Mkutano wa kila siku wa tathmini baada ya kumalizika kwa zoezi la upimaji VVU baina ya viongozi wa taasisi za dini na wa serikali za mitaa mkoani Shinyanga ukiendelea
 Mkutano wa tathmini ya zoezi  ukiendelea
Ushauri nasaha kwa makundi ya vijana kabla ya zoezi kuanza
Wananchi wa Shinyanga wakisubiri kupimwa VVU
Mama akiwa tayari kupimwa Shinyanga

Taasisi za dini za kiislamu na kikristo mkoani Shinyanga zimefanikiwa kuwapima Virusi Vya UKIMWI wakazi wa maeneo ya kata za Kolandoto na Ibadakuli  ikiwa ni miezi mitatu tangu kusimama kwa zoezi la Upimaji VVU mkoani humo kutokana na uhaba wa vitenganishi vinavyotumika kupima VVU.
Taasisi hizo zilizo chini ya Baraza Kuu la Waislam Tanzania (BAKWATA), Baraza la Maaskofu nchini (TEC) na Jumuia ya Kikristo (CCT) zilizo ndani ya ushirikiano unaofahamika kwa jina la Tanzania Interfaith Partnership (TIP) limefanikiwa kufikia jumla ya watu 1267 katika siku nne za mwanzo za zoezi la upimaji lililofanyika kwenye vijiji vya Kolandoto, Mwamagunguli, Garamba, Ibadakuli, Uzogore na Bugole ambapo kati ya hao wanaume walikuwa ni 628 na wanawake 641 kati yao waliokutwa na VVU ni  watu 65, wanawake wakiwa ni 38 na wanaume 27.
Zoezi hilo litaendelea tena kupitia uhamasishaji ndani ya nyumba za ibada (Misikiti na Makanisa), matangazo ya magari na radio sambamba na mabango, na litaendelea katika kata za Mwawaza, Bugisi na Ilola.
Aidha, katika zoezi hilo la upimaji VVU, mambo kadhaa yamejitokeza ikiwemo idadi kubwa ya vijana na wazee waliojitokeza kupima sambamba na makundi ya wanawake na watoto.
Baadhi ya wananchi waliohojiwa wakati wa zoezi hilo, walielezea kufurahishwa na namna taasisi za dini za imani tofauti kujitokeza kuunga mkono juhudi za serikali na kushirikiana kwa karibu na serikali hadi katika ngazi za vijiji kufanikisha zoezi hilo karibu na maeneo ya watu kwa kuzipeleka huduma hizo ndani ya vijiji.
Shinyanga ni moja ya mikoa yenye maambukizi makubwa kitaifa ambapo tafiti za kitaifa za mwaka 2007-2008 zinaonyesha Tanzania ikiwa na asilimia 5.7 ya wanaoishi na VVU wakati kwa Shinyanga kiwango kilikuwa ni 7.4%. Takwimu za ndani za mkoa kwa mwaka 2009 zinaonyesha Shinyanga ina kiwango cha maambukizi cha asilimia 6.7.
Miongoni mwa vichocheo vya kuenea kwa maambukizi ya VVU Shinyanga ni pamoja na tabia ya kuwa na wapenzi wengi, unywaji wa pombe kupindukia na biashara ya ngono, ambavyo vyote vinajadiliwa kwa kina na viongozi wa dini katika kuwaasa waumini kujiepusha na mambo hayo ili kujikinga na UKIMWI na pia katika kutenda mambo yanayompendeza Mungu.
 Sambamba na upimaji VVU washauri nasaha katika vituo hivyo vinavyosimamiwa na TIP  huwapa rufaa vijana na wanaume ambao hawajafanyiwa tohara kwenda hospitali ya mkoa kufanyiwa tohara chini ya mradi maalum wa kufanya tohara kwa wanaume  unaoendeshwa na hospitali hiyo. Shinyanga ina kiwango cha chini cha kutahiri wanaume ambayo ni chini ya asilimia 20 kitaifa.

Kwa msaada kutoka mfuko wa Rais wa Marekani wa kupambana na UKIMWI (PEPFAR), TIP inajaribu kukabiliana na changamoto zinazoukabili mkoa wa Shinyanga kwa kufanya jitihada za kuondoa unyanyapaa, kuweka vituo vinavyohamishika vya upimaji kwa kufikisha huduma karibu na wananchi.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...