Na Mwandishi maalum, visiwani
Rais Jakaya Mrisho Kikwete amesema kuwa fedha za uwezeshaji zinazotolewa na Serikali yake siyo za kujikimu ama kukopeshana viongozi na familia zao bali ni kwa ajili ya wananchi, hasa wenye kipato kidogo.
Rais pia amewataka polisi nchini kuongeza ukali kama moja ya njia za kupambana na ajali za barabara zinazopoteza maisha ya Watanzania.
Aidha, Rais Kikwete amewataka viongozi kuwasimamia kwa karibu wataalam ili kuhakikisha kuwa wanamaliza miradi ya maendeleo haraka na mapema, ili kupunguza kelele na vilio vya wananchi kuhusu upatikanaji wa huduma za kiuchumi na kijamii.
Rais ameeleza hayo jana wakati aliporejea tena katika ziara yake ya Tanzania Visiwani baada ya kuwa amekatisha kwa siku moja jana kwenda Mkoa wa Mara kushiriki mazishi ya mwenyekiti wa zamani wa CCM wa Mkoa huo, Ezekiel Mirumbe Waryuba.
Akizungumza mara baada ya kuwa amefungua Kituo cha Polisi cha Bumbwini, Wilaya ya Kaskazini Unguja B katika Mkoa wa Kaskazini Unguja, Rais Kikwete amesema kuwa mikopo ya uwezeshaji inayotolewa na Serikali zote mbili, yaani ya Muungano na Mapinduzi ya Zanzibar, siyo kwa ajili ya kukopeshana viongozi na familia zao.
Amewaambia wananchi katika eneo hilo: "Napenda kusisitiza kwa masheha, wakuu wa wilaya na wakuu wa mikoa kuwa fedha hizi siyo za kujigawia ama kuchoteana nyie viongozi na familia zenu. Hizi siyo fedha za kujigawia nyie, na wake zenu, na watoto zenu"
Fedha hizo, maarufu kwa Mamilioni ya JK, zimekuwa zinatolewa kwa miaka miwili ya fedha sasa kwa nia ya kutoa fursa kwa wananchi wa kipato cha chini ambao hawana uwezo wala mali za kuwawezesha kupata mikopo kutoka mabenki kujipatia mikopo midogo kuendeshea shughuli zao. Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ) nayo sasa imeanza kutoka mikopo ya namna hiyo.
Rais Kikwete amelazimika kutoka maelekezo hayo kuhusu mikopo ya uwezeshaji baada ya mama mmoja kuwa amelalamika kuwa wananchi katika eneo hilo hawajaanza kupata mikopo ya uwezeshaji, maarufu kwa jina la Mamilioni ya JK.
"Hatutaki kupata matatizo kama yale ya Biharamulo ambako Meneja wa Benki mmoja aliamua kujikopesha yeye mwenyewe fedha zote za wilaya na jamaa zake 13 tu.
Fedha hizo ni kwa ajili ya wananchi wote, hasa hasa wale wenye kipato cha chini na wasiokuwa na sifa za kuweza kukopa katika mabenki.
"Kuhusu ongezeko la ajali ambazo lilizungumzwa katika risala ya Polisi, Rais Kikwete amesema: "Hapa tunalo tatizo kubwa la mafanikio. Tumejenga barabara nyingi na nzuri lakini sasa uzuri wa barabara umeanza kutuzalia balaa la ajali. Lakini nataka kusisitiza kuwa polisi wetu wakiwa wakali hili la ajali litapungua sana."
Amesisitiza: "Haiwezekani polisi wetu wakamaliza tatizo la ajali kwa kugongeana mikono na madereva wavunja sheria. Polisi wanazungumza nini na madareva nyuma ya magari? Polisi anazungumza nini na dereva mhalifu?"
Kuhusu umuhimu wa viongozi kusimamia miradi ya maendeleo ya wananchi na ile ya huduma za jamii na uchumi, Rais amewaelekeza viongozi: "Tatizo ni kwamba watalaama wetu hawana haraka ya kumaliza hii miradi. Msipowasimamisha nyie viongozi, wananchi wataendelea kulalamika hata kama tunao uwezo wa kuondoa kelele hizi za wananchi kwa kukamilisha miradi ya kuwapa huduma."
"Tunachelewesha bure miradi, na wananchi wanaendelea kuteseka na kulalamika. Nyie viongozi msipokuwa makini katika kuwasimamisha watalaamu hawa, miradi hii itaendelea kuchelewa, haitamalizika," amesema Rais na kuongeza:"Mkiwadekeza hawa wataalamu wataishia kuwapeni maelezo tu, maelezo leo, maelezo kesho, maelezo keshokutwa."
Tunampongeza sana rais na watendaji wake. Nafurahi kusikia ana nia njema na ya haraka kupunguza ajali za barabarani ila mweshimiwa rais vifanyio kazi vinahitajika kwa mapolisi wetu. Kama huku kuna vifaa vya kutest dereva amekunjwa pombe au hajanywa.
ReplyDeletethanks
mwananchi mkereketwa
netherland