Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari,Utamaduni na Michezo,Bw.Ceth Kamuhanda akitoa tamko la serikali kuhusu wamiliki wa kumbi ambao wanaziendesha kinyume cha sheria, kanuni na taratibu za nchi.Kulia kwake ni Mkurugenzi wa Idara ya Utamaduni, Profesa Hermas Mwansoko.
Katibu Mtendaji wa BASATA,Ghonche Materego akisisitiza jambo.Alisema kwamba,BASATA linatoa muda hadi Desemba mwaka huu wamiliki wote wa kumbi wawe wamesajili kumbi zao vinginevyo hatua kali za kisheria zitachukuliwa.
Mjumbe wa Shirikisho la Sanaa za Ufundi,Mzee Nkwama Bhalanga alipendekeza kwamba, waandaaji wa matukio ya sanaa wawe wanapewa masharti magumu yakiwemo ya kutaja idadi ya watu wanaohudhuria kwenye onyesho lao na sifa za ukumbi.
Rais wa Shirikisho la Sanaa za Ufundi,Adrian Nyangamale akichangia mada kwenye Jukwaa la Sanaa.Aliitaka serikali ianzishe Jumba la Sanaa ambalo litakuwa na kazi mbalimbali za wasanii ndani yake kama ilivyo kwa mataifa mengine.
Mbunifu wa mavazi maarufu nchini,Mustapha Hassanally naye aliwasilisha mada yake kuhusu Soko la Sanaa ya Ubunifu wa Mavazi Tanzania na Changamoto zinazowakabili.



===== ===== ========


Wizara ya Habari, Utamaduni na Michezo imetoa miezi mitatu hadi Desemba 31 mwaka huu kwa wamiliki wa kumbi kuhakikisha wanafuata kanuni, taratibu na sheria za kuendesha kumbi zao ikiwa ni pamoja na kuzisajili Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA) vinginevyo hatua kali za kisheria zitachukuliwa.


Akizungumza kwenye Jukwaa la Sanaa linalofanyika kila Jumatatu BASATA, Katibu Mkuu wa wizara hiyo,Bw.Seth Kamuhanda alisema kwamba, kumekuwa na ukiukwaji wa makusudi wa sheria,kanuni na taratibu za kuendesha kumbi hali ambayo imekuwa ikisababisha maafa makubwa yakiwemo yale yaliyotokea Tabora mwaka jana na yale ya Sherehe za Idd El Fetri kwenye Ukumbi wa Luxury wilayani Temeke,Dar es Salaam.


“Tatizo kubwa la watanzania, ni kufanya mambo kiholela, kutokufuata sheria, kanuni na taratibu.Hili limekuwa kwenye mazoea na kwa kiasi kikubwa limekuwa likisababisha matatizo mengi yakiwemo majanga kama yale ya Tabora na Temeke kwenye Ukumbi wa Luxury” alisema.


Alisisitiza kwamba, serikali kamwe haiwezi kuendelea kufumbia macho vitendo visivyozingatia sheria hivyo wamiliki wa kumbi lazima wahakikishe wanafanya marekebisho kwenye kumbi zao na kuhakikisha kufikia Desemba mwaka huu zinakuwa ziko kwenye kiwango kinachokubalika kisheria na zimesajiliwa Baraza la Sanaa la Taifa.


“Serikali inasikitishwa sana na vifo ambavyo vimekuwa vikitokea kwenye kumbi za burudani hasa vya watoto na vijana na inaagiza wadau wote wa burudani hasa wamiliki wa kumbi kuzingatia sheria, kanuni na taratibu zilizopo zinazosimamiwa na BASATA”, aliongeza.


Awali Katibu Mtendaji wa BASATA,Ghonche Materego alizitaja sifa za kumbi zinazokubalika kisheria kuwa ni pamoja na kuwa na milango ya kutosha inayofungukia nje,vyoo nadhifu vya wanawake na wanaume, miundombinu kwa walemavu, vifaa vya kuzimia moto, maegesho ya vyombo vya usafiri na ulinzi kamili.


Aidha, alisema kuwa kumbi zote lazima zisajiliwe Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA) lakini changamoto kubwa ni kasi ndogo ya wamiliki kusajili kumbi zao.Katika hili Katibu Mkuu,Bw.Kamuhanda alisema kwamba, ifikapo Desemba mwaka huu kama kutakuwa na kumbi zitakuwa hazijasajiliwa basi hatua kali za kisheria zichukuliwe.


Kwa upande wake,Mkurugenzi wa Idara ya Utamaduni Bw.Profesa Hermas Mwansoko alisisitiza kwamba, muda uliotolewa kwa wamiliki wa kumbi kurekebisha kumbi zao ili ziendeshwe kwa mujibu wa sheria, kanuni na taratibu ni wa mwisho na baada ya hapo hakutakuwa na huruma yoyote.


“Nafasi hii ni ya mwisho kwa wamiliki wa kumbi,BASATA wameshatoa maelekezo yote kuhusu sifa za kumbi.Hatutakuja kukumbushana tena suala hili lazima wamiliki wa kumbi watumie fursa hii iliyotolewa na serikali kufanya marekebisho” aliongeza Profesa Mwansoko.


Pamoja na Jukwaa la Sanaa wiki hii kujikita kwenye suala la kumbi masuala mbalimbali yaliibuka ikiwemo mada ya Soko la Sanaa ya Ubunifu wa Mavazi Tanzania na Changamoto zinazowakabili iliyowasilishwa na mbunifu maarufu wa mavazi Mustapha Hassanaly na kuvuta hisia za wadau wengi.


Wiki ijayo katika Jukwaa la Sanaa, Katibu Mtendaji wa Baraza la Habari nchini (MCT) Bw.Kajubi Mkajanga atazungumzia mada ya Vyombo vya Habari na Utandawazi Katika Tasnia ya Sanaa.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

Kuna Maoni 4 mpaka sasa

  1. Sio kuhusu pesa, health and safety should be given hire priority. things like fire escape, first aid and stewards who should be available in any major events.

    ReplyDelete
  2. Tanzania eeee, Nchi yangu eeeeee, yapendeza eeeee, njoni muoneeee!

    Jamani hawa wazee wanajidhalilisha. Walikuwa wapi mpaka watu wanamiliki kumbi zisizo sifa? Wazee wazima wanasubiri maafa ndio wazinduke!

    Nchi yangu TZ una viongozi wa aina gani wasioweza kuona mbele mpaka maafa yawazindue?

    Ona! Bomoa bomoa! watu wanajenga mpaka wanamaliza wanaishi. viongozi nastuka ohhhhh mmejenga kwenye hifadhi ya barabara! hii ni akili au mat.......

    ReplyDelete
  3. M.M. MwanakijijiSeptember 22, 2010

    Hapana mnatudanganya tu! Tumewaambia kuhusu hili kwa miaka sasa lakini mmeweka pamba masikioni. Ati leo ndio mnakumbuka shuka asubuhi! Kwanini hamkufanya hivyo walipokufa watoto 19 kule Tabora?

    ReplyDelete
  4. Tunaomba serikali isimamie amri yake ya kumbi za starehe kuweka vimeza sauti ( sound proof) kwani ni kero huko mitaani. Unakuta muziki unafunguliwa sauti ya juu sana kiasi kwamba majirani karibu na bar hawasikilizani. Wananchi wengine wana wagonjwa ndani,wengine watoto wadogo na ukifuatilia nyimbo zinazoimbwa ni za kikubwa ,matusi ndani yake nazaidi hazina maadili kwa watoto,au hata maadili ya dini zetu.

    ReplyDelete

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...