![]() |
Afisa Uhusiano wa Jeshi la Polisi Zanzibar Inspekta Mohammed Mhina |
Na Mwandishi wa Jeshi la Polisi Zanzibar
Jeshi la Polisi Zanzibar limegundua mbinu mpya zinazotumiwa na wafanyabiashara wa mihadarati kuingiza bidhaa hiyo haramu katika visiwa vya Unguja na Pemba.
Afisa Uhusiano wa Jeshi la Polisi Zanzibar Inspekta Mohammed Mhina, amesema kuwa kugundulika kwa mbinu hiyo kunatokana na kukamatwa kwa mkazi mmoja wa Kilindoni Mafya mkoani Pwani Athumani Issa Mdaba(25) aliyekuwa na mito ya kulalia iliyojazwa mafurushi ya mihadarati ndani badala ya sufi ama sponchi.
Akizungumzia matukio hayo Kamanda wa Polisi mkoa wa Mjini Magharibi Zanzibar ACP Aziz Juma Mohammed, amesema hadi sasa watu watano wamekamatwa kwa tuhuma za kupatikana na kiasi kikubwa cha mihadarati na mmoja kati ya hao amekamatiwa bandarini akiingiza mihadarati hiyo kwa kutumia mito ya kulalia.
Amesewataja wengine waliokamatwa kuwa ni hamadi saidi Omari(38) mkazi wa Kilwa mkoani Lindi, Mahenga Is’haka Jalumeti(39) mkazi wa Saateni mjini Zanzibar, Surea Ali masudi(35) mkazi wa Magogoni Zanzibar na Nyange makame Ali (61) mkazi wa Shaurimoyo mjini Zanzibar ambao walipatikana wakiwa na vifurushi 150 vya mihadarati hiyo pamoja na viroba viwili.
Kamanda Aziz amesema kuwa kukamatwa kwa watuhumiwa hao kunatokana na kupatikana kwa taarifa za siri kutoka kwa wananchi za watuhumiwa hao kujihusisha na biashara haramu ya mihadarati.
Amesema kuwa baadhi ya watuhumiwa hao ni mawakala wanaopokea mihadarati hiyo kutoka mikoa mingine ya Tanzania bara na wengine ni wasambazaji na wauzaji wa rejareja na jumla kwa watumiaji na wauzaji wadowadogo.
Kamanda Aziz amesema kuwa kutokana na kuenea kwa dhana ya Polisi Jamii na Ulinzi Shirikishi kwa wananchi wa mikoa yote ya Visiwa vya Unguja na Pemba, kila mhalifu anayeingia visiwani humo wakiwemo majambazi wa kutumia silaha ama madawa ya kulevya ni lazima wakamatwe kwani taarifa zao zinapatikana mapema hata kabla ya kuwasili Zanzibar.
Hivyo kamanda Aziz ameendelea kutoa wito kwa wananchi kuendelea kutoa taarifa za kihalifu kila zinapopatikana ili wahusika wawekewe mitego mapema ya kuwatia nguvuni.
Kutokana na mpango huo, Polisi Viisiwani hapa wamefaniikiwa kukamata silaha nyingi na majambazi yaliyopanga kufanya uhalifu mkubwa kwa kutumia silaha huku wakiwa na magari yenye namba za bandia.
Naye Kamanda wa Polisi Kikosi cha Wanamaji na Bandari Zanzibar SP Martin Lisu, amesema kuwa hivi sasa Jeshi la Polisi kwa kushirikiana na Vyombo vingine vya ulinzi na Usalama kama vile Maafisa wa mamlaka ya Mapato nchini (TRA), Maafisa wa Mamlaka ya bandari nchioni (THA) Usalama wa Taifa na Askari wa Vikosi vya serikali ya Mapinduzi Zanzibar, wamejenga ushirikiano mkubwa na kufanya kazi kwa pamoja.
Amesema kuwa ni kwa njia hiyo imefanikisha kumnasa mtuhumiwa huyo wa mihadarati akitokea Mafya ambaye alikamatwa bandarini hapo akiwa na mito 11 iliyokuwa na mabunda 277 ya mihadarati hiyo.
Kamanda Lisu amesema kuwa hiyo ni mara ya pili katika kipindi kisichaozidi mwezi mmoja kukamatwa kwa kiasi kikubwa cha mihadarati ikiingizwa Zanzibar kupitia bandarini ambapo mihadarati mingine ilikamatwa mwanzoni mwa mwezi huu ikiwa imefungwa kama mahindi ya kuchoma.
Tanzania tuko nyuma sana katika viti vya madawa ya kulevya. Na madealer wa nje ya nchi wanalijua hili vilivyo na ndio maana Tanzania kumejaa wabugiaji. Serikali na viongozi kila siku wanasema wanapigana vita na biashara hii ukweli ni kuwa tanzania hatuna hata vifaa vidogo vya kugundua uingizaji wa madawa haya. Itakuwaje watu wawe wanajaribu kuingiza madawa katika mito ya kulalia? nchi zote duniani katika boarder zao wana scanner zinazofichua madawa yaliyofichwa mwilini na katika mabegi na mikoba kwa hivyo waingizaji wa madawa hawajaribu hata siku moja kuingiza kwa kuficha ndani ya mito ya kulalia. Serikali inapaswa kuomba msaada kutoka katika mataifa mengine kusaidiwa katika kupiga vita uingizaji wa madaya haya nchini. Peke yetu hatutofanikiwa kamwe kwani waingizaji wako mbele kwa mbinu kuliko serikali.
ReplyDelete