Wabunge katika Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, viongozi wa vyama vya siasa na asasi za kiraia, watahudhuria tamasha kubwa la kuhamasisha uzalendo nchini, linalotarajiwa kufanyika Machi 26, 2011 kwenye Viwanja vya Biafra, Kinondoni, Dar es Salaam.
Tamasha hilo linaloandaliwa na Kampuni ya Global Publishers & General Enterprises Ltd kwa kushirikiana na Clouds Media Group, litashirikisha pia watoa mada kutoka kada mbalimbali na wasanii wa fani karibu zote likiwa na kauli mbiu “TAMASHA LA UZALENDO: TANZANIA KWANZA, SISI SOTE NI NDUGU.”
Mratibu wa tamasha hilo, Juma Mbizo kupitia taarifa yake kwa vyombo vya habari jana, alisema kuwa wabunge hao, viongozi wa kisiasa na wale wa asasi za kiraia, wamekubali mwaliko wa kufika kusikiliza mada zitakazotolewa zenye dhumuni la kuwatuliza wananchi na kuipenda nchi yao.
“Wabunge kama ilivyo viongozi wa kisiasa ni wawakilishi wa wananchi, kwa hiyo ni busara kuona wamekubali kufika kusikiliza kitakachozungumzwa,” alisema Mbizo na kuongeza: “Tamasha ni la wazi na bure, hivyo kila mtu afike. Litaanza saa 5:00 asubuhi na kufika mwisho saa 12:30 jioni.”
“Tunawahimiza Watanzania waje kwa wingi kusikiliza ujumbe utakaolewa. Kutakuwa na wasanii wakubwa wa Bongo Fleva, Reggae, nyimbo za Injili, bendi za muziki wa dansi. Vilevile kutakuwa na burudani za sarakasi na maigizo yenye ujumbe wa kuhamasisha uzalendo,” alisema Mbizo.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...