Katibu Mtendaji wa Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA),Ghonche Materego (Kulia) akisisitiza jambo wakati akichangia mada kwenye Jukwaa la Sanaa Jumatatu hii.Katikati ni mwasilishaji wa mada, Bi.Mabel Masasi na Katibu wa CAJAtz,Hassan Bumbuli.
===== ===== ===== ===== ======
Wadau, kama kawaida Jukwaa la Sanaa ambalo sasa limekuwa ni mkombozi kwa wasanii wetu na chanzo mahsusi cha habari na kisima cha elimu, Jumatatu hii lilibeba mada ya Mchango wa Sekta ya Utangazaji Katika Kulinda Maadili ya Mtanzania iliyowasilishwa na Bi.Mabel Masasi kutoka Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA).
Akiwasilisha mada yake ambayo ilivuta idadi kubwa ya watu,Bi Masasi aliyataja majukumu ya mamlaka yake ambayo ni pamoja na kulinda haki na maslahi ya wateja, kuchochea kuwepo kwa watoa huduma waliosajiliwa, kutoa leseni kwa watangazaji, posta na mawasiliano ya kielektroniki, kuweka viwango vya huduma katika mawasiliano nk.
Aidha, aligusia suala la maadili katika vyombo vya habari ambapo alisema kwamba, kumekuwa na kazi za sanaa chafu ambazo zimekuwa zikipita kwenye vyombo vya habari na mamlaka imekuwa ikichukua hatua na kuvitoza faini vyombo hivyo kwa kupitisha kazi chafu za sanaa.
Aliongeza kwamba, mamlaka ya mawasiliano imekuwa ikifuatilia kwa makini programu zote katika redio hususan zile zinazorusha muziki na filamu na kuhakikisha kuwa hakuna kazi chafu za sanaa zinazopita.Katika hili wadau wengi walihoji lugha chafu zinazotumiwa na watangazaji katika vituo vya redio hususan vya FM.
Hata hivyo, wadau wengi waliochangia mada hiyo, walilalamikia sana rushwa miongoni mwa watangazaji na Ma DJ wa redio na wamesema kwamba, zimepelekea gemu la muziki kupwaya.Katika hili wadau wameiomba Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) kuanza mkakati wa kuvibana vituo vya redio kwani vimekuwa ni tatizo kwa maendeleo ya muziki.
Suala lingine lililoibuka, ni suala la vituo vya redio kutokuwalipa wasanii mirabaha ambapo ilishauriwa kuwa TCRA iwaze sasa kuvibana vituo vya redio na TV ambavyo havilipi mirabaha kwa wasanii.Wazo hili liliungwa mkono na wadau wengi hasa ikizingatiwa kwamba,TCRA ndiyo wanaotoa leseni kwa vituo hivyo.TCRA walisema kwamba, watalifanyia kazi kwa kushirikiana na COSOTA.
Hata hivyo, kumekuwa na tatizo la wasanii wenyewe kusaini mikataba na vituo vya redio ya kutolipwa chochote na badala yake wanaruhusu kazi zao zichezwe bure.Ilielezwa kwamba, wasanii wamekuwa hawajali mikataba na wengine wamekuwa wakisaini kazi zao kupigwa bure bila wao kulipwa.Tatizo hili linaonekana kuwa kubwa na wasanii wamekuwa wakilalama bila kuchukua hatua na kujali kai zao.
Kwa ujumla wadau,Jukwaa la Sanaa ni Mahali ambapo wasanii wanapaswa kufika kwa wingi kila Jumatatu kuanzia saaa 4 hadi saa 6.Ni kupitia Jukwaa hili la Sanaa, tutaweza kufika mbele kutokana na mijadala inayoibuka, elimu inayotolewa na kuwepo kwa masuala ya msingi kuhusu sekta ya sanaa na utamaduni yanayoibuka na kujibiwa.
Jumatatu ijayo yaani Tarehe 23/8/2010, Jukwaa la Sanaa Kama kawaida litakuja na Mada ya URASIMISHAJI WA WASANII,ambayo pamoja na mambo mengine itahusu utambuzi wa wasanii ili kufuta dhana inayojengeka sasa kwamba Msanii ni mtu muongo,mbabaishaji, mchovu na asiye na dili.Tafadhali Usikosekane,Fika.
napongeza sana TCRA kwa kazi nzuri ya kuelimisha jamii, nimebahatika kumsikiliza bi Masasi akiwasilisha mada dodoma kwa kweli ilivutia washiriki wengi na wengi wetu tulielimika. nashauri TCRA iweke utaratibu wa kuelimisha jamii juu ya kazi zake ili waweze kuchangia katika kusimamia maadili ya vyombo vya habari
ReplyDeletenapongeza sana jukwa la sanaa na wasilishaji mada. kwa ujumla TCRA ni taasisi ambayo imefanya vizuri sana katika usimamizi wa sekta nashauri magazeti pia yapelekwe tcra ili yasimamiwe vizuri zaidi
ReplyDeletewasaniii wanajiua wenyewe kwa kukubali kurubuniwa. waweke msimamo kuwakatalia wenye vyombo vya habari waone kama hawatalipwa kazi zao
ReplyDeletewasanii wapunguze kulalamika waboreshe kazi zao
ReplyDeleteHongera sana Mabel nadhani unaapply lectures za hayati Mzee Hokororo wa chuoni Diplomasia katika kutoa mada.
ReplyDeleteMimi hapo nimeivulia kofia Bongo: rushwa kwenye vituo vya redio?! kwa vipi? TAKUKURU kazi mnayo!
ReplyDeleteHata vivyo nimefurahishwa na kuwepo jukwaa hili.Lidumu.