'MAEMBE'' AINA ZAKE NI NGAPI?

1.Ulimwenguni matunda,ni mengi yaso kifani,
Idadi yananishinda,kuhesabu sibaini,
Ila embe nalipenda,linanikidhi moyoni,
Jamani nijulisheni,aina zake ni ngapi?

2.Aina zake ni ngapi,wajuzi nijulisheni,
Au ni vitabu vipi, vilochambua makini,
Nipate japo ni kopi,nidurusu nibaini,
Jamani nijulisheni,aina zake ni ngapi?

3.Dodo ninalifahamu,limeshinda kwa thamani,
Hili halinishi hamu,kwangu ni nambari wani,
Sifa na wake utamu,limepasi mtihani,
Jamani nijulisheni,aina zake ni ngapi?

4.Ninalijua viringe,nalijua kwa undani,
Hili kwa mimi Mayange,namba mbili hesabuni,
Sitoingia mkenge,nilionapo gengeni,
Jamani nijulisheni,aina zake ni ngapi?

5.Tabu inapoanzia,ninapofika sokoni,
Fungu linapoanzia,la kwanza na la mwishoni,
Nashindwa tofautia,lipi niweke begani,
Jamani nijulisheni,aina zake ni ngapi?

6.Akianza muuzaji,kuyanadi mnadani,
Hili hapa embe maji,nyonyo ni lile pembeni,
Haya yatoka Rufiji,yale pale ya Pangani,
Jamani nijulisheni,aina zake ni ngapi?

7.Yale yalio kibao,wanunuzi yaoneni,
Yamechumwa leoleo,mali kutoka mtini,
Jina ni embe popoo,hayana dosari ndani,
Jamani nijulisheni,aina zake ni ngapi?

8.Yako mengine kwa pombe,ndiyo yake dizaini,
Sijui yaitwa kwembe,embe papai nadhani,
Ukitwika hiyo pombe,uharo u hatarini,
Jamani nijulisheni,aina zake ni ngapi?

9.Mengine ni kwa achali,majina sijabaini,
Si matamu ni makali,yasisimsha mwilini,
Mango piko pilipili,nayo ni maembe gani?
Jamani nijulisheni,aina zake ni ngapi?

10.Kwa hesabu nimeshindwa,nimefeli mtihani,
Nawaachia wapendwa,nyie magwiji wa fani,
Edita wangu mpendwa,liweke ukurasani,
Maembe yalivyo mengi,aina zake ni ngapi?

Na Mdau M. A. MGAMBA

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

Kuna Maoni 2 mpaka sasa

  1. Malenga uko juu!

    Kuna embe bolibo pia nyonyo!
    La tanga lipo tena rojorojo!

    Wasalaam!

    ReplyDelete
  2. AnonymousJuly 08, 2010

    Haahaa shairi no 8 linanichekleshaaa. Malenga oye oyeeoyee. Je embe ng'ong'o.ankal bwana mwambie malenga atunge kitu cha jambochatt mue natamani nifurahi najua hilo shair litanicheklesha saana. Shairi litakuwa na visa vingi vya chatty wapiiiii malenga tunga mie nitakutunza. Mapesa.

    Yabinty

    ReplyDelete

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...