Na Mwandishi Maalum
Rais Jakaya Mrisho Kikwete na wakuu wa elimu nchini wamekubaliana kurudisha, haraka iwezekanavyo, utaratibu wa shule zote nchini kutumia vitabu vya aina moja vya kufundishia, badala ya mtindo wa sasa wa kila shule kutumia aina yake ya vitabu.
Wakuu hao pia wamekubaliana kuhusu umuhimu wa kuleta utulivu katika mfumo wa elimu kwa kuweka mitaala inayoeleweka badala ya hali ya sasa ambako shule mbali mbali zinakuwa na mitaala tofauti kulingana na malengo ya kila shule.
Aidha, wakuu hao wamekubaliana kuwa iko haja ya wasomi na maprofesa nchini kuandika vitabu kwa ajili ya kufundishia katika shule mbali mbali nchini badala ya kazi hiyo kuachiwa watu wasiokuwa na ujuzi wa kutosha wa shughuli hiyo – yaani makanjanja.
Hayo ni baadhi tu ya yaliyokubaliwa katika mkutano kati ya Rais Kikwete na wakuu wa Wizara ya Elimu na Mafunzo na taasisi zake nchini, ikiwa ni mfululizo wa mikutano ya kutathmini utendaji wa Serikali ya Rais Kikwete katika miaka mitatu iliyopita.
Mkutano huo uliofanyika leo, Jumatano, Februari 18, 2009, Ikulu, mjini Dar Es Salaam, umejadili kwa kina athari za kuruhusu kila shule kuwa na aina yake ya vitabu vya kufudishia na kukubaliana kuwa hali hiyo irekebishwe haraka iwezekanavyo.
Rais Kikwete ameanzisha mjadala kuhusu suala hilo kwa kuwaambia wakuu hao wa elimu, wakiongozwa na Waziri wa Elimu na Mafunzo, Profesa Jumanne Maghembe:
“Zamani tulikuwa na sera ya kitabu kimoja cha kufundishia kwa shule zote nchini bila kujali mwanafunzi yuko shule gani, iwe hapa Dar es Salaam, ama Ngara, ama Mbinga. Sasa kila shule inacho kitabu chake cha kufundishia. Hivi tulikosea wapi?”
“Tuwe wawazi na kuambizana ukweli. Hii ni sera yetu ama tumeletewa na mtu mwingine? Na kwa kweli katika hili hatuna sababu ya kumfurahisha mtu yoyote. Lazima tuwe na ujasiri wa kuwakatalia watu katika mambo haya. Kwa sababu hapa tunashughulikia elimu ya watoto wetu. Mimi binafsi naogopa sana, kwa sababu hii kweli ndiyo sera inayotumikia elimu ya watoto wetu kwa ubora zaidi? Hili linatupeleka siko…”
Ameongeza Rais Kikwete: “Tunahitaji elimu iliyo sawa, elimu sare kwa shule zote. Hivi hiki kinatushinda nini kiasi cha kwamba sasa tumeipeleka elimu yetu sokoni ambako kila mwalimu mkuu anajadiliana na mwandishi wa kitabu anayemtaka, ili kununua vitabu kutoka kwake. Hii ni rushwa moja kwa moja, tunatengeneza mazingira ya rushwa kwa kuruhusu jambo hili…give us a break”
Imeelezwa kwenye mkutano huo, kuwa sera ya kuwepo kwa vitabu vya kufundishia vya aina moja iliondolewa mwaka 1992, na kuanzishwa sera huria ya vitabu vingi vya kufundishia, lakini hatua hiyo ilikuwa ya majaribio na ya muda tu.
Baada ya kuwa amesikia hoja hiyo, Rais amesema: “Katika mageuzi yote tuliyoyafanya katika nchi hii, kwenye hilo tumepita mipaka. Kuweni na vitabu vingi, lakini hivi vitabu viwekwe kwenye mkataba. Kitabu cha msingi cha kufundishia kiwe kimoja, sana sana viwili ama vitatu siyo zaidi ya hapo.”
Amesisitiza Rais: “Tuifanyie elimu ya watoto wetu haki. Sioni busara yoyote kwa kila mwalimu mkuu kuchagua aina ya kitabu anachotaka. Sitoi agizo katika hili…mimi nahoji tu busara ya kila mwalimu mkuu kujadiliana na mzabuni anayemtaka. Mwalimu mkuu akibadilika na mzabuni anakadilika na vitabu vinabadilika. Mimi siyo mwalimu, mimi mwalimu tu wa jeshi, lakini sioni busara katika hilo. Yaani sasa imefikia mahali ambako elimu ya watoto wetu kutegemea makubaliano kati ya mwalimu mkuu na mzabuni.”
Mkutano huo pia umekubaliana kuwa athari za kuwepo kwa vitabu vya kufundishia kulingana na uamuzi wa kila mwalimu mkuu katika kila shule, zinajitokeza pia katika utungaji na usahihishaji mitihani nchini.
Kuhusu hoja na haja ya maprofesa nchini kuandika vitabu kwa ajili ya kufundishia, Rais amesema kuwa haoni sababu kwa nini wasomi hao hawaandiki vitabu kwa sababu wao ndizo bongo kali zaidi nchini.
Ameonya kuwa hatua ya maprofesa kutokujihusisha na uandishi wa vitabu vya kufundishia watoto, inakaribisha makanjanja kuingia katika uandishi wa vitabu vya kufundishia nchini.
“Kwa nini uitwe profesa kama hata hawezi kuandika vitabu kwa ajili ya kufundishia watoto wetu…sitarajii kumsikia profesa akilalamikia ukosefu wa vitabu vya kufundishia nchini kwa sababu hilo liko kwenye uwezo wake,” amesema Rais na kuongeza:
“Kazi hii ya uandishi wa vitabu vya kufundishia haiwezi kuachiwa aliyemaliza shule ya msingi, ama sekondari. Haiwezekani mtu wa elimu ya namna hiyo akaandika kitabu cha kufundishia. Kama kitabu cha hadithi sawa…kama riwaya anaweza kuandika mtu yoyote…lakini kitabu cha kufundishia…”
“Mnagingiza ukanjanja katika uandishi wa vitabu vya kufundishia wanetu badala ya kutumia watalaam wetu, wasomi wetu na taasisi zetu kama vile ile ya Taasisi ya Elimu Tanzania.”
Kuhusu haja ya kuleta utulivu katika mfumo wa elimu kwa kuwa na mitaala inayoeleweka na kukubalika, mkutano umekubaliana kulingalia jambo hilo badala ya sasa ambako kuna mitaala ya kila aina kutegemea na lengo la kila shule.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

Kuna Maoni 8 mpaka sasa

  1. kwa mtazamo wangu kwamba tatizo lilikuwepo katika awamu ya tatu ya utawala!!!!!!!!enzi za awamu ya tatu mitaala imebadilishwa sana na walikuwa hawaliangalii hili maana ilifika kipindi masomo kama geography.history,na siasa(civics)yalivunjwa na kuwa somo moja maarifa ya jamii sasa hapo wewe unaona inawezekana kweli kuyaunga masomo yote hayo na kumfundisha mtoto kwa mwaka mzima?si utakuwa unamjaza vitu vingi kwa muda mfupi!!!!namuunga mkono sana kikwete na namuomba afuatilie hilo!!!!inauma sasa hv elimu imeshuka thamani sana hasa elimu ya msingi na sekondari!!!ujue tatizo mkapa alikuwa anamwaga pesa tu bila kuangalia watoto wataathirika vp!!!kweli askari wake wa miamvuli hawakuwa macho kabisa!!!all the best kikwete!!!pia sijailaumu awamu ya tatu ila tu niliona kulikuwa na mapungufu hapo ingawa bado kuna mengi mazuri mliyafanya kwa sekta hii ya elimu!

    ReplyDelete
  2. JK umenena, elimu bora kwa wote bila kujali unatoka ktk tabaka gani la jamii au eneo unaloishi.

    ReplyDelete
  3. Mh. JK na jamaa zako wanaoshughulikia elimu kwanini hamkujadili masuala yanayosababisha migomo ya wanafunzi na mishahara ya walimu?? Au wakati wa kujadili hayo mnaona haujafika? Mnangojea mpaka ma-DC washike viboko ndio muwamwagie unga wao??
    Huyo Prof. Maghembe mwenyewe ameshatunga angalau kitabu cha vichekesho?
    Je mmejiuliza wale wa shule ya St.Francis wanatumia vitabu gani na wanafanya mitihani ya Baraza gani la Mitihani?
    Nami nilikuwa naongeza chachandu kidogo katika suala hilo la elimu.

    ReplyDelete
  4. elimu ya siasa ni ya nini mashuleni. hayo yalikua mambo ya ujamaa. ujamaaa tumeuacha hata china na urusi zinauacha. toka lini masoma ya history, geography na siasa yakawa kitu kimoja. vitu kama hivi ndio vilidilute masomo yetu. namna hii inafanya vigumu wanafunzi kulijua somo vizuri. raisi tafadhali ifanya elimu yetu iwe strong. haina faida kwa watoto wengi kwenda shule na wote kumaliza shule bila ya elimu ya kutosha.

    ReplyDelete
  5. kabla ya kufanya uamuzi wa kubadili vitabu vya shule nashauri kwanza wadau wa elimu wakutane na waajiri kutoka sekta mbalimbali ili kujadili na kukubaliana: ni elimu ya aina gani inafaa Tanazania? Je, elimu tunayoitoa hivi sasa inakidhi mahitaji ya soko na nchi kwa ujumla? Je, inasaidia kubadili ama kuboresha maisha ya wanaohitimu? inaendana na mazingira yetu? Walimu tulionao wanamsaidiaje mwanafunzi kukabiliana na maisha yake? Walimu wenyewe wameiva? Ufundishaji ukoje? Bila kufanya tathmini nachelea kusema kuwa tutaendelea kubadili vitabu hadi mwisho wa dunia na hatutakuwa na mabadiliko!

    ReplyDelete
  6. SIKUBALIANI NA MKUU KUHUSU MAPROF KUTOANDIKA VITABU, SERIKALI NDIO CHANZO CHA MATATIZO HAYO. WAJARIBU KUWAFADHILI WAANDISHI WA VITABU NDIO TUZUNGUMZE KAMA KWELI HAWAWEZI.COPYRIGHT & TRADEMARK IS NOTHING IN Tz.hata ukiandika kitabu NI HASARA TUPU KWA MWANDISHI.AU MNANGOJA NYAMBARI NDO AWAFADHILI WAANDISHI?
    INASIKITISHA SANA KUONA MKUU ANAONGEA BILA KUFANYA UTAFITI WA KINA

    ReplyDelete
  7. Nashukuru sana kwamba suala hili la Mitaala ya Elimu na Vitabu vya Kufundishia limeibuka hivi sasa katika kikao hicho cha Rais Kikwete na Wahusika Wakuu wa Masuala ya Elimu nchini,hususan baada ya matokeo mabaya na yasiyo ridhisha ya Kidato cha Nne ya hivi karibuni.Kuna shule zilizofanya mitihani tofauti katika somo lile lile moja,kwa mfano Geography!eti ilipogundulika tu imevuja katika shule fulani palikuwepo na Paper B ya somo lile lile iliyotolewa badala yake.Hilo ni kwa mitihani tu.Lakini katika usahihishaji,wanafunzi wote watapimwa sawasawa kama vile wamefanya mtihani mmoja!This is not fair to the students.Kuna Madudu mengi sana katika Mfumo mzima wa Elimu hapa nchini.Siyo rahisi kuyataja yote hapa.Ninacho omba hapa Kauli ya Kikwete ichukuliwe kama "AGIZO na siyo OMBI" kwa watendaji wote wakuu wa sekta ya elimu nchini.Uovu huu umekuwa ukiendelea hapa nchini kwa kipindi kirefu lakini hakuna aliyejali kwasababu wakubwa wengi wanasomesha watoto wao nchi za nje!Kwamba Kikwete hili kaliona na kathubutu kulikemea ni hatua moja kubwa.Lazima Pawepo na Kitabu Kimoja Maalum cha msingi cha Kufundishia kwa kila Somo na kwa kila ngazi ya Darasa kwa shule zote hapa nchini zilizo jiandikisha kufanya Mitihani ya Baraza la Mitihani la Taifa chini ya Mitaala ya Elimu iliyothibitishwa na Waziri wa Elimu nchini.Wizara ya Elimu isifanye mchezo katika hilo.Tuna pesa nyingi za kuchezea katika semina elekezi lakini hatuna pesa za kuwaweka Walimu Bora kabisa katika somo kambini wakapata wasaa wa kuandaa Mitaala ya kila somo kuanzia darasa la kwanza hadi chuo kikuu,na kisha wakatunga vitambu maalum vya kufundishia kwa kila somo na kwa kila ngazi ya darasa.Hebu tuangalie vitabu vinavyotumika kwa wenzetu nchini Uganda na Kenya bila ya kwenda mbali sana kama Uingereza na Mareakni!Tanzania tunatia aibu,tena sana!Kuandika Vitabu bora na vya uhakika vya kufundishia ni jambo linalo wezekana sana tena sana!Kwanini tunachezea Taifa letu la kesho?Kwanini watu binafsi wasio na uwezo mkubwa wa kuandika academic books waachiwe jukumu hilo kwa kisingizio tu cha uchumi na sosko huria?Je,ni madhara kiasi gani tayari tumesha wasababishia watoto wetu waliofanya mitihani yao katika miaka michache iliyopita?Vitabu mbali,bado suala la jinsi ya kuwapima na kuwatathmini wanafunzi uwezo wao kitaaluma!Je,ni busara kuendelea kutumia mtihani wa mwisho tu peke yake kama kigezo tosha cha kumpima mwanafunzi iwapo amefuzu somo husika na hivyo kustahili kuendelea na ngazi za juu zaidi katika sosmo lile?Jamani,hata hili nalo tusubiri ushauri kutoka IMF? Nafikiri,wakati sasa umefika tubadilike.Hakuna kubembelezana katika hili.Lazima watu sasa wawajibike kwa matokeo ya utendaji wao katika nafasi zao za kazi wao kama watendaji na wasimamizi wakuu!Katika hilo tusingependa kumwona Rais Kikwete akibembeleza mtu,this is serious!Katika hili Rais Kikwete upo katika mstari ulio sahihi kabisa,hutakiwi kuwa mwoga katika kutoa Maagizo na siyo Maombi!Rais haombi kitu bali anaagiza!Baada ya yeye mwenyewe kulifanyia jambo utafiti wa kutosha na kuridhika na kile atakacho kiagiza kwamba kitakuwa sahihi.Waalimu wengi sana tunao wajua wamenufaika sana kujitajirisha kwa kuutumia mwanya huo wa kila mwalimu mkuu kujichagulia aina ya vitabu atakavyopenda kuvitumia katika kufundishia.Na baya zaidi,vitabu vingi vilikuwa havinunuliwi na kupelekewa wanafunzi mashuleni.Hili liligeuzwa kuwa Dili kati ya Mwalimu Mkuu wa shule na Muuzaji Vitabu na Mchapishaji!Hili limekuwepo hapa nchini kwa kipindi kirefu sana.Lakini cha ajabu viongozi wa juu wizara ya elimu walilifumbia macho.ULAJI!Wizara ya Elimu sasa ipange Ratiba ya jinsi ya kulishughulikia suala hili mara moja na siyo kesho!we will be following it up very closely.---concerned parent--

    ReplyDelete
  8. kwanza sylabus iwekwe wazi kwa kila mhusika. halafu mwalimu mkuu aamue kutokana na sylabus atumie kitabu/vitabu gani kufundishia.

    ReplyDelete

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...