"Kipekee napenda kuchukua fursa hii kuwashukuru wajumbe wote wa Baraza kwa kuchaguliwa kwenu na kuhudhuria mkutano huu pamoja na kuwa na majukumu mengi yanayowakabili ya kikazi na kifamilia. Ni Matumaini yangu kuwa kuhudhuria kwenu katika mkutano huu kutaibua changamoto zenye tija kwa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania na kwa Taifa kwa ujumla.
Aidha, nachukua fursa hii pia kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutuwezesha sisi sote kuwa na afya njema na hivyo kuweza kuhudhuria mkutano huu wa Baraza Kuu la Wafanyakazi la Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania. ni vizuri ieleweke kwamba kuna uhusiano bayana kati ya Haki na Wajibu. Ni wajibu wa wajumbe wa Baraza kusoma na kuelewa Mpango Mkakati wa Mamlaka, Sheria, Kanuni, Miongozo na Taratibu mbalimbali zinazohusu haki na stahili za Wafanyakazi pamoja na utawala bora. Kwa kufahamu mambo haya kutawawezesha kusimamia vizuri haki na wajibu wa wafanyakazi na vile vile haki na wajibu wa mwajiri kwa mfanyakazi. Kwa kutekeleza hili Baraza litakuwa ni kiungo madhubuti kati ya Menejimenti ya TAA na Wafanyakazi.
Hivyo basi, natoa wito kwa Menejimenti kuhakikisha kwamba TAA kunakuwa na mazingira mazuri ya utendaji kazi, mawasiliano mazuri na wafanyakazi, haki na stahili za wafanyakazi kutolewa kwa muda muafaka na pale inaposhindikana taarifa sahihi zitolewe kwa wakati kwa wahusika. Hakika kila mmoja wenu, yaani Menejimenti na Baraza na Wafanyakazi, mkiwajibika ipasavyo katika maeneo yenu, TAA itakuwa imezingatia Dira, Dhima na Malengo yake vizuri na hivyo kufanikiwa kuchochea kasi ya maendeleo ya kijamii na kiuchumi nchini.
Akiongea na wafanyakazi juu ya janga la sasa la Ukimwi Mhe.Chambo alisema;
"Ni vyema pia tukumbushane kuhusu ugonjwa wa UKIMWI ambao hauna chanjo wala tiba na ambao umeendelea kuwepo katika nchi yetu kwa zaidi ya miaka 20 sasa tangu ulipoingia mapema miaka ya 1980. Athari za ugonjwa huu katika jamii yetu zipo wazi, jinsi tunavyougua, tunavyouguzana, kuzika ndugu zetu na kulea yatima. UKIMWI umekuwa janga la Kitaifa kwa sababu umeendelea kuathiri nguvu kazi ya Taifa letu.
Kama ilivyotamkwa kwenye Sera ya Taifa ya Kudhibiti Ukimwi, UKIMWI unazuilika, tatizo lililopo ni kwamba jamii haijawa makini katika kujilinda na maambukizo ya Virusi vya ugonjwa huo. Hivyo natoa wito kwenu wajumbe wa Baraza, kuwa na dhamira thabiti kwa mujibu wa nafasi zenu kuhakikisha kwamba juhudi madhubuti zinafanyika ili kujikinga na maambukizo hayo. Katika kudhibiti kuenea kwa ugonjwa huu, Mamlaka katika mwaka wa fedha 2011/12 ijipange Kutoa mafunzo kwa watumishi wake kuhusu mbinu za kujikinga na maambukizi mapya ya UKIMWI sehemu za kazi na katika familia zao. Suala hili halihitaji fedha nyingi kwani linaweza kufanyika mahali pa kazi na wakati wa kazi kwa kuita wataalamu kuja kutoa elimu au kuendesha semina ambazo zitajumuisha wafanyakazi wengi kwa pamoja.
Changamoto iliyopo sasa ni kutojitokeza watumishi ambao wameambukizwa ugonjwa huo ili Mamlaka iweze kuwahudumia kama inavyoelekezwa katika mwongozo uliotolewa na Serikali kuhusu kuwahudumia Watumishi wenye UKIMWI. "


Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...