JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA





TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

Tarehe 27 Aprili, 2011, Katibu wa Bunge, Dr. Thomas D. Kashililah alizunguza na vyombo vya habari kuhusu masuala makuu matatu:-

1. Utaratibu wa kutunga sheria Bungeni kwa mambo ya jumla
2. Mamlaka ya Spika katika Kazi za Bunge
3. Mwenendo wa Bunge la Kumi hasa Mkutano wa Tatu

Katika maelezo yake Katibu wa Bunge alitoa ufafanuzi wa kina juu ya namna mchakato wa Muswada wa Marekebisho ya Katiba na matumizi ya hati ya dharura (Certificate of Urgency).

Aidha, Katibu wa Bunge pia alifafanua mamlaka ya Spika katika Kazi za Bunge kwa kueleza kuwa katika kazi zake Spika anaongozwa na Kanuni za Bunge ambazo zinampa fursa ya kutoa adhabu kwa Wabunge ambao wanavunja Kanuni au kuonesha vitendo visivyostahili Bungeni na kusababisha uvunjifu wa amani na utulivu Bungeni.

Katika hilo na kuzungumza yaliyojiri katika Mkutano wa Tatu, Katibu wa Bunge alieleza kuwa Spika pia kwa kutambua kuwa wengi wa Waheshimiwa Wabunge ni wapya (asilimia 69 ya Wabunge wa sasa) ambao hawana uzoefu wa mambo ya Bunge, hutumia busara katika maamuzi yake kwa kuwa kutokana na ugeni wao, Wabunge hao bado hawajawa na uelewa mpana wa Kanuni na hivyo lililo muhimu sio kutoa adhabu bali kutoa elimu na kuwaelekeza wanapotenda/kutoa kauli sizo.

Aidha, ni kwa kuzingatia hilo, Ofisi ya Bunge iliandaa semina mbili elekezi zilizofanyika Jijini Dar es Salaam na pia kugharamia semina za vyama vikuu Bungeni – Chama cha Mapinduzi (CCM) iliyofanyika Dar es Salaam na semina ya Wabunge wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) iliyofanyika Bagamoyo, mkoani Pwani.
Ofisi ya Bunge imesikitishwa na taarifa potofu zilizotolewa na baadhi ya vyombo vya habari kuwa Katibu wa Bunge amewaita Waheshimiwa Wabunge “mbumbumbu” neno ambalo halikutumika katika mazungumzo.

Ofisi ya Bunge inatambua na kuheshimu kwa kiasi kikubwa elimu na taaluma za Waheshimiwa Wabunge na hili halikuwa sehemu ya mazungumzo na waandishi wa habari.

Ofisi ya Bunge inaheshimu na kuzingatia uhuru wa vyombo vya habari katika kufanya kazi yao lakini inasisitiza kuwa uhuru huo usitafsiriwe kama ni fursa ya kuchonganisha pande mbalimbali katika jamii. Kupachika neno “mbumbumbu” kama kielelezo cha Wabunge kupewa muda wa kuzielewa Kanuni ni upotoshaji mkubwa wa maudhui ya aliyozungumza Katibu wa Bunge ambao hauna lengo jema.

Ofisi ya Bunge inatoa wito kwa waandishi kuzingatia maadili na miiko ya kazi zao wanapotekeleza kazi zao hasa habari za Bunge na Wabunge ambao ni wawakilishi wa wananchi.


Imetolewa Ijumaa tarehe 29 Aprili, 2011 na:-

Idara ya Habari, Elimu kwa Umma
na Ushirikiano wa Kimataifa
Ofisi ya Bunge
S. L. P. 9133
DAR ES SALAAM.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

Kuna Maoni 1 mpaka sasa

  1. Hapa bado sijafahamu vipi hawa wabunge wa vyama vingine kama TLP,NCCR,CUF inamaana semina zao hazita gharamiwa. Hivi huu ni utaratibu gani hapa bado haipandi. Vyama vidogo vinaruzuku ndogo kisha mnaviachia vijigharamie vyenyewe semina muhimu kama hizo vikishindwa mtasema nini. Hivi inamaana hao wasomi wote ambao sio mbumbu hawajaliona hilo.Hii ofisi ya bunge hivi haijui kwamba hizi ni fedha za wananchi?

    ReplyDelete

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...