KLABU ya soka ya AFC iliyojipatia tiketi ya kushiriki ligi kuu msimu ujao "inayemelewa na bundi"mara baada ya katibu wa muda wa klabu hiyo,Athuman Mhando kudaiwa kutofautina na kamati ya usajili ndani ya klabu hiyo inaoongozwa chini ya mwenyekiti wake John Mhala.
Taarifa za uhakika zilizolifikia gazeti hili zinadai ya kuwa chanzo kikuu cha mtafaruku huo umesababishwa na kitendo cha kamati ya usajili ya klabu hiyo kuwatema wachezaji 17 ndani ya klabu hiyo katika usajili wa mwaka huu kitendo kilichopingwa vikali na katibu huyo.
Taarifa hizo zinadai ya kuwa hivi karibuni kamati ya usajili ya klabu hiyo iliwatema wachezaji 17 na kupeleka orodha ya majina ya wachezaji hao kwa katibu huyo kwa lengo la kuridhia kitendo hicho ikiwa ni pamoja na kutia sahihi yake katika karatasi yenye orodha ya majina ya wachezaji hao kwa lengo ya kuyapeleka katika shirikisho la soka nchini TFF.
Hatahivyo,inadaiwa ya kuwa katibu huyo alikataa kutia sahihi karatasi yenye orodha ya majina ya wachezaji hao kitendo kilichopelekea kamati hiyo ya usajili kuamua kuipeleka kwa mwenyekiti wa muda wa klabu hiyo,Peter Temu na hivyo kutia sahihi kwa niaba yake.
Katibu wa muda wa klabu hiyo alipoulizwa juu ya madai hayo alikiri kutotia sahihi karatasi yenye orodha ya majina ya wachezaji hao waliotemwa na kutoridhika na hatua iliyochukuliwa na kamati hiyo huku akidai taratibu muhimu hazikufuatwa.
“Ni kweli waliniletea orodha ya majina waliotemwa nitie sahini yangu nikakataa ,mimi niliwaambia ya kuwa walipaswa kuyaleta hayo majina kwanza kwenye kamati tendaji ya AFC tutoe baraka ndipo wachukue uamuzi wao”alisema Mhando
Naye mwenyekiti wa kamati ya usajili wa klabu hiyo,John Mhala alipoulizwa juu ya hatua hiyo alidai ya kuwa wao walipoona katibu kashindwa kuridhia uamuzi wao waliamua kumpelekea mwenyekiti wa muda atie sahihi yake na alifanya hivyo.
“Sisi tulimpelekea katibu atie sahihi akakataa ndipo tukachukua uamuzi wa kumpelekea mwenyekiti akatia sahihi na kuridhia hatua hiyo na orodha tayari tumeipleka TFF tatizo ni kwamba kuna viongozi wanaendesha soka lakini hawajui soka”alisema Mhala.


Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...