Mh. Daniel ole Porokwa

Kwa muda wa takribani wiki mbili sasa, vyombo vya habari vimeripoti maelezo yaliyotolewa na Mkurugenzi wa Fedha na Utawala wa Chadema, Mh. Anthony Komu, kwamba Nape Nnauye alikuwa mwasisi wa Chama Cha Jamii (CCJ).
 

Madai haya yakathibitishwa na aliyewahi kuwa mbunge wa Kishapu (CCM), Fred Mpendazoe ambaye alitaja watu kadhaa nikiwamo mimi, kuwa walishiriki au waanzilishi wa chama hicho ambacho hakikuwahi kufanikiwa kupata usajili wa kudumu.

Hivyo basi, nimewaita hapa leo hii, ili pamoja na mambo mengine, kueleza ukweli wa hiki ambacho kimeelezwa vizuri na Mheshimiwa Mpendazoe na kimenukuliwa vema na vyombo vya habari, hasa gazeti la kila wiki la MwanaHALISI.

Nimeamua kufanya hivyo kwa misingi miwili mikuu. Kwanza, sisi kama viongozi ni sharti tuwaonyeshe wananchi wetu na wanachama wa chama chetu njia sahihi tunayotakiwa kupita na tuamini katika hiyo njia tunayoelekea.

Pili, mmoja wa msingi mkuu wa chama chetu, ni kusema ukweli, na kwamba uwongo na fitina ni mwiko kwa viongozi na wachama wa CCM.

Ni kweli niliwahi kuombwa kuwa mmoja wa wanachama waanzishi wa CCJ. Nilikutana mara kadhaa na Mh. Nape Nnauye, Mh. Dk. Harrison Mwakyembe na Mh. Fred Mpendazoe.

Aidha, nilikutana mara moja na Mh. Samwel Sitta baada ya Mh. Nape na Dk. Mwakyembe kunitajia kuwa ni miongoni mwa waanzilishi wa CCJ, nami kutaka uthibitisho wa hicho walichonieleza. 

Naye Mh. Sitta alinieleza kuwa nilichoelezwa na Mh. Nape na Dk. Mwakyembe hakina chembe ya mashaka.

Katika mikutano zaidi ya mitano niliyofanya na Mh. Nape na Dk. Mwakyembe wenzangu walinieleza mpango wao wa kuanzisha chama cha siasa kuwa umelenga kuondokana na utawala wa kiimla wa CCM kwa hoja kuwa kilipofikia chama hicho hivi sasa, hakiwezi tena kuaminiwa kukabidhiwa madaraka ya kuongoza dola.

Walisema CCM hakiaminiki tena machoni mwa wananchi na kimepoteza mvuto mbele ya umma; yote haya ni kwa kuwa chama hiki kimekuwa kinaacha ile misingi kama ilivyoasisiwa na waasisi wake, Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere.

Walinieleza, kihistoria Chama Cha Mapinduzi ni chama cha ukombozi na kilijipa kazi ya kupigania wanyonge, lakini kikafika mahali historia hiyo ikaporomoka kwa kuingia katika mikono ya watu wasiojali, wasiokuwa na maadili ya uongozi na labda wasiowaaminifu.

Wakati wote wa mazungumzo yetu, Mh. Nape na Dk. Mwakyembe walikuwa wakisisitiza umuhimu wa mimi kukubali kujiunga haraka na CCJ, ili kurahisisha upatikanaji wa usajili wa kudumu wa chama hiki, lengo likiwa CCJ kiweze kishiriki katika uchaguzi mkuu wa 2010.

Hata hivyo, kila muda ulivyozidi kusogea, ndivyo nilivyopata kujua undani Mh. Mwakyembe na Mh. Nape wa kutaka kuanzisha chama chao cha siasa, kwamba kinachowasukuma katika mpango huo, ni matakwa binafsi ya kisiasa na hivyo nikaanza taratibu kuwa mbali na mkakati wao.

Nimeamua kuyasema haya baada ya kuwasikia Mh. Nape na Dk. Mwakyembe wakimkana Mh. Mpendazoe na kimsingi wakikana chama chao – CCJ. 

Napenda kuwaambia Watanzania, kwamba CCJ ni chama kilichoanzishwa na kuasisiwa na viongozi hao wawili, pamoja na Mh. Sitta kama ambavyo Mpendazoe alivyoeleza.

Katika mpango huu, mimi niliahidiwa kusaidiwa kugombea ubunge katika jimbo la Monduli kupitia CCJ, huku Mh. Nape akiahidi kusimama katika jimbo la Ubungo.

Nimeyasema haya ili kuondoa unafiki unaojengeka ndani ya chama chetu na taifa kwa jumla, kwamba kuna kikundi cha watu wanaotaka kupotosha umma juu ya uanzishwaji wa CCJ na ujio wake ili umma uwapime na uamue juu ya watu hao.

Mimi kama kada wa CCM niliyefundishwa na kuaminishwa kwamba uongozi ni dhamana na ninayeamini katika misingi ile aliyotuachia Mwalimu Nyerere, nimeamua kuyasema haya ili ukweli ubaki ukweli katika historia ya nchi yetu.

Kuyumba kwa chama chetu na hata kufikia hatua ya kuanza kuporomoka kwa kupoteza nafasi mbalimbali kwa vyama vingine kwa wingi tokea kuanzishwa kwa mfumo wa vyama vingi katika nchi hii, ni kwa sababu ya kuwa na viongozi wenye malengo na agenda zao binafsi, tofauti na zile za chama chetu.

Hii bila mashaka inanipa sababu ya kuamini kwamba Bunge la Tisa kama mmoja wa mihimili muhimu wa dola, chini ya Mh. Samwel Sitta lilitumika vibaya kufanikisha agenda nyingine ya kuanzisha chama kingine badala ya CCM.

Ni vema Rais Jakaya Kikwete akajua kuwa ndani ya timu yake, kuna wachezaji ambao wako tayari kujifunga na kuinyima timu yao ushindi. Ni vema akaamua kuachana nao kwa maslahi yake na chama chake.

Ni maoni yangu kwa dhati kabisa na rai yangu kwa viongozi wa chama, kwamba ni wakati mwafaka watu kama hawa wawajibike au wawajibishwe kwa matendo yao. 

Baada ya mimi kushutukia na kutokuwa na imani na minendo ya waasisi wa CCJ na hivyo kujiondoa, nilipata taarifa kuwa baada ya kujiridhisha kuwa chama chao hakitasajiliwa na kuwahi uchaguzi wa 2010, waliamua kufanya mazungumzo na viongozi wa Chadema na kukubaliana kuwa wote kwa pamoja watajiondoa CCM na kujiunga na Chadema ili kugombea nafasi mbalimbali kupitia chama hicho.

Kwa ushahidi ninaoutoa, ninawachukua hawa niliowataja kuwa si wasaliti kwangu tu, bali hata kwa chama chenyewe. Nisingeshutuka mapema yangenipata yaliyompata Mpendazoe. Ninampa pole sana ndugu yangu Fred Mpendazoe.

Na hili la Mpendazoe ambaye alikuwa mbunge, akaacha mishahara kadhaa na mafao yake kwa makubaliano ya kazi ya pamoja ambayo nilishirikishwa katika hatua za awali na mwisho wake wakamtosa na sasa wanamkana hadharani, ni moja ya sababu iliyonisukuma sana kutoa ushuhuda huu. 

Daniel ole Porokwa,
Kada wa Chama Cha Mapinduzi (CCM).

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

Kuna Maoni 12 mpaka sasa

  1. AnonymousMay 23, 2011

    tutayasikia mengi mwaka huu daah! sasa tuseme siasa ni kuwa muongo au kuwa mbinafsi au kuwa na nini has? i hate siasa!

    ReplyDelete
  2. AnonymousMay 23, 2011

    Sasa ngoma inaelekea patamu,sisi hatujui ila Mungu anajua yaliyo sirini,kwa sababu kusema tu haitoshi hata JK mbona anaweza kuambiwa naye alitaka kuazisha chama chake ili iwe historia aitwe Baba wa Taifa wa chama.Bado mengi yatakuja tusubiri

    Comments: NO COMMENTS

    ReplyDelete
  3. AnonymousMay 23, 2011

    Nyinyi nyote ni CHA-DEMA msitubabaishe, na mna mpango wa kukichafua CCM. Lakini mwisho wenu umefika. Kwanza tunakung'oweni kwenye chama, baadae kwenye ubunge. Walio wengi wanakuchagueni ili muwaondoshee kero za maisha. Lakini kumbe mnaitumia nafasi hiyo kujilimbikizeeni utajiri kwa kutumia ufisadi.

    ReplyDelete
  4. AnonymousMay 23, 2011

    Nimemuangalia jamaa kwenye TV wakati anaongea na wanahabari, the guy is a liar. Alikuwa anasoma a prepared statement, ambayo alikuwa hata facts hazijamkaa kichwani lazima azisome.

    ReplyDelete
  5. AnonymousMay 23, 2011

    hongera sna mh ole porokwa. ila kwanza maneno yako yananitia wasiwasi sana kwa vile umeyatoa bila vithibitisho vyovyote (evidence) hta moja? uliukutana nao sawa. bci ungetueleza mahala,lini,namdaa ..unavyoongea na kutoa maneno inadhihirisha unafiki na uwongo ulionao.. au umepadikizwa kusema??...kwanini ukesema anzia kipindi kile uje useme leo? kama misingi ya chama chenu ni kusema ukweli uwongo fitna kwenu mwiko? fitina ndio umeiona leo hii?..moja kwa moja inanidhihirishia kwamba wewe nimfitini na unamaslai yako binafsi.

    ReplyDelete
  6. AnonymousMay 23, 2011

    Wakati wote alikuwa wapi kusema hayo mambo, mmmh kweli ccm imeharibika watu wanalopoka tu na kusema hovyohovyo tu bila misingi yoyote, mnavyofanya hivyo wanachama waelewa wanakichukia chama.

    ReplyDelete
  7. AnonymousMay 23, 2011

    HUYU NDUGU ANGELIKUWA KWELI ANA UCHUNGU NA CHAMA ANGEKISAIDIA WAKATI ULEULE WA MIKUTANO ANAYOSEMA YA CCJ,PIA ANGEMSAIDIA MUHESHIMIWA JK KUTOCHAGUA WALIOTAKA KUKISALITI CHAMA KATIKA NAFASI MBALIMBALI ZA UONGOZI.HUYU BWANA KATUMWA TENA YEYE NDIO MWENYE MALENGO BINAFSI NA HANA MSIMAMO,INAMANA MAMBO YANGEKUA SAFI CCJ ANGELITIMKIA HUKO,BILA CCM IMARA INCHIYETU ITAYUMBA HIVI SASA CCM INAJIPANGA KURUDIA MISINGI YAKE NA NDIO MAANA KUNA MABADILIKO YA UONGOZI WA JUU WA CHAMA,USITUCHANGANYE KWANZA HUO UKADA WA CCM WEWE KAKUPA NANI,NA KWA MUONEKANOWAKO TU UNAONEKANA UMEKAA KI CHADEMA CHADEMA,MFUATE MPENDAZOE KAMA KWELI UNA UCHUNGU NAE ASIE NASUBIRA NA UVUMILIVU.WEWE NA WALIOKUTUMA MSHINDWE MLEGEE KWA JINA YESU.

    ReplyDelete
  8. AnonymousMay 23, 2011

    Facts hazisomwi kwenye prepared statement kaka, acha unafiki...ilitakiwa uongeee kichwani ukimaanisha ukweli wa matukio hayo na si vinginevyo.

    ReplyDelete
  9. Common mwananchiMay 23, 2011

    Mheshimiwa Kiongozi

    Umegundua lini kusema ukweli na uwongo na fitina kwako ni mwiko? Nina wasiwasi sana na wewe kutumika na unajishushia hadhi na utu wako. Kama kweli wewe ni mkweli na uliona kuna wana-CCM wanampango wa kukisaliti chama je ulitoa taarifa kwenye kikao chochote au mtu yeyote mwenye dhamana ndani ya chama????? Je kama huu mpango ungefanikiwa na kukiathiri chama, mchango wako katika chama ungekuwa ni upi? Au unafaikiri kwa kuongea sasa ndio unakisaidia chama na mwenyekiti wake?? Nitashangaa kama mwenyekiti na wana CCM makini watakusikiliza sasa. Wewe sio mzalendo kwenye chama hata kidogo.

    Na kwa kukaa kimya muda wote napata picha kuna role uliyoplay wakati huo na unahisi it was not significant. Lakini nataka uelewe, kukaa kimya tu nakuangalia watu wanaboa chama chako huku ukiwa na taarifa sahihi hiyo yenyewe ni "significant role" katika kufanikisha mpango huo. Kama ni kweli kwa mwanaCCM kushiriki kuanzisha chama kingine cha siasa ni kosa na usaliti kwa chama,basi hata wewe uliyekuwa na taarifa na hukuzitoa ili chama kichukue hatua stahili ni mkosaji tu. Wote ni wale wale.

    Ninachokiona hapa ni kama ule mchezo au watu wamekubaliana wafanye uhalifu, na unaposhindikana au kutiwa mikononi mwa dola ndio baadhi yao hujitokeza na kusema sio mimi ni yule. Huyu ni hatari zaidi maana anacheza "double usaliti". Mheshimiwa Kiongozi, ulikisaliti chama kwa kukaa kimya wakati ule na unawasaliti wenzako sasa, na ndio maana nilianza kwa kukuuliza umegundua lini kusema ukweli na fitina kwako mwiko? Hapa hauwafitinishi wenzako na mwenyekiti wao?

    Unasema ni vema Mh Kikwete akajua timu yake maana kuna ambao wako tayari kujifunga. Hapa napata shida kidogo maana unamwambia leo kweli??? Unajuaje kama wameshajifunga? Au wameshatoa pasi za kufungwa?Kwanini hukumwambia mwanzo ili asiwapange kwenye timu wakati ulikuwa na taarifa hizi "nzuri"?? Hapo umemsaidia mwenyekiti na chama kwa lolote? Kwa mawazo yangu, nilitegmea kwa uzalendo wako halisi kwa chama,ungetoa taarifa kunakohusika mara moja ili kuzuia hilo unaloamini leo ni uhalifu. Huo ndio uongozi unaojivunia hapa?

    Namaliza kwa kusema, wanasiasa acheni kuona watanzania ni wajinga, watu wanaupeo mzuri tu wa kuona na kuchambua hoja. Wanajua zuri na baya, uongo na ukweli na masilahi ya umma na binafsi. Hapa nahisi ni masilahi binafsi maana kwa kusema haya leo, hakuna masilahi yoyote kwa umma wala chama. Tuache hizi siasa za mazingaombwe na za kufikiri kwa tumbo badala ya kichwa. Dadisi

    ReplyDelete
  10. AnonymousMay 23, 2011

    Na bado, ndimi zitachonganishwa mpaka kieleweke! Mtayaweka mambo yote peupe sasa, CCM nchi imewashinda, mmeamua kujikita kwenye majungu na fitina. CCM hakuna aliye msafi bwana, au mnadhani sisi wananchi ni maamuma? Jisafisheni na muongoze nchi vile walala hoi tunavyotarajia, acheni bla-bla zenu hapa. Eti utasema kweli daima fitina kwako mwiko, ulisubiri uangushiwe zengwe ndiyo useme kweli, ulikuwa wapi wakati wote huo kuuweka huo upupu hadharani? Eti unamwambia JK kuwa atambue kuwa kwenye timu yake kuna wasaliti, hao amewalea mwenyewe muache ahangaike nao, CCM wote ni wa hivyohivyo tu, hakuna mwenye nafuu, hata wewe ni mamluki tu. Msituchanganye, karibu kitaeleweka tu!

    ReplyDelete
  11. AnonymousMay 23, 2011

    Hao mnaosema kuwa taarifa kwa vyombo vya habari angeitoa kichwani si wana habari. Taarifa uandikwa, kisha usainiwa na mtoa taarifa. Kwa hiyo mtoa taarifa akisha isoma, baadaye anawapa nakala wana-habari wote waliohudhuria kwa ajili ya kumbu-kumbu. Kwa hiyo huo utetezi siyo wa msingi. Ukweli unabakia kuwa hao jamaa walitaka kuitosa CCM lakini haikuwezekana.

    ReplyDelete
  12. AnonymousMay 24, 2011

    Nilikuwa nasikia siku zote kuwa kuna watu wanafiki, wanaosema uongo "with a straight face" ndio huyu Ole Porokwa! kama habari hizi alikuwa anazijua siku zote, kitu gani kilimshinda asi tete na Mwenyekiti wa Chama chake, akamuachia akawapa "wabaya wake" vyeo halafu saa hizi ndio anakurupuka, anajitia kueleza! Watu kama hawa ndio wanafik kuliko maelezo, na sina shaka anatumiwa na wanaotakiwa kujivua gamba ili ionekane hakuna msafi. Kwa maoni yangu, hata kama Sitta, Nape na wengineo, walitaka kutoka CCM ile ya mafisadi, walikuwa na haki, na kama baada ya kuona kumbe wako wengi ndani ya CCM wasiopenda ufisadi, na kuna uwezekano wa mafisadi kutoswa, na wao wakabaki na CCM safi, huo si usaliti bali ni U-CCM Damu

    ReplyDelete

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...