Mkurugenzi Mtendaji na Ofisa Mtendaji Mkuu wa Kampuni ya ndege ya Precision Air Bw. Alfonse Kioko (kushoto), akiwafariji waathirika wa mafuriko ya Kilosa, alipowatembelea jana kwenye kambi ya Mazulia, muda mfupi kabla ya kukabidhi msaada wa mifuko 200 ya saruji na mabati 200 vyenye thamani ya sh. milioni 5.4, kusaidia ujenzi wa nyumba za walioathirika hao, wilayani humo. Mkurugenzi Mtendaji na Ofisa Mtendaji Mkuu wa Kampuni ya ndege ya Precision Air Bw. Alfonse Kioko (kulia), akimkabidhi Mkuu wa Wilaya ya Kilosa, Halima Dendego, msaada wa saruji mifuko 200 na mabati 200 vyenye thamani ya sh. milioni 5.4, kusaidia ujenzi wa nyumba za walioathirika kwa mafuriko wilayani humo. Hafla hiyo ilifanyika juzi mjini Kilosa.
Meneja Masoko wa Kampuni ya ndege ya Precision Air, Bw. Emillian Rwejuna (kushoto), akimkabidhi Mkuu wa Wilaya ya Kilosa, Mh. Halima Dendego, kofia na fulana za kuwagawia waathirika wa mafuriko, hafla iliyofanyika sanjari na kampuni hiyo kukabidhi mifuko 200 ya saruji na mabati 200 vyenye thamani ya sh. milioni 5.4, kusaidia ujenzi wa nyumba za walioathirika hao.


* Serikali kuanza kuwajengea nyumba mpya Juni
* Watoto wengi wabainika hawajaandikishwa shule


Na Ripota Wetu, Kilosa

KAMPUNI ya ndege ya Precision Air imetoa msaada wa mifuko 200 ya saruji na mabati 200 vyenye thamani ya sh. milioni 5.4 kwa waathirika wa mafuriko wilayani Kilosa.

Msaada huo ulioambatanana na fulana na kofia, ulitolewa mjini Kilosa juzi (Machi 10, 2010) huku Mkurugenzi Mtendaji na Ofisa Mtendaji Mkuu wa Precision Air, Alfonse Kioko akikabidhi kwa Mkuu wa Wilaya ya Kilosa, Halima Dendego.

Ujumbe wa viongozi na wafanyakazi wa Precision Air ukiongozwa na Kioko ulikwenda mjini Kilosa juzi kuwafariji waathirika hao, na Dendego aliwashukuru kwa msaada huo.

"Precision imetoa mfuko 200 ya saruji na mabati 200 ikiwa ni pole kwa waathirika, kuitikia mwito wa Rais Jakaya Kikwete kuwasaidia waathirika wa mafuriko... tunatoa mwito kwa kampuni na mashirika mengine kujitokeza kuwasaidia," alisema Kioko.

Mkuu wa wilaya huyo alisema msaada huo utatumika kuwajengea nyumba za kudumu waathirika hao katika eneo maalumu lililotengwa na Serikali, ujenzi unaotarajiwa kuanza Juni mwaka huu.

Akitoa mchanganuo wa athari za mafuriko hayo yaliyoikumba Kilosa wakati wa mkesha wa Sikukuu ya Mwaka Mpya Desemba 31 mwaka jana, Dendego alisema kaya 6,168 zenye watu 25,806 zimeathirika katika wilaya hiyo yenye wakazi 582,000.

Alisema mpaka sasa watu wapatao 9,000 wanaishi kwenye kambi nne tofauti za Mazulia, Kimamba, Kondoa na Chanzulu, zilizojengwa kwa mahema ambayo hata hivyo alisema hayawezi kuhimili mvua za masika zilizoanza kunyesha sasa, na zinazotarajiwa kufikia kikomo Mei mwaka huu.

"Tunahitaji zaidi vifaa vya ujenzi ili kuwajengea nyumba waathirika wakati huu wakiendelea kuhifadhiwa kwenye kambi zao... nyumba nyingi zimebomoka kutokana na mafuriko, na maeneo yaliyoathirika zaidi tumewazuia wananchi wasirejee.

"Wapo baadhi bado wanakaidi agizo la Serikali... wale waliogoma kuhama kwenye maeneo ya hatari yaliyoathirika, wataondolewa kwa nguvu na kupewa viwanja na vifaa vya ujenzi ili wajenge makazi mapya ya kudumu," alisema Dendego.

Akizungumzia waathirika 7,647 (wanaotoka kaya 1,600) walioko kwenye kambi ya Mazulia iliyopo katika kiwanda cha zamani za kutengeneza busati, Dendego alisema wamebaini kuwa watoto wengi kwenye kituo hicho hawajaandikishwa shule, hivyo wataanza mchakato wa kuondoa tatizo hilo.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

Kuna Maoni 2 mpaka sasa

  1. Kwa wanaopokea misaada hii ili wawakilishe huko inakoenda ninaomba ifike. Ndugu zetu wanapata taabu sana. Isije kuwa ikaishia kwenye mikono ya watu WASIOSHIBA. Nchi hii sasa hivi imegubikwa na wajanja, walafi na wasio na huruma. CHAO ni chao, CHETU ni chao na CHA WENZAO ni chao. Ndugu zangu naomba huruma tumuogope Mungu. Misaada inayotoka IFIKE JAMANI IFIKE HIYO.

    ReplyDelete
  2. wewe Rwejuna weweeeee simu na ndege wapi na wapiiii
    any way umejitahidi. Panono hapo

    ReplyDelete

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...