenye ujumbe mbalimbali unaohoji kifo cha Mh. Wangwe, walitawala hapo kilioni. Juhudi za Mkuu wa mkoa wa Mara Mh. Issa Machibya kuwatuliza hazikuzaa matunda.

Hata juhudi za kututuliza ghasia hizo za Wah. Zitto Kabwe na mmoja wa wanafamilia waandamizi kama vile Profesa Samwel Wangwe na Mkuu wa zamani wa Halmashauri ya Tarime Mh. Peter Wangwe pia hazikuambulia kitu.



Prof Wangwe aliwaambia waombolezaji hao wenye hasira kwamba familia ya Wangwe imeamua kumtafuta mtaalamu huru kuifanyia upya uchunguzi maiti ya hayati Chacha Wangwe ili kubaini alifariki kwa njia ipi.



Wengi ya waombolezaji wanatuhumu kwamba Mh. Wangwe hakufa kwa ajali ya gari. Mtu moja aliyekuwa na marehemu wakati wa ajali, Bw. Mallya, anahojiwa na polisi na uchunguzi wa kina unaendelea.















Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

Kuna Maoni 9 mpaka sasa

  1. AnonymousJuly 31, 2008

    C/HQ/ADM/SG/02/185 30 Julai, 2008


    MKUU WA JESHI LA POLISI,
    P.O. BOX,

    DAR ES SALAAM ,
    TANZANIA.

    YAH; KIFO CHA MHESHIMIWA CHACHA ZAKAYO WANGWE MBUNGE WA TARIME.

    Kutokana na ajali iliyotokea tarehe 28 Julai 2008 katika eneo la Pandambili Wilaya ya Kongwa Mkoa wa Dodoma na kusababisha kifo cha aliyekuwa Mbunge wa Tarime Marehemu Chacha Zakayo Wangwe, ninalazimika kukuandikia rasmi kuhusiana na taarifa mbalimbali ambazo zimekuwa zikiripotiwa na vyombo mbalimbali vya Habari hapa nchini juu ya utata ambao umekighubika kifo hicho na haswa mazingira ya ajali yenyewe. Katibu Mkuu wa CHADEMA, katika mahojiano yake na TBC1 katika mahojiano yake kwenye kipindi cha Jambo Tanzania alielezea pia utata huo na kutaka Jeshi la Polisi lifanye uchunguzi wa kina.

    Maelezo ya Ndugu Deus Mallya ameyatoa kwenye vyombo mbalimbali vya habari kuhusiana na jinsi ajali hiyo ilivyotokea na eneo ambalo yeye alikuwa amekaa wakati ajali inatokea , pamoja na kusema kuwa yeye alikuwa amekaa kiti cha nyuma huku Dereva wa Gari akiwa ni Marehemu Chacha Wangwe yameongezea kwenye utata huo.

    Taarifa ambazo zimetolewa na watoto wa Marehemu kama walivyohojiwa na vyombo mbalimbali vya habari na kuripotiwa na vyombo hivyo na haswa maelezo yaliyorushwa na Shirika la Utangazaji la Taifa (TBC), na vituo vingine vya Television, pamoja na Habari za Magazeti mbalimbali ya tarehe 30-07-2008 ,kama vile Magazeti ya The Guardian, Nipashe, Tanzania Daima ,Mwananchi na mengineyo ambayo yaliandika kuhusiana na maelezo aliyotoa Ndugu Deus Mallya pamoja na watoto wa Marehemu yakilinganishwa na maelezo ya Deus Mallya yanahitaji kupatiwa majibu ya kina, jambo ambalo CHADEMA kama mwathirika wa ajali hiyo isingeliweza kulifumbia macho.

    CHADEMA , tumefuatilia kwa kina sana kuhusiana na maelezo hayo ambayo yametolewa kwa nyakati tofauti na watu tofauti kuhusiana na ajali hiyo na hatimaye msiba huo.


    Hivyo basi , Chadema kama Chama kilichoathirika kwa kumpoteza Mbunge wake, Mwenyekiti wake wa Mkoa na aliyekuwa Makamu Mwenyekiti na hivyo kuwa na maslahi ya karibu sana katika uchunguzi huu, tunalitaka Jeshi la Polisi wakishirikiana na vyombo vingine vya Usalama kufanya uchunguzi wa kina kuhusiana na mambo yafuatayo;

    1. Kujua huyu ambaye alikuwa (Deus Mallya) na Marehemu kwenye gari lake wakati anafariki ni nani na anafanya shughuli gani.
    2. Deus Mallya alienda Dodoma kufanya shughuli gani na ana uhusiano gani na Marehemu na au Familia ya Marehemu.
    3. Ndugu Deus Mallya alikuwa amekaa kwenye kiti gani wakati ajali inatokea.
    4. Ni nani alikuwa anaendesha Gari wakati ajali na hatimaye umauti unamkuta Mheshimiwa Chacha Wangwe.
    5. Ni mazingira gani yaliyopelekea na au kusababisha ajali hiyo kutokea .
    6. Tunataka Polisi wachukue hatua stahiki za kisheria ili Deus Mallya akaisaidie Polisi na kuhojiwa kwa kina juu ya suala hili kwani maelezo yake yana utata mkubwa sana.
    7. Jeshi la polisi liitoe ripoti ya uchunguzi huo mapema na kuiweka ripoti hiyo hadharani.

    Tunapendekeza hatua hizo zichukuliwe mara moja kwani tunaamini kuwa kifo hiki kimeghubikwa na utata mkubwa sana na haswa kutokana na maelezo ambayo yamekuwa yakitolewa na aliyeshuhudia ajali (Deus Mallya) pamoja na watoto wa marehemu.


    Tunaamini kuwa utatupatia ushirikiano wa kina ili kuhakikisha kuwa hatua za haraka na za dharura zinachukuliwa mara moja kwa ajili ya kuujua ukweli wa kifo hiki tata.

    Pamoja na hayo, hivi karibuni wabunge wa CHADEMA wamekuwa wakipata taarifa za vitisho pamoja na kuzushiwa vifo kwa njia ya ujumbe mfupi wa simu za mkononi na ujumbe huo kusambazwa sana kama ilivyoripotiwa kwako na Mheshimiwa Zitto Kabwe (MB).

    Tunaomba wabunge wetu wapatiwe Ulinzi na pia taarifa hizo zifanyiwe kazi kwa kina.

    Nakutakia kazi njema.

    Wako katika ujenzi wa Demokrasia na Utawala Bora.




    ……………………
    John Mnyika - 0754694553,
    Kaimu Katibu Mkuu,
    Na Mkurugenzi wa Vijana Taifa ,

    Nakala:
    1. Mhe.Lawrence Masha – Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi
    2. Mhe.Dr. Willbrod Slaa (MB) - Katibu Mkuu CHADEMA .
    3. Robert Manumba -Mkurugenzi wa Upelelezi na Makosa ya Jinai.


    Nimepatiwa majibu yafuatayo. Bado mengine tunaweza kusahihisha kwa kadiri nzi anavyoruka ruka. So, right now I'll give the following info 80% ya usahihi.

    3.Huyu kijana yeye ndio alikuwa wa kwanza kuipigia polisi simu na kuwataarifu kuhusiana na msiba huo. Sasa hapa panaleta utata mkubwa sana ;

    a) Alipata wapi number za simu za polisi?Tena hapo hapo?
    b)Ni kwanini awapigie polisi wa kwanza ,na je?yeye kama alikuwa na simu za Wangwe aliwezaje kuzipata kwa hali gari lilivyokuwa?
    c)Huyu kijana aliwapigia simu watu wa Tarime na kuwafahamisha kuwa Wangwe amefariki ,na mmoja wapo ni aliyekuwa rafiki wa karibu wa Chacha ambaye alikuwa katibu wa CHADEMA wilaya ya Tarime aliyehamia CCM.
    D) Alimpigia simu mke wa Marehemu pamoja na ndugu zake marehemu, ila hakupiga simu kwa kiongozi yeyote wa CHADEMA ,ile hali kama alikuwa anatumia simu za Wangwe basi number za simu za viongozi wa CHADEMA zilikuwepo.
    e) Mkuu wa wilaya ya Kogwa alienda eneo la ajali in 30 minutes time ,baada ya ajali na ndio alimfahamisha Mkuu wa Mkoa ,then Waziri wa mambo ya ndani na then Spika.....
    f) Zitto alipigiwa simu na waziri Masha, na baada ya simu kukatika alimpigia spika na spika akasema hata yeye kayasikia hayo .

    4.Huyu kijana Mallya ,kwa taarifa za leo ni kuwa amekubali kuwa yeye ndio alikuwa anaendesha gari ,na hilo kalisema polisi .

    5.Huyu Mallya kuna taarifa kuwa ameiharibu simu yake na ameondoa simu card yake pamoja na kingine kikubwa na cha kustaajabisha ni kuwa ameondoa memory card ya simu yake .

    Sasa hili la memory card linatupa wasiwasi zaidi na hatujui ni kwanini hilo limefanywa hivyo na hii inaonyesha kuwa aliyefanya hivyo lazima atakuwa ni expert mzuri sana .

    6.Kwa taarifa za kiuchunguzi ni kuwa huyu Mallya alikutwa na bastola, na alisema kuwa ni ya kwake ,sasa hatujui kama hili polisi watalisema kwani hilo limesemwa na watu ambao walikuwepo wakati polisi walipokuwa wamefika eneo la ajali na kuanza upekuzi.

    7.Huyu Mallya ,inasemekana kuwa alikuwa na mtu mwingine kwenye gari ambaye wanakijiji wa pale hawakuweza kumfahjamu mara moja, na haijulikani alipo.

    8,kwenye eneo la tukio mzee wa pale kijijini ambaye alisaidia kumtoa Wangwe kwenye gari anasema kuwa huyu wangwe alikuwa amekaa kiti cha abiria mbele ,na alikuwa amefunga mkanda, na huyu mzee ndio alimtoa huop mkanda na kumtoa nje.

    My Take:
    - The burden of proof, iko kwa Polisi kumuweka kijana huyo kizuizini. My gut tells me something about assassination. It is just my gut and I probably am very wrong.
    - Kama kweli Mallya alikuwa na bunduki, was it discharged for any reason even "accidentally"?
    - Kuna mtu aliomba lift aidha walipoenda kununua "voucher" kutokana na ushauri wa Mallya. Huyo mtu wa tatu hakuwepo mwanzo wa safari, na kwa hakika hakuwepo mwisho wa safari. Who is he?

    ReplyDelete
  2. AnonymousJuly 31, 2008

    Oyaaaa Mbowe ahojiwe. Scotland Yard waletwe nchini kumaliza ubishi, Polisi wetu hawana ubavu.

    ReplyDelete
  3. AnonymousJuly 31, 2008

    Hakika katika mazingira ya utata ulioghubika katika mazingira ya kifo cha Mh. Chacha, wananchi hasa wawakilishwa wenyewe wana Tarime,hawana budi kabisa kuhoji na kuuliza hasa ni nini kimetokea,na kwa emotions/hisia tofauti zilizopo kwa sasa, lazima matukio km hayo ya ghasia tuyatarajie, tusisahau ki asili na ki historia wakurya wanajulikana kwa kuwa na hasira sana na wao hupenda sana kutetea maslahi yao ikibidi hata kwa "judo" ama aina ya kichapo ama "kipigo" cha aina yeyote, na ndio maana hata mke wa mkurya asipopigwa penzini huwa anadhani hapendwi...
    But all in all, lazima maswali yafuatayo YA MSINGI yajibike/yajibiwe kabla mwili haujazikwa:-
    1.Nani hasa alikuwa Dereva wa gari?
    2.Kwanini km ni kweli, watoto wanatoa taarifa tofauti kuhusu aliyetoka nyumbani anaendesha gari kuwa alikuwa Malya, kitu ambacho Malya anapinga kwamba hata kuendesha gari hajui.
    3.Watoto walipeleka gari garage gani?Ambayo ilitengeneza ama kuharibu nini?
    4.Gari ilikuwa na abiria wangapi na ambao walikaaje ndani ya gari?
    5.Nani hasa alikuwa dereva wa gari?
    6.Gari lilisimama mara ngapi na wapi na kwa lengo gani tangu wameanza safari na kabla ya ajali?
    7.Katika ajali iliyotokea usk na tena katika kajipori, Malya alipataje Simu ya marehemu, na kuitumia kuwajulisha watu juu ya ajali hiyo,maana kawaida simu lazima nayo ilitupwa mbali?
    8.Kwanini wakati anaita watu kuomba msaada huyo Malya,hakumtaja wala hakusema lolote juu ya mtu(inayesemekana kuwa abiria wa tatu)aliyekuwa akifukuza watu kusogelea gari na aliyekuwa akipiga sachi kwa marehemu?
    9.Je jeraha la marehemu usoni lilikuwaje? La kuchomwa kwa ncha kali, risasi, au chupa za vioo vya gari?
    10. Je damu iliyokuwa kwenye kiti imefanyiwa DNA kubaini km aliyekufa ni chacha?Na je kwa mujibu wa wataalam wa FORENSIC je damu ile ilikuwa imetoka saa ngapi au muda gani kabla(time frame) tangu ianze kutoka hadi walipoikuta pale kwenye gari??VERY VERY IMPORTANT.
    11.Mwenyekiti wa chama-CHADEMA "Mbowe",mbona hajatoa masikitiko au hata salam za pole za msiba na badala yake ni makatibu tu ndio wanaoongea? Yaani kweli ki protokali na ki siasa, mwenyekiti mkuu wa CCM Taifa(hata km alifanya km Rais) anaweza kutoa salam za pole walau kwa Familia na mwenyekiti wa CHADEMA(Tena Chama cha marehemu) asitoe neno hata moja,walau la pole hata kwa familia tu? Ni nini kimefichika hapo?
    Mungu ibariki Tanzania, na wote wanaoitakia mema.
    Mh Chacha na apumzike kwa Amani,AMEN

    ReplyDelete
  4. AnonymousJuly 31, 2008

    Huyu jamaa anayejiita Muombolezaji-Mdanganyika, lazima ni FBI. Ila kweli Wakurya watu wa kazi. Unacheki jinsi walivyotikisa kwenye msiba huu? Hawa jamaa kiboko, ndiyo maana Jenerali Ulimwengu anawasifia sana. Hawana unafiki, hawalazi jambo. Na ndiyo maana walipokuwa wengi jeshini rushwa haikuwemo jeshini. Washikaji watu wa shughuli kweli kweli.

    ReplyDelete
  5. michuzi,

    hizi habari sio za kweli. Tulioko Tarime kwenye msiba hatukuona fujo yoyote dhidi ya viongozi wa ccm au chadema.

    Watu wamekataa kuzika kwa vile kulikuwa na fununu kuwa risasi ilipatikana kwenye mwili wa Wangwe na hivyo familia ya marehemu ikaamua kusubiri uchunguzi ufanyike kabla ya kuzika.

    Si vizuri hivi umefanya kuweka habari ambazo inaonekana kama zina uongo kiasi fulani.

    ReplyDelete
  6. Ebana Kweli Mafia Imekomaa Bongo.Ila Cha Ajabu Umafia Wao Uko winjiwinji au waziwazi tatizo changa la macho lina take over.Ya ballal haijaisha limesanuka lingine.Wanasiasa mtamalizana bora wabox

    ReplyDelete
  7. MIMI NIMEWAHI KUPATA AJALI NIKIWA KAMA DEREVA NA MY WIFE WANGU ABIRIA KITE CHA MBELE NA ABIRIA MMOJA KITI CHA NYUMA KATIKA VITARA GRAND, WOTE TULIFUNGA MIKANDA NA GARI ILIHARIBIKA KUPITA HII INAVYOONEKANA HAPA SOTE WATATU TULITOKA SALAMA BILA HATA MKWARUZO,KWA KWELI MIKANDA INASAIDIA, NA PIA GARI ILIKUWA NA AIR BAGS ZILIVUMUKA NA KUTUSUKUMA NYUMA HIVYO HATUKUGONGA HATA KIOO KIMOJA, HII GARI ALIYOKUWA ANASAFIRI NAYO SI GARI YA SAFARI NDEFU WALA HAIFAI KWA SAFARI NDEFU, NA NINAWASII WATANZANIA KUTOFANYA SAFARI NA GARI KAMA, HIYO NI GARI YA MJINI TU KUENDEA KAZINI HASA UKILINGANISHA NA HALI HALISI YA ROAD ZETU. MWISHO POLENI WAFIWA.

    ReplyDelete
  8. hiyo bastola inaweza kuwa ya WANGWE mwenyewe na kama kulikuwa na risasi mwilini inaweza kuwa ilifyuatuka wakati wa ajili.

    ReplyDelete
  9. bwana...hii ishu nzito. Watu kibao wana interest zao hapa ambazo zinahitaji kuminywa chini. Siri za nchi na chama wadhani mchezo?! Its a cruel world out there...and i say it again...politics is a dirty game. Lakini mimi ninachopenda kuona ni polisi ya Tanzania kuweza kuwa na uwezo wa kuendesha uchunguzi kama huu ki-demokrasia na kwa uwazi. Yani ni aibu kuomba polisi nyingine kusaidia. When are we going to be independent? Mpka lini? Basi mimi naona nafuu hata tusingepata uhuru kama ni ivyo! How do u make the police into an independent, anti-corruption organisation?

    ReplyDelete

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...