Dear Wadau,
I know some of you might say 'zimepitwa na wakati' but if you read between the lines, they are somehow relevant.
Mdau Lilly
----------------------------------------

Katika kipindi hiki ambapo jamii mbalimbali duniani zinapigania haki na usawa hasa ule wa kumiliki rasilimali ambazo zimepokwa na zinazidi kunyakuliwa na waumini wa itikidi ya uliberali mamboleo ni vyema tukajikumbusha Nguzo Tano za Ujamaa hasa nguzo ya nne inayogusia rasilimali kuu ya ardhi:

NGUZO TANO ZA UJAMAA - KWA MUJIBU WA JULIUS K. NYERERE, SABA SABA 1970

1. 'WATU WOTE NI SAWA'"...

Kama hukubali hilo, yaani kama unadhani watu wengine ni miungu wengine, malaika, wengine nusu-nyani, basi hukubali ujamaa. Ujamaa kwako hauna maana, kwa sababu ujamaa unahusu usawa wa watu: hapo ndipo unapoanza...Sisemi usawa wa urefu wala ufupi; kwa urefu namzidi Kawawa, sana tena. Sisemi maguvu, hata; nasema utu, watu, na ubinadamu wao. Kuna binadamu zaidi ya mwenziwe? Kama huliamini hilo, utakuwa mjamaa? Hilo la kwanza... mkaliulize-ulize, mlielewe maana yake. Na mtu anayepinga ujamaa naye ajiulize kama anapinga hilo nalo. Mtu mpingaji ujamaa aseme, 'Hilo nalo, usawa wa watu, napinga; kwamba binadamu wote hivi si sawa'" - Mwalimu Julius K. Nyerere

2. 'LAZIMA MTU AFANYE KAZI'

"...Binadamu hao unaotuona hapa, na hao waliosambaa dunia nzima wanaishi kwa kazi. Hawana namna nyingine ya kuishi. Wakiacha kufanya kazi watakufa; hawana namna nyingine; kuishi kwao, na kuendelea kuishi, lazima wafanye kazi...Lakini binadamu haishi kama farasi. Binadamu haridhiki kuishi kama farasi au punda; binadamu ana kitu anakiita maendeleo; lazima aendelee...Wakati mwingine ili kusudi maendeleo haya yaje wana shughuli za kupigana misasa akili, wanapanuana mawazo tu, nayo ni kazi...nendeni mkaulizane...kama kazi si kitu cha lazima, kama binadamu anaweza kujikalia tu hafanyi kazi, akaishi, na maendeleo yakaja bila kazi. Na huyo anayepinga ujamaa naye ajiulize kama hilo analipinga? Na hilo la kufanya kazi analipinga au kuna jingine analopinga?" - Julius K. Nyerere

3. 'HAKUNA MTU KUMNYONYA MTU'"...

Kama binadamu ni sawa, tunalikubali hilo...Pili tunasema kitu kazi ni jambo la lazima kwa kila mtu, hakuna aliyesamehewa kazi. Basi siwezi kukufanyia kazi. Kukufanyia kazi maana yake ni kwamba wewe unasamehewa kazi! Siwezi kukufanyia kazi. Wewe utafanya kazi, na mimi nitafanya. Sio mimi nifanye, wewe hufanyi; lazima ufanye kazi. Kwa hiyo wewe utafanya kazi, na mimi nitafanya kazi; kila mtu atafanya kazi. Yaani namna ya kulitamka hilo ni kwamba kunyonyana hakuna. Hakuna mtu kumnyonya mtu; sasa tena msingi wa kumnyonya unatoka wapi? Tumesema watu sawa; na mtu ili aishi hana budi afanye kazi, na kazi ndio msingi wa maendeleo. Sasa mwanachama... ajiulize kama anaweza kuwa mjamaa na huku ananyonya! Unamnyonya mkeo; mkeo anakwenda kufanya kazi wewe unakwenda kupiga chibuku; hivi kweli mjamaa wewe? Tunasema kazi jambo la lazima, lakini wewe hufanyi kazi, unamnyonya mkeo. Wewe mjamaa? Nasema na hilo mjiulize...Unaweza kuwa mjamaa na huku unanyonya? Na anayepinga ujamaa ajiulize hilo nalo analipinga, kwamba yeye anaona kunyonya ni sawa tu! Sawa yeye kunyonya mwingine au wengine kumnyonya yeye, huyu anayesema kunyonya ni sawa. Kama kunyonya ni sawa baba, sasa tuanze kunyonya, au mkuki kwa nguruwe?" - Julius K. Nyerere


4. 'VYOMBO MUHIMU VIMILIKIWE PAMOJA'


"...Kama watu ni sawa; binadamu wote ni sawa; kazi ni jambo la lazima kabisa; kunyonya ni haramu; la nne linafuata: Vyombo vyote vya lazima, vinavyohitajika kwa maisha ya binadamu kwa kufanyia kazi lazima vimilikiwe kwa jumla. Ardhi lazima imilikiwe kwa jumla maana tusipoimiliki ardhi kwa jumla tutamwachia Rashidi Kawawa na Sheikh Karume wao wawe ndio wenye ardhi, na ardhi ni kitu cha lazima kwa maisha, hebu tuone kwanza usawa utakuwaje. Itakuwa lazima twende kwa Rashidi na kwa Karume, 'tafadhali bwana nataka ardhi'. Umekwishamwita 'Bwana' huyu; usawa umekwisha. Lakini vilevile kama Sheikh Kawawa ana ardhi, na Sheikh Karume ana ardhi, hawa hawalazimiki kufanya kazi. Kwa nini wafanye kazi? Hawawezi kufanya kazi. Tumesema kazi ni kitu cha lazima kwa kila mtu, lakini hawa hawawezi kufanya kazi, watakaa tu wanatutoza kodi kwa ardhi yao. Ndiyo wanatunyonya hivyo tena. Mimi nafanya kazi; mimi nalima. Halafu Rashidi anasema, 'Ukishalima mahindi ukapata magunia matano, moja langu'. Ndio ananyonya hivyo. Anavunja kanuni ya usawa; anavunja kanuni ya kazi; anavunja kanuni ya kutonyonya. Kwa nini? Kwa sababu tumemruhusu amiliki yeye vitu ambavyo vinastahili viwe vya wote. Mtu ambaye yeye ana ardhi; umemkabidhi viwanda, ukishakuwa umemkabidhi majambo mengine haya, umemwongezea nguvu zake, yeye utu wake umeongezeka-ongezeka na wangu mimi umeupunguza-punguza. Kwa hiyo vitu vilivyo vya lazima kwa kila mtu, kama ardhi ambayo ni ya lazima kwa kila mtu, lazima vimilikiwe na wote. Sasa...mjiulize kama unaweza kuwa mjamaa kweli huku unajidai ardhi yangu? Na wanaopinga wanatakaje? Hao wanaosema ujamaa mbaya. 'Eti vitu vyote viwe vya ujumla'; wengine waongo, 'Eti wanasema hata wakina mama wawe wa jumla'. Tunasema ardhi, hatusemi kina mama, tunasema ardhi viwanda, madini: kwa nini mtu mmoja anakwenda kuvinyakua vikawa vyake hivi!" - Julius K. Nyerere


5. 'KUUNDA NCHI BILA MATABAKA'

"..Kama tunakubali kuwa watu wote ni sawa; na watu wote ni lazima wafanye kazi, mtu asimnyonye mtu; na mali, mali kubwa, sikusema shati langu liwe la Rashidi: misingi ya uchumi kama mabasi yale yanapita iwe kwamba tunasema mabasi yetu, asiweko mheshimiwa mmoja pale anasema 'Basi langu lile!' Basi lako! Yupo dereva mle anaendesha, anasema dereva wake! 'Dereva wangu' - dereva wako, wewe unaweza kuwa na dereva? Dereva anaweza kuwa dereva wa umma, sio dereva wako. Dereva ni sawa sawa na mwalimu; mwalimu wa umma, daktari wa umma, dereva wa umma. Huyu anakuwaje 'wako'? Hata askari siku moja utasema wako. Kama tunakubali watu wote ni sawa; watu wote lazima wafanye kazi, hakuna kunyonyana; mali,vitu vyote vile vya jumla lazima viwe vya umma; maana yake ndio kusema tunataka kuunda nchi ambayo haina tabaka: hakuna mabwana na watwana." - Julius K. NyerereNUKUU ZIMETOKA KWENYE UJAMAA NI IMANI: MOYO KABLA YA SILAHA, 1973: EAPH

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

Kuna Maoni 33 mpaka sasa

  1. AnonymousJune 17, 2009

    Hizi nguzo zote zilizikwa baada ya utawala wake, sasa hivi nguzo kuu ni "Viongozi na ndugu zao kumiliki mali za nchi"

    ReplyDelete
  2. AnonymousJune 17, 2009

    nimeipenda sana hiyo ya tatu "HAKUNA MTU KUMYONYA MWENZAKE" Mbona siku hizi watu WANANYOONYANA SANA na usipomnyonya mwenzako unaonekana mshamba?
    IT ME KISSA

    ReplyDelete
  3. AnonymousJune 17, 2009

    Hizi nguzo kama umezinukuu kiusahili, zina maana kubwa katika maisha haya. Nyerere alifuata mienendo muhimu katika ujamaa iliyolenga katika kuboresha maisha ya kila mwenye juhudi.

    Kwa sasa tunaelekea katika muundo mwingine! Ila baadhi ya vipengele si haba kuvifanyia kazi!

    ReplyDelete
  4. AnonymousJune 17, 2009

    hizo naona kama zimebaki hadithi kwa vizazi vya sasa,usawa ulikwisha baada ya kifo cha mwalimu,hata wafuasi wake ndio walikuwa wa kwanza kumsaliti.HIVI UMEONA JINSI MTUHUMIWA MLALAHOI ALIEBAMBIKIWA KESI ANACHOFANYIWA? NI SAWA NA HUDUMA ANAZOPATA FISADI MBELE YA VYOMBO VYETU VYA SHERIA? mi sioni usawa kama kupata ajira kwenye taasisi zenye neema za serikali hadi baba yako au ndugu awepo hapo.utawala umekuwa kama wa kifalme kila kiogozi anajitahidi kumuandaa mtoto wake aje arithi kiti chake.hivi unazinkumbuka ahadi za mwana TANU? haya itazame CCM ya leo.Ahsante mdau kwa kutukumbusha.

    ReplyDelete
  5. AnonymousJune 17, 2009

    THIS GUy WAS A Visionary Leader , a Genious pure and simple ......If only we listen and followed his teachings ,saa hizi tusingekuwa na TUME zinaundwa kila siku mapa EPA, mara MADINi ,mara East Africa Community na land yetu, mara Liyumba kafanya ubadhirifu,mara Chenge katuibia mapesa yetu ,mara oooh mara eeeh mara hili mara lile yaani kwa kweli ni headache ilimuradi you wake up in the morning and somebody else has amazed you !..! MAsikini sie mungu tuu ndio aneweza kutusaidia sasa . MUNGU AKULAZE PEPA BABU YETU NA HEKIMA ZAKO !

    ReplyDelete
  6. AnonymousJune 17, 2009

    Unaweza kusoma na kusoma bila kuchoka. Sijaona hivi mtu aliyeweza kuweka filosophia yake inayoweza kuhimili vishindo vya jamii inayoendelea. Nyerere alikuwa ni moto wa kuotea mbali. Nawasilisha

    ReplyDelete
  7. AnonymousJune 17, 2009

    Mungu amlaze mahali pema peponi mzee wetu huyu JK Nyerere. Alituwekea misingi ambayo ama kwa hakika kama CCM yetu ya leo ingesimamia hilo tungekuwa mbali sana. Leo kila kitu kimekuwa " WIZI MTUPU" mwenye pesa ndiyo mwenye "HAKI" na husikilizwa na wale "MAKAPUKU" ndiyo wanapata SULUBA. Nadhani wazee wetu CCM waanhalie tena na kurejea kwenye MISINGI NA KANUNI hizi nadhani kila mtu angekuwa anafurahia. Mdau tunashukuru sana kwa MADA hii. "ZIDUMU FIKRA SAHIHI ZA MWL JK NYERERE"

    ReplyDelete
  8. AnonymousJune 17, 2009

    Hizo nguzo zinge tosha kuwa bajeti ya MKULLO.

    ReplyDelete
  9. AnonymousJune 17, 2009

    Je nguzo tatu za chama zilizokuwa kwenye katiba?

    ReplyDelete
  10. AnonymousJune 17, 2009

    ni maneno yakutoa machozi, anyway ujamaa huo mwalimu uliowaamini walishaweka kapuni maana nasikia hata barabara ya lami butiama waliweka ulipokufa na ulikuwa mkuu zaid ya miaka 20 lkn wenzako ndani ya miaka miwili wamenyonya na wameweka lami mpk vichochoroni.
    usingekuwa mjamaa leo hii mara ingekuwa ndo dar/mwanza na maofisini wangejaa wakurya

    ReplyDelete
  11. AnonymousJune 17, 2009

    La tano halikufanikiwa na wala halitofanikiwa nchini tanzania. bado watanzania tunabaguana na kuchukiana kwa ukabila na urangi. situation yetu sio mbaya kama nchi nyengine za afrika, lakini tatizo hili lipo. tunabaguana na kupendeleana katika nyadhifa za kazi, elimu na hata katika mambo yasio muhimu kama miss tanzania (mnakumbuka comments za matokeo ya mwaka jana?). Mwarabu na mhindi ambae generation na generation zake wamezaliwa tanzania, bado watanzania wengi hawawakubali kama watanzania. mpemba na mbongo bado wanabaguana. Kuna nyadhifa tele jeshini zinamilikiwa na makabila fulani tu. Wakati watanzania wanafanya kazi katika sekta mbali mbali idadi kubwa ya wanaofanya kazi za serikali ni wa makabila machache tu.

    ReplyDelete
  12. AnonymousJune 17, 2009

    Well, the guys was smart but how about the implementation of Ujamaa?

    I like Nyerere as an academician, philosopher sort of; but I am afraid most of his policies doesn't seem to take hold.

    Ujamaa is one of those things, sounds sweet and rosy but it NEVER WORK.

    so, without being critical I think we need to deeply think of these things before jumping up and down with praise.

    ReplyDelete
  13. AnonymousJune 17, 2009

    Najua michuzi utabania lakini ndio ukweli "Nyerere preaches what he cannot practice" yeye ndiye mbaguzi/Mnafiki mkubwa katika Ma-Rais wote Tanzania. Hii ni hoja ya nguvu sio nguvu ya Hoja: soma hapa
    a) Kwa miaka 24 kulikuwa na 75% ya wabunge ni wakristo wakatoliki na 78% of Goverment intake to secondary schools walikuwa wakristo...hii siyo concidence ni state well planned "ubaguzi" hapa tunaongelea hata shule za pwani ambako asilimia 90 ni muslims
    b) Kwa miaka 24 kulikuwa kati ya DC's district commisoners 113; 105 ni wakristo wakatoliki hii siyo coincidence ni well planned "ubaguzi" haki sawa mdomoni tuu moyoni tofauti
    c)Kwa miaka 24 "waziri" wa Elimu alikuwa lazima awe Mkristo Mkatoliki coincedence NO at all well planned ubaguzi haki mdomoni moyoni siri nzito
    d)Aliruhusu makanisa kupokea misaada kutoka kwa wafadhili wa nje na ndani ya nchi lakini wakati huo huo alikataa kata kata kwa waislamu kupokea misaada kutoka kwa wafadhili wa nje na wandani walichunguzwa vilivyo hatima yake makanisa na wakristo wakawa nauwezo kifedha na rasimali watu hii siyo watu wote ni sawa hii planned ubaguzi
    source:http://www.njas.helsinki.fi/pdf-files/vol3num1/lodhi.pdf

    Is this a mere coincedence "No at all" mambo mengi hapo sijasema"
    Nyerere=failure=manenomengi=vitendo sifuri=haki kwa wateule ndio maana sirudi huko'=ambao ni wakatoliki.

    ReplyDelete
  14. AnonymousJune 17, 2009

    wewe unayesema barabara mpaka vichochoroni kwakweli haupendi maendeleo. nyie wengine wanafiki mmesahau jinsi watu walivyo teseka wakati wa ujamaa. ulikua huwezi hata kupata sabuni dukani. magari jumapili ulikua unaendesha kwa kibali. huo ujamaa ulikua theory peke yake.

    ReplyDelete
  15. AnonymousJune 18, 2009

    mhh jamani hili dongo si la kawaida ni ukweli mtupu na sasa moto ndo unakokwa tutafika ?

    kila kukicha sampuli mpya !

    zidumu fikra za mwalim na ziwe kanununi za kuwasulubu viongozi wetu .akiba haiyozi nchi inaelekea kubaya sasa !

    ReplyDelete
  16. AnonymousJune 18, 2009

    Richmond hadi leo hii wanalipwa Tsh milioni 150 kwa siku.
    Kwa kweli Mwalimu ulikua mtu muhimu kwa Tanzania,leo hii ikulu imekua kama Supermarket.

    ReplyDelete
  17. MediaViabilityJune 18, 2009

    Tanzania ni nchi ya mbeleko tangu enzi zile ndo maana hatujaenedlea halikadhalika nyerere aling'atuka kwa aibu kwa sababu yeye mwenyewe alikuwa mzee wa kubeba kwa sana na hizo nguzo aliziweka baada ya kuona psyche ya waliomzunguka wana Imani hiyo, He didnt Mean It.

    Baada ya watu kumgundua ni mtu wa kubeba, wengi wamepita njia ndefu kufika walipo. Kibaya zaidi vizazi vya kubebwa vina lalamika kwa nini baadhi ya watu wamefika hapo? why? wao walitegemea ni wao tu wange exel.

    Kutoka na hiyo mentality ya kubebwa watu hawafanyi kazi maofisini, kazi yao ni kudelegate tu kwa wachapa kazi kutoka kwenye tabaka lisilobebwa.

    Michuzi isibane comment hii

    ReplyDelete
  18. AnonymousJune 18, 2009

    Wananchi msikate tamaa, bado tunaweza kurudisha misingi ya Imani ambayo mwalimu alituachia, kama tukiwa pamoja na tukishikamana kama alivyokua akituasi!

    LAZIMA KIELEWEKE, MADINI,MAFUTA,MIKATABA FEKI,NA UNYONYAJI,
    MAFISADI!

    Tukishikamana tutashinda, sisini wengi kuliko wao wanao tuongoza tukishikamana lazima kieleweke, nadhani mmeona yanayo endelea Iran!

    MWENYEZI MUNGU IBARIKI TANZANI:

    ReplyDelete
  19. AnonymousJune 18, 2009

    Mimi naishi Uingereza na jambo moja la filosofia ya kijamaa walilo nalo ni HUDUMA BORA YA AFYA KWA WOTE BILA KIJALI KIPATO.

    Uingereza kupitia National Health Service (NHS) huduma ni za kiwango cha juu na kupelekea huduma zinazotolewa ktk hospital za serikali kuwa bora zaidi ya private hospital.

    Sie Tanzania 'wenyenchi'ndio wana uhakika wakupata huduma bora za afya kwa kupelekwa India, Uingereza au Afrika ya Kusini.

    Mdau
    Muumini wa Ujamaa

    ReplyDelete
  20. AnonymousJune 18, 2009

    Watanzania siwaelewi kabisa. Chini ya serikali ya Mwalimu tulikuwa hatuna haki yoyote. Kama mdau juu alivyosema, hamna sabuni wala vyakula madukani, vijijini ndio hali mbaya zaidi. Kila kona ya nchi kuna askari wake. Ukiwa na dola moja tu, unaenda keko.

    Mimi sielewi kwa nini watu wanamfagilia kiongozi aliyetupeleka nyuma badala ya mbele. Yaani, tumesahau kabisa njaa aliyoileta na Ujamaa wake. Au, labda wadau hapa hawajaenda madukani kununua sukari yao na mchele kwa resheni kwa mwezi.

    Mdau, Tokyo, Japan

    ReplyDelete
  21. AnonymousJune 18, 2009

    ...Mwalimu kama binadamu alikuwa na mapungufu yake...kama alivyo baba yako na mama yako.Mapungufu aliayakiri wazi wazi kabla hajafariki.Ubaya wetu tanaendeleza mabaya yasio ya msingi.Tunaacha ya msingi.

    ...Makosa ya mwalimu yalitokana na kuwa yeye ni binadamu lakini hayakutokana na kujinufaisha au kuwekeza kwa namna yoyote.Nchi nzima inakiri kuwa Mwalimu hakuwa mwizi,fisadi alipenda maisha ya watu woteyawe sawa kitu amabcho ni kigumu.

    Mimi sio muumini wa chama cha ccm ila naaminimwalimu aliweka misingi mizuri ingawa hata baba zetu aliwafukuza katika siasa kwa kipindi chake.

    ReplyDelete
  22. AnonymousJune 18, 2009

    MIMI SIKU ZOTE NASHANGAA WATU WANAEMPONDA NYERERE KUWA ATI ALIKUWA DIKITETA AMA HILI AU LILE, JAMANI YULE MTU ALIKUWA WA MTU WA WATU, HAYO MAMBO YOTE HAPO NDIYO HAYO HAYO YANAFANYWA NA WATU WA MAGHARIBI KWA WANANCHI WAO, SISI TUNAYAONA HUKO, NI UJAMAA WA KISAYANSI, WATU WASIO NA KAZI WANASAIDIWA KIMAISHA, ELIMU BURE KWA WOTO AU NCHI ZINGINE WANATO MIKOPO RAHISI YA ELIMU MATIBABU BURE, AMA RAHISI HASA KWA WATOTO, WAZEE, AKINA MAMA . EBU NENDA USA, UK, CANADA NA KWINGINEKO NA FUATILIA SANA SIASA ZAO NI SAWA KABISA NA ZA NYERERE, ALITAWALA WAKATI MBAYA NDO MAANA AKAPATIWA SIFA MBAYA NA WAZUNGU, KISA ALIKUWA AFUNGAMANI NA UPANDE WOWOTE, ALIKUWA RAFIKI WA KILA MTU NA WA PANDE ZOTE MBILI, MLENGO WA KUSHOTO NA KULIA, LAKINI WAZUNGU WALITAKA AWE KWAO TU NA NYERERE AKASEMA KATU SISI NI MASIKINI TUNATAKA MISAADA TOKA UPANDE WOWOTE ULE. NYERERE ANGETAWALA WAKATI HUU TUNGEKUWA MBALI KAMA NCHI ZA CHINA , INDIA, NA ASIA YA KUSINI. NATOA HOJA VYUO VIKUU VIFANYA MJADALA JUU YA SIASA, POLICY NA UTAWALA WA NYERERE LIVE KWENYE TV ILI WATU WAMJUWE NYERERE NI NANI, WASOMI HASA WALIOBOBEA NA KUTEMBEA DUNIA NA WAWE WAKWELI WASIFUNGAMANA NA SIASA ZA VYAMA VYETU, WAFANYA RESEARCH ZA KUTOSHA JUU ZA NCHI ZINGINE NA WATAWALA WAO, NAWAKILISHA

    ReplyDelete
  23. AnonymousJune 18, 2009

    Ndugu wana blog wenzangu. Nadhani wengi wanaosema haya maneno kuwa JK.Nyerere hakufanya mazuri na sera zake zilikuwa na kasoro ni wale ambao wamelewa maisha ya UGHAIBUNI. Mimi nimekaa nje miaka 7 pale USA na mara nyingi nimekuwa nikikumbuka SERA hizi za mwalimu kwa kuona mambo ya wenzetu.
    1. Mwl alitaka usawa kwa wote na alihakikisha hakuna ambaye yuko juu ya sheria na yeye alikuwa ni KIOO alifanya yote kwa vitendo. Hakujikweza wala kujiweka mbali na wananchi na kiongozi aliyefanya UZEMBE hakumwonea AIBU. Leo ni tofauti wenye PESA ndiyo wenye HAKI hakikuwepo hiki wakati ule, Mimi nimesoma pale FORODHANI P/S wakati huo nimesoma karibia na watoto wote wa VIGOGO ambao pamoja na nyadhifa zao hukuweza jua walikuwa ni watoto wa vigogo wote tulikuwa tunavaa viatu vya BORA SHOES, na KAPTULA za URAFIKI. leo hii watoto wa wakubwa wote wako nje wanasomea KODI ZETU na wengine wako ENGLISH MEDIUM.
    2. Suala la kuwa Nyerere alibana WAISLAMU siyo kweli kabisa Mimi nimesoma pale Forodhani nikiwa Muislamu na Nikafaulu sehemu zote hadi pale MLIMANI kwa majina yote ya KIISLAMU na hata nikapata Scholarship kwenda nje kwa PESA ya SERIKALI. Mwalimu hakubana mtu yoyote na alichagua watu kutokana na JUHUDI ZAO NA UFANISI WA KAZI siyo UKRISTO wala kujuana. Kama angakuwa anabana Prof.IBRAHIMU LIPUMBA, Prof. Malima (MOLA AMLAZE SEHEMU NJEMA), na hata RAIS wetu JAKAYA KIKWETE walisoma na hata kufikia hapo walipo kwa mikono ya NYERERE siyo kweli alikuwa Mkristo. Mimi kama Muislam nashauri tuache mambo ya kusisitizia watoto wetu kusoma sana CHUO " MADRASSA" na badala yake tuwape ELIMU zote. Kwa kusema hilo nakukumbusha kuwa kwa wakati huo IDADI ya WAISLAM wasomi haikuwapo na ndo maana WALIKUWEPO wachache. Mwalimu hakuchagua kutokana na UDINI napinga hilo na nitalisimamia hilo.
    3. Sera ya UJAMAA ni sera nzuri sana ila sisi Watanzania tunataka MAENDELEO YA HARAKA. Hivi sasa tuna maendeleo gani? TUMEUA VIWANDA VYETU VYA NDANI na KUJIDANGANYA TUNA MAENDELEO KWA KUAGIZA TOKA NJE. Hayo ndo MAENDELEO? Mwalimu alikuwa anatupenda sana na kuipenda nafsi yake ndo maana alitaka tujifunge mikanda na KUZALISHA kila kitu ndani. Siku zote alisema TAIFA linalotegemea sana kuagiza kila kitu toka nje liko hatarini. Hivi sasa tumefanywa DAMPO kila kitu kinaletwa RUKHSA hatuangalii ATHALI zake. Unaletewa ARINETI inachubua ngozi unasema hayo ndo maendeleo? Vyakula vinaletwa kila siku toka ng'ambo hatuangalii hata VIWANGO hebu pata picha miaka 15 ijayo tutakuwaje? Nyerere aliamini kila kitu kikizalishwa hapa tutakuwa na usalama mkubwa "WA TAIFA LETU NA HATA RAIA WETU" sasa leo TAIFA limekuwa tegemezi kila kitu kinaletwa unajua athali za vyakula au bidhaa hizo huko USONI? Dada zetu wana CHUBUKA SURA kila kukicha badala ya kuwa weupe wanakuwa WANJANO ndo MAENDELEO? Nipe miaka 3 uone jinsi tutakavyopata wagonjwa kibao wa CANCER pale OCEAN ROAD. Nakurejesha nyuma kidogo kukueleza Mwalimu hakutaka TABAKA MOJA LIWE JUU NA LINGINE LIWE CHINI na akaonesha kwa vitendo akafungua viwanda kadhaa kuajiri watu. NAKUPA HIVI: VOIL - MWANZA ( Sabuni zetu za Gardenia,Mbuni bidhaa ambazo hata huko ng'ambo ziliuzika) tulikuwa na mafuta yetu TANBOND leo tumeiponda tunachekelea BLUE BAND tulikuwa na mafuta ya OKAY mafuta ambayo hadi nje yalikuwa na sifa na UBORA na salama kwa sababu yalitengenezwa nchini. Naweza kukuandikia mengi ila naona niishie hapa.

    ReplyDelete
  24. AnonymousJune 18, 2009

    KUNAWENGINE UWEZI KUWALAUMU KWA COMMENT ZAO,WAMEZALIWA KIPINDI CHA MIEZI 18 DAADA YA NCHI KUTOKA VITANI,KULIKUWA NA VITA BARIDI NA NCHI YETU ILIKUWA AIFUNGAMANI NA UPANDE WOWOTE,MWALIMU ALITILIA MKAZO KULETA UKOMBOZI WA NCHI ZA AFRIKA KWA KAULI MBIU TANZANIA HAIKO HURU MPAKA AFRIKA NZIMA IJITAWALE,NDIPO ALIPO JIJENGEA UADUI NA MABEBERU(UK,USA)NAKUANZA KUMUWINDA WAMTOE ROHO WAKASHINNDWA AKABAKI PROPAGANDA ZA KUMCHAFUA NAKUMKASHIFU,BABA WATAIFA AKUTETEREKA AKUWAHI KUIIBIA NCHI ALIAMINI TANZANIA NI NCHI YAKE,NAWEWE ANONY ULIO INGIZA UDINI UNACHUKI ZAKO BINAFSI BAADA YA UHURU TUJIULIZE TULIKUWA NA WASOMI WANGA NA WENYE UWEZO WA KUONGOZA NCHI WALIPEWA NAFASI BILA KUJALI DINI KABILA WALA RANGI,SWALA LA WAKATOLIKI WAMISSIONARY WALIKUWA WANAKUJA KUJENGA KANISA NA SHULE,WAARABU WALIKUWA WANAKUJA NA MAJAAZI NA KUCHUKUWA BABA ZETU UTUMWA,MBONA KIGOMA MALIMA AMESOMA KTK SHULE YA KIKATOLIKI NA HAKUUKANA UISLAMU WAKE,USHAHIDI WA HILO HAKUNA MWARABU ANAITWA KHAMISI KWA KISURI/KIBEDUI KHAMISI SHATI BOVU/BAKARI NG'OMBE.MAMBO YA UDINI MWALIMU AKUYAPA NAFASI WAISLAMU WAZEE WETU NDIO WALIOMPA NAFASI AWE RAISI WETU TENA WALIMUAMINI NA MADUWA WALIMSOMEA KILA MWAKA BAGAMOYO MPAKA TUKAPATA UHURU.KIPIMO CHA UNGWANA WAKE NDIO MAANA MPAKA LEO ANAHESHIMIKA DUNIANIA KOTE MZEE WETU HANA KASHFA TUJIVUNIE HILO,PIA TUMKUMBUKE YEYE NI BINADAMU KAMA WENGINE ILA NI MWENYE HERI,NAWAKILISHA KTK KEY WEST STATE OF SUNSHINE MIAMI.

    ReplyDelete
  25. AnonymousJune 18, 2009

    Palikuwa na Julius Nyerere mmoja tu, na wala hatatokea mwingine!! Munge amlaze pahala pema peponi... Kumbukumbu zako hazitafutika kiurahisi, na sasa zinazidi kuwa dira ya muongozo wa kisiasa Tanzania na duniani kote.. (dRU)

    ReplyDelete
  26. AnonymousJune 18, 2009

    Ndugu yangu uliyechangia kutoka Helsinki unayelaumu kwamba Nyerere alikuwa Mbaguzi kwa kuwatetea na kuwapendelea zaidi wa kristo na kuwabagua waislamu nafikiri utakuwa unakosea sana. Kwanza nianze kwa kukusahisha huo ni uongo na si kweli wewe ni mtu usiokuwa na hoja za msingi kwa kifupi naweza kuuita ni upuuzi. Leo unafurahia maisha ukiwa huko Helsinki tena ukijinadi hauwezi kurudi Tanzania kwa sababu ya ubaguzi. Nani amewabagueni? Twende mbele na kurudi nyuma Tanzania ya leo iliyokupa nafasi wewe kwenda FINLAND ni juhudi na maarifa ya Mwalimu ndiyo yaliyotufikisha hapa. Kama kuna watu waliona mwalimu alikuwa anawabagua huo ni ufinyu wa kufikiri, sehemu ya kwanza Tanzania kuwa na wilaya ni Kisarawe ambapo watu wake wengi ni muslim sasa iweje walikuwa wanabaguliwa? Shule ya kwanza Tanzania ya sekondari ilikuwa Tanga school tena ambapo 95% ni waislamu. Shule ya kwanza kuwa na Alevel Tanzania ilikuwa Minaki High School (S.t Andrew) Mkoa wa pwani. Kwa mifano hii michache muslims walionewa wapi? Mlikuwa hamtaki kwenda shule ndiyo maana wakristo tukapiga bao tulikuwa hatupendelewi bwana we strive for that. Mimi nafikiri muheshimiwa ungeadmit kwamba by that time you were too lazy muamko wa elimu hamkuwa nao, ningeona you think on positive way. Au mlitaka mwalimu awasomee? Raisi Kikwete ambaye ni muislamu ni juhudi za mwalimu angesoma wapi bila shule hizo za Mwalimu. Na kwa wakati huo suala la mwalimu kushirikiana na taasisi za kidini za kikristu lilikuwa haliepukiki kwa sababu hali yetu kiuchumi ilikuwa mbovu, so ilikuwa ni lazima watusaidie katika ujenzi wa mashule mbalimbali pamoja na hata mahospitali. So nafikiri ndugu yangu wa Helsink you neeed to come up with concrete ideas na si kukulupika like what your doing. SUALA LA UBAGUZI KATIKA UJAMAA HILO HALIKUWEPO. Nafikiri ufike wakati sasa tubadilike na tuweze kudadavua mambo kiundani zaidi kuliko kubwabwaja kama ndugu yangu huyo wa helsinki. Nikilejea katika hoja ya msingi kuhusiana na ujamaa nia ya Mwalimu ilikuwa safi na njema kabisa kwa watanzania. Alidhamiria kuona watanzania wote tunaishi maisha ya amani bila kuwa na matabaka kama ilivyo hivi sasa. Bila ya mtu yeyote yule kutumia cheo chake, uwezo wake na hata rangi yako kuifisadi haki ya mtu mwingine. Ndiyo maana wewe ndugu yangu wa Helsinki kwa sababu ya pesa za baba yako ambaye ni fisadi upo FINLAND leo na hautaki kurudi Tanzania. Sikatai there was minor side effect za UJAMAA, lakini siyo kwa kiwango kama inavyoainishwa na wachangiaji hapa. Kaka michuzi always nalalamika sana kuhusiana na taifa letu la Tanzania where are we going? Siipatii picha tanzania ya baada miaka kumi na tano mbeleni, we are always looking back and want to correct where are Leaders go wrong? Hujiulizi wewe role yako uliyo play ni ipi au kufungua matawi ya CCM ughaibuni ndiyo umewajibika kwa nchi yako. Lets come with concrete and innovative ideas za kuwasaidia watu wetu. Lets our hero Nyerere rest in peace he have strive and done alot for this country. Imebakia sehemu yetu tuwajibike for our country and not for our own interest. Ubinafsi ndiyo unaotutafuna sisi, ni wazuri wa kuzungumza nakuzusha hoja ila implementation is chronic disease. Lets stamp toward achievement of our beloved country. Amen. Naomba niwakilishe kaka michuzi.

    Stephen Nyagonde
    University of Dar es salaam.

    ReplyDelete
  27. AnonymousJune 18, 2009

    Kama kawaida kuna watu wameibuka na udini! Unaweza kumpeleka punda mtoni lakini huwezi kumlazimisha kunywa maji. Marehemu mchonga alitaifisha mpaka shule za makanisa akazifanya za umma ili kila Mtanzania mwenye nia ya kusoma asome bure mpaka achoke mwenyewe. Sasa kama watu wa Pwani wameamua kujikita kwenye madrasa ulitaka Mchonga afanyeje akishakufundisha kusoma na kuandika? Mbona kina Jakaya Kikwete na Ibra Lipumba ni Waislamu na wamesoma bure mpaka wakapata shahada za uchumi na sasa hivi mmoja wao amekaa Ikulu?
    Wadau mnaotaka kuingiza udini katika enzi za mwalimu kumbukeni kwamba katika enzi hizo hapakuwa na fomu ya serikali hata moja iliyokuwa inakuuliza dini yako ni ipi. Kumbukeni vilevile kwamba nchi ilipopata uhuru ilikuwa na idadi ndogo sana ya wasomi. Kwa mfano idadi ya wahandisi ilikuwa ni wawili. Waliobahatika kusomasoma kidogo walikuwa watu waliokuwa karibu na shule za misheni kwa hiyo kuna uwezekano kwamba wakristo walikuwa wengi zaidi hapo awali kwa sababu kwa wakati ule ndio waliokuwa wana kaelimu kidogo. Baada ya marehemu mchonga kusomesha watu wake bure sasa hivi tuna watu wa kila namna ya imani ambao wamesoma kiasi cha kutosha, ndio maana serikali ya sasa ina Waislamu kwenye nafasi zote nyeti kama vile Wizara ya Fedha na Wizara ya Ulinzi.
    Mnaotaka kupandikiza mbegu ya udini msitake kuturudisha nyuma.

    ReplyDelete
  28. AnonymousJune 19, 2009

    Nyerere alikuwa mbaguzi na mdini nimetoa data pale za jinsi alivyogawa madaraka kwa miaka 24 nauliza ....
    a) je hiyo ni coincedence? au ni planned? haiwezi kuwa bahati kwa miaka 24 acha kuwa wanafiki
    swala la mimi kuwa Finland hajafanya nyerere ila ni juhudi za wazee wangu kwasababu ya ubaguzi wake ndio maana watu tukakimbia so don't tell bullshit
    b) Kina kikwete na lipumba wangekuwa wengi sana kama ingekuwa fursa sawa kwa wote kusingekuwa na tension kama sasa!
    c) Nyerere was a failure kwasababu "UNAFIKI" preaching what you don't practice"
    d) siku ukweli ukisemwa ndio tutaendelea lakini kwa unafiki huu ndoto "Good heads" zitaondoka Tanzania kila siku.
    mdau finland

    ReplyDelete
  29. AnonymousJune 19, 2009

    Ndugu yangu wa FINLAND kwanza nikupe tena pole kwa kuhisi ulibaguliwa hapa Tanzania.Kwa nadharia hii unayoiongea hapa, inanikumbusha maneno ya mkuu wangu wa shule enzi hizo MINAKI SECONDARY "You will never reach on conclusion pertain to religious issues or saga" Kwa mantiki hii naufunga mjadala wa kubishania MUSLIMS Vs CHRISTIAN, kwani mie naamini we are all equally. Bila Mwalimu kutengeneza mahusiano mazuri na nchi za kigeni hao wazee wako wangekufikishaje huko FINLAND, try to think positive guy you'r a genttle men. Nafikiri you need to have more and detailed concern to that kuliko unavyoiwakilisha sasa, its better to admit kwamba mlikuwa vilaza ndiyo maana mkahisi mnabaguliwa. Lets be realistic viongozi wangapi wakubwa walikuwa wanatoka kwenye dini gani? Na kwa nini waislamu wasiwe wengi? Hapo ndipo utakuja na jawabu kwamba mlikuwa hamko tayari kusoma bwana, elimu ilikuwa ni fursa sawa kama ilivyoainishwa kwenye maazimio ya ujamaa. Kaka rudi nyumbani tuijenge Tanzania yetu, using'ang'anie huko bwana Nyerere alishamaliza part yake imebaki ya kwetu. Nawakilisha kaka michuzi kutoka nyumbani. The Hill kitovu cha elimu.
    Nyagonde

    ReplyDelete
  30. AnonymousJune 19, 2009

    Ninaelewa kama msomi na Mtanzania kuwa Mwalimu Nyerere alifanya mazuri mengi pia nchini.

    Mali za wazazi yangu ilitaifishwa na serikali ya Nyerere kwa kuwa wazazi wangu walifanya kazi kwa juhudi na kutajirika bila ya kuiba. Wakaanza upya kufanya kazi. Alipokuja Sokoine, wakataifisha tena mali za watu wengi pamoja na mali za wazazi wangu. Huwezi kusema kuwa aliheshimu haki za watu.

    Katika kitabu changu, Nyerere alikuwa sio kiongozi mzuri kwa kuwa alishika wathifa kwa miaka mingi na tulikuwa hatuna demokrasia yoyote. Hata Raisi Bush wa Marekani alipendwa asilimia 50% na wananchi wake na hata hivyo, aliacha ngazi baada ya muda wake kwisha. Sisi tuko hapa tunamfagilia kiongozi wa zaidi ya miaka 20, halafu tunalalamika kwa nini nchi za Kiafrika haziendi mbele miaka yote hii. Sababau moja wapo ni kuabudu viongozi wetu kama Mungu hata kama hawaheshimu haki zetu wala kura zetu. Tuko katika karne ya 21 lakini fikira zetu bado ziko katika karne ya 18.

    Mdau, Tokyo, Japan

    ReplyDelete
  31. AnonymousJune 19, 2009

    Mdau wa Chuo Kikuu,
    a) Nyerere hakunifikisha Finland ila "alikuwa sababu ya mimi kuondoka nchini kwangu kwasababu alikuwa anabagua (systematically) favouring christians kama nilivyosema hapo mwanzo.
    b) Hakuna hata siku moja atakuja mtu kupingana na Statistics ya kugawa madaraka wala haikuwa coincedence ndugu yote yana mwisho
    c) Dunia ni pana kama jamaa wanabana hapa unatokea upande mwingine that is what we did me and my parents
    d) siku zote if you preach what you don't practice you will fail' amebagua eeh lakini amekufa failure.. the very idea ya kugawa mali za watu wenye bidii kwa maskini ni "Ujinga mtupu"
    e) Waislamu walikuwa wasomi kabla ya uhuru kuliko makabila mengi ya bara (upcountry) kwanini wasisome wakati wa uhuru hayo unayosema ya madarasa ni propaganda tuu, kwa sisi waislamu madarasa ni lazima na muhimu na elimu nyingine ni muhimu pia hakuna hoja hapo "isipokuwa na wewe ni mbaguzi kama mwenzako" l

    ReplyDelete
  32. AnonymousJune 19, 2009

    Wana Blog nadhani ukichunguza sana utaona wale wote wanaosema MABAYA kuhusu Mzee wetu Nyerere wanadhihirisha na jamii ile ya MAFISADI wote wako nje huyu yuko Finland na mwingine Tokyo. Wote hawa ni wale wale tusipoteze muda wetu kwa ajili yao.
    Mwalimu ni kiongozi ambaye lazima tumuenzi na hata bila shaka nasikia raha ninaposema MWALIMU ALIKUWA KIONGOZI WANGU. Kama binadamu ana mapungufu yake lakini ni machache sana kulinganisha na yale MEMA aliyotuonesha.
    HAKUPENDA JILIMBIKIZIA MALI NA ALIIPENDA NCHI YAKE NA WATU WAKE NA ALIKUWA TAYARI KUFANYA CHOCHOTE KULINDA "SLAHI LA TAIFA".
    Mwalimu alitupenda sana na katu hakukubali mtu yoyote amnyanyase mwenziwe. Wanaosema wamebaguliwa nadhani wao ndiyo MAKABURU wakubwa ambao leo tukiwapa NCHI watatunyonya kama KUPE. Utajiitaje Mtanzania na kujisifia kuishi nje? Kama unaipenda nchi njoo nyumbani tuijenge NCHI YETU Mwalimu alisema siku zote " TANZANIA ITAJENGWA NA WATANZANIA WENYEWE TENA WALE WENYE MOYO" Sisi tupo hapa tulikuwa NJE na sasa tumerudi tunawakilisha. NJOO NDUGU YETU TUIJENGE NCHI YETU.
    Hivi kuna kiongozi gani anaweza dhubutu jilinganisha na Mzee huyu? Unakumbuka mashamba yetu ya KATANI KULE TANGA? Viwanda vyetu vya MUFINDI kule Iringa? Unakumbuka MOPROCCO, CANVAS MILL, TANALEC,SUNGURA TEX, MUTEX, MWATEX, URAFIKI, VOIL, WAZO HILL, TANGA CEMENT, na vingine vingi kama BUKOP,TANICA, na vile viwanda vya CHAI vya CHIVANJE kule Tanga na Mbeya Tanzania tulikuwa tuna EXPORT chai BORA kabisa ambayo hata katika Soko la Dunia ilikuwa inashindana ya AFRICANPRIDE, Unakumbuka mafuta ya OKAY, PRIDE? viko wapi hivyo vyote? hebu achane kumsemea mabaya mzee wetu na tumuenzi kwa MEMA aliyotutendea.

    ReplyDelete
  33. AnonymousJune 21, 2009

    wewe unayesema tanzania ilikua na viwanda vingi wakati wa ujamaa unajua kua viwanda vyote hivyo viliendeshwa kisiasa bila ya utalaam wowote ni vikaleta hasara kubwa sana. huwezi kuchanganya biashara na siasa hata siku moja. angalia hata china ilivyo badilika baada ya kuondoa siasa kwenye biashara. ujamaa ulituletea umasikini wa kupindukia. tukizungumza juu ya usawa kwakweli kulikua hakuna usawa wowote kwasababu hata watoto wa nyerere walisoma north america wakati watoto wa watanzania wengine walisomea chini ya miti. waheshimiwa wengi tu walipeleka watoto wao kusoma nje ya nchi. kama mwalimu hakua dikteta mbona wanasiasa kama bibi titi waliwekwa vizuizini. hii mambo ya kusema ikulu ya sasa inafanywa mahali pa kufanyiwa biashara is not fair. wakati wa mwalimu kulikuwa na ufisadi lakini ulikua unafanyika kisirisiri.

    ReplyDelete

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...