Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Mohammed Gharib Bilal, akisalimiana na Rais mpya wa saba wa Jamhuri ya watu wa Comoro Dkt. Iclilou Dhoinine,mara baada ya kuapishwa rasmi katika sherehe zilizofanyika katika Viwanja vya Bunge la nchi hiyo jijini Moroni.
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Mohammed Gharib Bilal, akisalimiana na Rais wa Madagascar, Andrew Rajouline, wakati wa sherehe za kuapishwa rasmi kwa Rais mpya wa saba wa Jamhuri ya watu wa Comoro, Dkt. Iclilou Dhoinine. Sherehe hizo zilizofanyika Moroni.
Picha na mdau Amour Nassor wa VPO
Na Mwandishi Maalum – Comoro
Ijumaa – Mei 27, 2011
Makamu wa Rais Dk. Mohammed Gharib Bilal alikuwa miongoni mwa viongozi waliohudhuria sherehe za kuapishwa Rais wa Visiwa vya Comoro Ikililou Dhoinine ambako alimwakilisha Rais Jakaya Kikwete.
Sherehe hizo ambazo zimefanyika jana (Alhamisi) kwenye viwanja vya Bunge mjini Moroni zilihudhuriwa pia na Rais wa Madagascar Andry Rajoelina, Makamu wa Rais wa Mauritius, Waziri Mkuu wa Chad pamoja na mabalozi mbalimbali waliowakilisha nchi zao.
Baada ya kuapishwa viongozi na wageni waalikwa walipata fursa ya kumpongeza Rais Dhoinine ambaye alishinda nafasi ya urais katika uchaguzi mkuu uliofanyika Disemba 27, 2010.
Rais Dhoinine mwenye asili ya kisiwa cha Moheli anachukua nafasi ya Ahmed Abdallah Sambi ambaye amemaliza muda wake wa uongozi wa kipindi cha miaka mitano.
Wakizungumza katika sherehe hizo Rais Sambi anayeondoka madarakani alielezea mafanikio yaliyopatikana katika kipindi cha uongozi wake yakiwemo ya kiuchumi na kijamii wakati kwa upande wake Rais Dhoinine alielezea matarajio yake ya kuleta maendeleo zaidi katika visiwa hivyo.
Wakati huo huo, Makamu wa Rais Dk. Bilal anaondoka nchini kesho (Jumamosi) kuelekea Abuja, Nigeria, ambako atamwakilisha Rais Jakaya Kikwete kwenye sherehe za kuapishwa kwa Rais mteule wa Nigeria Gooluck Jonathan.
Sherehe za kuapishwa kwa Rais huyo Mteule wa Nigeria zitafanyika Jumapili mjini Abuja kufuatia ushindi alioupata katika uchaguzi mkuu wa nchi hiyo uliofanyika mwezi April, mwaka huu. Makamu wa Rais anatarajia kurejea nchini Jumatatu ijayo.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...