JK akiongea na bwana george haily wa marekani huko washington dc,bwana haily ni kiongozi wa taasisi ya vyuo vya tekinologia barani afrika iliyopewa jina la nelson mandela akizungumza na rais wa kituo cha maendeleo duniani,center for global development,dr.nancy birdsall huko washington mwisho wa wiki
JK akizungumza na waandishi wa habari wa tanzania aliofuatana nao kwenye msafara katika hoteli ya intercontinental jijini new york mwisho wa wiki
Tutatokomeza malaria ifikapo 2015- Rais Kikwete
Na Mwandishi Maalum, New York, Marekani
Tanzania itatokomeza kabisa ugonjwa wa malaria katika miaka saba ijayo, yaani ifikapo mwaka 2015, kwa kutumia njia tatu zilizothibitishwa kimataifa kuwa zinamaliza ugonjwa huo, Rais Jakaya Mrisho Kikwete amesema leo (Jumapili, Septemba 28, 2008) mjini New York, Marekani.

Vile vile, amesema kuwa ziara yake kwenye Umoja wa Mataifa (UN) mjini New York imekuwa ya manufaa makubwa kwa sababu Afrika imefanikiwa kuwasilisha sauti yake katika masuala muhimu yanayohusu Bara hili.
Rais Kikwete anaondoka leo kurejea nyumbani.

Akizungumza na waandishi wa habari wa Tanzania walioandamana naye katika ziara hiyo kuhusu mafanikio ya ziara hiyo, Rais Kikwete amesema kuwa moja ya mafanikio ya ziara yake ni kwamba Tanzania imepata uhakikisho kuwa itaweza kutokomeza malaria ifikapo mwaka 2015.

Amesema kuwa ahadi mpya za kupambana na matatizo ya Afrika, ukiwemo mwelekeo mpya wa kupambana na magonjwa, na hasa malaria, inayoua watu wengi zaidi katika Afrika, ni moja ya mafanikio ya ziara yake kwenye UN.

“Katika Tanzania, tunapambana na malaria kwa njia tatu zinazokubalika duniani- kuhakikisha kuwa wananchi wetu wanatumia vyandarua vyenye dawa, tunanyunyizia dawa za kuuwa mbu katika madimbwi ya maji, na pia kuhakikisha kuwa wagonjwa wanapata dawa,” amesema Raia Kikwete katika mahojiano hayo kwenye Hoteli ya Intercontinental, mjini New York, Marekani.
Amesema kuwa njia zote tatu tayari zimeleta mafanikio makubwa Tanzania Visiwani ambako vifo kutokana na malaria vimeteremka mno, kutoka vifo 120,000 hadi 60,000 tu kwa mwaka.

“Na mafanikio hayo yanatokana na matumizi ya asilimia 40 tu ya vyandarua Tanzania Visiwani, lakini Zanzibar haiwezi kutomokeza malaria bila kuhakikisha kuwa Bara nayo inakuwa salama.
Hii ni mara ya tatu, tunafikia hatua ya kutokomeza malaria Tanzania Visiwani na bado ugonjwa huo umerejea kwa sababu Bara haitiliwa maanani,” amesema Rais Kikwete.

Ameongoza kuwa Tanzania inahitaji kiasi cha vyandarua milioni 15 vyenye dawa, kwa kila Mtanzania kulala bila bugudha ya mbu, na kuwa vyanzo mbali mbali vya misaada vimekwishahakikisha kuwa vyandarua hivyo vitapatikana baada ya awamu ya kwanza ya vyandarua milioni 5.2 kuwa vimepatikana.

“Kama mlivyosikia, Waziri Mkuu wa Uingereza, Gordon Brown, pekee yake ameahidi kutoa kiasi cha vyandarua milioni 100 katika miaka michache ijayo. Tanzania itanufaika na sehemu na vyandarua hivyo. Pili, tunao msaada wa sekta binafsi ambayo pia itatoa vyandarua. Mpango ni kutokomeza malaria ifikapo mwaka 2015 ni dhahiri utafanikiwa,” amesisistiza Rais.

Rais Kikwete ambaye aliwasili mjini New York, Marekani Jumapili iliyopita, ameliwakilisha Bara la Afrika kwa maana ya kushiriki katika mikutano kadhaa muhimu ikiwa sehemu ya mikutano ya mwaka huu ya Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa.

Mikutano hiyo ni pamoja na ule iliojadili mahitaji ya maendeleo ya Afrika, Mkutano wa Mjadala wa Baraza Kuu la Mwaka huu, Mkutano kuhusu Malengo la Maendeleo ya Milenia (MDG’s) na yanavyotekelezwa katika Afrika, na mikutano kuhusu Afya ya Mama na Mtoto, pamoja na ule kuhusu malaria.
Rais Kikwete amesisitiza ujumbe wake katika mkutano wa mwaka huu wa Baraza Kuu kuwa sasa ni dhahiri kuwa Afrika siyo Bara lisilokuwa na matumaini, la ovyo, na lenye kukatisha tamaa.

“Nimewaeleza wenzangu kuwa Afrika siyo Bara la ovyo tena. Ni Bara linaloinuka. Demokrasia inapiga hatua, tunaendesha changuzi bora zaidi, hali ya kisiasa imeimarika zaidi, tuna amani ya kutosha, ni kweli bado tunayo matatizo pale Somalia, Darfur, na Mashariki mwa Congo, lakini kwingine hali ni rushwa,” amesema na kuongeza:

“Uchumi wa Afrika unakua kwa asilimia kati ya asilimia tano na sita. Lakini bado bara letu na watu wetu ni masikini. Huu ndio mpaka wa mwisho wa jitihada za binadamu kuleta maendeleo. Kati ya nchi 50 masikini dhalili katika Afrika, 34 ziko Afrika. Kazi bado ni kubwa na hivyo wakubwa hawa wanatakiwa kutelekeza ahadi zao za kusaidia Afrika ambazo wamezitoa katika mikutano mingi tu,” amesema Rais.

Amesema kuwa nchi tajiri duniani zinazo wajibu wa kihistoria na ulazima wa kiroho kuzisaidia nchi masikini, kwa sababu isitoshe ziliahidi zenyewe kutoa misaada hiyo. Hii ndiyo njia pekee ya kuisaidia Afrika kufikia malengo ya Milenia. Kikao cha hapa kilikuwa kinaangalia hili, yaani jinsi ya kuisaidia Afrika kuongeza kasi ya kuweza kufikia Malengo la Milenia.

“Wala siyo kwamba wakubwa hawa wana tatizo la kufanya hivyo. Wanazo pesa za kutosha kuisaidia Afrika kuweza kufikia Malengo haya. Miaka miwili iliyopita aliyekuwa Katibu Mkuu wa UN, Kofi Annan aliomba kiasi cha dola za Marekani bilioni 50 ambazo zingeiliwezesha Bara la Afrika kufikia malengo ya Milenia,”

Ameongeza: “Hiki ni kidogo sana. Fikiria wakubwa hawa wanatoa ruzuku ya kiasi cha dola bilioni 365, kiasi cha bilioni moja kila siku, kuwalipa wakulima wake wasilime chakula cha kutosha. Japan inatoa kiasi cha dola saba kila siku kwa ng’ombe mmoja. Pamba ya Mali haiwezi kuuzika duniani kwa sababu ya pamba ya Marekani inauzwa bei ya chee … hizi ndizo tunaita trade distorting subsidies …”

Rais amesema kuwa kinachoitajika ni utashi wa kisiasa wa kuisaidi Afrika,
kwa sababu kiasi alichoomba Anan ni kidogo sana kulinganisha na ruzuku kwa nchi tajiri kwa watu wao.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

Kuna Maoni 5 mpaka sasa

  1. BABA KWA SAFARI HUYU MHHHHHH!HAJACHACHA!!!!!!!!

    ReplyDelete
  2. Mh JK ACHA HIZO,
    TUNGEFURAHI KUONA UNATOA SCIENTIFC DATA ZA KUONYESHA NI JINSI GANI MALARIA YATAANGAMIZWA.
    KWA NINI UNASEMA MALARIA YATAISHA 2015 WAKATI UMESHAONDOKA MADARAKANI??
    SWALA LA KWAMBA ZANZIBAR HAKUNA MALARIA SI LA KWELI, MBU BADO NI WENGI NA MALARIA BADO WAPO.
    NI VEMA RAIS ANGEKAA KWANZA NA WANA SCIENCE WANAOJUA NINI CHA KUFANYA ILI KUTEKETEZA MALARIA, THEN RAIS AKATOA REPORT KAMA OUTCOME YA SCIENTIFIC RESEARCH.
    MDAU

    ReplyDelete
  3. Kwanza kabisa ni jambo la kufurahisha kusikia huo mpango kamambe wa kutokomeza malaria ifikapo mwako 2015. Tunampa pongezi Rais JK kwa kumshikia bango huyo mmojawapo ya adui wakubwa wa maendeleo. Lakini tungependa kumtahadharisha (kama hajui) Rais wetu kuwa kufanikiwa kwa mpango huo mzuri kabisa utabakia kwenye mashairi kama hauendi sambamba na mpango wa kutokomeza adui ufisadi. Tungeomba kusikia iwapo serikali ya JK inaweza kuweka lengo la kutokomeza huyo adui, kwa mfano tuseme ifikapo hata 2020!!!!!

    ushauri tu.

    ReplyDelete
  4. MSANII BWANA MISIFA PHOTO OPPORTUNIST, ANAPENDA SIFA NA KUPIGWA PICHA. NDO MAISHA BORA KWA WOTE HAYO, MARA AMEGEUKA ANASEMA UTAPA MAISHA BORA KWA KUFANYA KAZI KWA BIDII, BILA YA KUANDAA YA KUWEZESHA WATU KUFANYA KAZI KWA BIDII, ACHENI UJANGALA. NA PUNGUZA KUTEMBEA, HIYO NDO NJIA RAHISI YA UFISADI KWA SAFARI IMPREST SIYO??/

    ReplyDelete
  5. Adui mkubwa wa Tanzania sio Ujinga, Umaskini na Magonjwa tena...adui mkubwa ni UFISADI!
    Pigana na ufisadi mazee...utatumaliza.
    Target ya kumaliza Malaria by 2015 sidhani kama itafikiwa. Ukizingatia malaria ilivyo...ni tofauti kidogo na polio na hayo mengine walioweza kumaliza. Labda waje na cure tu...lakini so kutokomeza.

    ReplyDelete

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...