Mdau Willy Edward (hoto) akipokea cheti cha kuhitimu mafunzo na Mh. Richard Nyaulawa mwaka 1996. kati ni Mhariri mkuu wa majira, Sammy Makilla.

Kifo cha Nyaulawa kimenigusa, alikuwa mtu 'simpo' ALIZOEA kuitwa Nyaulawa, hususan wafanyakazi wa kampuni ya Business Times Limited (BTL) niliyowahi kuitumikia nikiwa mwandishi wa habari.

Ingawa kila nafsi itaonja mauti, lakini hakika kifo hakina huruma, kimetunyang'anya Richard Said Nyaulawa aliyekuwa Mkurugenzi Mtendaji wa BTL (ambaye pia alikuwa mmiliki) na Mbunge wa Mbeya Vijijini.

Nyaulawa aliyefariki dunia alfajiri ya saa 9, Novemba 9, mwaka huu akiwa na umri wa miaka 59, alikuwa kiongozi mwadilifu aliyechapa kazi kwa ufanisi mkubwa na hakuwa mpenda makuu.
Katika makala ya buriani ya gazeti la Uhuru toleo la leo Novemva 12, 2008, mwandishi Jacqueline Liana ambaye ni Naibu Mhariri Mtendaji wa Uhuru Publications Ltd (niliwahi kufanya naye kazi gazeti la Majira) amenikumbusha (mimi Willy Edward) matukio mengi kuhusu Nyaulawa.

Amenikumbusha kwamba wakati mmoja nikiwa kazini usiku nikisanifu kurasa za gazeti, Nyaulawa alinipigia simu katika chumba cha habari na kujitambulisha, hakika nilidhani ni mwandishi mwenzangu ananitania, niligoma kuzungumza naye nikimwambia: "Mimi ni mtu mdogo sana, Nyaulawa hawezi kunipigia simu, kwanza nakata unazidi kunichelewesha."

Nyaulawa alinisisitizia kwamba ni yeye ndiye alikuwa akipiga simu kuuliza kwanini gazeti lilikuwa halijafika kiwandani wakati huo kuchapishwa? Nilishikilia msimamo wangu kwamba Nyaulawa hawezi kunipigia simu.

(Wakati huo Mhariri Mkuu Majira alikuwa ni Mobhare Matinyi ambaye sasa anaishi Marekani). Punde si punde Nyaulawa aliendesha gari lake na kufika chumba cha habari nilikokuwa, baada ya kumuona sikuwa na ujanja zaidi ya kuamini alichokuwa akikisema kwenye simu, nikampa heshima yake aliyostahili na sote tukabaki tukicheka.

Hiyo inadhihirisha jinsi gani Nyaulawa alivyokuwa 'simpo' na asiyependa makuu, lakini alikuwa kiongozi makini.

Nyaulawa alianza kunifahamu zaidi kwa karibu mwaka 1996 wakati akinikabidhi cheti cha kuhitimu mafunzo ya uandishi wa habari yaliyoandaliwa na Business Care Services (BCS), na nakumbuka mwaka huo ndio nilipewa zawadi ya mfanyakazi bora wa mwaka (wakati huo nikiandikia zaidi magazeti ya Dar Leo na Spoti Starehe) kabla ya kuhamishiwa rasmi Majira.

Vyumba vya habari vya magazeti ya BTL wakati huo vilisheheni waandishi mahiri wakiwamo aliyekuwa Mhariri Mtendaji, Sammy Makilla, Theophil Makunga, Joseph Kulangwa (sasa Mhariri Mkuu Majira), Faustine Rwambali, Jacqueline Liana, Masoud Sanani, Mobhare Matinyi, Irene Bwire (sasa mwandishi wa Waziri Mkuu), Juma Pinto (yupo Uingereza), Jesse Kwayu, Danny Mwakiteleko, Rachel Lugoe, Sopa Castico, Fatma Mwassa (msaidizi wa Mama Kikwete), Nyaronyo Kicheere, Ponsian Rwechungura, Lilian Kalaghe, Jabir Idrissa, Boniface Wambura, Samson Mbega, marehemu Nicky Maira, marehemu Conrad Danstan (kiona mbali) na wengine wengi.

Hakika marehemu Nyaulawa alikuwa mtu mtaratibu, lakini makini na muungwana na alikuwa kipenzi cha wengi.

Kwa heri Richard Nyaulawa!
Willy Edward
Senior PR Executive (Zain)
ZK Advertising.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

Kuna Maoni 6 mpaka sasa

  1. DUUH, NAONA KA WORD PROCESSOR KWA MBAALI KAMETULIA....KWELI TUMETOKA MBALI

    ReplyDelete
  2. Rip Nyaulawa nimeshituka kumbe na Conrad Dunstan alifariki lini jamani? Mungu aweke roho za marehemu wote wapumzike kwa amani.Sopa kastiko na Jane MIHANJI WAKO WAPI SASA? Mwana majira wa kale aliye Ukerewe kwa sasa.

    ReplyDelete
  3. Kwa kweli Willy Edward umenigusa sana kwa kumbukumbu hiyo ya Nyaulawa. Alitufundisha mengi sana kazini; uwajibikaji, kujituma, kuheshimu utu wa mtu bila kujali nafasi ya mtu na pia kujiweka kwenye nafasi ya kuaminiwa na wenzio. Hakika Nyaulawa hakuwa mtu wa makuu. Nakumbukuka 1995, J mosi moja nikiwa mhariri wa zamu alizuiwa kuingia newsroom na mlinzi ambaye alikuwa mgeni akitimiza kazi yake. Hakujua Nyaulawa ni nani hivyo akamwambia asubiri aitiwe mhariri pale kwenye gate. Niliitwa kwamba kuna mgeni anang'ang'ania kuingia newsroom hivyo nikamsikilize. Kufika getini ni Nyaulawa!!!!Aliishia kucheka na kumsifu mlinzi kwa kazi nzuri! Huyo ndiye Nyaulawa... so down to earth!

    Mdau Lily

    ReplyDelete
  4. Kiukweli sikujua kama Nyaulawa amefariki, Binafsi nakumbuka Boss wangu wa zamani wa Idara ya Matangazo Mr Rutha aliponichukua na kunipeleka kwa Nyaulawa ili kujadili ajira yangu kama msanifu wa idara ya Matangazo.
    Nilikutana na Nyaulawa kwa mara kwanza akiwa amekaa juu ya meza na ufupi alikuwa nao na kavaa shati lake na suaruali casual sikutegemea kama huyu ndiye Boss na mmiliki wa Kampuni ambaye Boss Rutha alimuongelea barabara nzima toka ofisi yetu Bibi Titi Road hadi Majani ya Chai ziliko ofisi zake, Alikuwa amekaa juu ya meza na kuniuliza nataka mshahara wa Sh, ngapi? kwa vile nilikuwa nimetoka shule tuu nikataka kusema laki unusu, akanilazimisha niseme mimi nikasema si chini ya laki moja. hiyo ilikuwa mwaka 2000 akaniuliza laki moja???? unauhakika unaweza kuishi kwa laki moja? nikakaa kimya akaniambia tutakupa laki tatu pamoja na Over time mengine inategemeana na utendaji wako.... haya aanze kazi sikuamini... barua zilifuata baadaye nikaanza kazi sikuhiyo.
    Sikulitumikia sana gazeti huili kwani nilihama mwaka 2004 lakini kwa muda wangu pale siku wahi kufarakana na Boss mmiliki huyu isipokuwa kama gazeti litachelewa kama Willy alivyosema kwani alikuwa akisanifu upande wa Editorial na mimi upande wa matangazo ambapo tulikuwa tukitegemeana sana.
    Buriani Nyaulawa!!

    ReplyDelete
  5. Hakika mdau Willy Edward umenikumbusha mbali sana kuhusu kifo cha Nyaulawa. Mungu ailaze mahali pema peponi roho ya marehemu. Sopa Castiko nasikia yuko Australia na Jane Mihanji yupo Dar es Salaam, ni mwandishi wa Uhuru na Mzalendo.

    ReplyDelete
  6. Aaa jamani kifo cha Mheshimiwa Nyaula kimenigusa sana nasikitika kuchelewa kupost na mimi view zangu lakini kama wadau wengi walivyosema alikuwa ni mtu wa watu na ni mtu aliyependa uchapa kazi, alikuwa ni mtu anayependa juhudi binafsi. Naam kikubwa ninachomkumbuka ni vile alivyopenda watu wake wawe na upeo wa hali ya juu na kufanya kampuni yake kuitwa chuo cha mafunzo.

    Alihakikisha kampuni yake inakuwa ya kwanza katika teknolojia kwa kuintroduce utaalam wa kompyuta badala ya mashine za kuandikia typewriters jambo ambalo lilileta ufanisi kumbwa sana katika masuala ya magazeti na hakuwa mchoyo teknolojia hii ilisaidia hata magazeti ya nje mbali na yale yake kuchapwa katika kiwanda chake cha Business Printers.

    Alikuwa mcheshi sana na mwenye shukrani hasa pale uzalishaji unapokuwa mzuri alikuwa ana uwezo wa kuja newsroom na kuwapa wafanyakazi wake bahasha zenye fedha ikiwa ni kama bonus. Aliwapa watu changamoto na moyo wa kufanya kazi zaidi na zaidi kwa mbinu hizi.

    Alitutia moyo sana kiasi kwamba mwenzetu mmoja aliwahi kuvuliwa viatu njiani maeneo ya gerezani muda wa alfajiri kwani vijana wengi waliokuwa wakifanya kazi walijua mtu anavyojituma ndivyo stori zinavyotoka gazetini, mimi binafsi nilikuwa mingoni mwao kwani mbali na kazi yangu ya usanifu niliweza kwenda mitaani kuandika habari kutokana na fursa aliyokuwa ameitoa kwa wafanyakazi kuwa ukiweza kufanya kazi ya ziada mtu ulikuwa unalipwa. Namshukuru kwani aliniwezesha kufanya mambo mengi kwa kile kiasi cha ziada na nikawa siutumii mshahara wangu.

    Alitumia fedha zake nyingi kutuletea in house training ili kuwa na wafanyakazi bora na pia kuwa na gazeti bora jambo ambalo alifanikiwa kwa kiasi kikubwa sana. Na mfano mzuri ni hiyo picha ya ndugu yangu damu anayopokea cheti nami pia nilikuwa nyuma ya Willy nikisubiri kupokea cheti changu kwani tuliweza kufundishwa mambo mengi kuhusu uandishi wa habari na masuala yote ya upigaji picha katika hiyo kozi willy anayopokea cheti ikiwa ni pamoja na masuala ya kompyuta.

    Mdau Denis Maringo ambaye yuko Marekani kwa sasa hataweza kumsahau kwani kuna wakati alikuwa akilala ofisini kwa ajili ya kufanya kazi zake na ndiye aliyevuliwa viatu akiwahi ofisini.

    Kwa mengi ambayo nilijifunza katika kampuni yake siwezi kuyataja na kuyamaliza leo .

    Mungu ailaze roho yake mahali pema peponi

    wadau tukumbukane:aliaminadams@yahoo.com

    AMINA

    ReplyDelete

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...