JK akiwasili mahakama kuu kuhudhuria sherehe za siku ya sheria leo hapa dar. Shoto kwake ni Jaji Mkuu Mh. Augustine Ramadhani na kulia kwake ni mwenyekiti wa chama cha wanasheria dk. twalib akifuatiwa na Spika Mh. Samwel Sitta.
JK akipozi na majaji wa mahakama kuu (waliosimama nyuma) akiwa na Jaji mkuu Mh Augustino Ramadhani, Spika Samwel Sitta, Waziri wa Sheria Mh. Mathias Chikawe na Majaji wa Mahakama ya Rufaa.
JK akila pozi na wafanyakazi wa mahakama kuu
JK akiwa na majaji wa mahakama ya rufaa
JK akiwa na majaji wa mahakama kuu
JK na viongozi wa sheria na mahakama wakipozi na
viongozi wa vyombo vya ulinzi na usalama waliohudhuria
JK na viongozi wa sheria na mahakama akipozi na majaji wastaafu
JK na uongozi wa mahakama akipozi na viongozi wa vyama vya siasa waliohudhuria sherehe hizo
'Asante JK kwa kutoingilia uhuru wa mahakama'
Na Mwandishi Maalum
MAJAJI na mahakimu wa Tanzania wamempongeza Rais Jakaya Mrisho Kikwete kwa kutokuingilia uhuru wa mahakama, hata mara moja, iwe kwa matendo ama kwa kauli, katika miaka mitatu ya uongozi wake.

Majaji na mahakimu hao wamesema kuwa tabia hiyo ni tofauti na ile ya baadhi ya viongozi wakuu wa Tanzania waliomtangulia.

Pongezi hizo zimetolewa leo, Ijumaa, Februari 6, 2009 na Jaji Mkuu wa Tanzania, Jaji Augustino Ramadhani wakati wa sherehe za Siku ya Sheria ambayo huanzisha rasmi shughuli za Mahakama kila mwaka nchini.

Katika sherehe hizo zilizofanyika Makao Makuu ya Idara ya Mahakama, Dar Es Salaam, na kuhudhuriwa na Rais Kikwete mwenyewe, Spika wa Bunge la Jamhuri la Tanzania Samwel Sitta na wakuu wa vyombo vya ulinzi na usalama nchini, Jaji Mkuu Ramadhani amemwambia Rais Kikwete:

"Awali ya yote, nachukua nafasi hii kukiri kwa dhati kuwa kwa muda wote huu wa miaka mitatu na ushei ya uongozi wako, Mheshimiwa Rais, hujaingilia mahakama kwa matendo na hata kwa kauli."

Ameongeza Jaji Mkuu: "Hivyo ndugu zangu Maji na mahakimu tumpongeze kwa kishindo Mhe Rais kwa kuwa muumini na kielelezo cha kuheshimu dhana ya mgawanyoÚwa madaraka kwa vitendo na kauli. Mheshimiwa Rais, asante sana." Kauli hiyo ilipokelewa kwa makofi ya pongezi.

Katika kauli inayoonyeswa uwazi mkubwa, Jaji Mkuu ameongeza kumwambia Rais Kikwete: "Waliokutangulia waliwahi kuteleza na kuvunja mwiko huo. Lakini hatuwazungumzii hao na isitoshe, yaliyopita si ndwele."

Katika sherehe ambazo kaulimbiu yake ilikuwa "Nafasi ya Mahakama katika Kutekeleza Shughuli za Mamlaka ya Nchi na Dhana ya Mgawanyo wa Madaraka", Jaji Mkuu pia alieleza jinsi ambavyo Bunge limepata kuteleza katika utekelezaji wa dhana ya mgawanyo wa madaraka kati ya mihimili mitatu ya dola.

"Kwa bahati mbaya, kaka yangu Mhe Spika mara moja tu alighafilika na akatoa matamshi kuhusu sakata la mafuta ya petroli huko Morogoro pale amri ya EURA ya kuvifunga vituo kadhaa vya mafuta ilipositishwa kwa muda na Mahakama ya Hakimu Mkazi. Kauli hiyo ingetolewa ndani na wala sio nje ya Bunge ingekuwa stahili yake."

Ameongeza Jaji Mkuu huyo kuhusu Bunge: " Kwa upande mwingine Bunge liliwahi kutaka liwe na madaraka ya kimahakama dhidi ya watu ambao wanazozana na Waheshimiwa Wabunge. Kwa bahati nzuri wazo hilo halikufanikiwa."

Ameongeza: "Lakini bado Bunge lilichukua kazi ya Mahakama na kusikiliza tatizo kati ya Mhe Malima na Bw. Mengi ambaye si Mbunge."

Wakati huohuo, Jaji Mkuu wa Tanzania ameonya kuwa vyombo vya habari vimeanza kutishia uhuru wa Mahakama nchini kwa kushindwa kutofautisha ukweli (facts) na maoni.

Jaji Mkuu huyo pia amesema kuwa uhuru wa Mahakama pia unatishiwa na mwenendo wa baadhi ya watu ndani ya jamii ya Tanzania, ambao wamejipachika mamlaka ya kushinikiza mahakama kwa kuwahukumu watu ambao hata hawajafikishwa mahakamani.

Jaji Mkuu huyo ametoa tahadhari hizo leo, Ijumaa, Februari 6, 2009, wakati anazungumza katika Siku ya Sheria nchini, sherehe ambazo huashiria kuanza rasmi kwa shughuli za mahakama kila mwaka.

Katika hotuba yake kwenye sherehe hizo zilizofanyika Makao Makuu ya Idara ya Mahakama na kuhudhuriwa na Rais Jakaya Mrisho Kikwete, Jaji Mkuu huyo amesema: "Hivi karibuni limezuka tishio dhidi ya uhuru wa mahakama kutoka Mhilimi wa Nne wa Dola, kama vyombo vya habari vinavyojiita.
Vyombo hivyo havitofautishi kati ya ukweli (facts) na maoni. Baadhi ya vyombo huandika maoni kana kwamba ndio ukweli wenyewe na hii hupotosha wananchi na athari iletwayo haitibiki hata kwa shubiri."

"Kwa mfano, Mhe Rais, mgomo wa walimu ulipigwa marufuku na Mahakama Kuu Divisheni ya Kazi. Uamuzi huo ulifikishwa Mahakama ya Rufani ambayo iliona suala hilo halikuwa limewasilishwa kihalali mbele ya Mahakama Kuu," ameongeza Jaji Mkuu.
Alifafanua: "Hivyo shughuli yote mbele ya Mahakama Kuu ilifutiliwa mbali. Magazeti mengi yaliandika vichwa vya habari kuwa Mahakama ya Rufani imebariki mgomo. Mahakama ya Rufani haikuamua hivyo. Nilimtuma Msajili wa Mahakama ya Rufani atoe maelezo sahihi."
Kuhusu tishio kutoka kwa umma.
Jaji Mkuu amefafanua: "Tatu, mahakama inapaswa kuwa huru na umma ama sehemu ya umma. Hitajio hili nalo ni muhimu sana. Wananchi wanaweza wakaamini mshitakiwa ni mharifu kumbe Mahakama ikamuona siyo."
Ameongeza: "Sasa mahakama isishinikizwe kumtia hatiani mtu ambaye hana hatia. Uhuru huu ni muhimu sana katika nyakati kama hizi za tuhuma zilizo kithiri za ufisadi ambapo baadhi ya wananchi tayari wamekwisha watia hatiani baadhi ya watuhumiwa hata kabla ya kufikishwa mahakamani."
Jaji mkuu pia ameorodhesha mambo mengine yanayoathiri uhuru wa mahakama na kukamisha utendaji bora zaidii yakiwamo mahitaji ya chombo hicho muhimu katika utawala wa nchi.

Rais Kikwete ambaye alikuwa anahudhuria sherehe hizo kwa mara ya pili tokea kuingia madaraka ameoamba kuzungumza kidogo kwenye sherehe hizo, hata kama kwa jadi, kazi yake huwa ni kusikiliza tu na kuiachia mahakama kuongoza ajenda yake yenyewe.

Katika salamu zake fupi, Rais Kikwete ameahidi kuwa atayashughulia matatizo ya mahakama yanayohitaji msukumo wa Serikali, na kuahidi kuwa Bajeti ya Mahakama haitapungua hata kama mapato ya Serikali yameanza kuathiriwa na Zahama ya Kifedha inayoikabili dunia.









Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

Kuna Maoni 5 mpaka sasa

  1. Mbona Mh. Lawrence Masha amesahauliwa hapo mbele jamani?

    ReplyDelete
  2. Kwa sheria zipi basi!!kwani hivi nchi hii nayo pia ina sheria??SHERIA AU SHURUA??mafisadi hamna hata mmoja ambae kahukumiwa yupo jela wanapokewa tu majimboni mwao kwa vigelegele na vifijo.bungeni wanakwenda kuhongwa MASHANGINGI NA POSHO,KAZI KUSINZIA TU NA KUMWAGA UDOVUO.HAWA WAPIGA KURA WA BARIADI(CHENGE)MONDULI(LOWASSA)HAWA WALITAKIWA WAKATIWE HUDUMA ZOTE ZA MUHIMU IKIBIDI WAFE NA NJAA TU KWA KITENDO CHAO CHA KUWAPOKEA MAFISADI MAJIMBONI MWAO KWA SHEREHE.HUYU CHENGE NAONA SERIKALI IMEBANA SEHEMU ZAKE ZA SIRI ILI WATU WASAHAU.NA WEEE MICHUZI ISSUE KAMA HIZI ZA CHENGE UNAZIOGOOOOOPA NDIO MAANA WADAU WANASEMA BLOG INAPOTEZA MWELEKEO PICHA KIBAO ZA KATUNI TU

    ReplyDelete
  3. ni kweli annon wa pili,,,
    yani ushahidi wa mafisadi "haupatikani" na ina maana watakua huru soon,afu eti adi mtu ahukumiwe laa anaitwa "hajashtakiwa" na bado wapo bungeni na ni wabunge kama kawaida,jamani mbona nchi zingine watu kawa awa wanaotuhumiwa kuhujumu uchumi WANAKAA KANDO KABISA YANI OFISI ADI SIASA WANASIMAMISHWA KABISAAAAA ADI KESI ZIISHE NA ITAMKWE RASMI WAKO CLEAN THEN WAANZE KUGOMBEA UPYA WANANCHI TUKIWATAKA TUWACHAGUE LAAA WAKAE KANDO,,,yani adi mtu inaandikwa kabisa wazi ana vijisent new jersey eti adi ushahidi,UPIIII??
    sheria za nchi hii hazijatulia na ao woooote apo waoga tu na wamenunuliwa!!
    michu post hii

    ReplyDelete
  4. Ndugu Balozi Michuzi,

    Tunafahamu kuwa Serikali inatembelea blog yako. Tunaomba kwamba muda umefika wa serikali kuruhusu sheria ifanye kazi yake bila ya kuingiliwa. Kuna watu wengi wameiba serikali ya sasa na iliopita lakini bado wako huru. Tunataka pesa zetu zirudishwe au itakuwa vichekesho tu na sheria zetu. Wananchi tumechoka kudanganywa.

    Pili, karibu miaka 20 imepita tangu Tanzania iwe na uhuru kamili wa siasa na wa kibinadamu. Wananchi wengi bado wanateseka wakienda mahakamani kuomba haki zao. Serikali inanunua magari ya mamilioni, lakini haiwezi kununua viti vya elfu tano ili wananchi waweze kukaa kusubiri hakimu au kusikiliza kesi za ngugu zao mahakamani. Kesi zinachukua miaka kusomwa na kutoa hukumu. Kesi ambapo wenzetu wanachukua miezi miwili au mitatu, sisi tunachukua miaka mitano au zaidi. Serikali lazima iwafukuze mahakimu wanaochukua rushwa pamoja na maofisa wa mahakama,ambao wanakula pamoja na hakimu. Si haki mtu kukaa jela miaka mitano au zaidi kusubiri hukumu, jela singekuwa na nafasi kubwa kama watu wangepewa hukumu za nje au walazimishwa kufanya kazi kama kusafisha mazingira kwa makosa madogo madogo na kuacha nafasi kwa kezi kubwa kama za ujambazi na wizi wa mali ya Umma.
    Wananchi wengi wananyima haki zao kila siku na ndio maana wanachukua sheria mikononi mwao. Tunataka serikali ionyeshe kuwa inaheshimu haki ya binadamu, sisi wananchi hatudanganyiki tena, wazungu wanasema " Action speaks better than words".

    Nawasilisha.
    Aluta Kontinua

    ReplyDelete
  5. Ukiufuatilia ule waya uliotoka kwenye Bomu uufukue polepole hadi ulioelekea bila shaka utakibaini Kitufe cha Kulipulia lile Bomu amekishika nani au kipo katika uwanja wa nani!Wanasiasa wa Nchi hii tokea awali walijenga uswahiba wa karibu sana na wenzao walioihitimu katika Sheria!Siasa na Sheria vikawa Pete na Chanda!No Doubt where we are now!Wale walioshindwa somo la Uchumi ndio waliokimbilia Siasa.Kwa maana hiyo wanasiasa na Wachumi(siyo wale kanyaboya au ndumilakuwili)wakageuka paka na panya!No wonder where we are now!Things moving in the opposite direction of the obvious.Kama tutataka kuanza na mwanzo mzuri na kujenga mwelekeo thabiti kwa faida ya vizazi vijavyo Lazima kwanza tuanze kwa kuubomoa USWAHIBA HUU na kuweka misingi imara na ya uhakika ili kulinda mustakabali wa Taifa letu.Watu wakali hawataki Katiba iliyopo isiguswe!Why?You now have the answers.Watu hawataki Status Quo iwe challenged!Why?Now you have the answers!Ukizungimzia Tume Huru ya Uchaguzi kwa nia safi kabisa,tayari umeshaonekana mpinzani na huna nia njema na nchi yako!Why?Now you have the answers!Huku ni kujidanganya.This is short term.Hakuna Kitu Duniani Kisichobadilika!Mungu ndivyo alivyo umba!Ni yeye tu asiyebadilika!

    ReplyDelete

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...