JK akijichanganya na wageni katika hafla ya Mo Ibrahim hivi karibuni jijini Dar
Hali ya siasa ‘yatulia’ miaka minne ya JK
Na Mgaya Kingoba
"NCHI hii haijawahi kuongozwa na malaika wala haitapata kuongozwa na rais malaika…Rais Kikwete si malaika, lakini ni kiongozi mzuri, msikivu, mvumilivu na mchapa kazi. Sasa linapojitokeza kundi la wachache na kufanya kampeni ya makusudi ya kumpaka matope, lina jambo.”

Hiyo ni nukuu ya mwanasiasa mkongwe nchini, Pius Ngeze ambaye kwa miaka mingi alishikilia wadhifa wa Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) wa Mkoa wa Kagera. Kauli hiyo aliitoa wiki iliyopita wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu maoni ya baadhi ya waliokuwa viongozi wa chama na serikali wakati wa kongamano la miaka 10 ya kifo cha Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere lililojadili mustakabali wa nchi.

Nimeitumia nukuu hiyo kama rejeo langu katika makala haya yatakayojikita kuangalia hali ya kisiasa nchini katika miaka minne ya utawala wa Rais Jakaya Kikwete aliyeingia madarakani Desemba 21, 2005.

Kwa maneno hayo ya Mzee Ngeze, hakuna shaka kuwa Tanzania haijapata kuongozwa na malaika na wala hatatokea malaika kuiongoza nchi hii, lakini ni ukweli usiopingika kuwa Rais Kikwete amekuwa msikivu, mvumilivu na mchapakazi aliyetoa uhuru wa watu wengi kutoa mawazo yao.

Ni kwa msingi huo, ndio maana yanayojitokeza katika siasa za Tanzania, iwe kwenye chama chake cha CCM, vyama vya upinzani au kwa wananchi kwa ujumla, ni kwa sababu ya uongozi wake mzuri.

Kwa ujumla, kwa miaka minne ya utawala wa Rais Kikwete, hali ya kisiasa nchini ni nzuri, kwa sababu hata ukilinganisha na nchi nyingine za jirani, tumeshuhudia masuala mengi ya kisiasa nchini yakijadiliwa kwa mapana, tena wakati mwingine kwa jazba, lakini Watanzania wameendelea kuwa wamoja.

Vyama vya siasa vimepewa uhuru mkubwa wa kuendesha siasa zao kuanzia CCM hadi kwa wapinzani ambao wamekuwa wakiikosoa serikali na chama hicho tawala kwa uhuru bila kuwepo kwa vipingamizi.

Vimekuwa huru kuendesha mambo yao kwa mujibu wa taratibu za vyama vyao na kwa mujibu wa Katiba ya Tanzania. Ndio maana leo kumekuwepo na Operesheni Sangara, ikaja Operesheni Zinduka na haitashangaza kabla ya Uchaguzi Mkuu wa mwakani, tutashuhudia operesheni nyingine.


Lakini zote hizo, zimefanyika bila ya vyama husika, Chadema na CUF kuwekewa mizengwe na haishangazi kuona helikopta inaruka bila kipingamizi! Hayo ni mojawapo ya matunda ya Kikwete katika kuhakikisha siasa nchini inakwenda kama ilivyoelekezwa na Katiba ya Tanzania na wananchi wake wako huru kushiriki katika sehemu hiyo muhimu ya demokrasia.

Na hata katika uchaguzi mbalimbali wa vyama vya siasa kuanzia CCM hadi vile vya upinzani, hali imekuwa nzuri kwa maana uendeshaji wa uchaguzi huo umekuwa wa amani na utulivu. Tumeshuhudia mvutano katika kuwania nafasi mbalimbali, na hata wakati mwingine baadhi ya wagombea kutishia kwenda mahakamani kusimamisha uchaguzi, lakini mwishowe, uchaguzi unapita kwa amani.
Hayo yameshuhudiwa kama nilivyoeleza katika vyama vya CCM, CUF, Chadema, TLP na vingine. Vyama hivyo vimetumia demokrasia kuwapata viongozi wao wanaowapenda, na mwishoni wale walikuwa na malalamiko, kila mmoja alikubali matokeo, kuonesha ukomavu wa demokrasia na siasa nchini chini ya uongozi wa Rais Kikwete.


Aidha, pia kumekuwepo na matukio machache ya vurugu katika baadhi ya uchaguzi hasa ule mdogo wa majimbo. Lakini kuanzia katika ngazi ya vyama hadi Uchaguzi wa Serikali za Mitaa uliofanyika Oktoba mwaka huu, Watanzania na wapenzi wa siasa, wamepewa fursa ya kushiriki katika mchakato huo kwa amani.


Ndani ya miaka minne ya utawala wa Rais Kikwete, kumekuwepo msuguano wa hapa na pale katika chama chake, CCM, kiasi cha siku za karibuni, kudaiwa kuwepo makundi kadhaa ndani ya chama hicho kikongwe. Kila linaloigusa CCM, linaigusa jamii ya Watanzania kwa sababu chama hicho ndicho kinachoongoza Dola, kwa hiyo uimara wake ni uimara wa Tanzania, na endapo kitayumba, basi nchi nayo itayumba, kama alivyowahi kueleza Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere enzi za uhai wake.

Hivyo, lolote linalotendeka ndani ya CCM, lazima Watanzania watapenda kulifahamu na ndio maana kumekuwepo na mjadala mzito kuhusu chama hicho kutokana na madai hayo ya msuguano na makundi. Kwa mfano, mwaka huu, imeilazimu CCM kuunda Kamati ya Wazee yenye kuongozwa na Rais mstaafu Ali Hassan Mwinyi, kutafuta kiini cha madai ya kuwepo makundi miongoni mwa wabunge wake, hali ambayo inadaiwa kudhoofisha utendaji wao ndani ya chombo cha kutunga sheria.

Hiyo imetokana na mijadala mizito inayojitokeza katika Bunge na pia ndani ya vikao vya CCM kama vile Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC), ambako inaelezwa katika kikao kimojawapo, wajumbe walipewa fursa ya kila mmoja kutoa dukuduku lake mbele ya Mwenyekiti Rais Kikwete.

Tayari pia wabunge hao wa CCM wamepata nafasi ya kutoa dukuduku zao mbele ya Kamati ya Mzee Mwinyi na sasa kinachosubiriwa na ripoti yao kwa waliowatuma kazi hiyo, NEC.

Lakini lililo wazi ni kwamba wapo watu, tena wengi, wanaoitazama mijadala na misuguano hiyo ndani ya CCM kama yenye busara na yenye kujenga ustawi wa chama chenyewe na Tanzania kwa ujumla. Wanaona ni suala zuri kwani mwishoni unapatikana mwafaka wa wengi ili kunusuru chama na nchi. Hao ni wale wanaoiona hali hiyo kama yenye siha kwa manufaa ya CCM na Taifa kwa ujumla, lakini wapo pia wanaoitazama hali hiyo tofauti.

Na hawa ni wale wanaomshutumu Rais Kikwete kwamba alipaswa kushika ‘rungu’ na kukemea au kumaliza matatizo hayo kwa nafasi yake aliyonayo katika chama, ya uenyekiti. Wanamwona Rais Kikwete hana msimamo, walitaka aje na uamuzi wa mwisho kuhusu misuguano hiyo ndani ya chama chake. Lakini hawa wanasahau kitu kimoja. Hiyo siyo staili ya uongozi ya Kikwete. Hawa ni wale wasioheshimu misingi ya demokrasia. Wasioruhusu kuwepo kwa mijadala hata kama wao wenyewe hawaipendi. Ndio maana mwanzoni mwa makala haya nilimnukuu Mzee Ngeze akisema kuwa Rais Kikwete ni kiongozi mzuri, msikivu, mvumilivu na mchapakazi.

Ni kweli, ndio maana amewaachia watu wajadiliane wanavyotaka, lakini mwishoni mwa siku wanaibuka na msimamo mmoja. Ndio msingi wa demokrasia. Na hili unaweza kuliunganisha moja kwa moja na hali ya kisiasa katika Zanzibar tangu Rais Kikwete aingie madarakani. Alieleza wazi katika hotuba yake ya kwanza bungeni Desemba 2005, kwamba atajitahidi kuhakikisha anamaliza mpasuko wa kisiasa visiwani humo; na amejitahidi kufanya hivyo.

Amesimamia kupitia chama na serikali yake, majadiliano ya kusaka mwafaka wa Chama cha Wananchi (CUF). Na amehakikishia mazungumzo ya kusaka suluhu kati ya vyama vya CCM na CUF yanakwenda sawa, ingawa yamekuwa wakati mwingine yakipata vikwazo, jambo ambalo katika siasa, haliepukiki.

Hatua ya hivi karibuni ya Rais Amani Abeid Karume kukutana na Katibu Mkuu wa CUF, Maalim Seif Sharif Hamad ni ishara mojawapo ya juhudi hizo za kusaka amani ya kudumu katika visiwa hivyo.

Ingawa hatua hiyo ya Rais Karume kuzungumza na Maalim Seif na kufikia maridhiano kwa nia ya kuijenga Zanzibar, inaweza kuonekana haina mkono wa moja kwa moja wa Rais Kikwete, lakini ukweli mkono wake upo. Kwa sababu Rais Kikwete wakati mwingine hapendi kufanya kile kinachoitwa ‘direct intervention’, lakini atakuwa ameingilia kwa upande mwingine na hasa ukizingatia mfumo wa chama chake cha CCM na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania; hivyo huwezi kumtupa nje ya maridhiano ya sasa ya Zanzibar.

Rais Kikwete ana tabia ya kutotaka “apande mlimani na kupiga baragamu” kila mtu amwone. Hakuna shaka katika hili amefanikiwa angalau sasa kuweka msingi mzuri wa ahadi yake ya kumaliza mpasuko wa kisiasa Zanzibar kama alivyoahidi bungeni katika hotuba yake ya kwanza. Hapa pia anastahili pongezi kwa kuweka mazingira mazuri ya siasa katika nchi, kuendeshwa kwa majadiliano na maridhiano.

Kwa hiyo, kwa miaka minne ya uongozi wake, kwa ujumla unaweza kueleza bila ya kusita kuwa hali ya kisiasa nchini imedhibitiwa, hakuna vurugu na watu wanaendesha shughuli za kisiasa kwa amani. Imani ni kubwa kwamba tunapoanza ngwe ya mwisho ya kipindi chake cha kwanza cha Rais Kikwete na kuelekea Uchaguzi Mkuu wa mwakani, hali ya kisiasa nchini inaonesha matumaini makubwa na uhuru katika kutekeleza moja ya majukumu ya demokrasia nchini.

Rais Kikwete anastahili pongezi kwa kufanikisha haya.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

Kuna Maoni 34 mpaka sasa

  1. Mimi Binafsi nakubali kuwa
    Rais Jakaya Kikwete ni Kiongozi mzuri, inawezekana kabisa watanzania waliowengi watakubaliana nami.
    (a) JK apendi mizengwe na fitina
    (b) kwa kuwa ni mchapa kazi aneyefanya kazi kwa maslahi ya waliomchagua,na waliomchagua maana yake walio wengi,na waliowengi na watanzania wa kawaida yaani wa kipato cha kawaida,sasa haya maslahi anayoyalinda ndio yanamfanya baadhi ya "Wanafiki wa Kisiasa" kutaka kumpaka matope.
    Kutokana na kutokubaliana nao katika mfumo wao wa kuligawa taifa katika matabaka ya walala hoi,Walala hai,na walala heri.
    Tujiulize ?nchi gani hapa afrika ina uhuru wa vyombo vya habari zaidi Tanzania?
    Rais Gani? hapa Afrika anaweza kuwekeza mda wa kuwasikiliza wapiga kura wake zaidi ya JK?
    kwa kuwa kuna baadhi ya makundi ya "Wanafiki Kisiasa" ambao hawapati maslahi yao kwa mfumo waliouzoea "Tua Tugawe" hili linawafanya kujenga chuki na Rais,na kutafuta vijisabu vidogo vidogo na kuvishikia bango,
    wanafiki kila siku ni watu wanaopenda nongwa na kuleta uchochezi pale penye AMANI.
    Msione vinaelea "Amani" Bongo Imeundwa."´Mungu Ibariki Tanzania"

    ReplyDelete
  2. Hajafanya chochote Zanzibar, kwasababu serekali ya mseto haijapatikana hadi sasa.

    Kilichofanyika ni mazungumzo baina ya wazanzibari hao wawili, nasie wengine tukakubali kama huo ni mwanzo mzuri.

    Lakini mgogoro wa Zanzibar hauwezi kuisha bila ya serekali ya mseto!Ambapo JK hana alilolifanya hadi sasa....labda kubembea huko Jamaica!

    ReplyDelete
  3. I can see Mr. President rubbing shoulders with billionaire George Soros, the founder of movon.org. Many people in America, especially conservatives, believe that Soros is the reason Obama is at the White House today.

    Apart from that Soros is also the best when it comes H-funds as well as stocks manipulation.

    ReplyDelete
  4. Jamani mbona wapiga debe mnajikanganya!!!!!!
    "NCHI hii haijawahi kuongozwa na malaika wala haitapata kuongozwa na rais malaika…Rais Kikwete si malaika..."
    Kwa vile tunakiri kuwa hatuwezi kuwa na kiongozi malaika, basi tukubali kuwa kiongozi huyo anavyostahili PONGEZI pale anapofanya vizuri ndivyo hivyo anavyostahili KUKOSOLEWA pale anapokosea. Sifa hiyo ya usikivu mnayosema itajidhihirisha akikubali kukosolewa. Ni kwa sababu hiyo hiyo kuwa JK sio malaika, wanaodiriki kumkosoa wanampenda sana kuliko hao akina Ngeze and the like wanaoongozwa na kujipendekeza.
    Baada ya kuwa madarakani kwa kipindi cha miaka minne ni wakati muafaka kumtathmini na kumpa alama yake ili anapopanga kuingia muhula wa pili ajenge dira ya kumwongoza katika muhula huo kwa manufaa ya wananchi. Inashangaza kusikia watu tena wasomi wanahoji kwa nini wakosoaji wajitokeze kipindi hiki cha kuelekea uchaguzi mkuu. huu ndio wakati muafaka wa kuhoji na kumpa changamoto huyo anayetaka kuendelea kutuongoza kama sio kututawala!!!! Na wanafanya hivyo kwa kuzingatia hoja yenu wapiga debe kuwa huyu ni binadamu, sio malaika!!!!!

    ReplyDelete
  5. Utulivu katika Umasikini NI Balaa. Hakuna Amani katika Umasikini. Kinaendelea kwa sasa ni Ukimya wa watu ambao wakiamka kusema kuhusu nini wanakifikiria ndio utajua balaa lake.

    ReplyDelete
  6. Inawezekana ni raisi mvumilivu lakini at the same time mi namuona ni weak leader.Natofautiana na mwandishi aliesema yanayojitokeza sasa ni kutokana na uongozi wake bora. Kwamtazamo wangu yanayojitokeza sasa mfano mgawanyiko uliojitokeza ndani ya CCM ni uongozi wake kama mwenyekiti kushindwa kusuluhisha mambo au kwa msemo mwingine (under control) kwahiyo mambo yanachemka ndani kwa ndani mpaka yanamwagika tu we unaangalia ndio unaundia tume. Inawezekana wakati wa uongozi wa Nyerere au kiongozi mwingine kutofautiana kulikuwepo lakini how it was handled ndio tunachokiangalia. Uongozi wa Kikwete umekua out of control sometimes mtu unajiuliza "who is running the show". Mawaziri wanasema na kufanya wanayotaka hivi umeshaona wapi waziri uliemchagua wa ethics anakua "unethical' alafu unakaa kimya au ndio uvumilivu wenyewe huo.As a person Kikwete anaweza kuwa mtu mzuri lakini as a leader i doubt. He seems tu be weak,unorganized,lack priorities,very undecissive but yet charming, and understanding.

    ReplyDelete
  7. mleta mada wewe unauzunguka ukweli halafu unajikuta kitanzini mwenyewe, nadhani hata wewe umeona ambavyo huyu mtu inakuwa ngumu kumtetea. Wewe ni siasa na misemo ya wakale tu, vipi kuhusu uchumi,maisha bora,ari mpya nguvu mpya na kasi mpya?????

    ningeendelea lkn sitaki kupoteza nguvu na muda wangu, najua comment kama hizi ni kapuni

    ReplyDelete
  8. ''Hali ya siasa yatulia''

    Mimi huwa sipendi kuchangia hizi mada maana wakati mwingine huwa nasema ni kama kumpigia mbuzi gitaa..wenyewe wanakula maisha tu na kuponda raha..ila nimeona kwa leo niongee kidogo kama mchango wangu (haya ni mawazo yangu)
    Mimi ni kama mmoja wa maelfu waliomuamini sana JK kuwa angeleta mabadiliko makubwa katika nchi yetu, ila sasa nimegundua kuwa nili-overlook..na nadhani hata yeye mwenyewe alijipa matumaini makubwa sana kuwa kuwa rais ni kazi rahisi sana bila kuangalia mbali zaidi (hata Mwl. Nyerere aliwahi kusema hivi). Matatizo tuliyonayo sasahivi nchini nadiriki kusema kwa kiasi kikubwa yamechangiwa na JK kwa kutokuwa makini ktk uongozi wake hasahasa ''maaskali wake wa miavuli''. Tangu aingie madarakani sijawahi kuona mawaziri wakijiachia kama wako majumbani mwao wanaongoza familia zao!! nchi imekosa muelekeo..kila kukicha ni porojo tuuuu hasa kutoka kwa viongozi wetu, leo mara kaongea huyu kesho kaibuka mwingine...tumefika pabaya mpaka viongozi wenye dhamana kubwa wanatukanana hadharani kama ''nyimbo za mipasho''!! eti leo tuna waziri kichaa anayetakiwa kwenda milembe!!kweli!!! na JK anawaangalia tuuuu!! chukulia mfano mdogo tu wa Jiji letu dar... kila kukicha magorofa yanaongezeka (ni vyema maana ni maendeleo), magari yanaongezeka (ni vyema maana ni maendeleo) ila jiulize vipi kuhusu miundombinu?...umeme ni uleule (pamoja na kuongezeka majumba!!), hospitali ni zilezile (pamoja na kuongezeka watu), barabara ni zilezile!!! na kila mwaka bajeti za mawizara zinapitishwa!!! labda kwa ajili ya kulipa watu mishahara tu!! na mawaziri wapo tuuuu!! leo hii Jiji kama dar eti hospitalini, wagonjwa wanalala mzungu wa nne!!!, hakuna mabadiliko yoyote. Tumeongeza shule za kata na sekondari (ni vyema maana ni maendeleo), vipi kuhusu kuongeza waalimu? vipi kuongeza vitendea kazi?? na je tumejiandaaje hawa watoto tuliowajaza shule za msingi na sekondari wakati uwezo wa vyuo ni mdogo??? ufisadi kila mahali..leo hata mitihani ya darasa la saba eti ''ina-leak''!!! kweli jamani!!! hawa watoto wanauwezo wa kuiba mitihani-kama sio watu wachache huko ktk sehemu nyeti wameamua hivi?? na waziri yupo tu amekaa!!! sasa hivi nchi yetu kila kukicha ni kuundwa tume...juzi tu ajali imetokea nasikia wameunda tume!! kweli!!yaani tatizo linaonekana wazi kabisa hata mtu asiyeenda shule anaweza kuliona tunang'ang'ania tume...kwani hiyo ni ajali ya kwanza ya hilo basi?? na kama ni sample za matairi...magari yako mangapi dar?? hivi tunavyoongea kuna watu wamekufa kwa njaa mikoani..yaani hapahapa nchini..na viongozi wamekaa tuuuu!!! kweli ukikaa mtu na kufanya tathmini ya hii miaka minne..huitaji kuwa na phd ili upate jawabu!!!
    Rais yumkini alikuwa na sera nzuri sana na yumkini moyoni mwake alikuwa na nia ya dhati sana kwa ajili ya nchi yake..ila aliowategemea kumsaidia kutimiza sera hizo asilimia kubwa wamemuangusha!!

    Tafakari..

    Mungu ibariki nchi yetu Tanzania
    DJ

    ReplyDelete
  9. Ndugu mwandishi Watanzania tushatoka huko kudanganywa kwa sera za amani.Usituletee siasa na propaganda za kina Kingunge ndugu yangu, zama za kupongezana kwa kudumisha amani zimepita, na kwa taarifa yako anayedumisha amani Tanzania sio Raisi, ni Watanzania wenyewe, Kwa mambo wanayotendewa watanzania na viongozi wao wana kila sababu ya kuivunja hiyo amani, lakini watanzania wanavumilia, nyie mnasema mmedumisha amani. Yani unapima mafanikio ya Rais katika miaka minne kwa helikopta ya chama pinzani kuruka angani, are you serious?? Tunajua we ni mpambe na hapo unapalilia " kula " yako come 2010, lakini ongea vitu vya maana.Ukiweza kuirudia mada yako ikielezea maendeleo Watanzania waloyapata ndani ya miaka minne bila kutaja wimbo wa "amani na demokrasia" itakuwa vyema, which i bet u can't.

    Anko,hope sijachafua hali ya hewa kwa hii comment, manake nawe umekuwa kama kiranja mkuu yani tukiwa tunaandika comment tunajitahidi kupunguza ukali wa maneno usitie kapuni. Ila nna hasira kuliko hayo maneno.

    ReplyDelete
  10. Hakuna asiyejua kwamba nchi aiongozwi na Malaika,Lakini kuna viongozi wachapa kazi na wenye uchungu na matunizi ya Pesa za umma,Unajua safari yake ya Jamaica ingechimba visima vingapi?

    ReplyDelete
  11. Kikwete ni rais msanii na mwoga!

    ReplyDelete
  12. Amekumbwa na kigugumizi kushughulikia suala la ufisadi, hili liko wazi,ni majuzi tu hapa nchi wahisani walitishia kusitisha misaada endapo hatua za kesheria hazitachukuliwa kwa mafisadi. Lakini JK amefanya nini hadi leo.

    JK hayuko makini hata kidogo, udhaifu wake ulianza kuonekana toka alipoliteua baraza lake la kwanza la mawaziri. Mfano kuwarudia mawaziri wakongwe ambao moja kwa moja walionekana kuwa na kasoro nyingi, lakini yeye kawafumbia macho, mfano Zakia Meghji,Profesa Kapuya,Mungai, Andrew chenge na mbunge ROSTAM AZIZ, BASIL MRAMBA NA DANIEL YONA.

    ReplyDelete
  13. MSIWALAGHAI WATU NA MASHAIRI YENU. VIONGOZI WALIOKO MADARAKANI NI MAFISADI..NA KIKWETE ANAWAKUMBATIA...KWAHIYO NA YEYE TUMWITE NANI???

    WOTE NI MAFISADI NA WANAKULA MALI ZA UMMA NA WALA HAWANA UCHUNGU NA NCHI....MUNGU AWAONGOZE LAKINI KAMA WATAKAIDI BASI TUTAWAONA HAPAHAPA DUNIANI...

    ReplyDelete
  14. JK anaandamwa kwa fitna tu,ni mchapaa kazi mzuri sana,na hii yote ni roho mbaya wa wanadamu

    ReplyDelete
  15. hapo ni chuki za udini tu ndo zinamuandama JK kama ilivyokuwa kwa alhaj mwinyi,mwinyi alisimwangwa japo kubwa aliwatoa watanzania kwenye wingu la giza na shida mpaka kwenye miguu,tz ya nyerere ilikuwa hata kupata sukari kazi,passport lazima uwe ndani ya serikali ndo usafiri,mwinyi alivyoingia aliitoa nchi kwenye giza lakini bado alisimangwa na kejeli kibao,nani atabisha leo hii ukimchukua mlalahoi wa tz umuulize wakati gani wa nchi alikuwa anamatumaini na kupata japo milo mitatu ya uhakika,atasema ni wakati wa mwinyi,amekuja JK ndo yale yale,anasulubiwa kwa mambo ya yaliofanywa na serikali zilizopita,namuhurumia sana rais atayekuja baada ya JK akiwa si muislam,maana waislam now wameamka,nchi hii haitatulia kabisa,iwapo atajaribu kuleta mambo ya ubaguzi huu.na kama 2015 rais atatokea znz atapingwa kwa kila namna.tz nakupenda sana

    ReplyDelete
  16. naomba mwenye takwimu anieleze au anielimishe safari za kikwete tangu ameanza uraisi zimegharimu kiasi gani na ameingiza kiasi gani(misaada au chochote anachopata kwa taifa huko aendako najua ni kikazi),naamini kama ametumia tsh 100 kwa safari akapata msaada tsh 1000 atakuwa ameziba watu midomo, je hizo safari zote anazokwenda hawezi kutuma wasaidizi wake?

    ReplyDelete
  17. SAFARI YA NCHI HII KUELEKEA KWENYE MAENDELEO YA KWELI NI NDEFU SANA.

    WATANZANIA TUNAPASWA KUANDIKA MAKALA ZETU KISOMI KWA KUANGALIA PANDE ZOTE. HAKUNA UBISHI RAIS AMEFANYA MAMBO MENGI MAZURI KWENYE UTAWALA WAKE LAKINI PIA KUNA MAMBO ANAFANYA AMBAYO SI MAZURI.

    NJIA NZURI YA KUMSAIDIA KUENDELEA KUFANYA VIZURI NI KUMULEZA PALE AMBAPO ANA-LAG BEHIND. BADO ANA OUTSTANDING ISSUES KIBAO WADAU WENGINE WAMEKWISHAZITAJA. MWANDISHI ALIPASWA KUANGALIA PANDE ZOTE SIO KUPAMBA TU. HOJA YA UHURU WA KUONGEA USI-OVERWRITE HOJA NYINGINE ZA MSINGI ZAIDI.

    TULISHAMBIWA 70% YA WATANZANIA NI WAFUATA UPEPO. HAWA WAFUATA UPEPO (THE VOTING FORCE) NDIYO SIKU ZOTE WAMEKUWA WAKITUCHAGULIA WATAWALA. SASA KWA UDHAIFU WAO WATU KAMA THE NGEZES, THE MGAYAS AND MANY OTHER WANAWATUMIA VIBAYA KWA MANUFAA YA WACHACHE.

    TUFANYEJE TUPUNGUZE KUNDI LA WAFUATA UPEPO, NI CHANGAMOTO KUBWA AMBAYO IKO MBELE YETU.

    ReplyDelete
  18. Mwandishi wa Mada ameonyesha mapungufu makubwa katika Kutumia mafanikio ya Siasa kama ndio kipimo cha Uongozi bora
    Kiongozi bora anapimwa kwa Mabadiliko ya uchumi,Upanuzi wa Demokrasi,mapinduzi katika Elimu na Teknolojia,upatikanaji wa huduma muhimu kwa wananchi kama Malazi,Maji,Umeme,chakula
    Je kwa hivi ni kiasi gani kikwete kafanikiwa,ndio hapo tunaweza kumwita kiongozi bora

    Mdau Istanbul

    ReplyDelete
  19. Kwa mwananchi wa kawaida kabisa, atapima uzuri wa kiongozi kwa kuangalia kama ametekeleza yale aliyoahidi kwenye kampeni za kugombea uongozi wake, be ujumbe wa nyumba kumi, udiwani, ubunge au Urasi, hicho ni moja ya vigezo vikubwa vya kupima uzuri wa kiongozi. Pamoja na hayo, vilevile tunaweza kuangalia ameweza kuendeleza yale mazuri ya kiongozi aliyemtangulia, kwa mfano kuendelea na amani iliyokuwepo, kupanda kwa uchumi nk nk.

    Sasa kwa rais wetu JK, tukianza na kauli mbiyu yake ya Maisha bora, imethibitisha kuwa imeshindikana, na yeye mwenyewe alithibitisha aliposema hajui kwanini sisi ni maskini. Alipokuwa anatoa ahadi ya Maisha bora kwa kila mtanzania, alipaswa kujua ni jinsi gani ataleta haya maisha bora, na kwa kujua ina maana angekuwa ana sababu kwanini waTZ hawana maisha bora.
    Sasa kama rais kashindwa hata kutimiza hata ahadi alizozitoa yeye mwenyewe how can someone say amefanikiwa sana?

    Kwa watu wote wenye mapenzi mema na nchi hii na JK, tufike mahali tuseme ukweli, kwani hata yeye ataona challenges ahead, kuliko kushinda kumvika kilemba cha ukoka.

    Na mimi naamini hata yeye ukimuuliza mafanikio yake atakuwa anayajua, lakini alipojikwaa inaweza ikawa ngumu kidogo kusema, so sisi watanzania wa kawaida tutamwambia rais wetu kwani tunapenda aone ili apime kama ana mapenzi mema na nchi hii achukue uamuzi wa busara.

    ReplyDelete
  20. SWALI LA MSINGI
    KWANINI LINAPOKUJA SUALA LA KIKWETE UDINI UNAKUWA KIGEZO?
    MTU AKIMSIFIA KIKWETE WATU WANASEMA NI KIBARAKA AU MUISLAM NA MTU AKIMPINGA KIKWETE BASI HUYO NI ADUI/SI MUISLAMU HII NI KWANINI?
    KWANI HAKUNA MUISLAM ANAYEMPINGA KIKWETE??AU HAKUNA MKRISTO ANAYEMUUNGA MKONO KIKWETE??
    MIMI NAAMINI WAPO WAISLAMU WANAOMPINGA KIKWETE NA WAPO WAKRISTU WANAOMUUNGA MKONO KIKWETE. NA KAMA HAKUNA MKRISTO ANAEMUUNGA MKONO KIKWETE AU MUISLAMU ANAEMPINGA KIKWETE(KWENYE MAMBO FULANI...SIO KUPINGA TU NA KUKUBALI BILA MSINGI) BASI WATANZANIA NI MALIMBUKENI NA MBUMBUMBU,HATUTAENDELEA KAMWE

    ReplyDelete
  21. Hakuna cha udini wala nini! Mimi mwenyewe ni muislam lakini JK hana sifa ya uongozi, Kuanzia speech zake, utendaji wake wa kazi, in short jamaa ni very weak. Amefanikiwa katika kuwa na totoz(vimada) mpaka uswahili hiyo sifa tunampa.. Handsome boy !! Lakini kumbukeni hakuna cha u handsome na utendaji wa kazi.... Angalia maisha ya mtanzania ndio utajua nchi inaelekea wapi!!!

    Hakuna cha uongozi mzuri wala nini, matatizo matupu!! Namsipo badilika kufanya maamuzi ya maana mtaendelea kukamata kwenye dala dala!! Watu (tu/wa) endesha gari ambazo wewe uwezi kuimagine ndani ya hapa hapa TZ!!! Mjinga umekalia kusifia ujinga

    ReplyDelete
  22. Wengine wamepewa ticket za kuzunguka sehemu mbalimbali duniani basi wanaishia kutoa habari za kikwete kwenye blong zao kila wakati...

    Kujipakulia minyama mara ohh anko nani akiwa bujumbura mara oh anko naniii kala pozi.. fanyeni kazi acheni porojo zisizo namsingi..
    Umeshazeeka acha usela usio na mpango.. Sura kama mizengwe pinda!!
    Unaboa watu wanashindwa kukuambia tu kwa kuwa ni blong yako...Hapa USA watu wamechoshwa na vijipicha vyako vya kishamba .
    Watu wanakujua kuwa wewe ni anko fulani acha ushamba kenge wewe...

    ReplyDelete
  23. mwenye macho haambiwi tazama hakuna udini wala mchawi wote tunajua ahadi za jk tunaona maisha yalivyo wewe mtoa maoni unayeleta mambo ya uisilamu wewe ndio mdini mkubwa JE LIPUMBA KILA SIKU ANATANGAZA KUWA ANAMFAHAMU KIKWETE TOKA WAKO CHUONI KUWA HANA SIFA JE LIPUMBA NI MGALATIA?watoa maoni wengine bwana ni bora mkanyamaza kimya kuliko kutoa pumba zenu humu

    ReplyDelete
  24. ndugu zangu waisilamu kila kitu ninyi mnalalamika ina maana kikwete akikosea watu waogope kumkososoa kwa sababu ni muisilamu?JAMANI WAISILAMU ANGALIENI JAMUHURI YA KIISILAMU YA IRANI VIONGOZI WOTE RAISI HADI BALOZI NI WAISILAMU LAKINI KILA SIKU KUNA MAANDAMANO YA KUPINGA SERIKALI SWALI JE KUNA WAKRISTO KULE IRANI?tujaribu kuwa na hoja za maana badala ya kukalia udini hautatusaidia kitu,tuwe tunajifunza habari za duniani kuliko kukurupuka tu,somalia mbona wote ni dini moja ila wanachinjana kila siku,kaka MITHUPU nasikitika sana tunapojadili mustakabali wa nchi wengine wanaanza udini ndio maana tunazidi kuwa maskini ok

    ReplyDelete
  25. mimi naona hii nchi tuwaachie ndugu zete wa nyota na mwezi labda wataridhika lakini bado hata wao wataanza kubaguana maana

    ReplyDelete
  26. Gazeti la Tanzania Daima 22 Desemba; 2009
    Ahadi za JK zaleta kizaazaa
    • WANASIASA WAANZA KUTUNGA UWONGO WA KAMPENI 2010

    na Grace Macha, Moshi

    BAJETI isiyotosha ya barabara imekwamisha utekelezaji wa ahadi ya Rais Jakaya Kikwete ya ujenzi wa barabara kiwango cha lami mwaka 2005, na sasa Bodi ya Barabara imeitaka Ofisi ya Wakala wa Barabara (TANROADS) mkoani Kilimanjaro iwafundishe wanasiasa namna ya kuwajibu wananchi.
    Mwenyekiti wa bodi hiyo ambaye pia ni Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Monica Mbega alisema hayo jana wakati wa kikao chao baada ya Meneja wa TANROADS mkoani hapa, Tumaini Sarakikya, kueleza kuwa barabara zitakazokuwa zimekamilika ifikapo mwakani ni sehemu tu ya barabara hizo. Sababu kubwa ya kutokamilika kwa barabara hizo ni bajeti ndogo waliyotengewa.
    Sarakikya alisema kwa sasa taratibu zote za ujenzi wa barabara hizo umekamilika na utekelezaji wake umeshaanza kwenye baadhi ya maeneo. Hata hivyo alidokeza kuwa utekelezaji huo wa awamu unakwamishwa na bajeti ndogo, kwani wametengewa sh bilioni 3.25 kwa barabara zinazohitaji kutengewa zaidi ya sh bilioni 28.
    Kutokana na majibu hayo, Mbega alisema jambo hilo litakuwa gumu kueleweka kwa wananchi wa kawaida, hivyo ni vema TANROADS wakawapa wanasiasa kauli nzuri ya kuwaeleza wananchi ambao wanataka barabara kama walivyoahidiwa na Rais Kikwete.
    “Tuwe na kauli wanasiasa wajue jinsi ya kuelezea hili kwa wananchi kwani wanataka barabara, haya ya taratibu zenu hawajui… ikiwezekana tuwaeleweshe kuwa utekelezaji wa ahadi ya Rais Kikwete utatekelezwa ndani ya vipindi vyake viwili vya utawala,” alisema Mbega.
    Alisema hiyo itawawezesha wanasiasa kutumika katika kutolea majibu kwa wananchi juu ya ahadi za ujenzi wa barabara zinazotolewa na viongozi, ingawa baadhi ya wabunge ambao ni wajumbe wa kikao hicho waliliambia Tanzania Daima kuwa wao watawaeleza ukweli wananchi kuwa ahadi hiyo ya Rais Kikwete haitekelezeki.
    Awali Mbunge wa Vunjo, Aloyce Kimaro (CCM) aliuliza swali akitaka kujua ujenzi wa barabara hizo utakamilika lini na endapo fedha za kuzijenga zipo kwa kile alichodai kuwa wananchi wanahitaji majibu ya uhakika.
    Naye Mbunge wa Mwanga ambaye pia ni Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Jumanne Maghembe, alisema madereva wengi wa magari nchini wanapewa leseni siku za Jumapili hali aliyosema inachangia madereva hao kushindwa kusoma alama za barabarani.
    Alisema hayo alipokuwa akielezea umuhimu wa kuwekwa kwenye barabara kuu eneo la Lembeni wilayani Mwanga kwa kile alichodai kuwa eneo hilo zimekuwa zikitokea ajali nyingi ambazo zimesababisha vifo vya wanafunzi 10 wa Shule ya Sekondari J.K Nyerere kwa kipindi cha miaka minne, hivyo akashauri suluhisho ni kuwekwa matuta.
    “Mnataka niwakaribisheni kwangu Krismasi kuna mtoto kafa mje kuzika ndio muelewe kuwa eneo hilo linahitaji tuta?” alihoji Maghembe na kuongeza kuwa kimsingi hapa nchini hakuna barabara kuu (highway) kwa kile alichosema kuwa barabara nyingi kuu ndizo hizo hizo zinazotumiwa kama za katikati ya mji.
    Hata hivyo, mbunge wa Moshi Mjini, Philemon Ndesamburo (CHADEMA), alisema ni vema wajumbe wa bodi hiyo wakaangalia hasara zinazotokana na kuwepo kwa matuta hayo kwenye barabara kuu kutokana na ukweli kuwa zinatumiwa na watu wa mataifa mbalimbali hivyo wazingatie sheria za kimataifa katika hilo.
    Aidha, kwenye kikao hicho ilionekana ni vema leseni za pikipiki zikatolewa kwa madereva waliopatiwa mafunzo kwenye chuo cha ufundi stadi (VETA) na wauzaji wa pikipiki hizo wawauzie wateja wale tu watakaoonyesha leseni zao.
    Pia iliamriwa matuta na viashiria matuta viwe katika kiwango kinachokubalika ili visiharibu magari wala kusababisha ajali, hivyo yale ambayo ni makubwa yapunguzwe.

    ReplyDelete
  27. DJ umenene vyema,

    ila mwishoni umeharibu,

    tatizo si wasaidiz, kwan hata hao wasaidiz wamewekwa na mtu/kichwa cha nchi, rais kikwete,kwa maneno mengine tatizo hapa ni rais tuu,
    rais hajui, ashikilie lipi, afuatilie lipi, na atekeleze lipi,

    mtoa mada, naona kaangaika tuu kwenye kuandika maneno mengi kuhusu malumbano, ila hajatoa mtizamo kwa mambo ya manufaa nchini, kama miundombinu(as DJ clarify), hospital, barabara, shule, walimu, vyuo, malecturer, ubora wa elimu, maji, vyanzo vya nishati, makazi, mipango mijina mambo mengine mengi,

    rais anakaa kimya, pale nchi inapopoteza ela nyingi kwenye kuwapa watu matrekta, ilihali wakulima hao wakiwa wanategemea kilimo cha mvua za msimu, ili haliitaji mtu mwenye degree ya kilimo kutambua kwanzo unaitaji vyanzo vya maji vya hakika, sabb ya umwagiliaj, then vitendea kazi sabb ya kilimo,

    all in all, mi s=hitimisha kwa kusema, rais wetu ni tatizo kubwa tena sana tuu, kila kukicha rais yupo nje ya nchi, na anasafiri na jopo la watu kadhaa, wi think we need someone atakeyetusaidia kutupa hesabu huyu bana mkubwa ametumia kias gan cha walipa kodi kwa safari zake walau za mwaka huu tuu.

    oca

    ReplyDelete
  28. anko michuzi wewe ni MAN OF THE PEOPLE tunakupenda sana unatupa habari nzuri Mungu akubariki bro

    ReplyDelete
  29. Aliyeandika hii article ana sound kama mwanafunzi wa primary school au mtu mwenye elimu ya darasa la saba. Hajaongea hoja yoyote ya nguvu wala point yoyote ya msingi. Amepiga porojo ya kisiasa na yeye alijua ndio maana hakuandika jina lake. Kaandika article nzima bila takwimu hata moja. This guy is a fool.
    Hali ya kisiasa ni nzuri (kipofu peke yake ndiye anaweza kusema hali ya kisiasa ni nzuri TZ). Vyama vya kisiasa vimepewa uhuru-lini havikuwa na uhuru (there is no difference from Mkapa and Mwinyi era). Kama CCM itayumba nchi itayumba -CCM inayumba sasa ivi than any other time in our history. Watanzania wamepewa uhuru na vyombo vya habari vimepewa uhuru wa kuongea. Watanzania wanataka uhuru mmoja tu-uhuru zidi ya umaskini na sio pumba za uhuru wa kuongea.
    Tupe takwimu ya nini Kikwete alichofanya ambacho ni bora zaidi ya Mkapa, Mwinyi au Nyerere. Mawaziri wake wote ni hovyo kasoro wale aliorithi kutoka kwa Mkapa.
    Hana dira hala mwelekeo at least Mkapa tulijua ali-concentrate kwenye Macro economic reform. Sasa niulize Kikwete ameconcentrate kwenye nin -sijui- All i see is him leaving the country and him coming back home for a week and leaving again. Mpaka sasa legacy yake ni u-vasco dagama.
    Watanzania sasa tumeamka hamuwezi kutu-fool ever again. Mnachemka!

    ReplyDelete
  30. Mawaziri wamekuwa na mgawanyiko mkubwa serikalini na hata bungeni kati ya wale wanaopinga ufisadi na wale ambao wameonekana kuutetea ufisadi.

    Rais hajajitokeza wazi kuziba pengo hili. hajajitokeza wazi kukemea. Hajasema wazi anasimama wapi katika hili. Au manaonaje kuhusu hili?

    ReplyDelete
  31. jk alifikiri akiwapa machinga pesa watafanya biashara kukuza uchumi kumbe anachemka tu,nafikiri huyu ni VASCO DAGAMA mpya

    ReplyDelete
  32. nchi inaoongozwa na katiba kuna mambo yako wazi kabisa kwenye katiba unatakiwa kusoma tu na kuwapa watu majibu lakini jk anakimbia maswali ajue kuwa running away is not a solution of solving plobem,mdau nipo canada ila bongo sirudi tena kwa mwendo huu

    ReplyDelete
  33. kila siku kusafiri na wazamiaji kibao wakati kuna watanzania hawasomi kisa hawana ada ya 20000

    ReplyDelete
  34. Balozi Michuzi unaudhi sana unavyobana maoni ya wananchi. Acha hii tabia ya Wana CCM, upo katika Blog ya Jamii sasa, sio Kibaruani.

    ReplyDelete

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...