
Bill Gates: Tunataka kuendelea kusaidia Tanzania
Na Mwandishi Maalum, New York, Marekani
MMOJA wa matajiri wakubwa zaidi duniani, Bill Gates, amesema kuwa taasisi yake ya Bill and Melinda Gates Foundation itaendelea kusaidia sekta za kilimo na afya nchini katika jitihada zake kusukuma mbele maendeleo ya Tanzania.
Gates, ambaye amesema kuwa kwa sasa anaifanyia kazi muda wote taasisi yake hiyo, pia ameonyesha nia ya kusaidia katika sekta ya elimu pamoja na kusisitiza kuwa ataendelea kujikita zaidi katika sekta ambazo taasisi yake inasaidia kwa sasa.
Gates ametoa msimamo huo leo (Jumatano, Septemba 24, 2008) wakati alipokutana na kufanya mazungumzo na Rais Jakaya Mrisho Kikwete katika Hoteli ya Intercontinental Barclay mjini New York, Marekani, ambako Rais anahudhuria kikao cha 63 cha Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa.
Katika mkutano huo, tajiri huyo ambaye alitengeneza fedha yake katika masuala ya teknolojia ya mawasiliano na kompyuta, mara kwa mara, amemwuliza Rais Kikwete ni kwa namna gani taasisi yake inaweza kuisaidia Tanzania.
Mbali na msaada katika maeneo ya afya na kilimo, tajiri huyo pia anasaidia katika kuanzisha chuo cha teknolojia kwenye Chuo Kikuu cha Dodoma.
Kabla ya kukutana na Rais, Gates ameshiriki katika mkutano wa waandishi wa habari ambako yeye na Rais Kikwete wametangaza Mpango wa Ununuzi wa Mazao ya Wakulima katika Afrika wa P4P, unaolenga kuwaunga mkono wakulima, kwa kuwahakikisha, miongoni mwa mambo mengine, masoko ya kuuza mazao yako.
Taasisi ya Gates inachangia Mpango huo utakaogharimu dola za Marekani milioni 72, na kujumuisha sekta za umma na binafsi chini ya Mpango wa Chakula Duniani (WFP).
Pamoja na Rais Kikwete na Gates kwenye mkutano huo wa waandishi wa habari walikuwa ni Rais Yoweri Museveni wa Uganda, Rais Paul Kagame wa Rwanda, Rais wa taasisi ya Howard Buffet, Howard Buffet, mke wa Rais wa Guatemala, Sandra Torres Colom pamoja na Mkurugenzi Mtendaji wa WFP, Josette Sheeran.
Kabla ya kukutana na Gates, Rais Kikwete amekutana na kufanya mazungumzo na Rais Lula de Silva kwenye makao makuu ya Umoja wa Mataifa (UN).
Katika mkutano huo, Rais Lula amemwalika Rais Kikwete kutembelea Brazil baada ya Mkutano wa Kwanza wa Afrika na Marekani Kusini uliopangwa kufanyika Novemba, mwaka huu, mjini Carcas, Venezuela. Rais Kikwete amekubali mwaliko huo.
Viongozi hao wamekubaliana kuwa kabla ya ziara hiyo ya Rais Kikwete, utumwe ujumbe wa wataalam wa Tanzania kwenda Brazil kujifunza kutokana na uzoefu wa nchi hiyo katika sekta ambazo Brazil inafanya vizuri duniani, kikiwamo kilimo.
Baadaye jioni, Rais Kikwete amekutana na kufanya mazungumzo ya muda mrefu na Rais Paul Kagame wa Rwanda kuhusu mipango ya ujenzi wa reli kati ya Tanzania na Rwanda.
Katika kikao hicho kilichohudhuriwa na watalaam wa reli, masuala ya fedha na mawaziri wa nchi hizo mbili, viongozi hao wamesikiliza maelezo ya wataalam kuhusu ujenzi wa reli hiyo inayotakiwa kuanzia Isaka, Tanzania kwenda Kigali kupitia Burundi.
Viongozi hao wawili wamewataka watalamu hao kuongeza kasi yao katika kufanikisha mpango wa ujenzi wa reli hiyo.
Mbali na mikutano huo, Rais Kikwete pia ameshiriki katika kikao cha viongozi wa Jumuia ya Madola kilichofanyika kwenye makao makuu ya UN.
Miongoni mwa mambo mengine, kikao hicho kilikuwa kinapokea ripoti kuhusu msimamo wa Jumuia hiyo juu ya mageuzi makubwa yanayotakiwa kufanyika katika taasisi za kimataifa zikiwamo zile za fedha.
Ends
Sio mbaya JK akitembea na kuona jinsi gani watu wengine wanaendeleza nchi zao..ni sehemu ya kujifunza...Jk fanya mambo tujenge reli hiyo na kama inapita Burundi mpaka Rwanda hapo ndio kwa kutengeneza fedha na kuzipa dili bandari za bongo mwisho wake mapato kwa serikali,kazi kwa wananchi bandarini..safari zitakuwa hazina maana kama hakuna tunachopata..badala ya kutumia fedha za walipa kodi
ReplyDeleteJAMANI TUKUBALI TUKATAE JK ANAJITAHIDI SANA KUTANGAZA NCHI YETU NAMUUNGA MKONO SANA MANAKE WAKENYA WAO WAMEJULIKANA ZAIDI KWA AJILI YA MICHEZO MBALIMBALI KWETU SISI JK ANATUSAIDIA SANA KWA KUFANYA ZIARA MBALIMBALI INAPENDEZA.
ReplyDeleteBALTAZAR
WWW.KIPEPEOTOURS.COM
BALTAZAR....
ReplyDeleteJiulize hao kina Bill Gates waliomba msaada kwa nani mpaka wakaendelea? Na hebu jiulize, jurani yako au rafiki yako akikuomba msaada wa kumjengea nyumba ya kuishi yeye, mkewe na watoto wake utamjengea? Jibu ni kwamba hutomjengea hata una pesa kiasi gani. Ila utamjengea pale unapotaka kupata kitu fulani toka kwake!
Jamani, kuwa na rais anayetembeza bakuli la kuomba omba misaada kila siku ni aibu isiyomithilika. Tulioko nje ya nchi tunaona aibu kwa niaba yake!!!!