Naibu Spika Wa Bunge Mh Job Ndugai akiongea na waandishi wa habari .
Mbunge wa Viti Maalum ambae ni Naibu Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Haki na Utawala  Mh Angellah Kairuki akijibu swali toka Kwa Baraka Baraka.
Mbunge wa Bariadi mashariki John Cheyo akijibu maswali.
Mbunge wa Ilala Mh Zungu akijibu maswali.
kutoka kulia mwandishi Nguli Freddy macha Akiwa na timu ya urban Pulse wakati wa mkutano.
Picha ya pamoja Baada ya Mkutano na waandishi wa habari.

Salam,

Wabunge wanne waliokuja Uingereza kuzungumzia mgogoro wa pesa za kampuni inayouza vifaa vya ulinzi –BAE Systems wamefafanua namna zitakavyotumiwa. Wakiongea katika Ubalozi wetu Uingereza mjini London, Ijumaa mchana, viongozi hao walihimiza wanachofanya ni kufuatilia matokeo ya mahakama ya sheria inayochunguza rushwa (Serious Fraud Office-SFO) maana kadri muda unavyokwenda ndivyo riba inaongezeka.
Wabunge walikutana na House of Lords ambao ni maofisa na viongozi wa ngazi za juu sana wenye usemi mzito katika masuala ya kisisiasa Uingereza.

Mwezi Desemba mwaka jana SFO iliiamuru kampuni ya BAE kulipa faini paundi laki tano na kuipa serikali ya Tanzania paundi 29.5 milioni sawa na shilingi 75.3 bilioni za kitanzania kama pesa za kujisafisha uso. Toka tamko hilo litokee miezi sita iliyopita imezuka migogoro kadhaa.
Upande mmoja BAE system wanataka fedha zisipewe serikali ya Tanzania bali kwa mashirika ya fadhila toka nchi za nje upande mwingine uongozi wa Tanzania unasisitiza serikali inao mfumo imara utakaohakikisha fedha zitawafikia wahusika.

Mgogoro ulianza mwaka 1999 wakati Tanzania ilipotaka kununua vifaa vya kusaidia ulinzi wa viwanja vya ndege toka kampuni ya BAE. Ilidaiwa kuwa mfanya biashara Shailesh Vithlani wa kampuni ya Merlin aliyefanya dili kati ya BAE na Tanzania alipewa asilimia 30 ya pesa ya mauzo kama hongo. Pesa hizo ziliwekwa katika akaunti yake ya benki Uswisi. Wahusika wengine ni aliyekuwa Wakili wa Serikali, Andrew Chenge na Gavana wa benki kuu, Idriss Rashid. Wote hawajashtakiwa na Vithlani anadaiwa kujificha Uswisi, ilhali SFO imetoa tamko afikishwe mahakamani.
Akijibu swali kuhusu kutokuelewana huku, mwenyekiti wa msafara Mbunge Job Ndugai ambaye ni Naibu Spika wa Bunge la Taifa, alisema si vizuri BAE kutuingilia au kutueleza nini cha kufanya na pesa hizo ambazo ni maslahi yetu .
“Sisi tunafahamu mfumo gani utakaohakikisha pesa hizo zinatumika sawasawa, zikienda kwa mashirika ya ufadhili ni kama zimetolewa kwa watu wa nje.”

Mbunge mwingine, John Momose Cheyo ambaye ni mwenyekiti wa kamati ya Bunge inayohusika na Hesabu za Umma, aliwahakikishia wanahabari kwamba katika miaka kumi toka tukio hilo la 1999 vyombo vya serikali dhidi ya rushwa vimebadilika na kuimarika. “Matumizi halali ya fedha yatakahakikisha pesa zitatumika kujenga elimu,” alisema Mbuge huyo wa Bariadi Mashariki.
Toka SFO ilipoamuru BAE Systems ilipe faini kwa mahakama na fidia kwa Tanzania yametokea pia madai kwamba wapo walioandikia BAE barua pepe kuwa wasiilipe serikali ya Tanzania pesa hizo.
Wabunge wanasisitiza pesa zitaendeleza elimu.

Mbunge Maalum, Angellah Kairuki ambaye ni pia Naibu Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Haki na Utawala, alielezea kwamba ingawa pesa hizo zinaonekana nyingi lakini hazitasuluhisha matatizo yote ya elimu nchini, mathalan, kuongeza mishahara ya waalimu.
Alitoa mifano ya ukosefu wa madaftari, vyoo na vitabu vya kusaidia waalimu kufundisha. Mifano hiyo inayolenga shule za msingi na sekondari inatokana na matizo makubwa ya wanafunzi kujisaidia porini na kukosa vifaa muhimu vya elimu.

Mbunge Mussa Zungu wa Ilala, na vile vile Naibu Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge inayohusika na Ulinzi, Usalama na Mambo ya Nje, alikumbusha kwamba tatizo halikuanzwa na Watanzania. “Ni suala lililoamuliwa na mahakama ya Uingereza; sisi tuchohitaji ni kuendeleza elimu.”

Habari imeandikiwa na Freddy Macha akishirikiana Jestina George pamoja na
URBAN PULSE CREATIVE

MUNGU IBARIKI AFRIKA, MUNGU IBARIKI TANZANIA

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

Kuna Maoni 7 mpaka sasa

  1. SFO haikuamuru BAE Systems itoe malipo yoyote. Fedha ambazo SFO itazitoa kama ex-gratia (hisani) ni maamuzi yaliyokuja baada ya makubaliano kati ya yake na SFO ambazo pande hizo mbili zilikubaliana kulimaliza sakata hilo. Ni katika makubaliano hayo ndio BAE walikubali kutoa paundi hilo kwa masharti kwamba SFO wasimshtaki mtu yeyote wa BAE (kinga), wasitishe uchunguzi wao, na kwamba hawamtamshtaki mtu yeyote kwa kosa lilitokea kuhusiana na suala la rada (hata kama kosa hilo halijajulikana bado).

    SFO wakawa tayari kusitisha uchunguzi wao endapo SFO itakubali hatia (plead guilty) kwenye makosa kadhaa- hakuna la ufisadi. Hivyo SFO wakakubali hatia ya makosa ya kihasibu - kutokutunza kumbukumbu na kutoripoti mahesabu yao sawasawa. Ndio kama alama ya makubaliano hayo BAE wakapigwa faini ya paundi 500,000 na kukubali kutoa fedha kama hisani "for the benefit of the people of Tanzania".

    Hivyo basi, fedha hizi siyo "compensation, refund, reparation, restitution, return'. Siyo deni tunalowadai na wala siyo fedha ambazo serikali yetu ilimpa Vithlani dalali aliyehusika pia na ununuzi wa dege la Gulfstream 550 la serikali wakati wa Mkapa. Vithlani hajaamuliwa kurudisha fedha alizopewa na BAE kuwagawia watendaji waliowezesha dili liende. Hatujamshtaki kwenye mahakama yoyote kwa uhujumu uchumi - chini ya hilo tungeweza kufilisi vitu vyake!, n.k Tumeshtaki Kisutu kwa "kusema uongo kwa mpelelezi!" na ni kwa sababu hiyo ndio tumeotoa International arrest warrant.

    Hivyo, ripoti japo inavutia kusoma ingekuwa imeweka ukweli kidogo basi.

    ReplyDelete
  2. AnonymousJune 26, 2011

    Je kama BAE wataamua kununua hivyo vifaa vya mashuleni kwa pesa yote hiyo kutakuwa na ubaya wowote? Au shida ya Serikali ni kuitia hiyo chenji mkononi kwanza? Mimi nafikiri serikali wawe wawazi kama shida ni shule si wawape bajeti ya hivyo vitu wanavyotaka kufanya kwenye elimu halafu mkataba utayarishwe ili mwisho wa siku BAE wawajibike wasipotekeleza.

    ReplyDelete
  3. AnonymousJune 26, 2011

    haki ya nani, haya sijui kitatoka kipi tena, maana zile nyingine mlianzisha kilimo kwanza. (natumai mmenielewa watanzania)

    ReplyDelete
  4. AnonymousJune 26, 2011

    Anony wa pili umenifurahisha. Wewe hujijui serikali yetu? Hiyo hela inatakiwa ikachakachuliwe. Ndio maana hawataki kuwaachia hao BAE walipie hiyo elimu. Wazo lako ni zuri sana. Wasingelikuwa wanataka kuichakachua wangepelekea nini wanataka kufanyia hiyo pesa na bajetu halafu wawaachie wao watekeleze. Sasa kulumbana hivyo mwisho tutaikosa hata hiyo pesa.

    ReplyDelete
  5. AnonymousJune 26, 2011

    Mimi nawapinga serikali. Waliingia dili baya na isingekuwa waingereza wenyewe kuibua issue hii, ilikuwa ndio imetoka. Halafu mbona EPA wamekula na hawabebi bango namna hii.

    Serikali wanatufanya wananchi wajinga. Hizi pesa zipewe Charity organizations ijulikane moja.

    Wakitaka kujenga shule wakarudisha pesa za EPA.

    ReplyDelete
  6. AnonymousJune 26, 2011

    Hivi jamani mnakumbuka enzi za rada mafisadi yalivyokuwa yakivimbisha kifua kwamba lazima jeuri ifanywe?halafu nini waziri mwingine katoka na mpya eti yuko tayari watanzania wale nyasi ila tu dege la raisi linunuliwe?kumbe wanajua vijidudu wanavyofanya

    ReplyDelete
  7. AnonymousJune 26, 2011

    kweli mimi naona serikali ya bongo isipewe hela hizo maana zitaiishia kwenye mifuko ya watu fulani,yale yale ya EPA. Kama hela zitatumika kwa kuendeleza elimu wacha hao BAE walipe kila kitu kuanzia majengo na mpaka mfagiaji wa hizo shule na malipo yafanywe once services zikimalizika na wao BAE should hire contractors. Serikali ikipewa hiyo pesa well tunajua watu gani wata ifaidi na wakati wanafanya hilo deal na BAE kwani hawakujua hili ni deal baya. Me naona walijua deal ni baya na litalipuka na hela itabidi zirudishwe na muda zikirudishwa ndiyo mafisadi kuchukua percent zao. Kila siku umeme unakatika kwa ujinga wa watu fulani na sasa mpewe ten 30 mil pounds jamani haa aibu hamna,time watanzania tufanye kweli na kubadilisha ujinga huu...deals zinafanywa kisirisiri kila siku sasa sijui madeal mangapi huwa yana bounce kama hili

    ReplyDelete

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...