

SHUJAA ALIYEPANDISHA MWENGE KWENYE KILELE CHA MLIMA KILIMANJARO SIKU YA MKESHA WA UHURU WA TANGANYIKA DESEMBA 9, 1961, MAREHEMU ALEX GWEBE NYIRENDA, AMBAYE ALIFARIKI DUNIA JUZI,ANATARAJIWA KUZIKWA KESHO MCHANA KWENYE MAKABURI YA KINONDONI, DAR.
KWA MUJIBU WA TAARIFA KUTOKA FAMILIA YA MAREHEMU, MIPANGO YA MAZISHI NI KAMA IFUATAVYO:
KUANZIA SAA SITA MCHANA (12:NOON) : HESHIMA ZA MWISHO KUTOLEWA NYUMBANI KWA MAREHEMU MBEZI BEACH FLETI ZA NATIONAL MILLING CORPORATION, KUCHEPUKA TOKA NJIA YA KWENDA AFRICANA.
MISA: ITAFANYIKA KANISA LA ST. COLUMBUS, UPANGA, USONI MWA PALM BEACH HOTEL MAENEO YA DARAJA LA SALENDER KUANZIA SAA SABA MCHANA (1.00PM) .
MAZISHI: MAKABURI YA KINONDONI SAA NANE NA NUSU (2.30PM) MCHANA.
MOLA AIWEKE PEPONI ROHO YA SHUJAA WETU HUYU
-AMINA
ina maana huyu shujaa wetu alikuwa bado akiishi kwenye nyumba za msajili wa majumba NHC ???kweli zama za nyerere hazikuwa zama za mafisadi leo hii tuna mabilionea zama hizi za mafisadi
ReplyDeletePOLENI SANA familia ya Meja Nyirenda! Poleni sana wanajeshi waliokuwa naye! Poleni sana wa-Tanzania wote, kwa ujumla!
ReplyDeleteMajor Alex Nyirenda alikuwa “nyota”…lakini iliyoanguka baadaye! Na sasa ametuacha!
Michuzi, umeandika, "Major Alex Nyirenda akiuweka Mwenge wa Uhuru kilelleni Kilimanjaro kwenye mkesha wa siku ya Uhuru wa Tanganyika Desemba 9, 1961."
Ingawa ni kitendo cha ushujaa mkubwa na uliyoandika ni ya kweli ki-picha kwamba yalitendeka lakini sio sahihi hata kidogo!
Hali ya hewa ya mchna na usiku huo huko mlimani, mwezi huo wa mwaka huo, ilikuwa ni mbaya sana: pepo kali, baridi na tufani la theluji!
Kutokana na hali ya hewa mbaya, Meja Nyirenda hakufaulu kufikia kileleni ilipofika saa iliyopangwa (sita usiku wa manane) wakati bendera ya m-Uingereza ilipoteremshwa na bendera ya wananchi wa Tanganyika huru kupandishwa!
Ukweli ni kwamba huo mwenge haukuwekwa hapo kileleni usiku huo. Baadaye, mwenge huo ulihamishwa na kuwekwa hasa kileleni!
Tusiwe kila mara tunayachukulia matukio "for granted!" Tuwe watundu wa kuchunguza na kuuliza maswali ("inquiring minds"), hasa hayo ya historia!
Vijana, mna bahati kuwa bado wapo wazee walioshiriki katika mengi ya historia yetu. Palipo na kutoelewa kwa nini, hamna budi kutumia "inquiring minds" senu kutoa giza lililopo.
Sio lazima yawe yale tuliyokuwa tunayajua, “according to TANU/CCM’s point of view”! Mengine yamepotoshwa potoshwa kwa kujenga hisia hiyo!
Kwa kweli hii pocha ya pili na maelezo yake imenisikitisha sana. Ina maana serikali ilimwacha kiasi mpaka mkewe akawa ndiyo anamshughulikia? Yaani baadaye ilishtuka?
ReplyDeleteNaamini kuwa ndiyo maana jamaa wakiwa madarakani wanajitahidi kwa kadri wawezavyo kufanya UFISADI ili mambo kama haya yasiwakute!
Wewe Anon wa pili, kama uliyoandika ni kweli, basi ungetoa jina lako. As far as facts are concerned, Alex Gwebe Nyirenda ni shujaa aliyepandisha Mwenge kileleni usiku ule wa mkesha wa Uhuru! R.I.P. Uncle Alex, umetuachia ukiwa, Mapenzi ya Mola wetu yametimizwa. Amen
ReplyDeleteYour Niece Mel
cha msingi ni kwamba huyu baba alikuwa mkakamavu na shupavu aliyeshiriki kikamilifu katika harakati za kupatikana kwa uhuru siku ile na picha inajieleza, kuwakumbuka na kuwaenzi watu walioshiriki katika kufanikisha mambo na matukio mbalimbali nchini kwetu ni jambo la muhimu na busara kwa kizazi kilichopo na kijacho.
ReplyDeleteMichuzi tunaomba pia picha za mashujaa waliopigana vita ya kwanza na ya piliya dunia wakitanzania kama bado wanaishi.
Anon. wa pili ulikuwa wapi kutoa huu upinzani huu wakati ule michuzi alipotuletea mahojiano aliyohojiwa na waandishi? Pale ndo palikuwa muafaka sio hapa msibani, au kuona huyu baba ameshafumba mdomo wake ndo ukaona useme? Hata kama hakuweka katikati hiyo bendera, hatujali masafa au kina cha urefu,Hicho kitendo cha kuweka kwenye mlima mrefu kuliko yote nchini mwetu , ni tendo lenye maana kubwa ukilitafakari kwa undani, tunachojua alipanda mlimani akaweka bendera ni huyu mzee na wapambe wake kama kumi chambile cha mwenyewe/alichosema mwenyewe,
ReplyDeleteHii picha ya kupandisha bendera ina historia nzuri sana.
Poleni wafiwa, Mungu amrehemu mzee wetu mwana mapinduzi, mpiganaji, shujaa.
HE WAS AN ICON THAT THE LATTER GENERATIONS OF ARMY CADRES WILL HAVE A HARD TIME TO EMULATE
ReplyDeleteAnonymous wa December 24, 2008 9:26 AM, sitembelei hapa kila siku. Ndio maana sikutoa maoni hayo. Sawa?
ReplyDeletemahojiano aliyafanya yaliniacha na maswali mengi sana. wasifu wake pia hauelezi Brig.Gen.Alexander Nyirenda alikuwa wapi tangu aondoke Jeshini Agosti 1964.
ReplyDeleteAmiri Jeshi Mkuu Mstaafu Ali Mwinyi alimpandisha cheo toka Luteni Kanali mpaka Brigedia. naamini hilo lilifanyika ili kuliwezesha Jeshi kumtunza Brig Nyirenda kama afisa mstaafu.
NI NINI KILIMUONDOA JESHINI BRIG.NYIRENDA? KATI YA 1964 na 2008 BRIG.NYIRENDA ALIKUWA AKIJISHUGHULISHA NA NINI? JE, ALIZIKWA KWA HESHIMA ZA KIJESHI?
December 23, 2008 10:27 kasema maneno ya ukweli. Ingawa walijaribu kuuwasha mwenge huo, ilikuwa ni vigumu sana kuweza kuendelea kuwaka shauri ya hali mbaya ya hewa na upepo!
ReplyDeleteManeno hayo ya Nyerere: "We, Tanganyikans, will light a candle ...." hayakulenga Watanganyika!
Nyerere alisema hivyo kwenye mahojiano yake na gazeti la Drum la huko kwa Makaburu kulikokuwa na ubaguzi wa rangi na kunyanyaswa kwa ndugu zetu, ikiwa ni pamoja na ujumbe huo kuifikia nchi ya Amerika yenye kubagua Weusi!
Nyerere kayasema kwa Kiingereza. Lakini hapo baadaye yalitafsiriwa kwa Kiswahili.
Kumbukumbu rasmi iliyoko ya maneno hayo ni ukanda ulionasiwa hapo redio yetu na kusomwa na mtangazaji mmoja, Bwana S.S. Mkamba!
Mh.Balozi
ReplyDeleteHistoria kamilifu ya Marehemu Brig Nyirenda toka gazeti RAIAMWEMA
Mwalimu Julius Nyerere alisema, Meja Alex Nyirenda akatenda. Mpira ukarudi tena kwa Nyerere ambaye safari hii alifanya kweli kuhakikisha kwamba Afrika nzima inakuwa huru kabla ya kufariki kwake Oktoba 14, 1999.
Lakini Mwalimu alisema nini? Alisema: “Sisi tunataka kuwasha Mwenge, na kuuweka juu ya Mlima Kilimanjaro, umulike hata nje ya mipaka yetu, ulete tumaini pale ambapo hakuna matumaini, upendo mahali palipo na chuki na heshima palipojaa dharau.”
Desemba 9, 1961 wakati bendera ya kikoloni ya Mwingereza inateremshwa kwenye Uwanja wa zamani wa Taifa mjini Dar es Salaam, Alex Gwebe Nyirenda, mwanajeshi Mtanganyika alifanya kile Nyerere alichosema.
Lakini, si tu aliwasha mwenge kwenye kilele cha Mlima Kilimanjaro, bali alisimamisha pia bendera ya Tanganyika huru ipepee kwenye kilele hicho kirefu zaidi barani Afrika.
Katika miaka iliyofuata, Mwalimu Nyerere aliongoza mapambano kwa kuwa mwenyekiti wa nchi zilizo msitari wa mbele kusaidiana na wapigania uhuru kukomboa nchi ambazo bado zilikuwa zinatawaliwa kimabavu.
Hivyo hadi anafariki Oktoba 14, 1999, hakuna nchi ya Afrika iliyokuwa inateseka kutokana na ukoloni wa aina yoyote.
Kutokana na tukio hilo la kupandisha bendera na mwenge kwenye kilele cha Mlima Kilimanjaro, Alex Nyirenda amekuwa alama muhimu ya taifa katika kutimiza azma ya Mwalimu ya kuona Afrika nzima iko huru.
Lakini Jumapili iliyopita ya Desemba 21, 2008 shujaa huyo wa mwenge alifariki dunia katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili, Dar es Salaam baada ya kusumbuliwa na kansa ya koo.
Alilazwa kwanza katika Taasisi ya Magonjwa ya Moyo Kinondoni (THI), Dar es Salaam na baadaye Muhimbili kabla ya kupelekwa India kwa matibabu zaidi Februari mwaka huu.
Baada ya kupata nafuu huko India, alirudi nyumbani Mei mwaka huu na kwenda tena India kwa vipindi viwili vya uchunguzi wa afya yake ilivyokuwa ikiendelea. Mara ya mwisho alitoka huko Septemba mwaka huu.
Alex Gwebe Nyirenda alikuwa ni mmoja wa maofisa wachache Watanganyika katika jeshi lililoachwa na wakoloni la Tanganyika Rifles.
Katika mahojiano ambayo nilipata kufanya naye Machi mwaka 2001 mjini Dar es Salaam, Nyirenda alisema hata uteuzi wake wa kwenda kupandisha bendera na mwenge kwenye Mlima wa Kilimanjaro ulitokana pia na cheo alichokuwa nacho.
Lakini aliingiaje jeshini? Kwa mujibu wa maelezo yake, ukakamavu wake na kipaji cha uongozi alichokuwa nacho ni vitu vilivyomfanya mmoja wa walimu wake, aliyemtaja kwa jina la Grabbe kumwambia kwamba kazi itakayomfaa baada ya kumaliza masomo itakuwa jeshini.
“Mimi nilikuwa kiranja wa shule tangu shule za msingi. Popote niliposoma nilichaguliwa kuwa kiongozi. Kwenye shule ya Sekondari ya Malangali nilikuwa mkuu wa bweni na baadaye kiranja mkuu wa shule,” alisema.
Alipokuwa Tabora School alikuwa kiranja mkuu msaidizi. Kiranja mkuu alikuwa Wilbroad Ntuyabaliwe ambaye ni mzazi wa Miss Tanzania wa mwaka 2000, Jacqueline.
Akiwa anafuata maneno aliyoambiwa na mwalimu wake, Nyirenda aliomba kuingia jeshini baada ya kumaliza masomo. Alipata majibu kwamba anatakiwa kufanyiwa usaili mjini Dar es Salaam.
Miongoni mwa aliokutana nao katika usaili huo alikuwa Mirisho Sarakikya ambaye baadaye alikuja kuwa mkuu wa kwanza wa Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ).
Nyirenda alisema kwamba Sarakikya wakati huo alikuwa akijulikana zaidi kwa majina ya Sam Hagai Sarakikya. Katika usaili huo kulikuwa pia na mwingine aliyekuwa na asili ya kiasia, S. M. A. Kashmir.
Kwa mujibu wa Nyirenda usaili ulikwenda vizuri na wote walikubaliwa kuingia katika jeshi ambalo lilikuwa wakati huo likiongozwa na maofisa Waingereza.
Nyirenda, Sarakikya na Kashmir walikuwa Watanganyika wa kwanza kuandaliwa kupelekwa Uingereza kwa masomo ya juu ya kijeshi yaliyokuwa yakitolewa katika chuo cha kijeshi cha Sandhurst.
Walipofika Nairobi kwa ndege wakiwa njiani kwenda Uingereza walipata taarifa iliyowasikitisha. Kulikuwa kumeletwa simu ya maandishi ikimtaka mmoja wao, Sarakikya arudi nyumbani kwa madai kwamba alifeli mtihani wa Kiingereza hivyo hakuwa na sifa ya kuchukua masomo wanayoendea.
Nyirenda alisema kwamba ilikuwa ni jambo la kushangaza kwa sababu Sarakikya alikuwa amefaulu vizuri masomo yote 12 ambayo yalikuwa kwa lugha ya Kiingereza hivyo alijiuliza ilikuwaje ashindwe somo la Kiingereza?
Sarakikya ilibidi azuiwe Nairobi arudi nyumbani kufanya safari hiyo ya Sandhurst sasa iwe na Watanganyika wawili tu, Nyirenda na Kashmir.
Nyirenda alisema katika mahojiano nami kwamba anaamini kuwa kitendo cha kumzuia kwenda Uingereza kilimpa nguvu Sarakikya kupambana vizuri na vizuizi vya maisha.
Alisema Sarakikya alijibidisha kwa mambo mengi ikiwa ni pamoja na kurudia mtihani wa Kiingereza waliokuwa wanadai ameshindwa. Alifaulu vizuri na hatimaye nay eye kwenda Sandhurst katika msafara mwingine wa Watanganyika wa kwenda huko.
Akizungumzia masomo ya Sandhurst, Nyirenda alisema walipokuwa huko, kwa muda mfupi waliokuwa pamoja, yeye, Kashmir na Sarakikya walikuwa na mshikamano mkubwa na ulikuwa ni mshikamano wa aina yake ulioambatana na nidhamu ya hali ya juu ya kijeshi.
Nyirenda alisema ni mshikamano kama huo na nidhamu ya hali ya juu ya kijeshi ambavyo vilimsaidia sana maishani kiasi na kufanya ailee vyema familia yake.
Nyirenda alisema kuwa ubaguzi wa rangi wakati huo ulikuwa wa waziwazi. Ingawa yeye na Kashmir walikwenda Sandhurst wakiwa na sifa zinazolingana, walipofika huko Kashmir kwa vile alikuwa na asili ya Kiasia alionekana bora zaidi yake.
Wakati mwenzake alianza mara moja kozi iliyowapeleka huko, yeye alitakiwa kwanza afanye mafunzo ya maandalizi ya miezi sita kabla ya kuanza kozi iliyowapeleka huko.
Katika hali hiyo, Kashmir alimaliza mafunzo miezi sita kabla yake na kwa heshima ya jeshi, muda huo ulitosha kumfanya awe mkubwa zaidi yake. Kwa maneno mengine kuwa afande wake.
Uasi wa jeshi uliofanyika Januari 1964 ndiyo uliomtoa Nyirenda jeshini. Alisema hakuhusika kwa namna yoyote na uasi huo, lakini matukio yaliyofuata baada ya uasi huo hayakumpendeza na aliona njia pekee ya kufanya ni kuliacha jeshi.
Nyirenda alikuwa ni miongoni mwa maofisa wachache wa Kiafrika waliokuwa kwenye Tanganyika Rifles (jeshi aliloacha mkoloni). Kwa cheo chake alikuwa amepewa nyumba nzuri katika kambi ya Calito (sasa Lugalo). Pia kutokana na cheo chake alikuwa bega kwa bega na maofisa wenzake wakiwamo Waingereza.
Alisema katika mahojiano nami kwamba ingawa askari wa chini walikuwa wanaujua ukweli huo, walikuwa hawataki kuukubali hivyo kumwona kama mtu anayejidai na anayejifananisha na Wazungu.
Hata kitabu ha ‘Tanganyika Rifles Mutiny’ January 1964’ kilichochapishwa baada ya kuidhinishwa na JWTZ mwaka 1993, kinathibitisha mtazamo huo hasi dhidi ya Nyirenda.
Pamoja na mambo mengine, kitabu hicho kinasema kwamba uwezo mkubwa wa Nyirenda wa kuzungumza kwa ufasaha lugha ya Kiingereza ulimfanya awe karibu zaidi na maofisa Waingereza waliokuwa jeshini.
Kitabu hicho kinasema kwamba katika uasi huo, wanajeshi walioshiriki walikuwa wakibishana ni nani anayefaa kuwa kiongozi watakayempandisha cheo kuwa Brigedia kati ya Luteni William Chacha na Kapteni Nyirenda.
Nyirenda aliyekuwa amesoma katika Shule za Sekondari za Malangali na Tabora Schoool na baadaye kupata mafunzo ya juu Sandhurst, Uingereza ndiye aliyeonekana kuwa na sifa kubwa zaidi. Lakini wengi walimkataa kwa vile walikuwa wanamwona kama Mzungu aliyekuwa amejivika ngozi nyeusi.
Aidha, tabia yake ya kucheza ‘michezo ya Kizungu’ kama skwashi na tenisi ilikuwa inawakera baadhi ya watu kwa kumwona kuwa anajidai.
Kitabu hicho kilichoidhinishwa na JWTZ mwaka 1993 kimedai kwamba wakati wote wa uasi Nyirenda alichukua jukumu la kuhakikisha kwamba wake wa maofisa wa Kizungu pamoja na mbwa na paka wao wanakuwa salama.
Baada ya kubishana sana kuhusu nani wamfanye mkuu wao wa jeshi, wakaamua kumfanya kuwa Brigedia, ofisa mdogo katika jeshi, Luteni Usu Elisha Kavana.
Hata Kavana mwenyewe alishitushwa mno na uteuzi huo na kupanda huko kwa cheo kusikokuwa kwa kawaida na kufanywa mkuu wa jeshi.
Kavana alikuwa miongoni mwa maofisa waliokamatwa na alipoambiwa kwamba amefanywa kuwa Brigedia hakuamini masikio yake. Kitabu hicho kinasema alipoonyesha wasiwasi alitishwa kwamba asipokubali atauawa hivyo hakuwa na la kufanya ila kukubali tu.
Kavana ananukuliwa na kitabu hicho akisema: “Mmoja wa askari aliingia katika chumba ambacho tulikuwa tumefungiwa na kutaja jina langu. Luteni Marwa akaniombea heri na kusema ananisikitikia.”
Aliendelea kusema: “Nilikuwa siwezi kuliongoza jeshi lakini nilikuwa na jukumu la kuhakikisha kuwa familia za maofisa zinaendelea kuwa salama.
“Ningewezaje kuliongoza jeshi. Ilikuwa ni ndoto. Ninaamisha kuwa suala zima lilikuwa halileti maana. Nilikuwa naachiwa kutoka kuzuizini na kufanywa Brigedia! Lilikuwa ni jambo lisilokuwa la kawaida kabisa.”
Kavana ameelezwa katika kitabu hicho kwamba alikuwa anashangaa ni kwa vipi askari wa kawaida wakawa na uwezo wa kumfanya kuwa Brigedia . “Hivyo niliposita kupokea kofia nyekundu (ya ubrigedia) askari wakatishia kunipiga risasi papo hapo.”
Je, ni kweli kwamba wakati maofisa walipokuwa wakikamatwa, Nyirenda alikuwa katika harakati za kulinda wake, mbwa na paka wa Wazungu?
Katika mahojiano hayo Nyirenda alikataa kata kata kwamba alifanya jambo hilo. “Ningefanya vipi hivyo wakati na mimi nilikuwa nimekamatwa?” aliuliza.
Alsiema kuwa yeye, kama walivyokuwa maofisa wote katika kambi ya Calito, alikamatwa hivyo alikuwa hajui ni kitu gani kinachoendelea.
Alikiri kuwa ni kweli alikuwa na uhusiano mzuri na maofisa wa Kizungu jeshini lakini uhusiano huo ulikuwa wa kikazi kulingana na vyeo vyao na si zaidi ya hapo.
Lakini alisema ya kuwa pamoja na kuelewana mno na maofisa wa Kizungu, na yeye alikuwa anapata shida kama ‘weusi’ wenzake kutokana na rangi yake.
Alisema kuwa mara kadhaa alijikuta anazuiwa kuingia katika sehemu wanazoingia Wazungu tu na hiyo wakati mwingine ilikuwa inawakera hata maofisa wenzake wa Kizungu aliokuwa akiambatana nao na kumpigania aruhusiwe kuingia.
Anaitaja Dar es Salaam Club ambayo baadaye ikafanywa kuwa Hoteli ya Forodhani (sasa Mahakama ya Rufaa) kuwa ni sehemu mojawapo aliyokuwa akiingia kwa shida kutokana na rangi yake.
Sehemu nyingine ambayo alisema anaikumbuka kuwa alinyanyasika kwa sababu ya rangi yake ni Itigi ambako walikuwa ziarani na maofisa wenzake wa Kizungu kuwashawishi vijana wa Tanganyika kujiunga na jeshi.
Je, nini ulikuwa mtazamo wake juu ya uasi uliofanyika jeshini ambao ulitikisa taifa na kumfanya Mwalimu na msaidizi wake wa karibu, Rashidi Mfaume Kawawa waikimbie Ikulu?
Nyirenda alisema kuwa askari wa chini waliokuwa na madai lukuki kwa serikali walikuwa na haraka mno. Mambo waliyokuwa wakiyataka si ya kufanywa kienyeji kama walivyokuwa wanafikiria.
Alisema ya kuwa serikali ilikwisha kutoa ahadi kuwa suala la ‘africanization’ (kutoa vyeo kwa Watanganyika) litafanyika lakini wao hawakutaka kuwa na subira.
Alisema ya kuwa wao kwa kuwa Waafrika walitaka kupewa upendeleo usiokuwa wa kawaida jambo ambalo lilikuwa haliwezekani kwani walikuwa katika chombo nyeti cha taifa.
Nyirenda alisema kuwa vyeo vya jeshi ni nyeti kama madaraja ya madaktari hospitalini. Alisema ya kuwa watu wanapanda kwa hatua kulingana na sifa wanazokuwa nazo na si hivi hivi.
“Ni kama hospitalini, mfunga vidonda hata kama ni mchapakazi namna gani, hawezi, akapanda ghafla bali kwa mlolongo wa kazi yake. Hawezi ghafla akapanda kuwa daktari,” alisema.
Alisema kuwa askari wa chini wakati huo walitaka kuvunja mwiko huo kwa kutaka vyeo vitolewe kama pipi.
Nyirenda aliamua kutoka jeshini kufanya shughuli nyingine za kuendeshea maisha yake miezi michache baada ya uasi huo kuzimwa na majeshi ya Uingereza na Tanganyika Rifles kuundwa upya kuzaliwa kwa JWTZ.
Ni kwa nini Nyirenda aliamua kufanya hivyo wakati alikuwa katika nafasi nzuri ya kuwa mmoja wa viongozi wa juu wa jeshi hilo?
Katika mahojiano hayo, Nyirenda alisema alifanya uamuzi wa kuachana na jeshi baada ya kufadhaishwa na kebehi za mara kwa mara alizokuwa akizisikia kuwa si Mtanganyika halisi.
Alisema ya kuwa kebehi hizo zilianza kuota mbawa wakati wa uasi wa jeshi. Baada ya maofisa wote kukamatwa akiwamo yeye, kukawa na mjadala wawafanye nini baada ya kuwakamata.
Alisema walifikia uamuzi wa kuwarudisha Uingereza maofisa wote Waingereza. Walipofika kwa Kashmir kwa kuwa yeye alikuwa na asili ya kiasia wakasema anarudishwa kwao Bombay.
Walipofika kwake Nyirenda wakasema watamwingiza katika kundi la Waingereza kumrudisha Uingereza kwa kuwa ati na yeye ni Mzungu.
Wakaleta lori maalum ambalo waliwapakia maofisa wote wa Kizungu pamoja na yeye kwa safari ya kwenda Uwanja wa Ndege ili warudishwe Uingereza.
Lakini haikuwa hivyo, kwani lori hilo lilikwenda kuwabwaga sehemu nyingine na siyo Uwanja wa Ndege kama ilivyokuwa imetangazwa na hao askari wa kawaida kwenye kambi ya Calito.
Nyirenda alisema kwamba hata baada ya uasi kuzimwa, kebehi za hapa na pale ziliendelea kusikika dhidi yake.
“Safari hii walikuwa hawasemi tena kwamba mimi ni Mzungu, bali walikuwa wanasema kwamba ni Mnyasa,” alisema.
Nyirenda alisema kuwa madai hayo yalimshangaza kweli kwa sababu Nyasaland, nchi ambayo sasa inaitwa Malawi hakuwa anaikubali kuwa ni nchi yake.
Hata hivyo, alikiri kwamba ni kweli kwamba wazazi wake wana mizizi ya huko, lakini maisha yao yote yalikuwa Tanganyika.
Alisema kuwa yeye alizaliwa Karonga, Nyasaland Februari 2, 1936 kwa bahati mbaya tu kwani wazazi wake walikwenda huko kwa likizo kutembelea ndugu mama yake akiwa na mimba yake.
“Mimi leo (mwaka 2003) ukinipeleka Malawi ni kama unanionea. Inawezekana kweli nina ndugu ambao wanatoka katika koo za wazazi wangu lakini mimi mwenyewe sijawahi kuishi huko na sikujui,” alisema.
Alex Gwebe Nyirenda alipata elimu yake ya msingi katika shule za Mchikichini mjini Dar es Salaam na Mlandege, Iringa kabla ya kwenda Shule ya Sekondari ya Malangali, Iringa na baadaye Tabora School.
Alikuwa akiwakumbuka wengi aliosoma nao. Miongoni mwao ni Brigedia mstaafu Hashim Mbita aliyekuwa naye darasa moja na Bakari Mwapachu aliyekuwa nyuma yake.
Mwingine ni aliyekuwa jaji Mkuu, Francis Nyalali ambaye alikuwa mbele yake katika Shule ya Sekondari ya Malangali. Pia mwanasheria Peter Bakilana aliyekuwa naye darasa moja Tabora School.
Wengine ni Hatibu Lweno aliyekuwa mbele yake na Jaji Lameck Mfalila aliyekuwa nyuma yake. Pia alisoma na Godwin Kaduma katika Shule ya Malangali.
Kiongozi wa siku nyingi wa mpira wa miguu nchini ambaye pia ni mwanasheria, Said Hamad El Maamry na Bob Makani walikuwa mbele yake Tabora School.
Aliyekuwa balozi wwa Tanzania kwenye Umoja wa Mataifa, Daud Mwakawago alisoma naye Shule ya Msingi ya Mlandege, Iringa.
Baada ya kutoka jeshini alifanya kazi katika kampuni binafsi ya BP Shell ambayo kwanza ilimpeleka kufanya kazi Nairobi, Kenya kwa muda wa mwaka mmoja kabla ya kurejea tena Dar es Salaam.
Baadaye aliiacha kampuni hiyo na kuingia kazi katika kampuni nyingine binafsi ya AMI. Kampuni hiyo ilimpeleka Zambia kufanya kazi kwenye tawi lake la nchi hiyo.
Alikuwa Zambia kwa miaka 18 na kurejea Dar es Salaam kuendelea na kazi katika tawi la kampuni hiyo.
Wakati Tanzania inapigana vita yake na nduli Idi Amin wa Uganda mwaka 1978/79, Nyirenda alikuwa nchini Zambia.
Nyirenda amefariki akiwa na watoto wanne baada ya mtoto wake wa kwanza wa kike kuzaliwa kufariki dunia.
Je, anajuta kwa nini aliliacha jeshi? Katika mahojiano hayo Nyirenda alisema hajutii hata kidogo uamuzi huo akisema maisha ni popote na mtu hawezi kulazimisha mambo ambayo hupangwa na Mungu.
“Ninachoweza kusema tu ni kwamba nilipokuwa jeshini nilitimiza wajibu wangu kama Mtanganyika ninayeipenda nchi yangu,” alisema.
Hadi katika miaka ya mwisho ya uhai wake, Nyirenda aliendelea kuwa mtu anayendelea kucheza skwashi na tenisi katika Klabu ya Gymkhana, Dar es Salaam ambako alikuwa mdau mzuri.
Source:www.raiamwema.co.tz 24/12/08