CHADEMA YAPETA TARIME KWA KURA NYINGI. MATOKEO YALIVYOTANGAZWA SASA HIVI NI KAMA IFUATAVYO

UBUNGE:
CHADEMA - 34,545
CCM - 28,996
NCCR-MAGEUZI - 949
DP - 305
UDIWANI
CHADEMA - 4,820
CCM - 3,239
HABARI NDIYO HII...
CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kimeibuka kidedea katika uchaguzi mdogo wa ubunge na udiwani wa Tarime uliofanyika juzi.
Mgombea ubunge wa chama hicho, Charles Mwera, alitangazwa kumrithi Chacha Wangwe aliyekufa ajalini Julai mwaka huu, baada ya kushinda kwa kupata kura 34,545 huku mgombea wa CCM Christopher Kangoye akipata kura 28,996.
Mgombea wa NCCR-Mageuzi, Haruni Marwa alipata kura 949 wakati mgombea wa DP Benson Makanya alipata kura 305.
Kwa ushindi huo wa ubunge na udiwani Chadema inaendelea kuongoza halmashauri ya wilaya ya Tarime huku CCM ikiendelea kubaki chama cha upinzani katika halmashauri hiyo.
Kwa upande wa udiwani mgombea wa udiwani wa Chadema, John Heche, alishinda kwa kupata kura 4,820 akifuatiwa na mgombea wa CCM, Peter Wambura, aliyepata kura 3,239. Mdogo wake marehemu Wangwe, Gideon Wangwe wa NCCR- Mageuzi aliambulia kura 169, John Rotente wa CUF kura 79 na Johanes Sando wa DP alipata kupata kura 24.
Baada ya matokeo hayo kutangazwa jana na msimamizi wa uchaguzi huo Trasias Kagenzi, mgombea huyo wa CCM Kangoye alisema hakuridhika na matokeo hayo kwa kile alichodai kuwa kulikuwa na hitililafu wakati wa kuhesabu kura na wakati wa kampeni.
Kangoye ambaye alifika katika ofisi ya halmashauri muda mfupi baada ya kutangazwa matokeo hayo huku akiwa amefuatana na Katibu wa CCM wa wilaya ya Tarime, Iddi Stambuli, alisema atapinga matokeo hayo kwa msimamizi wa uchaguzi na ikishindikana ataenda mahakamani.
Mgombea huyo pia alikataa kusaini matokeo hayo na kukinzana na Msimamizi wa Uchaguzi ambaye awali alisema wagombea wote wamekubali na kusaini matokeo.
Licha ya msimamo huo wa Kangoye, msimamizi wa uchaguzi alimkabidhi Mwera hati ya kumtambua kuwa ni mbunge wa halali wa jimbo la Tarime.
Kangoye alisema msimamizi alitangaza matokeo huku akiwa bado anajumlisha kura za vituo alizopewa na mawakala wa CCM.
Alianisha kasoro nyingine kuwa ni vitisho vya nguvu vilivyowafanya wapiga kura wasijitokeze kupiga kura. Akizungumza kwa huzuni, Kangoye alisema vitisho vya mambo yatakuwa kama Kenya na makundi ya vijana ya kujaa katika vituo vya kupigia Kura, ndivyo vilivyofanya wapiga kura 78,186 ambao hawakujitokeza kutumia demokrasia yao kati ya 146, 919 ambao walijiandikisha katika Daftari la Kura.
Kangoye alipingana na kauli ya Katibu Mwenezi wa Chama hicho, John Chiligati, ambaye alisema mwishoni mwa wiki kuwa kama wagombea wao watashindwa watakubali matokeo kwa maelezo kuwa hiyo ndio demokrasia ya kweli.
Kwa upande wake, Mwera licha ya kutangazwa mshindi, alikiri kuwa uchaguzi huo ulikuwa na kasoro nyingi za vitisho vya polisi, watu kukatwa mapanga lakini wananchi wamekubali sera zao na wamemchagua awe mwakilishi wao bungeni na kuahidi kuwa ataanza kazi mara moja ya kuwatetea bila kubagua Itikadi za vyama.
Mwera alifafanua kuwa atavaa viatu cha marehemu Wangwe kwa kutetea haki za wanyonge. Naye Naibu Katibu Mkuu wa Chadema, Zitto Kabwe alisema amepata mpiganaji mwenzake ambaye ataongeza nguvu ya upinzani ya kuwashughulikia mafisadi.
Zitto alikumbusha kuwa ni mara ya kwanza katika kuanzishwa mfumo wa vyama vingi mwaka 1992 kwa Chadema kushinda uchaguzi mdogo.
Kabla ya kutangazwa matokeo wafuasi wa Chadema walianza kushangilia kutokana na matokeo ya awali kuonyesha ilikuwa inaongoza kwa kwenda ofisi za Halmashauri ya Wilaya zilizotumiwa na Tume ya Uchaguzi.
Wakiwa bado mita 400 kufika eneo ambako matokeo yalikuwa yatangazwe walikumbana na kigingi cha polisi na kushindwa kujizuia huku wakiimba nyimbo kuwa Chama cha wahuni chashinda, mende kaangusha kabati na kuanza kujibizana na polisi waliokuwa na silaha mbalimbali.
Baada ya majibizano hayo, polisi walianza kupiga mabomu ya kutoa machozi huku nao wakiwapiga na kuwajeruhi polisi kadhaa kwa mawe na kuanza kutimua huku wakipiga yowe.
Tukio hilo lilichukua saa nne na kufanya kazi za biashara mjini hapa kufungwa na shughuli za mahakama ya mwanzo kusitishwa. Katika sakata hilo polisi ambao walikuwa wanaongozwa na Kamanda wa operesheni maalum nchini Venance Tossi iliwakamata zaidi ya watu 50.
Wananchi hao walikuwa wakipiga kelele kuwa kucheleweshwa kwa matokeo ni jaribio la kuwapokonya ushindi. Polisi waliokuwa wamejipanga kila kona ya kuzunguka hizo za halmashauri walifikia hatua za kuwazuia hata watumishi mbalimbali wa Serikali akiwemo Hakimu wa Mahakama ya mwanzo ya Tarime Mjini, Samweli Gimeno ashindwe kwenda katika eneo lake la kazi.
Mchakato wa kuwania kiti cha ubunge Tarime kilianza Septemba 14 kwa vyama vyote kunadi sera zake kwa wananchi na kufikia tamati juzi huku kampeni hizo zikigubikwa na mbwembwe na vurugu, fujo za kila namna na kufikia hatua za watu kumwaga damu kwa kukatwa mapanga.
Miongoni mwa watu ambao walionja chungu ya kampeni ni kiongozi wa DP taifa Mchungaji Christopher Mtikila ambaye alishambuliwa kwa mawe mawe hadi kumjeruhi kichwani.
Pia baadhi ya watu wengine walijeruhiwa kwa mapango na wengine kuuana kwa ushabiki wa vyama. Miongoni mwa mwembwe katika kampeni hiyo ni kurushwa kwa helkopita tatu.
Chadema ndicho kilichoanza mbwembwe hizo kwa kupaua anga kwa kutumia Helkopta na CCM kujibu mapigo kwa kupeleka mbili kwa mpigo ambazo licha ya kuyafikia maeneo mengi vijijini lakini Helkopta ya mbowe imezitungua na kuibuka Mshindi wa Udiwani na Ubunge.
Nashon Kennedy anaripoti kutoka Mwanza kuwa Katibu Mkuu wa CCM Yusuf Makamba amesema CCM inakubaliana na ushindi huo na kukiri kuwa ingawa walijiandaa kwenda kumg'oa mtu lakini haikuwa bahati yao.
Aliipongeza Chadema kwa ushindi ilioupata lakini akawatahadharisha kuwa wakae mkao wa kuondoka ifikapo mwaka 2010 kwa maelezo kuwa CCM ni kama wamejikwaa tu.
"Unapoanguka usiulize umeangukia wapi, angalia ulipojikwaa, tunawapongeza Chadema kwa ushindi huu walioupata,” alisema.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

Kuna Maoni 31 mpaka sasa

  1. zidumu sera za mwenyekiti
    hehehe
    imekula kwa CCM pamoja na janja zote.
    Kweli i sense a "wind of change" coming to TZ. Safi sana

    mtoto

    ReplyDelete
  2. safi sana Mura, huu ndo mwendo wakazi wote wa Migodini mnapaswa kuwaenzi wana tarimr ni watu wenye msimamo hata baba wa Taifa alitokea huko

    ReplyDelete
  3. INA MAANA PAMOJA NA KUTISHA WATU KWA KUTUMIA VYOMBO VYA DOLA MA KUWAPIGA WAFUASI WA CHADEMA MAPANGA BADO CCM IMESHINDWA?

    ReplyDelete
  4. Thats what am talkin about!!!!!!!!!!!
    Congrats sana CHADEMA kwa kufanya kweli, chama cha mafisadi taratibu kitatokomea

    Ila inasikitisha kuwa wakati watanzania wa kawaida wasio na elimu huko Tarime wameamka lakini watanzania wanaojiita wamesoma na wana 'exposure' huko nje wako usingizi mzito kazi yao ni kufungua matawi ya CCM. Shame on you!!!!

    Na dongo lingine liende kwa watu wa mijini hapa TZ hasa Dar, Arusha, Mwanza etc inasikitisha kuona hawa watu ndio wangeongoza kwa kuleta mabadiliko lakini cha ajabu hakuna hata mbunge mmoja wa upinzani sehemu hizo badala yake wananchi wa huko vijijini Karatu, Tarime, Mpanda, Kigoma kaskazini ndio wanaoleta mabadiliko

    Wake up my brothers & sistaz

    ReplyDelete
  5. anon wa October 13, 2008 1:33 PM Kawaida change hasa haitoki kwa wasomi bali wale watu wa chini. Katika enzi za Rome raia walikuwa wanaitwa "the mob". Once the mob is dissatisfied lazima change ije tu. Walidhani wananchi ni wajinga wanaibiwa waziwazi tu? Kwanza nimeshangaa kuwa wamepata hata hizo kura 28,000. The mob has spoken...

    mtoto

    ReplyDelete
  6. Wasi wasi wangu mkubwa ni kuwa ikiwa baada ya nguvu zote za dola zilizotumika CCM imeshindwa basi watarudi tena kuchota mabilioni ya pesa kuongeza nguvu katika chaguzi zijazo. Si tumeambiwa kuwa sehemu kubwa ya yale mabilioni ya EPA yalichukuliwa na CCM kwa matumizi ya uchaguzi mkuu uliyopita na kujiwekea ''vijisenti'' kidogo kwenye mabenki ya nje.

    ReplyDelete
  7. Ogopa sana binadamua anaposema "IMETOSHA".Lolote linaweza tokea.Sio bunduki,kofia,khanga,takrima au helikopta zitakazoweza badili msimamo wake.

    CCM inabidi "isome alama za nyakati"..2010 sio mbali..

    Ni kweli mabomba yatatoa maziwa nchi nzima kama walivyohaidi?


    Huo sio ushindi wa CHADEMA bali ni ushindi wa WANYONGE dhidi ya MAFISADI.

    TUTAFIKA TU.

    ReplyDelete
  8. Sera mbaya ya madini inayojali wawekezaji wa Nje na kuwatimua na kutowajali wazawa ndiyo iliyoiponza CCM Tarime watu wakawachukia na kuwanyima kura.

    Nadhani CCM hawakuwa na mshauri mzuri wa kisiasa .CCM na Mtikila wangejua kuwa hoja ya wananchi wa Tarime si kifo cha Wangwe bali mambo ya madini wasingehangaikia hoja mufilisi ya kifo cha Wangwe.

    koloboi@yahoo.com

    ReplyDelete
  9. Tehe he he ,wacha ncheke mie ,CCM chali..labada wangetumia chopper 10,zingesaidia.Inafurahisha kuona watu wa vijijini wana mwamko mkubwa kuliko hata watu wa mijini.Bravo CHADEMA.

    ReplyDelete
  10. Ni lazima tuwapongeze watu wa Tarime kwa uamuzi wao wa busara wa kutokukubali kuburuzwa. Hili lichama lipo madarakani miaka yote hakuna mabadiliko, we need a wind of change,mpaka sasa ninawakubali Mura na watu wa Kigoma siku zote wamekuwa wakifanya yasiyotarajiwa na CCM. Ni kweli tuwazomee wanaojiita wasomi, wengine wanataka mabadiliko utakuta matangazo kibao hata kwenye vyuo vikuu tawi la vijana wa CCM. Hii yote ni kwa sababu watanzania wengi ni wabinafsi, wanataka kujipendekeza wagawiwe elfu 5 ili wawauze watanzania. Itabidi sikumoja watu waaccount kama kweli elimu imewasaidia. utasikia CCM reading, ccm uk, hata aibu hamna?? mnataka nin??? au mnaona ni sawa nchi inavyoendeshwa?? u r very selfish!!shame on u!! Hurree Tarime

    ReplyDelete
  11. PONGEZI ZANGU ZA DHATI ZIWAFIKIE WANA TARIME WOTE KWA UPEO MKUBWA WALIO NAO. KWA KULINDA KWA HALI NA MALI KURA ZAO, KWA KUSHINDA KWA KISHINDO, JAPO NAAMINI WAMEIBIWA KURA NYINGI. KWA KULA TRAKRIMA KWA SANA HALAFU MWISHO WA SIKU MAMBO KUWA MSTARI, CCM CHAMA CHA MAFISADI, MNATAKIWA KUJIREKEBISHA SASA, NI WAKATI WENU WA KUJITAKASA. NAMI NIMEKIHAMA RASMI CHAMA CHA MAJAMBAZI.HAMNA MAREFU YASIYO NA NCHA.TARIMEEEEEE OYEEEEEEE!

    ReplyDelete
  12. Kweli nimeamini Wakurya hawapendi `longolongo'. Na ili tuendelee na kutokee mabadiliko ya kweli inahitajika tufanye hivi. Vinginevyo tutaishia kuwaneemesha mafisadi. Wewe huoni wanavyofanya hata katika `wizi' wa mitihani. Fikiria watoto wengi wa wazito waliofaulu kwa njia hii...tunawajua, na wengi wamepelekwa/walipelekwa nje na wamerudi na kuajiriwa kwenye makampuni, mashirika ya maana .

    ReplyDelete
  13. Ni vigumu kuhitimisha kuwa watz wanaikataa C.C.M ikitiliwa maanani kuwa viti vyote viwili vilikuwa vinashikiliwa na Chadema.
    Sasa wapinzani (Chedema) wajiandae vizuri ili baada ya miaka 2, sisiemu iwe wapinzani.

    ReplyDelete
  14. Kenya imeshinda uchaguzi Tarime?
    Tanzania iende nayo kugombea ubunge Kisumu?

    ReplyDelete
  15. Hapo si suala la usomi ndugu zangu, ni watu na itikadi. Kwanza kabisa, kuwa Dar,Reading, NY, Mwanza au Tarime hakumaanishi usomi. Wengine tunaishi dar kwa kujishughulisha na mambo magumu magumu yasiyo rasmi kwa ajili ya kujipatia mkate wa kila siku. Hilo darasa hatulijui saana kama wengi wanavyodhani. Upataji wa habari na uwezo wa kupambanua mambo hauwezi kujengeka kwa kuishi Dar, Machame au Reading. Aina ya exposure tunayoipata inategemea saaana aina ya maisha tunayoyatarajia na tunayoyaishi. Kama mimi nilikuja huku kwa ajili ya kuchuuza mbogamboga, si ajabu nikajidanganya kuwa mambo mengine yasiyohusu mbogamboga ni irrelevant kwangu.

    Kwa maana hiyo usishangae kuona mwana Tarime anaupeo mkubwa kuliko mimi wa NY. Kwani ni asilimia ngapi ya hawa wanaoitwa wasomi wako katika miji mikubwa kama Dar? Wanatosha kuleta mageuzi kwa kura? Wenye njaa za kuhongwa kwa elfu tano tano huku Dar na Tarime wanawiana kwa uwing? Na hao wa Reading anayesuport uwepo wao huko ni wao wenyewe au? Wana matarajio gani baada ya kurejea nchini? So itikadi inajengwa na mambo mengi. Usomi maana yake nini?

    Nadhani tusitarajie sana kuwa wasomi au wa mijini ndio watakaoleta mabadiliko. Aina za exposure ziko tofauti sana kwa watu tofauti. Vijana wa kijijini kwetu wakija town wanafikiria kuishi maisha fulani ya kisanii zaidi. Hayo ndiyo mambo wanayopenda kuyajua na kuyasimulia, bila kujali nini wanachangia katika jamii kwa huo usanii. Kwao mafanikio ni kuwajua wangapi wanaimba miziki wa kizazi kipya na kuyajua mashairi yao, bila kujali maudhui. Na hawa ndio wakazi wa Dar unaowataja. Wanaoweza kupambanua mambo ni wale wenye uwezo wa kusoma, tena kusoma sana na kuelewa maana ya maandishi ya vitabu vya sayansi asilia, sayansi ya jamii, nakadhalika. Vinginevyo watu wataishia kwenye ushabiki tuu bila hata kuelewa kama watakaowachagua ni kweli wataleta mabadiliko.

    Asanteni.

    Wa Milimani.

    ReplyDelete
  16. Na bado!! Haya yaliyotokea Tarime ni fundisho kwa hiki chama cha mafisadi. Ni aibu kwa serikali iliyopo madarakani, kwani kero kwa wananchi zimezidi, migomo kila kunapokucha tena kwenye sekta muhimu afya, elimu nk.
    Na haya yaliyosemwa na gazeti letu tulipendalo Mwanahalisi yatadhihirika muda si punde. Tuendelee hivi kama wanatarime na matunda tutayaona. Wanauza sura ehh!!Ni hayo tu.

    ReplyDelete
  17. Chadema hoyeeeeeee

    ReplyDelete
  18. CCM si wangesema tu tuwape lile jimbo la Tarime bure bila ya uchaguzi na mabilioni yale ya mapesa wapewe watoto wa walalahoi wanao hangaikia Ufadhili Vyuo Vikuu?Aibu kubwa hii!Na Bado.Vijana wa Tarime wametamka.Kwamba hawawezi kuongozwa na Mafisadi.Hawawezi kudanganywa tena kama watoto wadogo.CCM labda ikajichimbie Ukerewe na Bunda,labda!Kila mtu hivi sasa kaamka usingizini anatambua umaskini wake ni wa kuletwa,siyo wa kuzaliwa nao!CCM ijiandae kupoteza majimbo mengi zaidi katika maeneo yote yenye machimbo!Katika miji mikuu yote nchini!Na katika sehemu zote zenye umaskini uliokithiri!CHADEMA NA CUF WANATAKIWA SASA WAJIPANGE VIZURI.Wasipokee viongozi wowote kutoka vyama vya kibaraka kama DP NA NCCR MAGEUZI!Chadema njooni Mwanza Mjini peupe hatuna watu hapa upuuzi mtupu!Hali kadhalika katika miji mingi mikubwa CCM haina bao tena.Ni Chui wa Karatasi kama alivyo umbuka kule Tarime!Mtu Mzima Tarime hatishiwi Nyau bwana!

    ReplyDelete
  19. Annon wa 1:33 sio kweli sie wa ughaibuni tumelala,wanaofungua matawi ya CCM huku wengi wao ni watoto wa mafisadi na walio kwenye mtandao.Ni asilimia kiduchu cha wabongo waliko ughaibuni.Wengi wetu huku tunataka CHANGE ili nasie turudi nyumbani kulijenga taifa linaloliwa na mafisadi.Watu huku tumechoka na seara za CCM.Come On Freeman,Come on Chadema we need u in this CHANGE.
    Cha chandu - UK

    ReplyDelete
  20. Pongezi nyingi kwa Wana wa Tarime. Mmeonyesha njia ya kuikomboa nchi kutoka mikononi mwa mafisadi. TANZANIA BILA CCM INAWEZEKANA. Wananchi tujiunge na kampeni hii, ndio njia pekee ya kuikomboa nchi!!

    Hongera sana Wana wa Tarime.

    ReplyDelete
  21. .....MAMBO KAMA KENYA,NIMEKUBALI! NA BADO.MAKAMBA BYE BYE1

    ReplyDelete
  22. Hongera wana Tarime. Mwana mapinduzi wa Tanzania alitokea Tarime, Nyerere. Sina wasiwasi, mabadiliko ya nchi yetu yameanza, na yameanzia Tarime. "You can fool all the people some of the time, and some of the people all the time, but you cannot fool all the people all the time" (Abraham Lincoln) Tarime people were not fooled.

    ReplyDelete
  23. Hongera wana Tarime kwa ushindi mnono. Kubwa ni kupigania haki kuinua na kupata hali nzuri za maisha. Kama ni shule kwa watoto, huduma za jamii kama afya na usafiri.
    Ili CCM iweze kushinda katika uchaguzi wowote nchini yafuatayo yanatakiwa kufanyika.
    Mafisadi wa Tanesco (Richmond)wanaosababisha gharama kubwa kwa wananchi wanatakiwa wafunguliwe mashtaka na hatimaye jela.
    Mafisadi wa EPA mashtaka na halafu jela
    Mradi wa Kiwira urudishwe kwa serekali.

    ReplyDelete
  24. Pamoja na kujibu mapigo ya helikopta CCM bado wameshindwa?

    ReplyDelete
  25. wewe wa ughaibuni no. October 13, 2008 4:46 PM, ninacotaka kusema UK mmezidi hata kama ni watoto wa wakubwa lakini kuna wengine mnaozidi kujipendekeza
    Watu wale wanaosema hajaenda shule kama Mpanda, Kigoma, Tarime ndio wenye elimu ya mageuzi. Angalia Dar hakuna mpinzani, Arusha, Mwanza, Mbeya. Sasa uelewa uko wapi jamani
    Ureeeee Wanatarime kweli mmeonyesha mkiamua mnatema mraa kweli

    ReplyDelete
  26. Na bado

    Huu ndio mwanzo tu ndio maana wanakuja kuanzisha matawi nje ya nchi kumbe wameshajua nyumbani nobody cares about them anymore.

    Tulishawashtukia siku nyingi 2010 sio mbali

    What we need --- CHANGE

    When we need ----- NOW

    TUMECHOSHWA NA MAFISADI

    ReplyDelete
  27. I am so surprised kwa wewe Michuzi kupost hii habari ya ushindi wa Chadema kwenye blog yako!!!!.. Wewe ni SUPPORTER wa MAFISADI!

    ReplyDelete
  28. CHADEMA hawajashinda kwa halali, wametuhujumu. Kwa nini walichongea kwa polisi gari letu lenye silaha za jadi ambazo tulitegemea zitusaidie zikakamatwa? Polisi vipi, kwa hili mmetugeuka?

    CCM Oyeeeee!!!!!! Hata kama tumeshindwa Tarime, kwa ujumla tunaongoza. Tujiweke sawa, tukusanye mabilioni kwa ajili ya 2010. Njia za makusanyo ziko nyingi, hata kama watu watahisi tunaongeza mikataba ya 'TICS' bandarini, poa tu!

    CHADEMA msipokuwa chonjo tutawanyang'anya Tarime 2010. Sisi tunatumia na kuwaamini WAZEE TU kwenye chama chetu!

    ReplyDelete
  29. Mwanzo mgumu wana Tarime tunawaheshimu kwa ujasiri wenu wa kukataa fulana na khanga. Pamoja na kelele za Makamba n kauli zake za ajabu eti chagueni CCM kwa sababu CCM inaserikali na itawaletea maendeleo,hakujua masikini kwamba alikua akiidhalilisha serikali za Rais Kikwete kwamba hufanya jitihada za makusudi kutopeleka huduma za maendeleo kwenye majimbo yaliyo chini ya vyama vingine vya siasa Pia pongezi kwa CUF kwa kuonesha umoja wa vyama kwa vitendo kwa kitendo chenu cha kutosimamisha mgombea wa ubunge hapo Tarime. Hongereni CHADEMA pia kwa kujitwalia kada wa CCM bwana MWITA MWIKWABE namkumbuka sana huyu jamaa toka kitambo kile cha Azania secondary(1994 hadi 2001,FORM 1 HADI SIX )

    ReplyDelete
  30. CCM NI YA KUONDOLEWA MADARAKA NA AKNA MAKAMBA WAO, WATU WANAOJIPENDA WENYEWE TU NA FAMILIA ZAO SI WATANZANI WOTE, CCM TUJIPANGE TUIPIGE CHINI HAIFA. 2010 NI KESHO TUIONDOWE JAMANII INANICHEFUA!!!!

    ReplyDelete
  31. CHADEMA hoyeeeeeeeeee, waliwabania sana hadi sehemu ya kushushia helkopta yenu, yako wapi sasa.

    JAMANI TUNASUBIRI 2010

    ReplyDelete

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...