KAMPUNI ya simu za mkononi ya Zain Tanzania imekipatia kikundi cha burudani cha Tanzania House of Talent (THT) pesa kwa ajili ya kutoa elimu kupitia sanaa na maigizo katika programu maalum ya elimu ikiwa ni kampeni ya mapambano dhidi ya maradhi ya UKIMWI katika shule za msingi na sekondari nchini, na kupanua wigo wa maarifa ya maradhi hayo kwa wanafunzi.
Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam, Meneja wa Huduma za Jamii wa Zain Tanzania, Tunu Kavishe alisema Zain imetoa sh. milioni 35 katika mradi huo wa THT ili kusaidia kuelimisha wanafunzi na kizazi kipya kwa ujumla katika nyanja mbalimbali ikiwa ni pamoja na kujikinga na maambukizo ya maradhi ya UKIMWI.
"Zain inafurahia kufanya kazi na THT kwa lengo la kuwalinda vijana wa Tanzania. Vijana ndio taifa la kesho, na tunaamini mchango wetu kwa THT katika programu hii ya elimu itakayotumia sanaa kuelimisha wanafunzi katika shule za msingi na sekondari kuhusu kujikinga na maambukizi ya UKIMWI, utasaidia kizazi kipya kujikinga na maradhi hayo," alisema Tunu.
Rebecca Young, Meneja wa THT alisema: "Tunaona fahari kwa Zain kujikita kusaidia programu yetu na kutupatia pesa za kuendeleza programu yetu. Sanaa imedhihirisha ni njia bora ya kufikisha ujumbe kwa jamii, na THT ina uwezo wa kutumia njia hiyo kufikisha ujumbe kuhusu mada mbalimbali kwa njia ya sanaa jukwaani," alisema.
Pesa hizo zitaisaidia THT kupata mwamko wa kutoa elimu kuhusu maambukizi ya maradhi ya UKIMWI na mengine kwa ujumla. THT pia itaandaa semina zitakazoelimisha kuhusu mambo mbalimbali ya msingi kwa jamii ikilenga hasa kupambana na maradhi ya UKIMWI.
Vijana wa THT watatoa elimu hiyo kwa njia ya sanaa ikiwa ni pamoja na ujumbe kupitia muziki, dansi na ngoma. Vijana hao watafanya maonyesho katika shule 20 za Dar es Salaam, kwa lengo la kuwaelimisha wanafunzi hao.
Mbali na pesa hizo, Zain pia imetoa mchango wa basi kwa THT litakalowezesha vijana wanaounda kundi la THT kutumia kusafiri katika shule 20 za Dar es Salaam kwa lengo la kutoa elimu kupitia sanaa.
Kikundi cha THT kilianzishwa mwaka 2005 na kinaundwa na vijana wapatao 45 wenye umri kati ya miaka 14 na 24. Kundi hilo la vijana limekuwa likitoa burudani maridhawa katika matukio mbalimbali nchini.
"THT inaamini kwamba vijana wana jukumu la kutoa elimu kwa vijana wenzao na jamii kwa ujumla. Zain inawapa vijana wa THT nafasi ya kutoa elimu kwa jamii kwa njia ya muziki, dansi na ngoma," alisema Rebecca. THT inaamini itafikisha ujumbe kwa haraka zaidi kwenye jamii kupitia burudani katika karne hii ya 21.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

Kuna Maoni 2 mpaka sasa

  1. Michuzi nawewe, Miwaya ni nini?
    (Andika kiswahili fasaha)

    ReplyDelete
  2. sasa kumpa mwezie mkono uyu kitimoto asubiri nini??nyang'au kbs

    ReplyDelete

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...