Mhe. pole na majukumu,Najua kuna habari nyingi za huzuni na machungu na za kufurahisha; niwape wageni wa gulobu yetu dakika chache za kusahau machungu ya maisha na kutukuza nguvu ya upendo.
MABUSU YANGU DAZENI
Mabusu yangu dazeni, nayatuma kwako moyo!
Ulipo hapo mjini, natuma bila uchoyo,
Pokea wangu wa ndani, ni dazeni nikupayo,
Kwa hili Busu la kwanza, beti nazifungulia!
Mwah!!
Hilo la kwanza kwenye paji!
Mabusu yangu dazeni, moja moja narushia,
Nimeketi barazani, ujumbe nakutumia,
Wenye wivu jinyongeni, wa kwangu namwagia,
Kwa hili busu la pili, asante kwa yote pia!
Mwah!!
Hilo la pili, shavu la kushoto!
Mabusu yangu dazeni, tumetoka sisi mbali,
Nakumbuka vya zamani, tulipoanza wawili,
Mioyo ikashikani, mahaba yakashamili,
Kwa hili busu la tatu, mbali nakukumbushia!
Mwah!
Hilo la tatu, shavu la kulia!
Mabusu yangu dazeni, ninamshukuru Mola,
Mtukufu wa Mbinguni, mwenye kuzipinga hila,
Kakuleta ubavuni, ni bure siyo kwa hela,
Kwa hili busu la nne, ujue nakuhitaji!
Mwah!
Hilo la nne, shingoni kushoto!
Mabusu yangu dazeni, nisamehe nipokosa,
Yamenijaa pomoni, hata uliponiasa,
Kurudia sitamani, kufanya hivyo ni kosa,
Kwa hili busu la tano, nakuomba samahani
Mwah!
Hilo la tano, shingoni kulia!
Mabusu yangu dazeni, Mungu amekujalia,
Uzuri wako wa shani, binti wa Kitanzania,
Wengineo siwaoni, wewe najichagulia,
Kwa hili busu la sita, nashukuru wewe wangu!
Mwah!
Hilo la sita, mgongoni!!
Mabusu yangu dazeni, penzi lako limefana,
Twapendana kama nini, mitimani twashibana,
Kama tuliopeponi, mahaba yametunona,
Kwa hili Busu la saba, mpenzi nakutamani!
Mwah!
Hilo la saba, kwenye titi la kushoto!
Mabusu yangu dazeni, wanipa penzi si haba,
Wanipa kiulaini, tena siyo kwa kibaba,
Ya wengine siyaoni, la kwako limeniziba!
Kwa hili busu la nane, naapa mimi ni wako!
Mwah!
Hilo la nane, kwenye titi la kulia!
Mabusu yangu dazeni, wewe nakuaminia,
Mashaka kwako sioni, penzilo limetulia,
Habiba waniamini, moyo umenishikia,
Kwa hili busu la tisa, asante kuniamini!
Mwah!
Hilo la tisa, kitovuni!
Mabusu yangu dazeni, tusiwajali wakora,
Kulivunja watamani, penzi letu lawakera,
Visa wanavyovibuni, tuachane kwa papara,
Kwa hili busu la kumi, tugange mbele kwa mbele!
Mwah!
Hilo la kumi, nyongani kushoto!
Mabusu yangu dazeni, naapa mimi ni wako,
Moyo wangu mkononi, ushike unipe wako,
Kama kufuri langoni, funguo iwe ni yako,
Kwa hili kumi na moja, milele tutapendana!
Mwah
Kumi na moja, nyongani kulia!
Mabusu yangu dazeni, la mwisho nimefikia,
Wabarakatau Ma'nani, kwake nimejiachia,
Akupe afya mwilini, baraka kukumwagia,
Kwa hili busu dazeni, UJUE NINAKUPENDA
Mwah!
Busu hili dazeni!!......
M. M. Mwanakijiji (Sauti ya Shamba)
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...