
Chuo cha Muziki cha Zanzibar, DCMA, kinapenda kutoa taarifa inayohusu mwanafunzi aliyepata fursa ya kuhudhuria mafunzo ya utengezaji wa ala za muziki nchini Ujerumani kama ifuatavyo: -
Mwanafunzi wa Chuo cha Nchi za Jahazi, Ismail Muhsin Ali, ameondoka Zanzibar kuelekea nchini Ujerumani kwa ajili ya mafunzo ya utengezaji wa ala za muziki.
Mwanafunzi huyo ambaye pia ni msanii wa ala ya Oud amesafiri tarehe 15 Septemba 2010 kwa ajili ya kwenda kufanya kozi hiyo adimu itakayochukua miezi miwili kuanzia kati ya mwezi wa Septemba hadi mwezi wa Novemba 2010.
Akiwa nchini Ujerumani, Ali anategemewa kufanya kozi hiyo katika Chuo cha Turkish Music Conservatory kilichopo mjini Berlin. Kwa mujibu wa taarifa kutoka kwa mkufunzi wa kozi hiyo, Nima Ramazan, mafunzo atakayopata Ali ni misingi ya mbinu za kufanyia matengenezo ala za Oud na Qanun pamoja na utangulizi wa awali wa ujuzi wa kuunda ala hizo kikamilifu.
Kozi hiyo ya mwanafunzi Ali ni sehemu ya mafunzo ya ngazi ya Diploma yanayotolewa na Chuo cha DCMA kupitia ushirikiano na taasisi za nje na kwa ufadhili wa shirika la misaada ya kimaendeleo ya nchini Norway, NORAD, kama sehemu ya mradi wake wa Elimu ya Sanaa na Utamaduni.
Shirika hilo limekuwa likifadhili miradi mbali mbali ya Chuo cha DCMA tangu mwaka 2004 na kukiwezesha chuo hicho kufikia malengo yake ya kujenga misingi imara ya kuendeleza elimu ya muziki nchini.
Chuo cha Dhow Countries Music Academy ni taasisi isiyo ya kiserikali inayondesha mafunzo ya muziki kutoka kituo chake kikuu kilichopo Mji Mkongwe – Zanzibar kwa kengo la kuhifadhi na kuendeleza urithi wa muziki asilia unaotakana visiwa vya Zanziabr na sehemu nyengine za nchi za Majahazi.
Tunaomba hisani ya kuchapishwa taarifa hii kwa faida ya jamii. Kwa maelezo zaidi tafadhali wasiliana nasi kupitia anwani ifuatayo: -
Kheri A. Yussuf
Development, Marketing & PR Manager
Dhow Countries Music Academy, Zanzibar
Mobile: 077.3 62 0202
E:press@zanzibarmusic.org
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...