Mawakili wa Serikali na upande wa utetezi katika kesi ya uhujumu uchumi inayomkabili aliyekuwa Balozi wa Tanzania nchini Italia Profesa Costa Mahalu na Meneja wa Utawala na Fedha Grace Martin,  leo wamevutana  kuhusu nyaraka za hati ya kiapo ya Rais Mstaafu Benjamin Mkapa kutinga magazetini kabla ya kuwasilishwa rasmi mahakamani hapo.


Kesi hiyo imefanyika   leo Mahakama ya  Hakimu Mkazi Kisutu  kwa ajili ya upande wa utetezi kuanza kujitetea, Wakili kiongozi wa utetezi Mabere Marando aliomba kuwasilisha hati hiyo ya Mh. Mkapa ili Mahakama iiweke katika rekodi ya kesi hiyo.



Baada ya kuwasilishwa kwa hati hiyo, Wakili wa Serikali Ponsiano Lukosi alidai kuwa mawakili hao wameanza kujisahau kama ni maofisa wa Mahakama ambapo wanataka kuwasilisha hati hiyo tayari ilishazungumzwa 
katika magazeti.



Alidai kuwa katika gazeti la Mwanahalisi la Aprili 27, mwaka huu toleo Na. 239 ilizungumzia nyaraka hiyo ya hati ya Mkapa.



Pamoja na Mwanahalisi magazeti mengine yaliyoripoti kupokelewa kwa hati hiyo na Mahakama ni Tanzania Daima, Mwananchi, Citizen na Mtanzania ya Mei 6, mwaka huu.



Alidai kuwa wanachoona ni kwamba kama kesi inakuja mahakamani au kama kitu kitazungumziwa mahakamani, kuna haja gani maofisa wa Mahakama kupeleka taarifa katika vyombo vya habari.



“Kwa kufanya hivyo tutakuwa tunaidharau Mahakama na kuingilia uhuru wake, gazeti la Mwanahalisi katika ukurasa wake wa kwanza lilichapisha hati hiyo ya kiapo na kuichambua kipengele kwa kipengele kwamba  Mh. Mkapa 
ambaye alieleza jinsi kila kitu kilivyofanyika akiwa Rais Mtendaji wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania halafu mwisho wakatoa hukumu kwamba kutokana na kiapo hicho kilivyo ni kwamba upande wa mashitaka sasa 
ujiandae kukunja jamvi la mashitaka.



“Mheshimiwa humo ndani ya gazeti wametaja watu ambao wamewaambia, na Aprili 27 hati hiyo ilikuwa bado haijawasilishwa mahakamani, naomba Mahakama itoe onyo ili kila mtu awajibike inavyostahili, jambo 
lijadiliwe mahakamani kwanza kabla halijazungumzwa popote,” alidai Lukosi.



Akipangua hoja hiyo Wakili wa utetezi Marando alidai kuwa kuhusu suala hilo haoni cha kutolea onyo kwa yeyote na kama iko haja basi wa kupewa onyo ni  serikali kwa kuvujisha nyaraka za siri za Mahakama kwa watu
wasiohusika.



Alidai kuwa hata yeye anashangaa nyaraka hiyo imeingiaje kwenye vyombo vya habari na kwamba yeye ndio alipaswa kuwalaumu wao (Serikali) kwa kusambaza nyaraka za siri.



“Mawakili sasa tunaelekea kubaya, hii nyaraka ni yakwetu hasa mimi, niliiandaa kabla haijapelekwa kokote nikaiwasilisha kwa Serikali na nikawakabidhi kabla ya Aprili 27, naomba nisieleze nani nilimpa.



“Baada ya kama wiki moja na mimi nilishtuka kusoma kwenye gazeti, nikamhoji huyo bwana aliipata wapi hiyo nyaraka, hakuniambia, na hata barua niliyomwandikia Katibu mkuu kiongozi kuhusu nafasi ya Rais
imefika kwenye vyombo vya habari.



“Kupitia barua hiyo nilihojiwa na vyombo vya habari kuhusu nafasi ya Rais kutoa ushahidi mahakamani na ndio kichwa cha habari cha gazeti la leo (jana) la Mwananchi, kwa mujibu wa kifungu cha 9 (1) kinasema 
kwamba Rais aliyeko madarakani huwezi kumlazimisha kuja mahakamani, Mahakama inaweza kuomba kauli yake lakini kama atapenda atakuja na asipopenda haji.



“Walichofanya Mwananchi wameniuliza kama nimejibiwa barua yangu niliyomwandikia Rais nikajibu sikujibiwa, nikaulizwa na je asipokuja mtafanyaje, nikajibu tutasubiri mpaka amalize kipindi chake cha urais 
kwani ushahidi wake ni muhimu kweli.



“Kuhusu ombi la kunyamazisha, usikubali kufanya hivyo mahala ambapo sio lazima, labda mlalamikaji angelalamika kuhusu mwandishi wa gazeti lakini sio Wakili,” alidai Marando.



Aidha Marando aliomba nakala za mwenendo wa kesi hiyo kwani alizopewa awali zina makosa ya uchapaji ili aweze kuzipitia kabla wateja wake hawajaanza kujitetea.



Akiahirisha kesi hiyo Hakimu Mgeta alisema hawezi kulitolea uamuzi suala hilo na kuzitaka pande zote mbili kuendelea na kesi hiyo ya msingi, ambapo aliahirisha sahuri hilo hadi Julai 8 na 11, mwaka huu 
na litatajwa Juni 24, mwaka huu.



Katika hati yake ya kiapo Mkapa ametaja sababu 13 za kumtetea Mahalu katika mchakato mzima wa ununuzi wa jengo hilo la ubalozi lililoko katika mtaa wa Vialle Cortina d’Ampezzo 185 mjini Rome.



Rais Mkapa anadai kuwa  jengo la ofisi ya ubalozi mjini Rome lilinuliwa wakati  ambao yeye alikuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na kwamba ununuzi  wa jengo  hilo ulifanyika kwa mujibu wa 
sera ya serikali ya kumiliki  au kujenga ofisi  za kudumu na makazi kwa mabalozi nje ya Tanzania ikiwa ni njia mojawapo ya kupunguza gharama kwa serikali.



Washitakiwa Mahalu na Grace wanakabiliwa na kesi ya kuhujumu uchumi kwa kuisababishia serikali hasa ya zaidi ya Sh bilioni mbili wakati wakiwa maofisa wa ubalozi nchini Italia.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...