ZAIN, kampuni ya simu za mkononi inayoongoza kwa kutoa huduma bora katika nchi 22 barani Afrika na Mashariki ya Kati, imetangaza majina ya shule 26 kutoka mikoa yote ya Tanzania zitakazopewa vitabu vinavyotolewa katika programu ya Zain ya Build Our Nation (BON) kwa lengo la kuinua kiwango cha elimu nchini.
Shule hizo zilichaguliwa mwishoni mwa wiki jijini Mwanza katika bahati nasibu iliyofanyika katika Shule ya Sekondari Ibinza iliyoko wilayani Ilemela ikiongozwa na Mkuu wa Wilaya ya Ilemela, Samwel Kamote na Ofisa Elimu Taaluma wa Mkoa wa Mwanza, Stella Nyala na kuhudhuriwa pia na walimu kutoka shule kadhaa za Mwanza na wanafunzi wa Ibinza.
Shule zilizochaguliwa na mikoa zinakotoka katika mabano ni Shule ya Sekondari Kiranyi (Arusha), Shule ya Sekondari Chihanga (Dodoma), Shule ya Sekondari Miyomboni (Iringa), Shule ya Sekondari Nyambusozi (Kagera), Shule ya Sekondari Mtangani (Kaskazini Pemba), Shule ya Sekondari Biturana (Kigoma) na Shule ya Sekondari Kiselu (Kilimanjaro).
Nyingine ni Shule ya Sekondari Mtambile (Kusini Pemba), Shule ya Sekondari Maina (Kusini Unguja), Shule ya Sekondari Kinjumbi (Lindi), Shule ya Sekondari Gumanga (Singida), Shule ya Sekondari Bonga (Manyara), Shule ya Sekondari Hanyari (Mara), Shule ya Sekondari Chalagwa (Mbeya), Shule ya Sekondari Kidatu (Morogoro), Shule ya Sekondari Lengo (Mtwara), Shule ya Sekondari Ihanamilo (Mwanza).
Nyingine ni Shule ya Sekondari Mkwaya (Ruvuma), Shule ya Sekondari Chenge (Shinyanga), Shule ya Sekondari Itunduru (Tabora), Shule ya Sekondari Kivesa (Tanga), Shule ya Sekondari Kerezange (Dar es Salaam), Shule ya Sekondari Kaskazini Unguja (Kaskazini Unguja), Shule ya Sekondari Kijini (Kaskazini Unguja), Shule ya Sekondari Matimbwa (Pwani) na Shule ya Sekondari Kabungu (Rukwa).
Katika bahati nasibu hiyo iliyoendeshwa na Meneja wa Huduma za Jamii wa Zain Tanzania, Tunu Kavishe na Meneja Mauzo wa Zain Kanda ya Ziwa, Ali Maswanya, shule saba kutoka mikoa ya Ruvuma, Lindi, Mjini Magharibi, Kusini Pemba, Kusini Unguja, Kaskazini Unguja na Kaskazini Pemba iliyosalia mwezi uliopita, pia zilikabidhiwa vitabu vyao.
Build Our Nation ni programu ya Zain Tanzania yenye lengo la kusaidia na kuwajibika kwa jamii ambayo imekuwa ikichangia vitabu kwenye shule za sekondari kwa mikoa yote 26 ya Tanzania, ili kuhakikisha kiwango cha elimu kinaongezeka Tanzania.
Tunu alisema Zain imedhamiria kusaidia jamii na itaendelea kufanya hivyo ikiamini mchango huo katika sekta hii utasaidia kukuza kiwango cha elimu Tanzania na kuboresha maisha ya wanafunzi.
Baada ya kukabidhi vitabu vyenye thamani ya sh. milioni 1 kwa Mkuu wa Shule ya Sekondari Ibinza, James Chisanda, Mkuu wa Wilaya ya Ilemela, Samwel Kamote aliipongeza Zain Tanzania kwa mchango huo na huduma inazotoa kwa jamii, hususan sekta ya elimu.
"Elimu ni agizo la Mwenyezi Mungu, nawaasa wanafunzi mtumie vitabu hivyo kwa uangalifu mkubwa, hata vitabu vitakatifu vya Mungu, Biblia na Korani vinatuagiza vikisema: "Mkamate elimu, ndio uzima wako," alisema Kamote.
Alisema Serikali inaamini mchango wa Zain katika sekta hii muhimu utasaidia kukuza kiwango cha elimu Tanzania, kuboresha maisha ya wanafunzi na kusaidia kuimarisha uchumi.
Zain Tanzania ilizindua programu ya ‘Build Our Nation’ Mei 10, 2004 na programu hiyo inadhihirisha uwajibikaji wa kampuni hiyo katika kusaidia kuinua elimu nchini.
Mradi huo umegawanywa katika awamu nne ambapo ya kwanza, shule moja kutoka kila mkoa inachaguliwa katika bahati nasibu inayoendeshwa kwa kompyuta ili kupata vitabu vyenye thamani ya sh. milioni 1. Hii inaiwezesha Zain kuepuka uteuzi wa upendeleo kwa shule husika, na kutoa kipaumbele kwa shule zote.
Katika kila awamu, shule 26 zinachaguliwa kutoka mikoa yote Tanzania. Baada ya kuchaguliwa, Zain inapata orodha ya vitabu vinavyohitajika zaidi katika kila shule, na inachukua jukumu la kununua na kuvikabidhi.
Tunu alisema hadi kufikia mwishoni mwa mwaka huu 2008, Zain itakuwa imetumia zaidi ya sh. milioni 500 katika kutekeleza programu hiyo na zaidi ya shule za sekondari 516 zitanufaika kutokana na mradi huo.
Katika mradi wa BON, pia Zain inatoa ofa ya kuwasomesha wanafunzi wanane bora wa kike na kiume wanaopata ruhusa kutoka vyuo vikuu nchini. Kufikia mwishoni mwa mwaka 2008, Zain itakuwa inasomesha wanafunzi 31 katika programu hiyo.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...