BAADA ya kusota rumande kwa takribani miaka 3, hatimaye leo hii Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu imemuhukumu kifungo cha miaka 30 jela kijana Rashid Lemblis na kuwaachia huru wengine 9, katika kesi ya wizi wa Sh Milioni 168.5 mali ya benki ya NBC tawi la Ubungo.,

Rashid alihukumiwa kifungo hicho baada ya kukutwa na hatia ya kuhusika katika tuhuma za wizi wa kutumia silaha.

Washitakiwa walioachiwa huru katika kesi hiyo ni Ramadhani Dodoo, Philip Mushi, John Mndasha, Jackson Isawangu, Lucas Nyamaila, Hussein Idd, Mashaka Mahengi, Martin Mndasha na mwanamke pekee katika kesi hiyo Rahma Galos.

Hata hivyo mwanamke huyo ndiye aliyeachiwa huru kabisa na kurudi nyumbani, ambapo waliosalia walirudishwa rumande kutokana na kukabiliwa na tuhuma zingine za unyanganyi wa kutumia silaha, katika kesi nyingine za wizi.

Katika hukumu hiyo, iliandikwa na kusomwa na Jaji Pelogia Kadai, ambaye ndiye aliyekuwa akisikiliza kesi hiyo. Alisema kuwa kwa kutumia ushahidi na vielelezo pamoja na utetezi wa washitakiwa wenyewe, mahakama hiyo imeona kuwa washitakiwa hao wengine hawakuwa wahusika katika tukio hilo lilotokea mwaka 2006.

Mh. Kadai akielezea sababu ya kumkuta na hatia mshitakiwa Rashidi, ni kuwa mshitakiwa huyo baada ya kukamtwa akiwa Mkoani Kilimanjaro yeye ndiye aliyewaonesha polisi gari lilokuwa na silaha.

Mh. Kadai alisema kuwa baada ya uchunguzi na upelelezi wa kesi hiyo, ilibainika kuwa ganda la risasi lililookotwa eneo la tukio katika benki ya NBC, lilisadikiwa kutoka katika moja ya silaha zilizopatikana katika gari la mshitakiwa huyo.

Kutokana na sababu hiyo, mahakama ilimtia hatiani imshitakiwa huyo kwa sababu kuwa atakuwa akifahamu wahusika wakuu wa tukio hilo, kutokana na kukutwa na silaha hizo.

Hakimu huyyo alisema kutokana na mazingira hayo, ni lazima mshitakiwa atakuwa akifahamiana na mamjambazi au alihusika katika tuhuma hizo. Mh. Kadai alisema kuwa mahakama imewaona wengine hawana hatia, kwa sababu upande wa Serikali, ulishindwa kuthibitisha kesi hiyo dhidi yao .

Katika hatua ya awali, Mh. Kadai alisema kuwa upande huo ulishindwa kuthibitisha kesi hiyo hata katika hatua ya gwaride la utambulisho, mbali na kuwa ulidai hapo awali kuwa mashahidi walikuwa wakiwatambua washitakiwa hao.

Aliongeza kuwa utamnbuzi wa washitakiwa, ulimtia wasi wasi hasa kwa sababu ulifanyika miezi mitatu kabla ya washitakiwa kukamatwa na kuwekwa chini ya ulinzi.

Pia aliongeza kuwa washitakiwa hao, walichukuliwa maelezo yao ya onyo siku mbili baada ya kukamatwa kwao, na kwamba jambo hilo lilikiuka sheria inayotaka mtuhumiwa kuchukuliwa maelezo hayo ndani ya masaa 24 baada ya kukamatwa.

Aliongeza kuwa licha ya kuwa tuhuma walizokabiliwa nazo washitakiwa zilikuwa za wizi katika benki ya NBC, lakini upande wa mashitaka katika kuthibitisha kesi hiyo ulikuwa na vipengele vichache ambavyo vilikuwa vikizungumzia tuhuma hizo.

“Nasikitika kwamba upelelezi wa jeshi la Polisi ulishughulikia zaidi historia binafsi za washitakiwa, na kuacha kushughulikia kesi hii iliyowafikisha mahakamani washitakiwa”alisema Kadai.

Kuhusu mazingira ya kesi hiyo, Mh. Kadai alisema kuwa Polisi ilikuwa ikiwaunganisha washitakiwa hao kutoka katika tuhuma tofauti tofajuti walizokuwa wakikabiliwa nazo, na kuwahusisha na kesi hiyo.

Mh. Kadai alisema kuwa mshitakiwa Rahma aliunganishwa katika kesiu hiyo, kutokana na kuwa na uhusiano wa ndoa na mshitakiwa wa kwanza katika kesi hiyo Ramadhani Dodoo.

Baada ya hukumu hiyo kumalizwa kusoma, Kadai alimtaka Rashidi ajitetee ili mahakama iweze kumpunguzia adhabu, ambapo alishindwa kufanya hivyo na kudai kuwa angekata rufaa.

Akiiomba mahakama impunguze adhabu kwa mteja wake, Wakili Majura Magafu anayemtetea Rashidi, alidai kuwa mshitakiwa hiuyo ni mara yake ya kwanza kutenda kosa hilo na kwamba anategemewa na familia yake mbali ya kuwa ni kijana mdogo.

Hata hivyo Jaji Kadai alisema kuwa Sheria inamtaka kutumikia kifungo hicho, kutokana na tuhuma alizokuwa akikabiliwa nazo, na kwamba anayo haki ya kukata rufani kupinga hukumu hiyo.

Rahma aliondoka mahakamani kwsa furaha na nderemo akiongozana na ndugu zake amabo walifika mahakamani hapo.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

Kuna Maoni 2 mpaka sasa

  1. Changamoto kubwa kwa jeshi la polisi Tanzania.

    ReplyDelete
  2. TUNAELEKEA WAPI WADAU?
    Hii ni aibu kubwa kwa serekali, polisi na ofisi ya upelelezi kwa ujumla... maana kama hao sio wezi maana yake walitaka kuwabambikia kesi.. wezi wako wapi sasa?!wametudanganya watanzania kwamba wamekamata majambazi kumbe uongo mtupu.. wanataka wajisafishe wao waonekane wanafanya kazi.. haya sasa yamewatokea puani.. unajua nu bora ingekuwa ni kesi ya hao mafisadi kwa sababu ilifanywa kwenye makaratasi kweli tungesema ok.. inawezekana ushahidi usiwepo sasa hawa jamaa wamefanya ambush live!! kweli unashindwa kuwakamata wahusika unabambikia kesi watu wengine!!! ni aibu tosha.. na kwanini wasimbane huyo aliepatwa na hatia awataje wenzake wako wapi? nafikiri kuna harufu ya rushwa hapa!!! wameshadaka cha juu wanabambikiza kesi kwa wengine!!..

    ReplyDelete

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...