Rais wa Libya Kanali Muammar Ghadaffi akihutubia Marais wa nchi za Afrika mara tu baada ya Kuchanguliwa kuwa Mwenyekiti mpya wa AU
JK akikabidhi KIRUNGU kuashiria kumkabidhi uenyekiti kwa Mwenyekiti mpya wa UMOJA WA afrika Kiongozi wa Libya Muammar Ghadaffi

JK na Mwenyekiti mpya AU Muammar Ghadaffi mara tu baada ya kumkabidhi Uenyekiti wa Umoja wa Afrika
JK na Katibu mkuu wa Umoja wa Maitaifa Bank Moon mara tu Baada ya kukubidhi uenyekiti
Waziri wa mambo ya nje wa Tanzania Mh. Bernard Membe akiwa pamoja na Mawaziri mwenzie katika mkutano wa umoja wa nchi za Afrika. Toka shoto ni Mh. Shukuru Kawambwa, Mh.Wiliam Ngeleja na Mh. Machano Said wakati Rais Kikwete akisoma Hotuba yake ya kukabidhi Uenyekiti wa AU

HOTUBA YA MHESHIMIWA JAKAYA MRISHO KIKWETE, RAIS WA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA, WAKATI WA KUKABIDHI UENYEKITI WA UMOJA WA AFRIKA WAKATI WA MKUTANO WA 12 WA WAKUU WA NCHI NA SERIKALI WA UMOJA WA AFRIKA ADDIS ABABA, ETHIOPIA,
TAREHE 1 HADI 3 FEBRUARI, 2009

Mheshimiwa Meles Zenawi, Waziri Mkuu wa Ethiopia;
Waheshimiwa Wakuu wa Nchi na Serikali za Umoja wa Afrika;
Mheshimiwa Waziri Mkuu wa Ethiopia;
Mheshimiwa Ban Ki-Moon, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa;
Mheshimiwa Jean Ping, Mwenyekiti wa Kamisheni ya Umoja wa Afrika;
Waheshimiwa Mawaziri;
Waheshimiwa Wageni Waalikwa;
Mabibi na Mabwana:

Awali ya yote naomba nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutuwezesha kukutana hapa leo hii. Kwa kuwa ndio tunakutana kwa mara ya kwanza mwaka huu, niruhusuni nitumie fursa hii kuwatakieni nyote kheri ya mwaka mpya. Tumuombe Mwenyezi Mungu Mwingi wa Rehema mwaka 2009 uwe wa baraka na mafanikio tele kwa Bara letu.
Natumaini mtaungana nami katika kumshukuru Waziri Mkuu wa Ethiopia, Mheshimiwa Meles Zenawi, kwa mapokezi mazuri na ukarimu ulioonyeshwa na serikali yake na watu wa Ethiopia. Ukarimu ambao tumetokea kuuzoea na kuutarajia.
Waheshimiwa Viongozi wenzangu;
Tangu tulipokutana mjini Sharm el Sheikh, Misri tarehe 30 Juni, 2008, Umoja wetu umepata pigo kubwa kwa kuondokewa na viongozi wenzetu wawili. Wenzetu hao ni Mheshimiwa Levy Mwanawasa, aliyekuwa Rais wa Jamhuri ya Zambia na Mheshimiwa Jenerali Lansana Conte, aliyekuwa Rais wa Jamhuri ya Guinea.
Kwa niaba ya Umoja wa Afrika naomba tusimame kwa dakika moja kuwakumbuka viongozi na ndugu zetu hawa. Tumuombe Mwenyezi Mungu aziweke roho za marehemu mahali pema peponi. Amina.
Napenda pia kutumia nafasi hii kuwakaribisha rasmi Mheshimiwa Rupiah Banda, Rais mpya wa Zambia, Mheshimiwa Kgalema Motlanthe, Rais mpya wa Afrika Kusini na Mheshimiwa Sheikh Sharif Ahmed Said, Rais mpya wa Somali ambao hiki ni kikao chao cha kwanza kuhudhuria katika nyadhifa zao za Wakuu wa Nchi na Serikali za nchi zao tukufu. Nina hakika kuwepo kwao na mchango wao vitazidi kuimarisha umoja wetu. Rais mpya wa Ghana Mheshimiwa John Atta Mills hakuweza kufika lakini tunampongeza na kumtakia heri.
Waheshimiwa Wakuu wa Nchi na Serikali;
Tarehe 31 Januari, 2008 mlinichagua kuwa Mwenyekiti wa Umoja wa Afrika. Hii ilikuwa heshima kubwa kwangu mimi binafsi na kwa nchi yangu ya Tanzania. Wakati nikikubali heshima mliyonipa, nilitaja maeneo manne ambayo niliahidi kuyapa kipaumbele katika kipindi cha Uenyekiti wangu. Maeneo hayo ni (a) ulinzi na usalama (b) kutetea maslahi na kutafuta fursa za kiuchumi na kisiasa zitakazoleta maendeleo na ustawi wa bara letu (c) kushughulikia masuala ya jamii na utamaduni na (d) kuimarisha Umoja wa Afrika na taasisi zake.
Leo, wakati wa kumaliza kipindi changu cha uongozi na kukabidhi kijiti kwa kiongozi mwenzetu mwingine kuongoza Umoja wa Afrika, nawiwa na wajibu wa kuelezea jinsi kwa pamoja tulivyotekeleza majukumu yetu katika maeneo haya muhimu. Ni matumaini yangu kwamba tathmini hii itatusaidia kuweka wazi changamoto zilizokuwepo wakati ule, mafanikio tuliyopata na changamoto zilizobaki mbele yetu ambazo hatuna budi kuendelea kuzikabili siku za usoni kwa nguvu zetu zote.
Waheshimiwa Viongozi;
Wakati nakubali Uenyekiti nilisema kuwa mimi ni mtu wa matumaini. Leo hii ninapokamilisha kipindi cha Uenyekiti wangu nafurahi kuona kuwa katika kipindi cha mwaka mmoja, Umoja wa Afrika unajivunia mafaniko tuliyopata katika maeneo kadhaa.
Utatuzi wa Migogoro
Katika jitihada za kutatua migogoro inayolikabili Bara letu, mtakumbuka kuwa kwenye kikao chetu cha 11 mjini Sharm el Sheikh, nilieleza mafanikio makubwa ambayo Umoja wetu ulikuwa umepata kwa kutatua migogoro katika nchi za Kenya na Comoros. Nchini Kenya, tuliweza kuzipatanisha pande zilizokuwa zikivutana na kufikia makubaliano ya kuunda Serikali ya Umoja wa Kitaifa. Serikali hiyo ilirejesha amani nchini humo na hali ya maelewano na maridhiano imeendelea kushamiri Kenya hadi hii leo. Kwa niaba yenu narudia kuwapongeza wananchi wa Kenya na hasa viongozi wao, akiwamo Rais Mwai Kibaki ambaye tunaye hapa leo, kwa mafanikio hayo.
Aidha, nchini Comoro Umoja wa Afrika katika operesheni ya kwanza ya aina yake, ulituma majeshi kutoka Libya, Sudan na Tanzania na kufanikiwa kukomesha uasi katika Kisiwa cha Anjouan na hivyo kuweza kurejesha umoja wa kitaifa katika nchi hiyo. Hadi sasa mshikamano huu umedumu nchini Comoro.
Tumepata pia mafanikio ya kutia moyo katika kutafuta suluhu nchini Burundi, kufuatia juhudi za nchi za Kanda na usuluhishi wa Serikali ya Afrika Kusini. Tarehe 4 Desemba 2008, Serikali ya Burundi na Kikundi cha PALIPEHUTU-FNL zilikubaliana kumaliza tofauti zao na kuanza kutekeleza vipengele vya mwisho vya Mkataba wa Kusitisha Mapigano kati ya pande hizo mbili.
Katika makubaliano hayo Kikundi cha PALIPEHUTU-FNL kimekubali kubadilisha jina lake ili kuondoa muonekano wa kikabila. Aidha, Chama hicho kimekubali kupeleka wapiganaji wake kwenye makambi ya kukusanyia wapiganaji ili kuwezesha zoezi la kuwanyang’anya silaha kufanyika na mchakato wa kuwatangamanisha na jamii ya Burundi uanze. Kwa upande wake, Serikali imeandaa kambi kubwa huko Rubira kwa ajili ya kuwakusanya wapiganaji wa FNL. Aidha, Serikali ya Burundi imekwishatoa nafasi 20 za uongozi kati ya 33 ilizokubali kutoa kwa viongozi wa FNL. Ni mategemeo yangu kwamba pande zote husika zitaheshimu na kutekeleza ipasavyo makubaliano yao hayo.
Napenda kutumia nafasi hii, kutoa wito kwa jumuiya ya kimataifa kushirikiana na Umoja wa Afrika kusaidia kujenga nchi hiyo upya. Kwa kuanzia, jumuiya ya kimataifa haina budi kutekeleza ahadi yake ya kutoa msaada wa kuanzisha makambi ya kukusanyia wapiganaji, pamoja na chakula kwa nchi ya Burundi. Pili, kutoa misaaada ya maendeleo ambayo ilisitishwa kusubiri hatua hii.
Waheshimiwa Viongozi wenzangu;
Mwaka 2008 pia tumeshuhudia mambo ya kutia moyo yakiendana na changamoto kadhaa katika nchi ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (JKK). Hali ya amani na mafanikio ambayo ilipatikana nchini JKK iliingia dosari mwezi Agosti kufuatia kuzuka upya kwa mapigano kati ya majeshi ya Serikali na vikosi vya Jenerali Laurent Nkunda wa CNDP. Mapigano hayo yamesababisha vifo vya watu wengi na uharibifu wa mali na mateso kwa raia wengi wasiokuwa na hatia. Watu wapatao milioni moja na laki saba wamekuwa wakimbizi ndani ya nchi yao.
Katika jitihada za kusuluhisha mgogoro huo Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Mheshimiwa Ban Ki-moon kwa mashauriano nami nikiwa Mwenyekiti wa Umoja wa Afrika na Rais Mwai Kibaki wa Kenya ambaye ni Mwenyekiti wa Ushirikiano wa Nchi za Kanda ya Maziwa Makuu aliitisha mkutano wa Wakuu wa Nchi za Ushirikiano huo tarehe 7 Novemba 2008, mjini Nairobi, Kenya. Mkutano huo uliofanyika chini ya uenyekiti wangu ulijadili hali ya usalama na mapigano katika Jimbo la Kivu. Kwa kauli moja mkutano huo ulizitaka pande husika kusitisha mapigano mara moja na kuruhusu misaada ya kibinadamu kupelekwa kwa wananchi wanaohitaji. Pia, tulizitaka pande hizo zianze mazungumzo ya kutatua tofauti zao kwa njia ya amani.
Aidha, Wakuu hao walimteua Mhe. Benjamin Mkapa, Rais Mstaafu wa Tanzania, kuungana na Mhe. Olesegun Obasanjo, Rais Mstaafu wa Nigeria aliyeteuliwa na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa kufanya kazi ya kusuluhisha mgogoro huo. Nafurahi kueleza kuwa Wasuluhishi hao tayari wamefanya mazungumzo na pande zote zinazohusika na mgogoro huo. Jitihada zao zimeanza kuzaa matunda kwani pande husika zilikubali kusitisha mapigano na kuruhusu misaada ya kibinadamu kuwafikia wananchi.
Nafurahi kusema kuwa, pande zinazohasimiana zimeingia kwenye mazungumzo yanayoendelea hivi sasa huko Nairobi, Kenya. Nashauri Umoja wa Afrika utambue na kuwapongeza Katibu Mkuu wa Umoja wa mataifa na Wakuu wa Nchi za Ukanda wa Maziwa Makuu kwa uamuzi wao wa busara na hatua wanazoendelea kuchukua. Pia, kikao kiwatake waendelee kusimamia juhudi za kupata amani mashariki mwa Kongo.
Pia naomba kutambua na kuunga mkono ushirikiano baina ya Kongo na Rwanda na baina ya Kongo, Sudan na Uganda yenye lengo la kumaliza matatizo ya waasi katika mashariki ya Kongo.
Waheshimiwa Wakuu wa Nchi na Serikali, Mabibi na Mabwana;
Pamoja na mafanikio haya bado Bara letu limeendelea kukabiliwa na migogoro sugu na mingine iliyozuka hivi karibuni. Miongoni mwa migogoro hiyo ni pamoja na ile ya Somalia, Jimbo la Darfur nchini Sudan, Zimbabwe, Mauritania na Guinea.
Kuhusu Zimbabwe mtakumbuka kuwa wakati wa kikao chetu mjini Sharm el Sheikh, tulikubaliana kuikabidhi Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika (SADC) jukumu la kuendelea kusuluhisha mgogoro kati ya Serikali ya Zimbabwe na Chama cha Movement for Democratic Change (MDC) kinachoongozwa na Bw. Morgan Tsvangirai. SADC.
Kupitia msuluhishi wake Mheshimiwa Thabo Mbeki, aliyekuwa Rais wa Afrika Kusini, ilifanikiwa kuanzisha mazungumzo kati ya Chama cha Zanu-PF na Chama cha MDC kinachoongozwa na Bwana Tsvangirai kama tulivyoagiza. Katika mazungumzo hayo pia kilishirikishwa Chama cha MDC kinachoongozwa na Profesa Arthur Mutambala. Tarehe 15 Septemba 2008, pande hizo zilifikia makubaliano ya kumaliza uhasama na kuanzisha Serikali ya Umoja wa kitaifa. Katika makubaliano hayo, ilikubalika kuwa Rais Robert Mugabe aendelee kuwa Rais wa Zimbabwe na Bwana Morgan Tsvangirai awe Waziri Mkuu na Profesa Arthur Mutambara awe Naibu Waziri Mkuu. Pia walikubaliana kuwepo Naibu Waziri Mkuu wa pili kutoka Chama cha MDC cha Bwana Morgan Tsvangirai. Hali kadhalika pande hizo zilikubaliana kugawana nafasi za Mawaziri kwa uwiano wa nafasi 15 kwa Zanu-PF, 13 kwa MDC- Tsvangirai na nafasi 3 kwa MDC-Mutambara.
Maelewano hayo yaliingia dosari tarehe 11 Oktoba 2008 baada ya kutangazwa mgao wa wizara kwa vyama ambapo Chama cha MDC kilipoelezea kutokuridhika na jinsi mgao ulivyofanywa. Kilidai kuwa nafasi zote nyeti zilienda kwenye Chama cha Zanu-PF. Hali hiyo ya kutokuelewana imechelewesha utekelezaji wa makubaliano hayo.
Viongozi wa SADC wameendelea na juhudi za kuzipatanisha pande husika ili ziweze kufikia makubaliano kuhusu nafasi za Uwaziri. Juhudi hizo zimezaa matunda, Bw. Morgan Tsivangirai na Chama chake cha MDC wamekubali kujiunga na Serikali ya Umoja wa Kitaifa.
Taarifa ya uamuzi wa Chama cha MDC kujiunga na Serikali ya Umoja wa Kitaifa ni ya kutia moyo. Sisi katika AU tunafurahi kuwa uamuzi wetu wa Sharm al Sheikh umezingatiwa. Wakati tunawapongeza viongozi wenzetu wa SADC kwa kazi nzuri waliyoifanya kwa niaba yetu, tuwaombe viongozi wa Zimbabwe kuweka mbele maslahi ya taifa lao na watu wake. Nawaomba wenzangu wote na hasa Umoja wa Afrika uendelee kuwa pamoja na watu wa Zimbabwe hasa wakati huu wa kazi ngumu ya kuunda na kuendesha Serikali ya pamoja na kujenga upya uchumi wa nchi yao.
Waheshimiwa Wakuu wa Nchi na Serikali;
Namaliza Uenyekiti wakati hali ya Somalia ikiwa bado ni changamoto kubwa kwa Umoja wa Afrika na kwa dunia kwa jumla. Uharamia wa utekaji nyara wa meli katika Ghuba ya Aden unaufanya mgogoro huo sasa uchukue sura ya kimataifa badala ya kuwa ni wa ndani ya Somalia au wa ukanda wa pembe ya Afrika pekee. Hali hii inasisitiza hoja ya jumuiya ya kimataifa kwa pamoja kujihusisha kwa karibu na juhudi za kutafuta ufumbuzi wa haraka kwa mgogoro wa Somalia. Kwa maneno mengine, tungependa kuona Umoja wa Mataifa ukichukua nafasi yake stahiki ya uongozi kwenye maeneo yenye migogoro ukishirikiana na Umoja wa Afrika. Mgogoro huu umefikia mahali ambapo hauwezi kuachiwa Umoja wa Afrika pekee. Sisi tumetimiza wajibu wetu kwa uwezo wetu na tutaendelea kufanya hivyo. Tunaomba jumuiya ya kimataifa nayo ikiongozwa na Umoja wa Mataifa itusaidie. Tunausubiri kwa hamu uamuzi utakaofanywa na Baraza la Usalama mwezi Aprili, 2009.
Waheshimiwa Viongozi wenzangu;
Napenda kuitumia nafasi hii kuwapongeza wenzetu wa Uganda na Burundi kwa mchango wao mkubwa walioutoa katika juhudi za kutafuta amani nchini Somalia. Mchango wao wa wanajeshi wa kulinda amani katika AMISOM unathaminiwa na kupongezwa sana. Aidha, sina budi kusema neno la pongezi kwa Serikali na watu wa Ethiopia kwa uamuzi wa busara wa kupeleka majeshi nchini Somalia. Uamuzi ule wa kishujaa ndiyo uliosaidia Somalia kuendelea kuwa taifa moja na lenye Serikali tunayoiona leo. Kama si hivyo, sijui hali ingekuwaje. Tunawapongeza tena kwa uamuzi wao wa busara wa kuondoa majeshi yao baada ya kutoa mchango wao muhimu.
Kwa niaba yenu napenda kuwapongeza sana Wabunge wa Somalia kwa uamuzi wa hivi karibuni wa kumchagua Sheikh Sharif Ahmed Said kuwa kiongozi wa nchi yao. Tumeupokea kwa furaha uamuzi huo na kuwataka wanasiasa na wananchi wote wa Somalia kuunga mkono uamuzi huo. Wampe ushirikiano Kiongozi wao mpya kwa maslahi yao na nchi yao.
Waheshimiwa Wakuu wa Nchi na Serikali;
Kuhusu Darfur, napenda kuelezea faraja yangu kwamba muelekeo ni mzuri kuhusu kupelekwa kwa vikosi vya kulinda amani ya Umoja wa Mataifa na Umoja wa Afrika (UNAMID). Bado hali ya amani ya Darfur ni tete lakini naamini vikosi vya UNAMID vikikamilika hali ya amani itadhibitiwa na kutengemaa.
Wakati naipongeza Serikali ya Sudan kwa ushirikiano wake, niombe wahusika kwa upande wa Umoja wa Mataifa na Umoja wa Afrika kuongeza juhudi ya kupatanisha vikundi vya waasi ili mazungumzo na Serikali yaanze mapema iwezekanavyo. Hatima ya amani ya kudumu ya Darfur ipo katika kufanyika na kufanikiwa kwa mazungumzo hayo.
Changamoto mpya kwenye mgogoro wa Darfur inahusu ombi la Mwendesha Mashtaka wa Mahakama ya Makosa ya Jinai ya Kimataifa (ICC) la kutaka Rais Omar Al-Bashir wa Sudan kufunguliwa mashtaka ya makosa ya kivita. Kimsingi, Umoja wa Afrika hauna pingamizi kuhusu watuhumiwa wa makosa ya kivita kuwajibishwa. Hoja yetu ni kwamba hatua hizo zisivuruge lengo la msingi la kuhakikisha usalama wa watu walio wengi katika jimbo hilo. Rais Al-Bashir ni mdau muhimu sana katika kufanikisha hayo.
Umoja wa Afrika umewasiliana na mamlaka, taasisi na wadau husika kutaka ombi hilo kusitishwa kwa sasa. Hadi sasa jitihada hizo bado hazijafanikiwa. Ni vyema basi Umoja wa Afrika ukaendelea na juhudi zake, kwa kushirikiana na pande zote zinazohusika, kutafuta amani katika nchi hiyo. Ninaiomba jumuiya ya kimataifa iendelee kuunga mkono juhudi zetu.
Waheshimiwa Wakuu wa Nchi na Serikali;
Kama nilivyosema awali, Bara letu pia limeshuhudia kuzuka kwa migogoro mipya kufuatia mapinduzi ya kijeshi yaliyofanyika katika nchi za Mauritania na Guinea. Mapinduzi hayo ni kinyume na misingi ya Katiba ya Umoja wa Afrika, Mkataba wa kuanzisha Baraza la Amani na Usalama la Umoja wa Afrika, pamoja na Tamko la Lome la mwaka 2000. Umoja wa Afrika unakataa kubadilisha Serikali za nchi kwa kutumia njia zisizokuwa za kidemokrasia. Kwa kuzingatia misingi tuliyoiweka, nchi hizo mbili zimesimamishwa kushiriki shughuli za Umoja wa Afrika mpaka zitakaporudishwa katika utawala wa kidemokrasia.
Naomba kutumia fursa hii kutoa mwito kwa viongozi wa kijeshi katika nchi hizo kuheshimu katiba za nchi zao na kurudisha utawala wa kiraia haraka iwezekanavyo. Aidha, naziomba nchi wanachama za Umoja wa Afrika kukataa kuunga mkono viongozi hao wa kijeshi kwani kufanya hivyo ni kukiuka Katiba ya Umoja wetu. Pia jumuiya ya kimataifa haina budi kutuunga mkono kwa kukemea mapinduzi hayo na kutowatambua viongozi wa kijeshi wa nchi hizo.
Kwa misingi hiyo tunasikitishwa na hali ya wasiwasi inayoendelea sasa nchini Madagascar. Harakati za kuiondoa Serikali iliyochaguliwa kidemodrasia hazikubaliki. Tunawasihi wahusika waache kutumia njia za ghasia bali wazingatie na kuheshimu misingi ya kidemokrasia.
Waheshimiwa Viongozi;
Kwa jumla hali ya amani na utulivu Barani Afrika ni ya kuridhisha. Ni nchi chache tu zenye migogoro siku hizi ukilinganisha na miaka ya nyuma. Mimi naamini inawezekana kukawa na amani na utulivu katika nchi zote Barani Afrika. Siku hiyo haiko mbali kadri demokrasia inavyozidi kuimarika, utawala bora unavyozingatiwa, haki za binadamu zinavyoheshimiwa na uchumi wa nchi za Afrika unavyozidi kukua na umaskini kupungua. Hata hivyo, hatuna budi kufanya kila tuwezalo kuhakikisha hayo yaendelee kufanyika katika nchi zetu.
Mafanikio ya kiuchumi
Waheshimiwa Wakuu wa Nchi na Serikali;
Namaliza kipindi changu cha uongozi nikiacha nyuma yangu changamoto kubwa ya maendeleo ya kiuchumi na kijamaa ikiwa ndilo suala la msingi ambalo hatuna budi kuendelea kulipa kipaumbele cha kwanza. Afrika ndilo Bara maskini kuliko mabara yote duniani. Katika nchi 50 maskini sana duniani 34 zipo Afrika.
Bado upatikanaji wa huduma za kiuchumi na kijamii kama vile elimu, afya, maji, barabara, reli, usafiri wa anga, umeme n.k. ni wa kiwango cha chini sana.
Kwa upande wa usalama wa chakula, hali ya Afrika bado siyo nzuri. Kwa sasa, duniani kuna nchi 36 zinazokabiliwa na tatizo la upungufu wa chakula. Kati ya hizo, 21 ziko Afrika. Nayasema mambo haya tunayoyajua sote kusisitiza ukubwa wa tatizo la kujiletea maendeleo katika nchi zetu moja moja na kwa Bara zima la Afrika. Tuna safari ndefu na ngumu mbele yetu kufikia maendeleo tunayoyatarajia sote. Hatuna budi kutoa uzito unaostahili kwa masuala ya kukuza uchumi wa nchi zetu na kuwaletea maendeleo watu wetu.
Bahati mbaya sana, tunatumia muda mwingi kutatua migogoro na kuzungumzia masuala ya kisiasa tena kuhusu kugawana madaraka miongoni mwa wanasiasa au baadhi yetu kutaka kujiongezea madaraka au umaarufu. Nawaomba wenzangu tubadilike. Tupange vipaumbele vyetu vizuri na kuweka masuala ya maendeleo ya uchumi katika kipaumbele stahili. Nafurahi kwamba katika mkutano huu tutajadili suala muhimu la maendeleo ya miundombinu Barani Afrika.
Ndugu zangu, Viongozi wenzangu;
Pamoja na hali kuwa ngumu lakini nafurahi kusema kuwa muelekeo wetu ni mzuri. Lililo muhimu ni kuhakikisha haturudi nyuma bali tunasonga mbele. Mwaka wa jana uchumi wa Afrika ulikuwa kwa wastani wa asilimia 5.8. Hii ni kasi nzuri lakini haitoshi hasa kwa vile tuko nyuma sana kimaendeleo. Isitoshe, kiasi hicho ni pungufu ya lengo la asilimia 7 linalotakiwa kutuwezesha kutekeleza lengo la Milenia la kupunguza umaskini kwa nusu ifikapo mwaka 2015. Lazima tuongeze juhudi za kukuza uchumi wa nchi zetu kwa kasi kubwa zaidi. Naomba nipendekeze kuwa, tutafute nafasi siku za usoni tulizungumze suala hili. Tena itakuwa bora tuwe na kikao maalum kuzungumzia mikakati na mbinu za kukuza uchumi wa Bara la Afrika haraka ili tujiondoe katika aibu ya kuwa Bara la nchi na watu maskini kuliko wote duniani.
Uhusiano kati ya Afrika na Nchi na Kanda nyingine
Waheshimiwa Wakuu wa Nchi na Serikali, Wageni Waalikwa; Mabibi na Mabwana;
Kwa ajili ya kuendeleza shughuli za Umoja wetu na kusukuma mbele gurudumu la maendeleo la nchi zetu na Bara letu mahusiano mazuri na mataifa na mashirika ya kimataifa duniani ni jambo muhimu sana. Katika mwaka mmoja wa uongozi wangu kulikuwa na shughuli nyingi za namna hiyo. Tulianzisha rasmi ushirikiano wa kiuchumi na India na Uturuki na tumefanya mikutano ambayo ilitushirikisha sisi na wakuu wa nchi na Serikali wa nchi hizo. Nafurahi kwamba katika mikutano hiyo yaani tarehe 8-9 Aprili, 2008 na India na tarehe 18-20 Agosti 2008 na Uturuki makubaliano muhimu yahusuyo maendeleo na uhusiano wa kibiashara yenye maslahi kwetu yalifikiwa. Nawaombeni wenzangu tuchangamkie kufuatilia.
Katika mwaka uliopita kulifanyika mikutano muhimu nchini Japan na kwenye Umoja wa Mataifa New York iliyohusu maendeleo ya Afrika. Wa kwanza ni Mkutano wa Nne wa Ushirikiano kati ya Africa na Japan (TICAD IV) uliofanyika tarehe 28 - 30 Mei, 2008 huko Yokohama, Japan. Kama mtakavyokumbuka katika mkutano ule Mheshimiwa Takeo Fukuda aliyekuwa Waziri Mkuu wa Japan wakati ule alitangaza fursa nyingi za misaada ya maendeleo, uwekezaji na biashara.
Hatuna budi kujipanga vizuri katika ufuatiliaji ili tuzitumie fursa hizo kwa maendeleo yetu. Bahati nzuri marafiki zetu wa Japan walikubali, kwa mara ya kwanza, kuwapo utaratibu wa kufuatilia utekelezaji wa maazimio ya TICAD IV. Naomba Uongozi ujao wa Umoja wetu na sote kwa jumla tuzichangamkie fursa hizo na kuzitumia. Ni muhimu kwetu, zitatusaidia sana.
Waheshimiwa Viongozi Wezangu;
Tarehe 07 hadi 09 Julai, 2008, nilishiriki Mkutano wa G8 uliofanyika huko Japan. Nilipata fursa, pamoja na Waziri Mkuu Meles Zenawi wa Ethiopia, Rais Thabo Mbeki wa Afrika Kusini wakati ule, Rais Abdelaziz Bouteflika wa Algeria, Rais Abdoulaye Wade wa Senegal na Rais Yaradua wa Nigeria kuzungumzia masuala muhimu kwa maendeleo ya Afrika. Kama ilivyo kawaida ya viongozi wa nchi wanachama wa G8, walikuwa wakarimu kwa ahadi za kutusaidia. Naomba tuendelee kwa umoja wetu kufuatilia ahadi hizo na zile za nyuma walizotoa katika mikutano iliyopita. Ahadi nyingi zilizotolewa na Wakuu wa Nchi za G8 zikitekelezwa, hali ya maendeleo ya Bara letu itafikia mahali pazuri.

Waheshima Wakuu wa Nchi na Serikali;
Mwaka wa jana, Umoja wa Mataifa umetutendea wema sana. Kulifanyika mikutano miwili maalum kuhusu Afrika ambayo napenda kuitambua. Tarehe 22 Septemba, 2008 kulikuwa na mkutano kuhusu mahitaji maalum ya maendeleo ya Afrika (High Level Meeting on Special Needs for Africa’s Development). Mkutano huo uliitishwa na Rais wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa, Mheshimiwa Padri Miguel Brockmann. Tarehe 25 Septemba, 2008 Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Mheshimiwa Ban Ki-Moon aliitisha mkutano wa kuzungumzia kutekeleza Malengo ya Milenia ambapo Bara la Afrika lilipata nafasi maalum. Mikutano hiyo imeleta faraja kubwa kwetu sote viongozi na wananchi wa Afrika kwamba, Umoja wa Mataifa unajali mambo yenye maslahi kwa Afrika. Kwa niaba yenu napenda kumshukuru Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa na Rais wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa kwa moyo wao wa upendo kwa Afrika na watu wake. Naomba yaliyoamuliwa na kukubaliwa na mikutano hiyo miwili yatekelezwe ipasavyo. Tunasubiri utekelezaji wake kwa hamu. Naomba Mwenyekiti ajaye, Kamisheni ya Umoja wa Afrika na sisi viongozi mmoja mmoja na kwa umoja wetu tuwe makini kufuatilia.
Waheshimiwa Viongozi;
Mkutano wa Pili wa Ushirikiano baina ya Afrika na Amerika ya Kusini ambao ulikuwa ufanyike tarehe 01 Desemba, 2008 huko Caracas, Venezuela uliahirishwa. Sababu ya kufanya hivyo, ilikuwa kutoa nafasi kwa washiriki wa pande zote mbili waweze kushiriki mkutano wa kutathmini utekelezaji wa makubaliano ya Monterey kuhusu kugharimia maendeleo (Follow up Conference on Financing for Development)ya nchi zinazoendelea uliofanyika Doha, Quatar tarehe 29 Novemba hadi 02 Desemba, 2008. Mkutano kati ya Afrika na Amerika Kusini sasa utafanyika mapema mwaka huu. Napenda kuchukua nafasi hii kuhimiza nchi za Afrika kujiandaa vyema ikiwa ni pamoja na kutayarisha miradi ambayo itatekelezwa kwa pamoja na washirika wetu wa Amerika Kusini.
Ushirikiano wetu na Benki ya Dunia, Benki ya Maendeleo ya Afrika na Jumuiya ya Ulaya umeendelea kuwa mzuri. Benki ya Dunia na Benki ya Maendeleo ya Afrika zimeendelea kuwa washirika wa kutumainiwa na wahimili wakubwa wa maendeleo ya Afrika. Tunawashukuru sana. Tunaomba waendelee kutusaidia. Afrika inawahitaji sana.
Mkutano wa 10 wa Utatu wa Mawaziri (Troika Ministerial Meeting) wa Afrika na Ulaya ulifanyika tarehe 20 na 21 Novemba 2008 hapa Addis Ababa kuhakiki maendeleo ya utekelezaji wa Mpango Kazi wa Pamoja kati ya Afrika na Ulaya. Pande hizo zimeunda Timu za Pamoja za Wataalamu katika maeneo yote ya ushirikiano. Kazi ya kuandaa miradi ya pamoja inaendelea na nina imani kuwa mafanikio yatapatikana mapema kabla ya Mkutano wetu na Wakuu wa Nchi za Jumuiya ya Ulaya utakaofanyika mwaka 2010. Ni matumaini yangu kuwa nchi wanachama zitachangamkia fursa hizi zilizopatikana ili kukuza uchumi na kuondoa umaskini kwa raia wetu.
Waheshimiwa Viongozi wenzangu;
Changamoto kubwa iliyopo sasa ni namna ya kutumia fursa zilizojitokeza katika ushirikiano wetu na mataifa na mashirika mbalimbali ya kimataifa duniani kwa ajili ya kuleta maendeleo kwa nchi zetu za Afrika. Nataka nitumie fursa hii kuihimiza Kamisheni ya Umoja wa Afrika kuendelea kuratibu shughuli za ushirikiano na kuandaa tathmini za mara kwa mara ili tuweze kufahamu maendeleo yanayopatikana na changamoto zilizopo.
Waheshimiwa Viongozi;
Vilevile, wakati wa Uenyekiti wa Tanzania, ilifanyika pia mikutano mingi ya kisekta ambayo iliratibiwa na Kamisheni ya Umoja wa Afrika. Tumepiga hatua kubwa katika mchakato wa kuanzisha taasisi za fedha za Umoja wetu, hususan Benki ya Rasilimali ya Afrika. Aidha, Mawaziri wa Viwanda walikutana mwezi Oktoba mjini Durban, Afrika Kusini na kupitisha Mkakati wa Kutekeleza Mpango Kazi wa Kuendeleza Viwanda Afrika. Mkakati huo ukitekelezwa vyema, utaliwezesha bara la Afrika kujikomboa kutoka kwenye mtego wa kuuza malighafi duniani kwa nchi za Magharibi kwa bei nafuu. Vilevile, suala la uhaba wa chakula lilipewa nafasi yake ambapo Mawaziri wa Chakula walikutana mwezi Desemba 2008 mjini Sirte, Libya na kujadili namna ya kutumia rasilmali maji kwa ajili ya umwagiliaji mashambani na uzalishaji wa nishati kwa lengo la kuongeza uzalishaji wa chakula na maendeleo ya vijijini.
Misukosuko ya Mfumo wa Fedha Kimataifa
Waheshimiwa Wakuu wa Nchi na Serikali;
Kama tunavyojua, mwaka 2008 ulikuwa na misukosuko mingi ya kiuchumi duniani iliyotuathiri hata sisi katika Bara la Afrika. Tulianza na tatizo la kupanda sana kwa bei za mafuta, baadae bei za chakula na sasa mgogoro wa fedha na uchumi. Matatizo hayo yameathiri uchumi wa nchi zetu kwa namna mbalimbali na kutishia kupoteza mafanikio tuliyoyapata katika utulivu wa uchumi na maendeleo. Bei za mafuta na chakula zimeshuka lakini athari za mgogoro wa fedha na uchumi tutakuwa nazo mpaka hapo migogoro hiyo itakapoisha. Tuna kila sabubu za kuhofia matokeo yake kwa uchumi wa nchi zetu changa.
Nusura yetu inategemea ni kwa kiasi gani mataifa makubwa kiuchumi yaliyo chanzo cha kuwepo migogoro hiyo yatafanikiwa kukabiliana na matatizo haya. Tunawapongeza kwa juhudi kubwa wazifanyazo kurekebisha mambo katika nchi zao na tunawatakia mafanikio. Hata hivyo ni muhimu Afrika nayo ishirikishwe katika mikutano waifanyayo kutafuta ufumbuzi wa tatizo hili kubwa. Na sisi pia ni sehemu ya uchumi wa dunia na athari zinazotokana na misukosuko ya fedha na uchumi na sisi tunazipata.
Waheshimiwa Viongozi Wenzangu;
Kwa vile athari zinatupata sote hatuna budi na sisi wenyewe kujiwekea mikakati ya kuziepuka na kuzikubali. Nawapongeza sana Mawaziri wa Fedha wa Afrika kwa uamuzi wao waliofanya kukutana Tunis, Tunisia Novemba, 2008 na kwa maamuzi yao muafaka waliyoafikiana. Naamini yakitekelezwa ipasavyo yatasaidia kutuepusha au kutupunguzia makali ya tatizo. Nawaomba viongozi wenzangu tuyatafakari na kuchukua hatua zipasazo.
Kuhusu masuala ya jamii na utamaduni, chini ya Uenyekiti wangu Baraza la Uchumi, Jamii na Utamaduni lilizinduliwa rasmi tarehe 9 Septemba 2008 mjini Dar es Salaam, Tanzania. Mtakumbuka kuwa Asasi zisizo za Kiserikali zilizopo Barani ni wanachama wa Baraza hili. Kuanza kazi rasmi kwa Baraza hili ni fursa nzuri kwa raia wa kawaida kushiriki kwenye shughuli za kiuchumi, jamii na utamaduni ambazo zinahusu Bara letu. Ni matumaini yangu kuwa asasi zote zisizo za kiserikali zitatumia Baraza hili katika kutimiza malengo ya kuanzishwa kwake.
Waheshimiwa Wakuu wa Nchi na Serikali;
Wageni Waalikwa;
Mabibi na Mabwana;
Jambo lingine nililolishughulikia wakati wa Uenyekiti wangu ni suala la matumizi mabaya ya dhana ya uwezo wa kufungua kesi za makosa ya jinai yanayofanywa mahali popote ulimwenguni na ambayo yamekuwa yakitumika na baadhi ya majaji wa nchi za Ulaya, kufungua mashtaka dhidi ya viongozi wa nchi za Afrika.
Kufuatia uamuzi wetu tuliofikia wakati wa kikao chetu cha Sharm el Sheikh kuwa suala hili lijadiliwe kwa kina na Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, niliwasilisha uamuzi huo wakati nilipohutubia Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa mwezi Septemba, 2008. Suala hili sasa lipo kwenye Kamati ya Sita ya Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa. Aidha, Mwenyekiti wa Kamisheni, amewasiliana na Rais wa Kamisheni ya nchi za Ulaya kupendekeza kuwa suala hili lijadiliwe baina ya taasisi hizo mbili, kwa sababu matumizi mabaya ya dhana hii, yanaonekana zaidi kwenye nchi za Ulaya. Nategemea kuwa Mwenyekiti mpya tutakayemchagua, ataendelea kufuatilia na sote tutashirikiana na kuhakikisha kuwa jambo hili linakamilika kama tulivyotarajia mapema iwezekanavyo.
Uimarishaji wa taasisi za AU
Waheshimiwa Wakuu wa Nchi na Serikali; Mabibi na Mabwana;
Mtakumbuka kwamba nilianza uongozi katika kipindi cha mabadiliko ya uongozi wa Kamisheni. Katika kipindi cha Uenyekiti wangu tulifanya uchaguzi wa Kamisheni mpya na nilikuwepo kushuhudia Mwenyekiti aliyemaliza muda Mheshimiwa Prof. Alpha Omar Konare akimkabidhi Mwenyekiti mpya Mheshimiwa Jean Ping. Nilipata fursa ya kuzungumza na Makamishna wapya kuhusu majukumu yao na mategemeo yetu kwao.
Aidha, nilizungumza na wafanyakazi wa Kamisheni ya Afrika ambapo walinieleza matatizo mbalimbali yanayowakabili. Nafurahi kwamba katika kikao kilichomalizika juzi cha Baraza la Mawaziri wa Umoja wa Afrika, uamuzi wa kuboresha maslahi ya wafanyakazi wa AU umefanywa. Ahadi yangu kwao imetimia sasa ni wajibu wao kutimiza ahadi yao kwangu ya kufanya kazi kwa bidii.
Pamoja na hayo kazi ya kuimarisha Kamisheni kwa nyenzo na vifaa haina budi iendelee. Kazi hiyo ingefanikiwa zaidi kama nchi zote zitalipa michango yao kwa wakati. Naomba niwasihi viongozi wenzangu tuzingatie wajibu wetu huu wa msingi. Wenye kudaiwa malimbikizo walipe na tujenge mazoea ya kulipa michango yetu kwa wakati. Uimara wa chombo chetu hiki muhimu unategemea sana ulipaji wetu wa michango. Hili si jambo ambalo ninalazimika kulifafanua zaidi. Sote tunalielewa vyema.

Viongozi wenzangu;
Jambo lingine muhimu kuhusu Kamisheni yetu lililotokea katika kipindi cha Uenyekiti wangu ni ule uamuzi wetu jana. Tumeazimia kuongezea mamlaka na nguvu za kiutendaji wa Kamisheni yetu kwa kuifanyia mageuzi ya kimfumo na kimuundo. Tumeibadili Kamisheni kuwa Mamlaka ya Umoja wa Afrika. Uamuzi ule ni hatua kubwa kuelekea kutimia ndoto yetu ya Serikali ya Umoja wa Afrika na Umoja wa Mataifa ya Afrika. Hatuna budi kujipongeza kwa uamuzi ule wa kihistoria ambao unalihakikishia Bara letu umoja na mshikamano.
Mapendekezo
Waheshimiwa Viongozi;
Katika kipindi changu cha uongozi nimejifunza mambo mengi. Yapo baadhi nimeona yakifanyiwa marekebisho fulani fulani yatasaidia kuimarisha ufanisi wa shughuli za Umoja wa Afrika. Naomba niyataje mambo matatu.
Kwanza kabisa, ni suala la nchi ambayo ni Mwenyekiti wa Umoja wa Afrika kutokuwa mjumbe wa Baraza la Amani na Usalama la Umoja wa Afrika naona ni kasoro ambayo hatuna budi kuirekebisha. Bahati mbaya sana bara letu lina migogoro mingi na miongoni mwa mambo ambayo Mwenyekiti wa Umoja wa Arika anajikuta anatumia muda wake mwingi kushughulikia usuluhishi wa migogoro. Katika kufanya hivyo anastahili kufanya kazi na Baraza la Amani na Usalama la Umoja wa Afrika. Inapotokea kuwa nchi Mwenyekiti wa Umoja wa Afrika si mjumbe wa Baraza hilo anaikosa fursa hiyo. Mimi naamini kazi ya Mwenyekiti ya kusuluhisha migogoro ingerahisishwa sana kama ungewekwa utaratibu wa nchi yake kuwa mjumbe wa Baraza hilo. Kama ni mjumbe tayari kwa utaratibu wa kawaida tatizo linakuwa halipo.
Pili, napendekeza tuangalie uwezekano wa kuanzisha utaratibu wa Troika katika mtiririko wa vikao vyetu. Pendekezo langu limesukumwa na ukweli kwamba baada ya kikao cha Wakuu wa Nchi, kikao rasmi anachoweza kukitumia kupata ushauri au kujadili na kufanya maamuzi kwa mambo ambayo lazima Mwenyekiti ashughulikie. Nashauri tuutumie utaratibu huu tumuondolee Mwenyekiti upweke na kumuongezea uwezo wa kutimiza majukumu yake. Vinginevyo anakuwa Mwenyekiti anayepwaya, anayesubiri tu kuongoza vikao viwili cha Januari na Julai na sherehe za ufunguzi wa mkutano huu.
Na la tatu, naomba niwakumbushe tu kuwa utekelezaji wa majukumu ya Uenyekiti wa Umoja wetu ni mzigo mkubwa. Ni vyema tukafikiria namna ya kupunguza mzigo unaobebwa na nchi-Mwenyekiti, hususan rasilimali fedha, wakati wa kutekeleza majukumu yake. Nashauri tuangalie uwezekano wa kutenga fedha maalum kwa ajili ya kugharamia baadhi ya shughuli za Mwenyekiti. Bila kufanya hivyo, tunaweza kukosa mchango wa uongozi wa baadhi ya nchi wanachama, kwa kuhofia gharama kubwa zinazoendana na majukumu ya uenyekiti.
Hitimisho
Waheshimiwa Wakuu wa Nchi na Serikali;
Wakati ninapomalizia Uenyekiti wa Umoja wetu, napenda kwa mara nyingine tena kutoa shukrani zangu za dhati kwa imani na heshima kubwa ambayo mmeonesha kwangu mimi binafsi na kwa nchi yangu. Nimepata faraja kubwa kulitumikia Bara letu la Afrika kwa nafasi ya Mwenyekiti wa Umoja wa Afrika.
Kwa namna ya pekee, naomba niwashukuru nyinyi viongozi wenzangu kwa ushirikiano mlionionesha katika kipindi chote cha uongozi wangu. Naamini bila ushirikiano wenu mafanikio niliyoyataja ambayo tumeweza kuyapata katika mwaka mmoja uliopita yasingeweza kupatikana. Vilevile napenda kuwashukuru viongozi wa Kamisheni ya Umoja wa Afrika kwa ushirikiano walionipatia wakati wa kipindi chote cha uongozi wangu. Namshukuru Mhe. Jean Ping, Mwenyekiti wa Kamisheni, Makamu wake Mheshimiwa Erastus Mwencha na Makamishna kwa ushauri waliokuwa wakinipatia tangu walipochaguliwa katika nafasi hiyo. Naondoka nikiwa na kumbukumbu nzuri ya kufanya kazi na watu makini, mahili na wachapa kazi hodari.
Natoa shukrani za pekee ziende kwa Mhe. Alpha Oumar Konare, Mwenyekiti wa zamani wa Kamisheni kwa kunisaidia katika masuala mbalimbali hususan katika kipindi cha mwanzo cha uongozi wangu. Nilipoanza Uenyekiti wangu yeye alikuwa Mwenyekiti wa Kamisheni mpaka alipoingia Mheshimiwa Jean Ping. Nawashukuru wakurugenzi pamoja na wafanyakazi wote wa Kamisheni kwa msaada waliotoa katika kufanikisha shughuli mbalimbali za Umoja wetu katika kipidi chote cha Uenyekiti wangu. Nawashukuru pia viongozi mbalimbali wa taasisi na asasi za Umoja wetu kwa ushirikiano wao. Naamini ushirikiano mlionipa utaendelea pia kwa Mwenyekiti wetu ajaye ambaye tutamchagua hivi punde.
Kwa kumalizia, naomba wenzangu mnikubalie tutume salamu maalum za pongezi kwa Rais Barack Obama wa Marekani, kwa ushindi alioupata katika uchaguzi uliopita. Tunampongeza kama ambavyo tunastahili kufanya kwa kiongozi yeyote wa taifa lolote ambalo tuna uhusiano nalo mzuri. Lakini pia tunampongeza kwa sababu ya kuwa Mmarekani mwenye asili ya Afrika hususan Kenya. Kwetu sisi ni jambo la fahari na kujivunia. Naomba sasa kwa ruhusa yenu nisome salamu zetu.

Mungu ibariki Afrika!
Mungu ubariki Umoja wa Afrika!

AHSANTENI SANA KWA KUNISIKILIZA

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

Kuna Maoni 16 mpaka sasa

  1. Ikiwa Idi Amini dada alikuwa mbaya kama tulivyofundishwa katika siasa, lakini alikuwa mwenyekiti wa AU. Na ikiwa Amini alishirikiana na Gadafi ambaye ameitwa na mataifa kuwa ni mbaya.

    Je, kweli hawa ni wabaya au tuliwavika ubaya?

    Au ni uzalendo? Maana uzalendo lazima ushabikie nchi yako hata kama ina makosa.

    ReplyDelete
  2. Ah hapo picha imenichanganya kidogo.Kama JK alikuwa anahutubia kwa kiswahili sasa iweje akina Membe waweke hayo madude masikioni kutafsiri lugha?

    ReplyDelete
  3. Mkapa, Richmond: House is all ready

    2009-02-02 10:37:13
    By Guardian Reporter, Dodoma


    The National Assembly resumes today after a weekend recess, with six pending issues for the lawmakers to deliberate on.

    They include the involvement of former President Benjamin Mkapa in the controversial Kiwira coal mine project and the Richmond Development Company emergency power generation contract scam.

    A timetable issued on Friday by the Speaker`s Office shows that the government will give an official statement on the implementation of a legislators` resolution on Kiwira Coal Mine, whose ownership touches the third-phase (Mkapa) presidency and former key cabinet minister Daniel Yona.

    The government is also widely expected to give a statement on the implementation of House resolutions on Richmond Development Company LLC`s.

    Other statements due to be tabled will be on the poor performance of Tanzania Railways Limited (TRL), which is managed by Rites of India, as well as that of the Tanzania International Containers Terminal Services (TICTS), the controversial selling of government houses and the poor management of Air Tanzania Company Limited.

    A number of crucial private motions are lined up for presentation this week, including one by Leader of the Official Opposition in the House Rashid Hamad Mohamed concerning constitutional changes.

    Dr Wilbrod Slaa (Chadema - Karatu) is also expected to present a private motion concerning Home Affairs minister Lawrence Masha`s alleged violation of rules and regulations under the Public Procurement Act.

    Dr Slaa`s motion follows advice from National Assembly Speaker Samwel Sitta last week after the MP said he was not satisfied with Prime Minister Mizengo Pinda`s answers to him during the 30-minute session of the lawmakers` direct questions to the PM.

    Dr Slaa had asked the PM for explanation on Masha`s alleged interference in the tendering process of the national identity cards project.

    SOURCE: Guardian

    ReplyDelete
  4. Wadau naomba msaada kujua kitu kimoja ktk picha hiyo hapo juu. Namuona Membe na Kawambwa wakiwa wamevaa sijui niite mitambo, ni kwa ajili ya nini?Au ndio nyenzo ya kifaa maalumu ktk kutafsiri lugha?Na kama ni kifaa cha kutafsiri lugha, je Membe na Kawambwa hawajui Kiswahili?Maana Ngeleja hajavaa, na hapo Kikwete alikua anahutubia kwa Kiswahili...na hata angehutubia kwa Kiingereza, naamini hawahitaji mitambo hiyo.Nisaidieni wandugu ktk hili. Kama ni mitambo ya kazi nyingine, naombeni mnieleweshe tafadhali.

    MDAU

    ReplyDelete
  5. wewe mtowa maoni wa kwanza umezaliwa lini? umdogo kiasi gani? utasemaje kama idi amin tumemvika ubaya? idi amin kavamia tanzania na kuua watanzania wenzako, watanzania wamepigana vita kuwatowa jeshi la amin nchini tanzania, how dare you kusema kuwa tunamvika ubaya? labda huna ndugu au jamaa aliekwenda katika vita na hakurudi but don't you dare insult some of us ambao ndugu zetu wamepoteza maisha yao kwa sababu za tamaa na unyama wa amin

    ReplyDelete
  6. Hongera Mr President kwa kutumia lugha ya kiswahili. Na hilo liendelezwe kwani inabidi tuikuze lugha yetu katika ngazi za kimataifa. Kiingereza nacho kina umuhimu wake lakini pia tusiache kuipigania lugha yetu.
    Gadaffi naye alichukua madaraka toka sijui 1969 je yeye ni mfano mzuri kwa demokrasia. Pia alimpa Amini silaha atunyuke nazo. Pia watu wake walliangausha ndege na kuua abiria. Hii haijakaa sawa.

    ReplyDelete
  7. asante mzee wa kusafiri mara kushakuwa adid tumia muda wako

    ReplyDelete
  8. afuweni, sasa mheshimiwa JK atatulia nyumbani na kutumia muda mwigi zaidi kuwakabili mafisadi.

    ReplyDelete
  9. JK anahutubia AU kwa Kiswahili lakini Mashaka na wenzie wanawaandikia Waswahili kwa Kiingereza! Jamani kweli kutawaliwa ni kubaya. Ukishatawaliwa basi kitu cha mtu aliyekutawala - iwe rangi ya ngozi yake, dini yake, lugha yake nk nk - vinakuwa bora kuliko vyako weee. Tuadilike jamani. Tuko karne ya 21 sasa. Umeniskia Mashaka na wenzio? Kijaluo (kwako wee Majaluo Mashaka) ni bora kuliko Kiswahili na Kiswahili ni bora kuliko Kiingereza. Ukiwasiliana Wall Street tumia Kiingereza, ukiwasiliana hapa kwenye blog, tumia Kiswahili.

    ReplyDelete
  10. what?
    at last umehutubia kiswahili!
    ngeleja na mwezie na midude yao ni ushamba tuuuu si unajua sometime uzee unapoteza memory kidogo ni kitu cha kawaida,yan ni kama ukifikia menopouse!!hahahaaaa
    gadafi ana jeuri ya pesa na kawanunua AU tu mana utawala wake ni familia yake tu anyway,ilmradi nchi ipo na anaongoza watu.nguvu ya pesa lazima JK achekelee tu.
    wadau hahahahahaaaaa!!!ngeleja na uyo mwingine no kiswahili at all

    ReplyDelete
  11. Inapendeza Mr. president kuongea kiswahili, mbona Waarabu, china etc kwenye mikutano mikubwa wanaongea lugha zao, why not us with Swahili!
    I like that!

    ReplyDelete
  12. CHINESE, RUSSIAN AND ARABIC ARE OFFICIALLY AUTHORISED LANGUAGES IN AN INTERNATIONAL AUDIENCE, HATA HIVYO SI MBAYA KUKIPIGANIA KISWAHILI NI BOMBA SANA HATA VILE KINAVYO-SOUND AND VERY SIMPLE TO UNDERSTAND WITH NO COMPLICATION, KUHUSU HOW AKINA MEMBE KUVAA VIFAA VYA KUTAFSIRIA LUGHA, JAMANI KATIKA PICHA HIYO HAIONYESHI KAMA KIKWETE NDO ALIKUWA ANAONGEA KWA MBELE INAWEZEKANA NI MTU MWINGINE ALIKUWA ANAONGEA, TULIZENI BALL.

    ReplyDelete
  13. Mitambo hiyo inatafsiri kilugha...Kisukuma, nk
    Du kaachia hii sasa sijui nahisi angalau Choo cha ikulu kitatumika!!

    ReplyDelete
  14. Mkutano wa Wakuu wa Nchi za Bara la Afrika umemalizika hivi karibuni na huku Wakuu hao wakiwa hawakukubaliana kuhusu Uundaji wa Serikali ya Umoja wa Afrika!Au hata ile Mamlaka ya Umoja wa Afrika itakayo kuwa tofauti kidogo na AU iliyopo sasa.Hilo lilitarajiwa.Bado ipo kazi kubwa sana ya kufanya miongoni mwa nchi zenyewe za Afrika kabla ndoto hizo za kuwa na serikali moja ya kisiasa ya bara zima la Afrika hazija pewa nafasi yake katika usingizi huu mzito uliotukabili.Lazima nchi za Afrika zikubali kubadilika moja baada ya nyingine.Lazima Bara la Afrika liweke "Viwango vya Ubora wa Aina ya Utawala wa Demokrasia ya Vyama Vingi"ambavyo kila nchi ya Bara la Afrika italazimika kuvifikia na kuvitekeleza.Hili peke yake sio suala dogo.Litahitaji muda mrefu kulifanikisha.Kwa hivi sasa,ni nchi ngapi za bara la Afrika ziko tayari kulitekeleza hilo?Viongozi wangapi wapo madarakani kwa zaidi ya miaka 10?Vyama vingapi vya siasa viko katika Utawala wa Nchi zao kwa zaidi ya miaka 20?Kwa njia zisizo heshimu misingi ya mfumo wa utawala wa demokrasia ya vyama vingi vya siasa?Nchi ngapi barani Afrika hazina Tume Huru za Uchaguzi na Bado zimekumbatia Katiba za Nchi zilizorithishwa toka utawala wa Wakoloni?Ubinafsi,Uchu na Ulafi wa Madaraka bado ni tatizo kubwa katika nchi nyingi barani Afrika.Rushwa na ukandamizaji wa haki kwa raia ni tatizo sugu sana linalo endelea kukumbatiwa na taasisi za serikali zilizopo madarakani.Hiki nacho ni kikwazo kikubwa sana katika kutimiza ndoto hiyo ya kuwepo kwa serikali moja ya bara zima la afrika.Jumuia za Kanda katika bara la afrika nyingi zimekumbwa na matatizo makubwa na hatimaye hazikusonga mbele.Serikali Moja ya Bara la Afrika ianze kwanza kwa Uanzishaji wa serikali moja ya kisiasa kwa kila kanda ya bara la afrika.Serikali hizo za Kanda hazitawezekana iwapo hata huo Umoja wa Uchumi na Soko la Pamoja katika kanda hizo bado imeshindikana.Bado kuna vizingiti vingi vinavyozuia watu wa nchi majirani wasiwe huru kutoka nchi moja na kwenda kuishi na kufanya kazi katika nchi nyingine!Bado tuna kazi kubwa sana tena sana ya kufanya wajomba zangu wa bara la afrika!tusikurupuke kufikiria makubwa wakati hata yale ya msingi kabisa hayaja fanyika au yametushinda!Lakini ukweli utabakia kwamba Kuwepo kwa Serikali Moja ya Bara la Afrika ni jambo linalowezekana kabisa!Na lazima tulifanyie kazi kwa dhati.Kama halitawezekana katika umri wetu basi itawezekana katika kizazi kijacho!Mungu Ibariki Afrika!Kumbukeni Mvua huanza kwa TONE MOJA!ndipo yakaja mafuriko!---tonny----

    ReplyDelete
  15. JAMANI SI MITAMBO INAYOTAFSIRI LUGHA NI MTU YUKO KWENYE CHUMBA FULANI NI MKARIMANI WA LUGHA INAYONGEWA KWA WAKATI NA YEYE HUTAFSIRI KUTUMIA MIKE AMBAYO SAUTI YAKE HUWAFIKIA WAJUMBE KUPITIA HIZO SPEAKER WALIZOVAA MASIKIONI, HIZO NI SPEAKER TU.

    ReplyDelete
  16. weee annon!!acha kutuzuga apa,yan mtu akaaa chumba fulan anatafsiri yooooote ayo wanayoongea apo??
    wee acha izo,,,
    ni mtambo maalum unatafsiri lugha umo ndani (frequency)unabofya frequency inayousu lugha yako then safi...
    SIO MTU WEE ANNON APO JUU

    ReplyDelete

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...