1. UTANGULIZI

Hivi karibuni vyombo vya Habari, hasa vyombo vya Habari vinavyotumia njia za electroniki au mtandao, yametolewa madai kwamba lipo ombwe la uongozi (vacuum of leadership) katika Uongozi kwa ngazi za Mawaziri. Aidha, imeelezwa kwamba, kufuatia Rais kuliaga Bunge na kwamba, Rais anatarajia kulivunja Bunge la Tisa linalomaliza muda wake tarehe 1 Agosti, 2010, Makatibu Wakuu wa Wizara za Serikali ndiyo wanafanyakazi za Mawaziri.

Kwa kuwa kuwepo au kutokuwepo kwa Baraza la Mawaziri si suala la Katiba na kwa kuwa uelewa wa masuala haya si sawa kwa wananchi wanaosoma habari hizo, ninashawishika kutoa ufafanuzi huu kuepusha upotoshaji unaofanywa na waandishi wa makala hizo. Ama, ninawahimiza wananchi kusoma Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kila inapowezekana ili wajiongezee ufahamu wa uendeshaji wa shughuli za dola na Serikali kwa ujumla.


2. MAMLAKA YA BUNGE
Mamlaka ya Rais ya Kuvunja Bunge yanatokana na masharti yaliyomo kwenye Ibara ya 90(2) ya Katiba ya Nchi. Kwa ajili ya ufafanuzi huu, Rais analivunja Bunge kwa sababu Bunge limemaliza muda wa uhai wake kwa mujibu wa Ibara ya 65 ya Katiba. Hivyo, Rais alikwishalihutubia Bunge na kuliaga. Katika hotuba ile, Rais hakulivunja Bunge. Rais atafanya hivyo, kwa kutoa Hati Maalum itakayotangazwa katika Gazeti la Serikali. Shughuli za Bunge “zimesitishwa” hadi hapo Tangazo hilo litakapotolewa. Watu waliokuwa Wabunge wa Bunge hili wataendelea kuwa Wabunge halali hadi siku itakayotajwa kwenye hilo Tangazo la Serikali. Rais anapovunja Bunge kwa mamlaka aliyopewa na Ibara ya 65 ya Katiba na kwa kuzingatia sababu zilizoainishwa katika Ibara ndogo ya (2) ya Ibara ya 90 ya Katiba, mambo yafuatayo yanatokea:–
(a) shughuli za Mikutano ya Bunge kwa Bunge hilo zinakoma; na
(b) hakutokuwa na Mikutano ya Bunge ya kawaida mpaka Rais atakapoitisha Bunge Jipya.

3. BARAZA LA MAWAZIRI
Baraza la Mawaziri linaundwa chini ya Ibara ya 54 ya Katiba. Wajumbe wa Baraza la Mawaziri ni pamoja na Makamu wa Rais, Rais wa Zanzibar, Waziri Mkuu na Mawaziri. Manaibu Mawaziri si wajumbe wa Baraza la Mawaziri. Kwa mujibu wa Ibara ndogo ya (3) ya Ibara ya 54 ya Katiba, Baraza la Mawaziri ndicho chombo kikuu cha kumshauri Rais katika masuala yote yanayohusiana na utekelezaji wa madaraka yake kwa mujibu wa masharti ya Katiba na kwa masuala yote yatakayoletwa katika Baraza hilo kwa maagizo ya Rais. Wajumbe wote wa Baraza la Mawaziri, isipokuwa Makamu wa Rais na Rais wa Zanzibar, ni Wabunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Kwa mujibu wa masharti ya Katiba, kuvunjwa kwa Bunge hakuathiri kuwepo kwa Baraza la Mawaziri. Kwa maana nyingine, kuvunjwa kwa Bunge si moja ya matukio yatakayokifanya Kiti cha Waziri au Naibu Waziri kuwa wazi. Matukio yanayosababisha kiti hicho kuwa wazi yamewekwa na masharti yaliyomo kwenye Ibara ya 57(2) ya Katiba kama ifuatavyo:-
(a) endapo mwenye madaraka atajiuzulu au kufariki dunia;
(b) ikiwa mwenye madaraka hayo atakoma kuwa Mbunge kwa sababu yoyote isiyohusika na kuvunjwa kwa Bunge;
(c) ikiwa Rais atafuta uteuzi na kumuondoa kazini mwenye madaraka hayo;
(d) iwapo atachauliwa kuwa Spika;
(e) iwapo Waziri Mkuu atajiuzulu au kiti chake kikiwa wazi kwa sababu nyingine yoyote;
(f) ukiwadia wakati wa Rais Mteule kushika madaraka ya Rais basi mara tu kabla Rais Mteule hajashika madaraka hayo;
(g) iwapo Baraza la Maadili linatoa uamuzi unaothibitisha kwamba amevunja Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma.

Kutokana na masharti hayo, Mawaziri na Manaibu Waziri wataendelea kushika viti vyao na kutekeleza majukumu yao hadi Rais Mteule atakapoapishwa. Vile vile ikitokea kwamba Rais anahitajiwa kumteua Waziri au Naibu Waziri baada ya Bunge kuvunjwa, anaweza kufanya hivyo kwa kumteua mtu yeyote ambaye alikuwa Mbunge kabla ya Bunge kuvunjwa.

Katika kipindi hiki cha Uchaguzi Mkuu, kazi za kiutendaji zinatekelezwa na Makatibu Wakuu, Wakurugenzi na Watumishi wengine. Hata hivyo, kazi zote ambazo zimeelekezwa na Sheria kwamba zitatekelezwa na Waziri, haziwezi kutekelezwa na mtu ambaye si Waziri. Mfano, hati yoyote yenye asili ya kutunga Sheria, haiwezi kutiwa saini na Katibu Mkuu au mtumishi mwingine. Kama ni sharti kufanyika, Waziri ataitwa kufanya kazi hiyo kwa kuwa yeye bado ni Waziri katika Baraza la Mawaziri la Serikali iliyopo.

4. RAIS WA NCHI
Kwa mujibu wa Ibara ya 33(2) ya Katiba, Rais ndiye Mkuu wa Nchi, Kiongozi wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Amiri Jeshi Mkuu. Serikali ya Jamhuri ya Muungano ndiyo yenye mamlaka juu ya mambo yote ya Muungano na yale ya Tanzania Bara. Ibara ya 34(3) ya Katiba inaweka mamlaka yote ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano na yale ya Tanzania Bara mikononi mwa Rais.

Kwa kawaida, Rais anashika madaraka ya Urais kwa miaka mitano tangu achaguliwe kuwa Rais kwa mujibu wa Ibara ya 42(2) ya Katiba na ataendelea kuwa Rais wa nchi hadi muda mfupi kabla ya Rais Mteule hajaapishwa. Hii ina maana kwamba, hata baada ya kuvunjwa kwa Bunge na kuanza kwa mchakato wa kumpata Rais, Makamu wa Rais, Wabunge na Madiwani wapya kama inavyoainishwa katika Ibara ya 42(3)(a) ya Katiba Rais bado ni Mkuu wa Nchi, Kiongozi wa Serikali na Amiri Jeshi Mkuu. Kwa utaratibu huu, kuvunjwa kwa Bunge, kwa namna yoyote ile, hakuachi ombwe la aina yoyote katika Uongozi wa Nchi.

5. RAIS, MAKAMU WA RAIS NA WAZIRI MKUU
Kitendo cha kuvunjwa kwa Bunge hakubatilishi mamlaka wala kutengua wadhifa wa Rais, Makamu wa Rais au Waziri Mkuu. Nyadhifa hizo tatu zinaachwa siku ambapo Rais Mteule ataapa kushika kiti chake kwa masharti ya Ibara za 42(3)(a), 50(2)(f)) na 51(3)(a) za Katiba. Kwa mantiki hiyo, Rais, Makamu wa Rais na Waziri Mkuu wanaweza kushiriki katika mchakato wa kugombea nyadhifa mbalimbali za kisiasa, kwa maana ya kuwa wagombea, bila ya kupoteza hadhi au nafasi zao za kisiasa wanazozishikilia kwa kipindi hicho.

6. HITIMISHO
Kwa kuzingatia masharti mbalimbali yaliyomo katika Katiba, kuvunjwa kwa Bunge hakusababishi kuwepo kwa ombwe la Uongozi wa Nchi. Baraza la Mawaziri litaendelea kuwepo na linaweza kukutana wakati wowote. Hali kadhalika, Rais na Makamu wa Rais wataendelea kutekeleza majukumu yao ya Kikatiba au kisheria. Vile vile, kwa niaba ya Rais, shughuli zote za utendaji za Serikali, zitaendelea kutekelezwa na watumishi wa Serikali kama ilivyoainishwa katika Ibara ya 35(1) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Imetolewa na:

Jaji Frederick M. Werema, Mb
MWANASHERIA MKUU WA SERIKALI

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

Kuna Maoni 25 mpaka sasa

  1. AnonymousJuly 28, 2010

    Asante mwanasheria mkuu. Ukweli ni kwamba, maelezo yako yanachanganya zaidi kuliko kufafanua. Ndiyo maana wananchi tunataka wabunge wasiwe mawaziri. Hakutakuwa na vacuum mpaka serikali nyingine itakapoingia madarakani. Wewe kwa cheo chako unatakiwa uishauri serikali hivyo, lakini hilo haulitekelezi kwa sababu mnazozijua wenyewe.
    Mheshimiwa samahani, mwisho wa jina lako umeandika kifupi..(Mb). Nijuavyo kama local lay man ni kuwa hiyo maana yake ni mbunge, niko radhi kusahihishwa. Kwa maana hiyo na wewe ni mbunge ? Au ni kutokana tu na cheo chako ndiyo unaruhusiwa kuhudhuria vikao vya bunge ? Naomba ufafanuzi juu ya ufafanuzi.
    Asante sana.
    Mwananchi.

    ReplyDelete
  2. AnonymousJuly 28, 2010

    Ankal lazima tukiri kuwa tumekukubali kwa ukomavu wako katika masuala ya kubalance habari. Keep it on (not up, maana hiyo yako inatosha).

    ReplyDelete
  3. AnonymousJuly 28, 2010

    Shukrani,
    Mwanasheria Mkuu wa Serikali kwa kuja kutuelewesha masuala haya ya kikatiba na sheria, ambayo kama si msomi-wa-sheria-katiba inakuwa ngumu kuelewa katiba/sheria hata tukiazima nakala hizo maktaba na kuzisoma.

    Ni matumaini kuwa siku zijazo ukiona tena makala ktk hii globu ya jamii za kuhusu sheria/katiba unazohisi hazikuchambuliwa kwa makini na kwa kina, hutasita kuja ktk globu ya jamii kutupatia ufafanuzi kwa lugha rahisi tupate elewa.

    Ni matumaini watendaji wengine serikalini/mashirika pia watakuwa wepesi kujibu hoja za haja ambazo zinafaa kujibiwa na mwenye-ofisi hiyo.
    Mdau1
    GlobuYaJamii.

    ReplyDelete
  4. AnonymousJuly 28, 2010

    Hivi siku hizi haya majambo yafundishwi shuleni na vyuon vikuu?

    ReplyDelete
  5. AnonymousJuly 28, 2010

    Wewe mwananchi wa kwanza kutoa hoja, nyie ndio mnaozungumziwa na Mwanasheria Mkuu kwenye huu ufafanuzi.

    Kwanza kabisa, hakukuwa na sababu yoyote ya Mtanzania mwenye ufahamu na nchi yake, acha Katiba, nchi tu, kuhoji kuhusu ombwe la uongozi. Hii si mara ya kwanza Tanzania kuingia kwenye uchaguzi na si mara ya kwanza Bunge kuvunjwa.

    Pili, Tanzania si nchi pekee duniani yenye mawaziri wanaotoka kwenye Bunge. Huu ni mfumo ujulikanao kama Mfumo wa Kibunge.

    Suala la kuwa na mawaziri wasiokuwa wabunge limo kwenye utaratibu uitwao Mfumo wa Kirais. Hivi ni vitu viwili tofauti na havitoki hewani tu.

    Tanzania tunaweza kubadili mfumo wetu lakini si kwa sababu eti saa hizi kuna ombwe. HAKUNA OMBWE kwa mujibu wa Katiba ya Tanzania. HAKUNA.

    Aidha, swali lako kwamba Mwanasheria Mkuu ni Mbunge ama si Mbunge, huku ukidhani kwamba kwa kuwa anaingia kwenye Bunge kwa cheo chake basi si Mbunge, linaingia kwenye tatizo lile lile lililojibiwa na Mwanasheria Mkuu.

    Soma Ibara ya 59(5), inasema:
    MWANASHERIA MKUU ATAKUWA MBUNGE... haisemi ataingia bungeni, inasema ATAKUWA MBUNGE.

    Jamani tuijue nchi yetu na sheria zake na Katiba, tusiwe namna hii. Huhitaji kuwa mwanasheria kitaaluma ili kuifahamu nchi yako na mambo yake.

    Mdau,
    Mpiga Nondo Unyamwezini.

    ReplyDelete
  6. AnonymousJuly 28, 2010

    Mheshimiwa AG;

    Ninakubaliana kabisa na maoni ya Anon wa kwanza. Tatizo si maelezo yako au sisi kutoijua sheria au katiba; Tatizo ni hiyo katiba haikidhi hali halisi ya uongozi.

    Kifungu kimoja kinapingana na kingine. Waziri lazima awe mbunge, halafu hapohapo bunge halipo then mawaziri wanabaki yaani ni sawa na stori ya "kuku na yai".

    Ninajua na wewe ni mshauri mkuu wa rais kuhusu sheria na katika. Nina imani kuwa utamueleza kuwa sasa hivi watanzania wana utamaduni wa kusoma katiba na kuhoji vifungu tata, tuvirekebishe mzee. Huwezi kuwa na sehemu moja inayosema "kuchinja Ng'ombe ni kosa la jinai" na sehemu ingine katika kitabu hichohicho inasema " kutokula nyama ya ng'ombe ni kosa la jinai"

    Iwekwe wazi kuwa waziri si lazima awe mbunge ila rais anaweza kuchagua mbunge kuwa waziri. Mbona ni rahisi sana?

    Halafu suala la rais kuvunja bunge ni kinyume kabisa na "Demokrasia" wabunge wanachaguliwa na wananchi na haohao wananchi ndiyo wanaweza kumtoa kumtoa mtu ubunge kwa kuchagua mwingine tu na si vinginevyo.

    Nina hakika ukipekeleka ushauri huu kwa bosi wako basi, hatakuwa na haja ya kuwa na wabunge wa kuteuliwa 10 sijui wa nini zaidi ya kuongezea walipa kodi mzigo wa kuhudumia wawakilishi wa wananchi wasiowawakilisha mwananchi.

    Halafu mheshimiwa AG ningeomba sana pia umfikishie mjomba na kundi lake la CC kuwa nchi hii sasa hivi inahitaji rais anayeweza kuwajishwa na wananchi kupitia wawakilishi wao na si yeye kuwajibisha wananchi kwa kuwaweka kwa muda bila kuwa na wawakilishi wao. Rais awajibike kwa wananchi si CC au Kamati Kuu.

    Kuanza tu tuitishe mkutano wa katiba ili tuwekane sawa badala ya virakaviraka mnavyofanya baada ya kupata baraka za CC au Kamati Kuu

    ReplyDelete
  7. AnonymousJuly 28, 2010

    Anon wa 11.31pm nadhani unachanganya mambo. Tatizo si kuwa katiba inasema nini. tatizo ni kuwa kinachosemwa kinaendana na wakati uliopo? Kwamba nchi yetu sasa ni ya vyama vingi ? Lini tulibadili katiba yetu iendane na wakti huu ?Kama mawaziri wanatoka kwenye bunge na bunge likivunjwa hiyo waziri mbunge unamtoa wapi tena ? Inabidi tuchague mfumo unaotufaa kwa sasa, haya mambo ya ku copy and paste hayafai tena. Hope you are not doing the same kama kweli unapiga "nondo" And what is that to an academician ?
    Kusema kuwa mwanasheria ni mbunge is wrong. Anawakilisha akina nani ? Serikali au nani ? Anapiga kura kama wabunge wengine ? Au anapata tu posho na marupurupu kama mbunge mwakilishi ? And who pays for all that ? Ni hizo kodi setu tu ? Ndugu yangu, naomba uelimike ukisoma. Usijekuwa mfuata maandishi,maana tunao wengi na mpaka leo hii walipeleki taifa hili popote. Use your head to think critically, will you,Please.

    ReplyDelete
  8. AnonymousJuly 29, 2010

    we unayejiita Mdau, Mpiga Nondo Unyamwezini sijuwi ukisema unyamwezini una maana gani? mimi naelewa unyamwezini ni tabora na kidogo mitaa ya shinyanga.
    lakini kama unaongea kimjini kwamba unyamwezini ni marekani au ulaya, basi:-
    1.) mbona hujajifunza jinsi serikali za wenzetu zinavyoshirikisha wananchi kwa kutoa elimu za uraia mara kwa mara?
    umenikera uliposema, "Kwanza kabisa, hakukuwa na sababu yoyote ya Mtanzania mwenye ufahamu na nchi yake, acha Katiba, nchi tu, kuhoji kuhusu ombwe la uongozi. Hii si mara ya kwanza Tanzania kuingia kwenye uchaguzi na si mara ya kwanza Bunge kuvunjwa."

    2.) ni nani mwenye wajibu wa kutupa elimu ya uraia inayohusu katiba? ikiwa kila mtu atajitafutia namna yake kupata ufahamu juu ya katiba badala ya mamlaka husika, basi tutatoka na tafsiri elfu tofauti katika kila kipengele.
    umenikera tena kwa kusema, "Jamani tuijue nchi yetu na sheria zake na Katiba, tusiwe namna hii. Huhitaji kuwa mwanasheria kitaaluma ili kuifahamu nchi yako na mambo yake."
    nyongeza: ina maana michuzi kakuhudhi kumtafuta mwanasheria mkuu afafanue badala ya kumwacha 'mjuzi' kama wewe utufokee mtandaoni.

    ReplyDelete
  9. AnonymousJuly 29, 2010

    Pumba tupu, wote! Sirudi Bongo hata kwa nini. Eti ombwe, sijui nini, ... kila mtu anajifanya mjuaji Bongo! Hata mkijifanya mna misamiati, vumbi liko pale pale. We live only once in our lives, it's better to live in a better place in the world.

    Ukiishi Bongo, hata kama uko wapi huwezi kulikwepa vumbi na harufu mbaya!

    Oya Chiaz Mchizi

    ReplyDelete
  10. jibaba la nondozz muzumbeJuly 29, 2010

    jamani issa michuzi ni mwandishi wa habari mzuri sana hasa kwa uzushi. anapoona blogu yake haitembelewi sana, anaaza kuzusha. kama anavyozushaga na john mashaka. basi leo niwape siri ndogo, hakuna mtu anayeitwa Mashaka. Huyu ni character Fulani ambaye michuzi amemjenga ili blogu yake itembelewa sana. Nimejaribu kufanya uepelelezi hasa kwa watu wanaoshi marekani ili wangalau tumuone huyu Mashaka, lakini wote, hakuna hata mmoja amabeye amekiri kukutana au kumuona Mashaka. Na mara tu anapoandika kitu kwa michuzi, utadhania dunia inaama, comments ni nyingi kupita maelezo. Wa maana hiyo I AM SKEPTICAL WITH THE actual existence of this character the author, called John Mashaka. He is never opposed in the public, Michuzi isa lways glorifying him I am always fascinated with his unusual way of thinking. He has a very glossy means of presenting hia ideas to the right audience. Some times what you write seems to good to be true, and that makes me skeptical whether you are the true author of your articles. However, your assessment is mostly applicable in the US and Europe. Tanzania is not in the level or scale of your thinking, tone down your rhetoric, because even though you have convincing power and very valid arguments, it is unfortunate that you are pushing wrong agendas to wrong people. People like Zitto Kabwe are double dealers; they are trying to get what they can from Mining companies and at the same time trying to secure their votes with electorates by throwing any idea into the public. I second your article, it is well written and well researched, hope those in power do read them Mashaka Does not Exist. Globolization is something you (Michuzi) can discuss with your peers and don’t bring in the public forum. Michuzi hacha kutuchezea rafiki yangu sisi ni watu wazima mtu wangu, tuache ka amani, huyu Mashaka kamuuuze kwenye magazeti kwa sababu hakuna character kama Mashaka, ni jina tu umejitungia ili kupromote globu yako bwana, hacha janja ya nyani……….binadamu gani ana akili kama hivyo, hata kamau alisema kwamba huyo atakuwa mkenya kwa maana he does not exit. Wewe mtu awepo na hasiwepo hata mmoja nayemfahamu? kwa maana hiyo hili tatizo la boss utunzi tu wa michuzi kuvutia kwenye globu yake kwani anko kamau naye kafariki dunia, bongo balaa

    ReplyDelete
  11. Mbunge Mtarajiwa 2015July 29, 2010

    Mheshimiwa MM,Mb.
    Ingawa tumekuwa tunapitia vipindi hivyi vya mpito kila baada ya miaka 5, ni sahihi katiba inabidi iangaliwe upya.
    Kama katiba inasema Waziri Wa serikali ya JMT lazima awe Mbunge, Basi bunge likivunjwa, huyo waziri atakuwa amepoteza ubunge na hastahili kuwa waziri tena.
    Unaposema Waziri aitwe kusaini sheria, hio sheria imetungwa na nani? Hakuna kitu kama hiko bwana. Sheria inatungwa na bunge.......toka Rais kuhutubia bunge na kuvunjwa ni angalau siku 10--ambazo zinapewa kwa mawaziri kumalizia viporo kama hivyo. Sasa bwana mwanasheria unazidi kutuchanganya tu hapo.
    Binafsi sioni shida mbunge kuendelea kuwa mbunge mpaka pale atapodondoshwa kwenye chaguzi na bunge jipya kusimikwa. Watanzania tuamke sasa hivi.

    ReplyDelete
  12. AnonymousJuly 29, 2010

    Kwa maelezo ya mwanasheria mkuu na maoni ya wachangiaji, ni wazi kwamba katiba yetu ina mtazamo mkubwa wa chama kimoja na ni vigumu vyama vya upinzani kupata haki sawa. Wateuliwa wote wanaopewa madaraka wanakuwa ni wanachama wa chama tawala hamuoni kuwa bado kivitendo tupo ktk utawala wa chama kimoja?

    ReplyDelete
  13. AnonymousJuly 29, 2010

    Wanablogu,

    Kitendo cha Watanzania kuhoji katiba yao ya nchi na uamuzi wa Mwanasheria kujibu hoja zilizotolewa ni dalili nzuri sana kuwa (kama nchi) tumepiga hatua.

    Majibu ya Mwanasheria Mkuu na hoja za Watanzania kama zilivyoletwa hapa zinaonyesha dhahiri kuwa Katiba yetu imepitwa na wakati.

    Tunakoelekea ni kuzuri na tusichoke kuhoji, kila mmoja wetu mwenye duku duku na vipengele vya Katiba akihoji; iko siku kutakuwepo na mkutano wa Katiba.

    Kwa upande wangu sipendezwi kabisa na Madaraka makubwa tena lukuki anayopewa Rais na Katiba yetu. Kwa mfano, sioni mantiki yoyote yenye kuonyesha uwajibikaji na maendeleo (zipo mantiki za kisiasa) kwa Katiba kumruhusu Rais kuwa na mamlaka ya kuteua Wabunge na Majaji.

    Maoni yangu ni kuwa; Wabunge wote wawe wanachaguliwa na Wananchi. Kwa upande wa Majaji wote wapya majina yao yawe yanapendekezwa na Rais kwenye Bunge (kama ilivyo kwa Waziri Mkuu), kisha wanajadiliwa, kuhojiwa na kupitishwa na Bunge.

    Nawakilisha.

    Phares,
    Reading, UK.

    ReplyDelete
  14. AnonymousJuly 29, 2010

    yani wewe (Tarehe Thu Jul 29, 12:50:00 AM, Mtoa Maoni: Anonymous Anonymous)u actual set down ukasoma article yote halafu ukaandika comment kama hiyo!!! kama mtanzia tunakoomba hata usirudi wewe ni adui wa maendeleo yetu...soma rudi nyumbani jaribu change the system siyo ati unabaki huko kubeba box tu...yani wewe unatoa comment kama hiyo juu ya nchii yako...haki hata usiridi adui wamendelea tu wewe..kwanza i bet u wewe shule imakishinda huko umekaa umeoza u have nothing cha karudi nacho nyumbani siyo mari wala helimu unijidai ati tanzania vumbi harufu mbaya huwezi rudi ndiyo maana.....yani wewe ungekuwa rafiki yangu halafu najua umeandika comment shallow kama hii nisingeongea na wewe tena///BAKI HUKO ULIPO OZA WEW DONT SHORT MINDED PPL TOO BACK HOME,wenzako wanarudi na elimu zao na hata wale wanarudi na mali zao tu siyo elimu wee unakaa kuandika ati urudi tena na utarudi tu

    ReplyDelete
  15. AnonymousJuly 29, 2010

    HIVI KWANINI WATZ MLIOKO UGHAIBUNI KOMENTI ZENU MARA NYINGI NI ZA KUIPONDA NCHI YETU? JE MNAPATA FAIDA GANI KWA KUANDIKA UPUUZI KAMA HUU MRA OH, BONGO SIRUDI NG'O. SWALI NANI KAKUOMBA URUDI? AU OH BONGO VUMBI TUU, BONGO UZUSHI!!!!!!! N.K. N.K
    NYIE KAMA MLIIKIMBIA NCHI YENU KWA KUONA HAIFAI KWANINI MNARUDI NYUMA NA KUANZA KUFUATILIA MAISHA YA TZ NA KUKANDIA, KAMA NINYI NI RAIA WEMA KWA NINI MSITOE MCHANGO CHANYA KWA NCHI YETU?
    INAVYOONEKANA NINYI HUKO NI WAKIMBIZI TU, RAIA MWEMA HAACHI KUSAIDIA NCHI YAKE POSITIVELY

    ReplyDelete
  16. AnonymousJuly 29, 2010

    Mh.Jaji Welema, nashukuru kwa kuieleza vizuri katiba ya nchi na kila siku unaomba watanzania waisome na kuielewa kwani zamani watu walikuwa hawana mazoea ya kusoma katiba,mawazo ya wachangiaji wengine wanasema hawarudi Tanzania hawa siyo kwamba hawataki kurudi kwasababu ya katiba hawana nauri kutoka Marekani na kwingineko, na hawajapata green card au hawana visa za kutoka na kuingia kwenye nchi walizopo, ndiyo maana wanatukana Tanzania vumbi, haturudi na hasa hawa ni vijana watoto wadogo.Katiba inasema mwanasheria mkuu atakuwa mbunge kwa nafasi yake bungeni, wewe unasema anafanyakazi gani na kwa ajili ya nani? huyu anafanyakazi ya kupitia miswada yote inayokwenda bungeni na anakuwepo kutoa ufafanuzi wa miswada hiyo ambayo ikipitishwa na kusainiwa na rais inakuwa sheria hii ni moja ya kazi ya mwanasheria mkuu wa serikali hili lina tatizo gani? Nina mashaka na wachangiaji wengine na uwezo wao wa kuelewa mambo na kamahamuwezi basi kaa kimya.Kama mnataka katiba ibadirishwe fuata utaratibu sio mnaanza kupiga kelele, jaji Werema una maana nzuri lakini hapa unajadiri masuala na watu waliochoka na maisha, na mengi watabwabwaja hakuna la maana , kati yao ukiwauliza wangapi mneona katiba ya nchi yenu labda hakuna, lakini ukiwauliza miziki mingapi kwa siku wanasikiliza mingi tu kiasi hata wengine masikio yamekufa, hawa ndiyo watanzania wanaokaa nje ya nchi yao.

    ReplyDelete
  17. AnonymousJuly 29, 2010

    Ankal jambo jingine tunaomba umtafute Kamishna wa Kodi atuelimishe jinsi magari yanavyokuwa evaluate yakiingizwa toka nje, maana hapa ktk globu kila mtu alijifanya anajua sheria za kodi kuhusu mwaka wa usajili wa gari.
    Ankal mtafute Kamishna wa Kodi aondoe hali ya walipa kodi kutojua sheria za kodi mpaka wanatoa rushwa au kuomba rushwa.
    Mdau
    Japan.

    ReplyDelete
  18. AnonymousJuly 29, 2010

    Wee anonym wa Thu Jul 29, 10:32:00 AM, I mean what I say! And I'm serious about it. It's better to be a prisoner anywhere in the world, Somalia included, than being a free and even rich man in Bongo.

    Hata ukiwa unashato kutoka katika gari iliyoyoyozeka (yenye kiyoyozi) au offisi ya namna hiyo hiyo au hata homu pia, kamwe huwezi kukwepa adha ya kuishi bongo. You will for sure come accross what I have mentioned, it it true my dear, not a fabricated fact!

    I may come to Bongo just as a tourist to see animals, with a condition that you improve infrastructures! Otherwise I'll join the rest of the world to shun TZ!

    Habari ndiyo hiyo wanawani!

    Chiaaaaaaz Mchizi

    ReplyDelete
  19. AnonymousJuly 29, 2010

    MHESHIMIWA MICHUZI NAKUTOLEA KOFIA. JITIHADA ZAKO ZA KUUPASHA UMMA MAMBO MUHIMU YAWAHUSUYO KATIKA MAISHA NA MFUMO WA SERIKALI ENDELEA KWA SPEED HIYO HIYO BILA KURUDI NYUMBA SABABU YA WANAOPINGA KWA VILE HATUWEZI FANANA KIMTAZAMO WA MAMBO ILA SIKU.

    MWANASHERIA MKUU WA SERIKALI "BIG UP" NAKUPONGEZA KWA KUWA MWEPESI KUANGALIA SHAUKU ZA WATANZANIA NA KUWA MWEPESI WA KUTOA UFAFANUZI, ENDELEA HIVYO HIVYO KWANI TOFAUTI YA WATOA MAONI SI PAZIA LA WENGI WANAOTAKA KUJUA YAWAHUSUYO KUHUSU NCHI YAO.

    KWA TAARIFA WATANZANIA TUKO JUU SANA KATIKA KUJUA MAMBO YATUHUSUYO KATIKA MWUNDO NA UONGOZI WA SERIKALI KUTOKANA NA MFUMO WA ELIMU TANZANIA KUKAZANIA WATU SOMO LA CIVICS, KWANI MATAIFA MENGINE MFANO KAMA MAREKANI UTAONA RAIA WENGI HATA HAWAJUA TOFAUTI KATI YA CONGRESS, SENATOR, SECRETARY MTU MPAKA UNABAKI NA MSHANGAO NA KUJIULIZA WANAPOENDA PIGA KURA WANAPIGIA NANI KWA AJILI YA NINI.

    FIKRA ZA WENGI KUHUSU VIPENGERE VYENYE UTATA KATIKA KATIBA NI VIZURI MHESHIMIWA JARIBU KUVIPITIA NA KUISHAURI SERIKALI KUFANYA UTAFIKI WA KISHERIA KUHUSU KATIBA NA KUUNDA KAMATI YA KUDRAFT MAPENDEKEZO YATAKAYOFANYIWA KAZI ILI KUTOA UTATA UNAOTUPATA WAKATI FULANI.

    ReplyDelete
  20. AnonymousJuly 29, 2010

    kaka michuzi asante sanaa kwa kutuletea taarifa nzuri kama hii kutoka kwa mwanasheria mkuu wa serikali,lakini swali langu kwa mwanasheria ni hili,yeye kasema watanzania tuwe na utaratibu wa kusoma katiba,sawa nakubali ,lakini namuuliza hiyo katiba inauzwa wapi??,maana bongo mara ya mwisho niliiona katiba nikiwa form two 1986,mpaka leo katiba sijaiona,tena hiyo katiba niliiona ilikuwa ni ya mwalimu wetu wa somo la siasa,kaka michuzi hata wewe unaweza kunipa msaada katiba inauzwa duka gani hapo bongo?,maana hata kwenye maktaba yetu nimejaribu kuuliza jibu wanasema hawana!?
    msaada jamani

    ReplyDelete
  21. AnonymousJuly 29, 2010

    ANONY THU JULY 29, 11:14:00AM WATANZANIA WALIOKO NG'AMBO WANAHAKI YA KUIPONDA NCHI YAO KAMA IANONGOZWA KIHUNI IWPO KATIBA INASEMA WAZIRI LAZIMA AWE MBUNGE NA BUNGE LINAPOVUNJWA BADO YULE WAZIRI NI WAZIRI HATA KAMA HANA UBUNGE HUO SI UHUNI WA KATIBA AU NI NINI?

    JAMBO JINGINE HATA KAMA NCHI INAONGOZWA VIBAYA NINYI HUKO NYUMBANI MNACHAGUA WALEWALE WANAOWAONGOZA VIBAYA KWA NINI MSIPONDWE?

    HAPA MAREKANI BAADA YA BUSH NA CHAMA CHAKE CHA REPUBLICAN KUHARIBU WANANCHI WAMECHAGUA OBAMA NA CHAMA CHAKE CHA DEMOCRAT JE NINYI MNAUBAVU HUO? HERI YA WAZANZIBAR NAWAHESHIMU NA SI WATANZANIA BARA AMBAO NI KICHWA CHA MWENDAWAZIMU.

    ReplyDelete
  22. AnonymousJuly 30, 2010

    Mwanasheria Mkuu wa Serikali, asante kwa maelezo.

    Mzee Mwanakijiji, pia asante kwa ufafanuzi wako.

    Mtoa hoja, good questions!!

    (US Blogger)

    ReplyDelete
  23. AnonymousJuly 30, 2010

    Nyie mnaojiita watanzania mliopo nje ya Tanzania tumechoka na lugha na maneno maneno yenu, kwanza bakini huko huko turudishieni pasi za Tanzania. Maisha yenyewe mnayoishi wengi wenu ya shida kuliko hata ya omba omba wa Dar. Eti hamrudi, nani kawaita? Wapo walioko huko ambao tunatambua uwepo wao duniani na sio nyie mnadiriki kusema mambo ya ajabu. Nyie bebeni mabox ndio yawafaa.

    ReplyDelete
  24. AnonymousJuly 31, 2010

    TANZANIA NI NCHI YETU HATA TUKIWA NJE TUNAHAKI YA KUTOA MAONI KWA SABABU TUMEONA WENZETU WANAVYOONGOZA NCHI ZAO NA HAITOSHI TUTARUDI KUWAONGOZA ILI KUWAONYESHA NCHI INAVYOTAKIWA KUONGOZWA KUMBUKA HATA WAKATI WA UHURU NI WALIOTOKA NG'AMBO KAMA MWALIMU NYERERE, KENYATA, KAUNDA, KWAME NKURUMA, MUGABE, BANDA NA WENGINE NDIO WALIOKUJA KUFUMBUA MACHO YA WAKAZI WA NCHI ZAO NA KULETA UHURU.

    UNAMUONA JANUARY MAKAMBA, LAWRENCE MASHA, BERNARD MEMBE AU JOHN MASHAKA NI SHULE ZA NJE HIZO NDIZO ZIWAFANYAVYO WANG'ARE

    TULIOKO NJE TUNAUWEZO WA KWENDA NJE NA KURUDI NYUMBANI WEWE HUNA UBAVU WA KUJA HAPA AMERIKA AU KWENDA ULAYA KIINGEREZA CHENYEWE HUJUI UTAANZIA WAPI KUOMBA VISA? ISITOSHE ELIMU YAKO NI YA TWISHENI UPO HAPO GALAGABAHO? NA NAULI HUNA MILIONI MOJA LAKI NANE ZA TANZANIA UTATOA WAPI WAKATI MSHAHARA WAKO NI LAKI SITA?

    NANI KAKUAMBIA WATU WANAISHI KWA SHIDA ULAYA NA MAREKANI? OMBAOMBA WA ULAYA NA MAREKANI MAISHA YAKE NI TAMBARARE KULIKO ASILIMIA TISINI YA WATANZANIA KWA SABABU ANAUWEZO WA KULA KUKU, MKATE, MAYAI NA MAZIWA KILA SIKU MPAKA ATAKAPO KUFA UPO HAPO?

    NAMNUKUU MWALIMU NYERERE WAKATI ANAIPA BARAKA TUME YA NYALALI KWENDA KUTAFUTA MAONI YA MFUMO WA VYAMA VINGI MWAKA 1992 MWALIMU ALISEMA "nendeni mkakusanye maoni kwa wasomi, wafanya biashara na waliotembea msiende kumuuliza mwanakijiji pale Butiana kama mfumo wa vyama vingi unafaa au haufai kwa sababu wakati mzanaki anashangaa jinsi kombe anavyoweza kufanya maajabu wamarekani na warusi wanashindana jinsi ya kuutawala mwezi"

    KIJANA UMEONA MWALIMU ANAVYOTAMBUA UMUHIMU WA WALIOTEMBEA? AMBAO NI SISI HUKU MAREKANI NA ULAYA MAANA HATA YEYE ALITEMBEA KULE SCOTLAND WEWE CHA KUFANYA KATEMBEE HATA RWANDA UTABADILIKA KIDOGO SIO KUKALIA KUSIHI DAR MUDA WOTE HATER HAINA MAANA SIKU NJEMA KASAGE LAMI NAENDA KUBEBA BOX KWENYE KIYOYOZI HALAFU KUKU MZIMA ANANISUBIRI KWENYE OVEN WAKATI NINYI HUKO NYUMBANI KUKU MMOJA MNAKULA WATU WANANE NA LAZIMA PIA ABAKI WA KULA USIKU, SODA MPAKA WAJE WAGENI.

    ReplyDelete
  25. AnonymousJuly 31, 2010

    Michuzi hii kitu naomba itundike tena juu maana inaondoka kwenye blog wakati watu bado wanahamu ya kutoa maoni

    ReplyDelete

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...