DECI TANZANIA NI MFANO WA PONZI SCHEME?
KILIO KINGINE KWA WALALAHOI?
Na Waziri W. Kindamba, London
Nianze makala yangu ya leo kwa kumnukuu mwanazuoni na mwanafalsafa aliyetukuka marehemu mzee Shaaban Robert aliyepata kusema “Sitachelea kusema ukweli kwa hofu ya kutengwa na marafiki”.
Mwanafalsafa mwingine alipata kusema anayeona maovu au dhulma katika jamii yake na asiyaseme nae pia anakuwa ni sehemu ya uovu huo.
Mwanasiasa machahachari na mbunge wa Kigoma Mh. Zito Kabwe alikwenda mbali zaidi na kunena si lazima yawafurahishe wengi yale yanayostahili kutendwa na kusemwa kwa haki na ukweli kwa maslahi ya Taifa na umma wa Tanzania.
Mengi yamesemwa kuhusu DECI Tanzania (Development Entrepreneurship Community Initiative), mradi uliojizolea umaarufu kupita kiasi nchini kwa kuwapa mavuno yasiyomithilika wanachama wake kwa kipindi kifupi na kwa kiasi kichache unachowekeza kwa kuvuna faida kubwa ya ajabu.
Tunaambiwa wenzetu hawa wanatoa faida ya zaidi ya asilimia 150 kwa kipindi cha miezi minne bila ya kueleza kwa kina mzungusho huu unakwendaje na kujenga mantiki katika akili ya wanazuoni wetu wa masuala ya uchumi na fedha
Naandika makala hii si kutoa hukumu kwa ndugu zetu hawa wa DECI kwamba ni wa kweli au la katika mradi wao huu, bali kutoa angalizo kwa serikali, vyombo vya usimamzizi wa fedha haswa Benki kuu (BOT) na vyombo vya usalama nchini na wananchi kwa ujumla.
Angalizo hili ni juu ya mfanano wa mradi huu wa DECI na miradi mengine ya kitapeli inayofanana nayo haswa PONZI SCHEME ambayo imetokea nchi mbalimbali duniani na hata hapa nyumbani yaliwahi kujiri haya.
Ni wangapi kati yetu ambao wamesahau kile kilichopata kuitwa UPATU, mradi ambao uliwahusisha hadi wake wa vigogo kadhaa serikalini na ukaja kudondoka ukiwaacha maelfu ya walalahoi mama zetu,dada zetu na shangazi zetu wauzao vitumbua na chapati katika hali ya mashaka na wengine wakilia kilio cha kusaga meno kwa kutopata kile walichokitarajia na wengine kuwa katika hali ya kutaka kujiua kutokana dhuluma ile waliyofanyiwa.
Angalizo ninalolitoa leo ni kuhusiana na kubadlishwa kwa majina ya miradi hii ya kitapeli yenye lengo la kuwalaghai watu ili waingiae wazimawazima lakini ipo siku moja itaanguka na kuwaacha mamia ya walalahoi wa Tanzania wakilia kilio kilicho kikuu. Wamesema waswahili mchele mmoja, mapishi yako ya namna mbalimbali, na ndivyo watu wanvyokuja na majina lukuki lakini ni walewale.
Twayyibu watakuja manabii wa uongo na majina mbalimbali ya utapeli wa namna hii lakini ukiwachungulia kwa makini na kwa utulivu mkubwa utakuta ni walewale; yapo majina kama Pyramid scheme, Bubble scheme, Robbing Peter to Pay Paul n.k na majina mengi mazurimazuri ili kuwavutia wawekezaji ambao ni wavuja jasho wanaohangaika usiku kucha ili wachunwe kirahisi .
Labda kwa ufupi niweke hadharani ni nini hii PONZI SCHEME?
Ponzi scheme ni mfumo wa kitapeli ambao huwalipa wawekezaji wake (i.e wapandaji) malipo makubwa baada ya muda mfupi bila ya kuwapo maelezo ya kutosha yanayojitosheleza ‘wapi pesa hizo zimewekezwa kutoa faida kubwa kupita kiasi’.
Katika lugha ya wenzetu na wachambuzi wa masuala ya jinai katika fedha wanasema “Ponzi scheme is purely a fraudlent operation which intends to deceive the members who are promised huge lump sum returns with no economic sense at all’.
Pesa anazolipwa muwekezaji au mpandaji ni zao la wapandaji wengine ambao ipo siku moja wapo watakaokosa kulipwa kutokana na kukosekana kuongezeka kwa wanachama wapya wa kutosha au pale vyombo ya kiserikali vitakapoushukia mchezo huo mchafu na kuwatia kitanzini wahusika wakuu ambao hata watakapobanwa hukosa maelezo ya kutosha kuwashawishi wasimamizi wa fedha na serikali wapi ilipo miradi yao inayotoa faida hiyo nene.
Ni ukweli usiofichika pia kwamba ili kuweza kuanzisha mradi wa nanma hii wahusika wake walikuwa na kiasi fulani cha fedha ambacho walikitumia kuwalipa wanachama wao wa mwanzo. Kianzio hiki inawezekana kinatokana na vyanzo mbalimbali ambavyo ni halali au sio halali ikiwemo mikopo kutoka katika benki au vyombo vingine vya fedha..
Kama nilivyosema hapo awali miradi ya namna hii mwisho wake mara zote si mzuri ‘There is no happy ending’ kwa maana itafikia wakati kiasi cha pesa wanacholipwa wanachama huwa ni kikubwa kwa ujumla wake ukilinganishwa na kiasi ambacho wananchama wapya wanachangia kwa ujumla wao.
Kihistoria mradi wa Ponzi ulipata jina hilo toka kwa muasisi wake Bwana Charles Ponzi, tapeli la kutupwa lililohama kutoka nchini Italia kwenda Marekani mwaka 1903 na huyu alijulikana kwa umaarufu na utajiri wake kutokana na utajiri huo wa fedha nyingi alizojikusanyia kutoka kwa wanachama wake wa mradi huo mchafu.
Miradi hii ili ikubalike kirahisi katika jamii na kuungwa mkono wahusika wake kwa kiasi kikubwa hujitahidi sana kuwashirikisha watu wanaoaminika katika jamii kama vile wachungaji, mashekhe na viongozi wengine wa kidini, pia huwashirikisha wanataaluma kama vile madaktari, wafanyakazi wa benki na hata wanasiasa ili mradi tu wapate watu wanaokubalika na kuheshimika katika jamii na wao kufaidika na ushawishi wao. Maana ni vigumu kwa mfano ukiona kiongozi wa kidini ni mshiriki akili ya kawaida kukunbali kwamba kuna mchezo mchafu uliopangwa na wahusika..
Vinara wa mpango huu mchafu hujificha kwa ustadi mkubwa nyuma ya pazia la makundi ya watu hawa wenye ushawishi na nguvu kubwa katika jamii pasi na makundi hayo kujua au pengine kwa kujua kwamba wanatumika kama chambo cha kuwavuta wanachama hao katika mtego huo na wakishanasa mtegoni, mtego unateguka na unakuwa ni sawa na ule mchezo tuliopata kucheza utotoni wa ‘sadaka kalawe amina, mwenye kupata kapata na mwenye kukosa kakosa’ na waliokosa wanabaki na majuto ya milele.
Ndugu zetu wa DECI wanayo maswali mengi ya kujibu kwa wananchi wenzao au kwa serikali na vyombo vyake vya usalama na vya usimamizi wa fedha kama BOT ni kwa namna gani au kwa miradi ipi wanayowekeza na kuweza kutoa faida hiyo kubwa kwa muda mfupi.
Najua wapo watakaonihoji kwamba itawezekana vipi kuweka siri ya biashara zako wazi maana washindani wanaweza kutaka kuiga ili wakupiku. Basi kama hivyo ndivyo basi ndugu zetu wa DECI wakaweke wazi utendaji wao huo kwa BOT au Usalama wa Taifa ambao naamini inao wataalamu wa masuala ya fedha kuweza kubaini aina yeyote ya ubabaishaji.
Kama nilivyodokeza hapo juu maswali ya kupambanuliwa na ndugu zetu wa DECI yanaweza kuwa mengi lakini kwa kuanzia;
- Wapi wanawekeza mbegu zinazopandwa na wanachama kuweza kutoa faida nene kwa kipindi kifupi na wachumi wetu na wataalamu wa fedha wazipime hoja zao na kuona kama zinajitosheleza kutengeza mantiki kiuchumi.
- Tumeambiwa sasa ndio wanasaka leseni BOT ili waweze kwenda na sheria na taratibu zilizopo, je kwa nini hawakuwa wanafanya shughuli zao kwa mujibu wa sheria na kanuni hizo zilizopo toka mwanzo? Je, si kwamba hapo kapo kaharufu kanachonuka kuashiria kwamba kipo kiwingu kikubwa cha mizengwe na giza nene? Na haswa kwamba wameshaweza kukusanya ushawishi mkubwa wa walalahoi na kuufanya pia kuwa ni mtaji wao; Maana tunaishi katika ulimwengu wa nguvu ya ushawishi hata kama mantiki haipo.
Nimalizie makala yangu kwa kutoa angalizo kwa Watanzania wenzangu maana kukumbushana ni wajibu “Hakuna mafanikio ya kweli na ya kudumu yatakayokuja kwa njia ya mkato-mkato” wenye kusema walishasema “No Pain, No gain”.
Tafakari
Niandikie:


Kindamba tunashukuru kwa kutuhabarisha, hata hivyo hamna mpya hiyo habari na maelezo kama yako yalishaandikwa mara nyingi tu, ulichokifanya ni plagiarism, copy and paste na hata haujasema au haujafanya citation kana kwamba hiyo ni kazi yako mwenyewe.
ReplyDeleteUlipaswa useme chanzo cha habari yako na wala sio kuonyesha kuwa ni mawazo yako binafsi. Angalau basi ungefanya conclusion ili tupate mawazo yako kuliko kutafsiri kutoka wikipedia bila ya kusema kuwa umepata wikipedia.
Pia jaribu kuepuka kutumia official email ambayo haihusiani na habari uliyotuma, ungekuwa unatangaza chuo chako tungekubalina na wewe kwa ktutumia hiyo email otherwise huo ni utovu wa nidhamu na mwajiri wako anaweza kukuwajibisha kwa ku missuse huduma za kiofisi.Otherwise ninashukuru kwa mchango japo wa kukopi.
Wabongo bwana...lazima wakosoe, ndiyo maan mnatapeliwa, ujuaji mwingi sana nyie..sasa ndugu yetu kindamba anajaribu kutusaidia, anatokea mpumbavu mmoja anajaribu kujifanya mjuaji...kindamba, wee waache tu wabongo, too much know !!
ReplyDeletemhhhhhh kweli wadau wanafuatilia copy and paste is dishonest right? Nakubaliana na comment ya mdau wa 10:59, cite dude!!!!
ReplyDeleteBy the way mama yangu alikumbwa na mkasa huu wa DECI likini alichomoka mapema baada ya kupata mshiko wake! Ilikuwa hivyo baada ya kuniambia na mimi kwa kumjua Madoff nilimuonya!!
Mzee Kindamba nimekusoma 'Loud and Clear' usiwahofu 'Haters' maana wao kazi ni kukosoa hata pale pasipostahili kukosolewa.
ReplyDeleteKwa kuwa ulikuwa unajaribu kutoa mfanano wa DECI na Ponzi basi ni lazima ungegusa source zingine kama website, vitabu au journals,haliepukiki hilo, si vibaya ungewawekea source kama huo ndio ugomvi ulipo, lakini ktk academia umefanya kazi njema umeisoma ishu ukaipresent kwa uelewa wako na kwa mazingira ya Tanzania, JOB DONE Excellently na tumeshaona MH Pinda na serikali wamewashtukia ama kwa effort za watu wa aina yako au wadau wengine.
Usijibishane na watu wenye bifu watakupa presha bure, badala ya kujadili ishu wanajadili mtu, hivyo ndivyo baadhi ya akili za watu zilivyo. Keep up with the good work and all the best.
Ndugu zangu mara nyingi kama si zote kila kinachotokea leo huwa kilikuwapo tangu siku nyingi saaaana tuu Hebu kumbuka kuhusu DECI na linganisha na stori hii ya abunuasi Tangu kale tuu wakati hata elimu hii ya leo haikuwapo hivyo.Nalisoma kitabu cha abunuasi siku nyingi sana nikiwa shule ya msingi ambacho niliwahi kusikia umbeya mitaani wakisema ati kilipigwa marufuku kusambazwa tena mitaani hadithi yenyewe ni hivi. Abunuasi alikuwa na sherehe na alihitaji sana sufuria kubwa kwaajiri ya kupikia katika sherehe hiyo akaenda kwa jirani kuazima sufuria hiyo kwa makubaliano ya kuirudisha baada ya matumizi, sasa ikaja siku ya kurudishiana sufuria ile Abunuasi akairudisha ikiwa na nyingine ndani yake mkopeshaji akauliza mbona unarudisha sufuria mbili wakati uliazima moja? bila shakha Abuanuasi kajibu sufuria yako uloniazima imezaa hivyo nikaona si mbaya nije na mtoto bila kukuficha jirani yangu mwema, nae jirani bila kuuliza alishukuru kwa kuletewa uzao wa sufuria yake na kuahidi kumuazima tena wakati wowote akihitaji sufuria. siku nyingine akaenda kuazima sufuria nyingi zaidi kwa ahadi ya kuzirudisha tena lakini safari hii hakurudisha hata mpaka jirani akajiuliza vipi mbona Abunuasi harudishi vitu vyangu?, akaamua kumufuata hapo kwake kuulizia kuhusu sufuria yake, hali aliyo mkuta nayo alisikitisha alikuwa mnyonge akaulizwa vipi mbona kimya Jibu lilikuwa rahisi tuu kwamba sufuria zake zimekufa zote na amezika ana majonzi kweli kwa kufiwa na sufuria zile.Sasa ndugu zangu watanzania unawezaje kupokea hela eti ulipanda na imeota na kuzaa bila kuuliza hele hiyo imepandwa shamba gani na lini ilizaa na kutoa mavuno ya ghafla namna hiyo kama si kuja kuambiwa mbegu hizo mzopannda hazikuota wakla kuzaa ni nini? kazi kwenu wapandaji na wavunaji bila shamba wala bwana shamba hajulikani.
ReplyDeleteCHESCO MZEE WA MATUNDA.Dar
bwana waziri kindamba acha ujuzi mwingi...kama deci si nzur tuoneshe we una uwezo gan na vigezo gani vya kua lecturer apo city banking...acha mbuzi wale kwa urefu wa kamba zao...wadanganye city banking waafrica wenzako
ReplyDeleteWe anonymous 1:57pm ndio umesema ni nini hasa, umekaa kama mtu wa majungumajungu hivi.
ReplyDeleteMbuzi ale kwa urefu wa kamba yake unamaanisha nini? watu wazidi kutapeliwa au vipi? Kama alivyosema Dada Sophy hapo juu, tujadili ishu si mtu, huyo dogo kama ni Lecturer City Banking au London School of Economics au Cambridge sisi aituhusu, ni yeye kivyake ila alichokisema kimesimama chenyewe kwa hoja zenye nguvu bila ya kupigiwa misumari.
Jumaa (Japan)