

Na Mwandishi Maalum
Katika kuhakikisha kuwa nchi 48 ambazo ni maskini zaidi duniani zinahitimu na kujikwamua na umaskini uliopindukia. India imeahidi kuzisaidia nchi hizo kwa kutoa misaada ya fedha na kiufundi.
Ahadi hiyo imetolewa jana ( ijumaa) na Serikali ya India kupitia Waziri wake wa Mambo ya Nje, Bw. Shri SM. Krishna, wakati wa Kongamano la maandalizi ya mkutano wa Nne wa Nchi hizo maskini kuliko zote duniani utakaofanyika mwezi Mei, Instambul, Uturuki.
Dhima ya Kongamano hilo lililofanyika New Delhi, India lilikuwa ni kujadili jinsi ambavyo ushirikiano baina ya nchi za Kusini ( South-South Cooperation) umesaidia kuchangiza maendeleo ya nchi maskini nyingi kati ya hizo zikiwa ni kutoka Kusini.
Ujumbe wa Tanzania katika Kongamano hilo linalowashirika mawaziri ama manaibu waziri kutoka nchi 32 kati ya 48, umeongozwa na Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Mhe. Mahadhi Juma Maalim (MB).
Miongoni mwa misaada hiyo iyokusudiwa kutolewa na India kwa nchi zote 48 Tanzania ikiwamo, ni pamoja na ufadhili kwa wanafunzi watano kutoka kila nchi ,chini ya mpango wa ushirikiano wa kiufundi na kiuchumi.
Waziri Shri Krishna, anaeleza kuwa India itaanzisha mfuko maalum kwa ajili ya utekelezaji wa Mpango Kazi, mfuko huo ambao ni wa wa miaka mitano (2011-2016) na uonaotarajiwa kupitishwa katika mkutano wa Instambul utakuwa na kiasi cha Dola za Kimarekani 5 milioni .
Katika jitihada hizo za kuzisaidia nchi maskini kujikwamua na hatimaye kuhitimu pia serikali hiyo ya India, nchi ambayo ni kati ya Mataifa manne ambayo uchumi wao unakua kwa kasi duniani. Pia itaweka utaratibu wa mikopo hususani kwa nchi maskini, mikopo hiyo itakuwa na dhamani ya Dola za Kimarekani 500 milioni.
Akizungumza katika Kongamano hilo, Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Mhe. Mahadhi Juma Maalim (MB), ameisifu na kuipongeza Serikali ya India kwa kuwa moja ya nchi ambayo imeonyesha kwa vitendo kuzisaidia nchi maskini zaidi duniani kuondokana na hali hiyo.
Akifafanua zaidi mchango wa India kwa nchi maskini, Naibu Waziri Maalim, amesema kuwa Tanzania ni moja kati ya nchi hizo maskini ambayo kwa kiasi kikubwa imenufaika na misaada ya hali na mali kutoka india.
Anaitaja misaada hiyo kuwa ni Dola za Kimarekani, 132milioni ambazo Tanzania ilizipata kupitia Mfuko wa India-Afrika.
“ Kiasi hiki cha fedha tumepatiwa ili kusaidia sekta ya kilimo ambayo ni sekta muhimu sana katika kujikwamua na umaskini. Fedha hizi zinahusisha pia upatikanaji wa pembejeo za kilimo kama matrekta na kujenga uwezo wa ndani wa kuzalisha matrekta na zana nyingine kupita uhamishaji wa teknolojia” anaeleza, Naibu Waziri.
Anaongeza kuwa Tanzania pia imenufaika kwa msaada wa Dola za Kimarekani, 116 milioni, fedha ambazo India imezitoa kusaidia mradi wa African E- Network. Ambapo kupitia msaada huo Tanzania imeweza kuanzisha vituo vya ICT kwaajili ya huduma za elimu, afya na kituo cha kisasa cha teknolojia ya habari.
Kwa upande wa nafasi za Mafunzo, Mwakilishi huyo wa Tanzania , anaeleza kuwa India imekuwa ikitoa nafasi za mafunzo pamoja na kulipia mafunzo hayo kwa vijana wa kitanzania ambao hasa ndio wanaotegemewa kuiendesha nchi.
Pamoja na kuishukuru India, Naibu Waziri ametumia nafasi hiyo, kwa kutoa wito kwa mataifa mengine yaliyoendelea na hususani yale ya Kusini na yenye uchumi imara kuinga mfano wa India.
Akizungumzia kuhusu mkutano wa Instambul, Naibu Waziri amebainisha bayana kwamba, msimamo wa Tanzania katika mkutano huo, ni kuhakikisha kwamba maazimio yatakayotoka mwishoni mwa mkutano yatakuwa ni yale ya kuzisaidia nchi hizo kuhitimu.
“ Tuna kazi moja tu huko Instambul nayo ni ya kuhakikisha sisi maskini tunahitimu. Kwetu sisi Tanzania tunajua nini tunachokitaka. Tunataka fursa ya kweli ya kujiendeleza, na tunakaribisha washirika wa kweli wa kushirikiana nasi kutafuta ufumbuzi vikwazo vinavyotufanya tusifike huo” anasema Naibu Waziri.
Na kuongeza kuwa washiriki wote wa mkutano huo, kuanzia nchi za LDCs, zile zilizoendelea, zinazoinukia kiuchumi na zinazoendelea lazima kwa pamoja, wafanye tathmini upya ya utashi wa kisiasa wa ushirikiano kuelekea safari hiyo. Tathimini ambayo pia itahusisha ushirikiano kati ya nchi za kusini.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...