

NA MWANDISHI MAALUM, New York
Tanzania imeliambia Baraza Kuu la Usalama la Umoja wa Mataifa na Jumuia ya Kimataifa kwa ujumla kwamba Somalia si tatizo la Afrika.
Kauli hiyo imetolewa na Balozi wa Tanzania katika Umoja wa Mataifa, Ombeni Sefue siku ya alhamis wakati Baraza hilo lilipokutana kwa siku nzima kuijadilia Somalia.
Katika mkutano huo ambao pia ulihudhuriwa na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki Moon, Baraza hilo ambalo lipo chini ya urais wa China kwa mwezi Machi,limetoa taarifa yake inayosisitiza pamoja na mambo mengine, wito kwa jumuia ya kimataifa kutoa msaada wa haraka wa vifaa kwa vikosi ya Umoja wa Afrika vinavyolinda amani nchini Somalia.
Baraza hilo limekutana katika kipindi ambacho vikosi vya Afrika ( AMISOM) kwa kushirikiana na Serikali ya Mpito ya Somalia (TFG) vimekuwa vikikabiliana vikali na kikundi cha Al Shaabab na kufanikiwa kuchukua baadhi ya maeneo yaliyokuwa yakishikiliwa na kikundi hicho.
Naye Katibu Mkuu Ban Ki Moon, akizungumza katika mkutano huo ambao ulichangiwa na wazungumzaji 40.Yeye alisema vikosi vya Afrika na Serikali ya Mpito ya Somalia, siyo tu kwamba wanatakiwa kuongezewa askari, lakini wanatakiwa kupatiwa askari hasa, kuwezeshwa kwa zana na vifaa zikiwamo helkopta, mbinu za uwezo wa ukusanyaji wa taarifa , uchunguzi na upelelezi
Balozi Ombeni Sefue , akasema kwamba Somalia ni tishio kubwa kwa amani na usalama ndani ya Afrika na tishio hilo linakwenda mbali zaidi ya mipaka ya Afrika.
Lakini akasisitiza kwa kubainisha “ Somalia si tatizo la Afrika, hili ni tatizo la dunia nzima na limo ndani ya mapana na dhamana Baraza hili la Usalama”.
Na kwa sababu hiyo,Balozi Sefue alisema, Tanzania ambayo ni kati ya nchi zinazoathirika na hali tete ya Somalia. Inaunga mkono wito wa kuitaka Jumuia ya Kimataifa kutimiza wajibu huo wa kuvisaidia vikosi vya Afrika haraka iwezekanavyo.
“Afrika tumeshaonyesha uongozi katika suala hili, kwa hiyo ni muhimu Baraza Kuu nalo likachangia, likaidhinisha na kupitisha, maombi maalum yaliyowasilisha na Baraza la Usalama la Umoja wa Afrika. Ombi ambalo pia linahusisha kupanua na kuiongezea nguvu UMISOM” alisema Balozi Sefue.
Alisema kuwa Tanzania inazipongeza Uganda na Burudi kwa kutoa askari wake wanaolinda amani Somalia kupitia AMISOM. Na kutoa pole kwa nchi hizo kupoteza askari wake katika jukumu hilo kubwa na zito.
Aidha Balozi Sefue amelitaka pia Baraza Kuu la Usalama la UM, na Jumuia ya Kimataifa, kumpatia ushirikiano wa kutosha na wakaribu, Balozi Augustine Mahiga ambaye ni Mwakilishi Maalum wa Katibu Mkuu wa UM kuhusu Somalia.
“Mwakilishi huyu wa Katibu Mkuu, Balozi Augustine Mahiga anafanya kazi katika mazingira magumu sana. Na Tanzania tunampongeza na kumsifu kwa kazi kubwa na nzuri anayoifanya. Anahitaji msaada madhubuti na ushirikiano kutoka jumuia ya kimataifa lakini na pande zote zinazohusika ndani ya Somalia” akasisitiza balozi Sefue.
Akichangia kuhusu utendaji kazi wa serikali ya mpito ya Somalia, Balozi Sefue alisema serikali hiyo inawajibu wa kwanza wa kusimamia mchakato jumuishi wa pande zote zinazopingana lakini pia ujenzi wa taasisi muhimu zitakazo kuwa na uwezo wa kuwasaidia wananchi wa Somalia.
Hata hivyo akasema Tanzania pamoja na kuunga mkono juhudi mbalimbali zinazofanywa na serikali hiyo ya mpito ikiwa ni pamoja na kuitaka kuongeza kasi. Lakini akasema Tanzania haiungi mkono kitendo cha wabunge wa Somalia kujiongezea wenyewe miaka mingine mitatu.
Basi Afrika ndio tatizo la Somalia..!!??
ReplyDelete