Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dk. Mohamed Gharib Bilal, akizungumza na Maofisa Kilimo wa Wilaya ya Arusha wakati alipotembelea shamba la mkulima Suleiman Juma ambae ni mkulima wa mfano aliyepata maendeleo makubwa kwa kutumia Nishati ya BIOGES mjini Arusha leo. Kushoto kwake ni Mkuu wa Mkoa wa Arusha Mh. Isodore Shirima akifuatiwa na Waziri wa Nishati na Madini Mh. William Ngeleja

Mtaalam wa mambo ya umeme katika Taasisi ya Kitaifa ya Utafiti wa Teknolojia ya maendeleo ya Nishati ya Kilimo na Ufugaji CAMARTEC Msafiri Mhumwe akimuonesha Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dk. Mohamed Gharib Bilal, moja ya aina ya taa na baadhi ya vifaa vinavyotumia Nishati Jadidifu ya BIOGES kwenye uzinduzi wa Program mpya ya BIOGES katika ngazi ya kaya, uliofanyika leo katika viwanja vya Themi mjini Arusha. Katikati Waziri wa Nishati na Madini Mhe.William Ngeleja na Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara Mhe. Lazaro Nyalandu.


Mtaalam wa kufua mafuta kwa kutumia mashine ya kienyeji katika Taasisi ya Kitaifa ya utafiti wa Teknolojia ya maendeleo ya Nishati ya kilimo na ufugaji CAMARTEC Abubakar Mwenda, akimuonesha Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dk. Mohamed Gharib Bilal, utengenezaji na ukamuaji wa mafuta ya Alizeti kwa kutumia mashine hiyo, kwenye uzinduzi wa Program mpya ya BIOGES katika ngazi ya kaya uliofanyika leo viwanja vya Themi Mjini Arusha. Katikati Waziri wa Nishati na Madini Mhe.William Ngeleja , Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara Mhe. Lazaro Nyalandu kulia Mkuu wa Mkoa wa Arusha Mhe. Isidore Shirima.


Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dk. Mohamed Gharib Bilal, akiangalia Vifaa vya aina mbalimbali vinavyotumia nishati ya BIOGES vinavyotengenezwa na Bw. George Traser kutoka katika kampuni ya Kakute ya Ujerumani, kwenye uzinduzi wa Program mpya ya BIOGES katika ngazi ya kaya uliofanyika leo kwenye Viwanja vya Themi mjini Arusha.


Mkulima wa mfano aliyepata maendeleo makubwa kutokana na kutumia Nishati ya BIOGES Mkoani Arusha Bw. Suleiman Juma, akimfahamisha Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dk. Mohamed Gharib Bilal juu ya uandaaji na matumizi ya Nishati hiyo, wakati Makamu wa Rais alipomtembelea mkulima huyo shambani kwake Arusha leo, kabla ya kuzinduwa rasmi Program mpya ya BIOGES katika ngazi ya kaya. Katikati Waziri wa Nishati na Madini Mhe. William Ngeleja na Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara Mh. Lazaro Nyalandu . Picha na mdau Amour Nassor wa VPO


Na Penzi Nyamungumi – Arusha

Makamu wa Rais Dk. Mohammed Gharib Bilal amesisitiza matumizi ya teknolojia ya Biogesi nchini kwa maendeleo ya wananchi vijijini.

Alisema hapa nchini takriban asilimia 14 tu ya Watanzania ndio wanaotumia nishati ya umeme na kwamba hali ni mbaya zaidi vijijini wanakoishi takriban asilimia 80 ya Watanzania ambapo ni asilimia 2.5 tu ndio wanaotumia umeme kutokana na uwezo mdogo wa kifedha wa wananchi wakati upatikanaji wa nishati hizo nao hautoshelezi.

Akizungumza kwenye hafla ya uzinduzi wa programu ya uenezi wa Biogesi ngazi ya kaya mjini Arusha Dk. Bilal alisema teknolojia ya biogesi ina sifa ya kuwa nishati safi, endelevu na yenye gharama nafuu na hivyo ni muhimu kuwapatia wananchi ili kuboresha maisha yao.

“Asubuhi ya leo nimepata fursa ya kuitembelea familia ya mtumiaji wa biogesi hapa Arusha, kuona nini kinaendelea katika matumizi ya biogesi na tumeshuhudia namna walivyobadilisha maisha yao,” alisema Dk. Bilal.

Aidha alisema amejionea pia ubunifu wa wananchi katika maonesho yaliyokuwa yameandaliwa wakati wa uzinduzi huo ambapo hakutegemea baadhi yao kufikia hatua ya kutengeneza majiko ya gesi jambo ambalo linaonesha kuunga mkono juhudi za serikali za kuhimiza utumiaji wa gesi ili kupunguza matumizi nishati ya mkaa na kuni ambayo yana athari kubwa kwa mazingira na afya za watumiaji hususan akina mama.

“Tanzania ina gesi nyingi asilia na mtazamo wetu kuwa miaka ijayo tutaitumia kwa matumizi ya nyumbani. Wito wangu kwa vyuo vya ufundi vya VETA vianze kuandaa vijana ambao watakuja kubuni teknolojia za kutusaidia,” alieleza.

Alisema teknolojia ya biogesi ina manufaa katika Nyanja ya ugavi, nishati vijijini, kilimo, afya, usafi wa nyumbani, uhifadhi wa mazingira na hivyo inachangia katika kufanikisha malengo na sera mbalimbali za serikali za kupunguza umaskini na hatimaye kuwaletea maendeleo wananchi.

“Matokeo ya program ya kueneza teknolojia ya Biogesi yanaleta manufaa funganishi yanayohusisha sekta ya kilimo na mifugo, uongezaji ajira, uhifadhi wa mazingira na nishati kwa pamoja. Hili ni suluhisho endelevu kwa matatizo ya nishati vijijini na uharibifu wa mazingira,” alisema Dk. Bilal

Makamu wa Rais alitoa wito kwa Kituo cha zana za kilimo na teknolojia vijijini (CAMARTEC) kujiandaa na kazi kubwa ya uenezi wa biogesi nchini ili kuwawezesha wananchi wengi zaidi wa vijijini kutumia nishati hiyo kwa maendeleo endelevu.

Mapema, akitoa taarifa Naibu Waziri wa Viwanda, Biashara na Masoko Lazaro Nyalandu alisema programu ya biogesi ambayo ilianza mwaka 2009 hadi sasa imeenea katika mikoa 11 nchini na kueleza matumaini yake kwamba ikienea nchi nzima itapunguza ukataji wa miti na hivyo kuokoa hekta zipatazo 8,000 za misitu.

Utekelezaji wa program hiyo unafanywa na CAMARTEC chini ya usimamizi wa Wizara ya Viwanda,Biashara na Masoko na kufadhiliwa kwa pamoja na Serikali ya Uholanzi, mashirika ya HIVOS na SNV.

Kwa mujibu wa Nyalandu mwezi Julai mwaka 2010 Tanzania ilikuwa nchi ya kwanza kati ya nchi tisa za Afrika zinazotekeleza program hiyo kwa kujenga zaidi ya mitambo 100 na hivyo kupewa zawadi ya Ngao ya Afrika ya Biogesi na vile vile Disemba mwaka jana Tanzania ilikuwa nchi ya kwanza katika Bara la Afrika kuwa na mitambo 1021 ya Biogesi.



Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

Kuna Maoni 3 mpaka sasa

  1. haya sasa ndiyo mambo ya maana ambayo tanzania ilipaswa kuyandaa na kuyatumia tangu miakaya 1980s. nishati ya gei itapunguza uharibifu wa mazingira paoja na madhara yanayotokana na kuvuta moshi ktk kupikia kuni.
    ilipaswa familia zote za vijijini ziwe na teknolojia,
    sasa kinachofuata pia ni kuhimiza ujenzi wa makazi bora ya kudumu vijijini yaliyo karibu kabisa na huduma muhimu kama shule,zahanati,na maji. ilikupunguza upotevu wa muda ktk kujenga wa kuhamahama na kuharibu miti,kupunguza vifo vinavyotokana na uchafuzi wa mazingira kwa vinyesi maporini na ndani ya maji, kujenga malambo kwa ajili ya unyweshaji maji mifugo na kutenganisha vyanzo vya maji kwa ajili ya matumizi ya mifugo na kwa ajili ya matumizi ya binadamu. kuweka huduma za umeme wa juwa ktk makazi hayo ya kudumu. kuhimiza ufugaji wenye tija usio haribu mazingira wala kupoteza muda mwingi kwa mfugaji kuhudumia mifugo yenye faida kidogo. kuweka miundo mbinu na kuhimiza kilimo cha umwagiliaji ktk ngazi ya kaya,hii ikiwa ni paoja wa wataalam wa kilimo kutafiti maeneo yanayofaa kuanzishwa miradi hiyo na kuishauri serikali kupanga kugawa na kuweka miundombinu ktk maeneo hayo ili yatumike ipasavyo kwa wakulima. sio unakuta mtu anaishi juu ya mlima, anatembea kilomita 5 kwenda kulima mabondeni n.k.
    serikali inapaswa kuwa na watu wenye kona mbali wenye kupanga vitu vinavyotekelezeka na kuwaonyesha watu wake jinsi ya kuvitekeleza,si tu kukaa na kuotesha vitambi na porojo nyingi za kufurahisha umma nyakati za kampeni za kisiasa na kutumia termilogolie(lugha0 sizizoeleweka kwa mwananchi wa kawaida.'
    nchi zote zinazoendelea kwa kasi zilipitia huko na kwakuwa zilikuwa na watu wabunifu wenye kuonambali zimefika hapo zilipo sasa.

    ReplyDelete
  2. samahani wasomaji kwa michapio iliyo jitokeza hapo juu ktk comment yangu ya kwanza kabisa, ni mambo ya keyboard na haraka tu.nimechapia sio biogei-biogas, terminologies,lugha,kujenga kwa kuhamahama,sio paoja-pamoja.
    halafu ankal jana nimekutumia e-mail yangu ya kutafuta nanihii naona ukaibana,sio vizuri mkuu watu tuko serious kweli. nakutumia nyingine sasa hivi.

    ReplyDelete
  3. mdau wa hapo juu yaani kama ingelikuwa ni project ndio una hand in ningekupa mia kwa mia. Yote uliyoyazungumza yana ukweli halisi. Na kama kuendeleza sehemu kama hizo watangaze tu na waweke miji kwenye ramani ya kudumu kwani uzito upo wapi. Nakama ni ajira ndio zinanzia hapo. Leo ukiangalia watu wamejazana mjini utadhani kitu gani neema zote zimeachwa nyuma kwa mfumo mbaya wa serekali yetu. Na serekali isione tabu kuinvest kwenye mambo kama haya. tuna kila sababu ya kuinuka kimaisha nakuacha kutegemea cha "kudakishwa".

    ReplyDelete

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...