Makamu wa kwanza wa Rais Zanzibar,Seif Shariff Hamad
Na Mwandishi Wetu,Zanzibar.

Makamu wa kwanza wa Rais Zanzibar,Seif Shariff Hamad ametoa wito kwa mabenki nchini kutoa masharti nafuu kwa vikundi vya Ushirika vya kuweka na kukopa(SACCOSS).

Akizungumza na Menejimenti ya Benki ya Biashara ya Kenya(KCB),Makamu huyo wa Kwanza wa Rais alisema ikiwa Benki hiyo na nyenginezo zitatoa unafuu katika mikopo kwa vikundi vya Ushirika, kuna uwezekano mkubwa wa kupunguza umaskini Visiwani Zanzibar.

“Ni vizuri kuangalia masharti yenu na pia mkae na Wizara ya Kazi, Uwezeshaji wananchi kiuchumi ili kuwa na utaratibu mzuri wa namna mikopo kwa vikundi vya ushirika itakavyorejeshwa” Alisema Makamu wa kwanza wa Rais.

Awali, Maalim Seif amewaomba Wawekezaji katika sekta ya fedha hususan Mabenki kufikiria kuwekeza zaidi Zanzibar ikiwa ni hatua mojawapo ya kuharahakisha maendeleo ya wananchi.

Makamu wa Kwanza wa Rais amesema sekta ya Fedha ina mchango mkubwa katika kukuza uchumi na kupunguza umaskini hivyo, ameiomba KCB kuongeza matawi zaidi Visiwani Zanzibar.

Ameipongeza Benki hiyo ambayo imefungua Tawi Unguja akiitaja kama hatua mojawapo ya kutumia fursa ya soko la pamoja la Afrika Mashariki ambapo sasa nchi wanachama katika Jumuiya hiyo zimeanza kutekeleza itifaki hiyo.

“KCB ni Benki yetu hapa Afrika Mashariki, SMZ itaendelea kushirikiana na Benki yenu tukiamini kuwa kuwepo kwenu ni miongoni mwa faida za kukuza ushirikiano katika Jumuiya ya Afrika Mashariki katika sekta ya fedha” Aliongeza Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar.

Akizungumzia sekta ya mazingira, Maalim Seif alisema kwamba Serikali imadhamiria kuongeza kasi katika utunzaji na uhifadhi wa mazingira ikiwa pamoja na kuwashajiisha wananchi kushiriki katika kampeni za upandaji miti.

Meneja wa KCB Tawi la Zanzibar, Mawese Mmbaga alisema Benki hiyo kwa kushirikiana na Serikali imepanga kupanda miti 1500 katika eneo ambalo Serikali itaelekeza.

Meneja huyo ameihakikishia Serikali ya Mapinduzi Zanzibar kuendelea kutua huduma bora kwa wateja wake ikiwa pamoja na kuboresha mtandao wake katika Visiwa vya Zanzibar hatua kwa hatua.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...